Thursday, September 12, 2024

MOYOWENYE MASHAKA sehemu ya pili


“TWENDE BEACH.”

        “Opamiss, twende Beach.”  Lameck alihitaji mie niongozane naye kwenda kwenye fukwe  ya Bahari kujimwaga  na kubarizi, tukipigwa kwa upepo mwanana wa Bahari ya Hindi.

 “Poa.” Nilimwitikia akatabasamu, akahisi kama vile bado ninampenda kama zamani, ukweli ni kwamba kwangu Lameck Keisha oza, simtamani. Sijui kwa nini? Au ni moyo wangu ulioanza kuota mizizi ya penzi la kinafki?

                        Nikaingia chumbani, ndani ya kile chumba amabacho nilimkuta Lameck yupo juu ya kitanda kile ninachokichukia leo, nilimkuta akiwa na yule umbwa Malaya wake wakibanjuka kama vile hawana akili timamu. Aah! Nina tabia za kidume dume ukali kiasi fulani na chuki kiasi fulani. kukitazama kile kitanda nilianza kukichukia moyoni, hata hivyo nina kama mwezi sasa sijalala juu ya hicho kitanda ninachokiona kama mkosi kwangu, kipindi chote hiki tangu namemfumania Lameck akila uroda na huyu malaya Umbwa wake. Mie nimehamisha makazi yangu, nimehamia sebuleni, ninalala juu ya hilo sofa kubwa la kutosha watu watatu wajapo keti. Wakati mie nalala sebuleni ninamwacha Lameck akiwa juu ya kitanda hicho, kalala pekee. Anayajua makosa yake ndio maana hanilazimishi nikalale pamoja naye basi anakaa kimya kama maji ya mtungini, asitake kunena neno.

                   Mie Opamiss nikachukua pesa mingi, nikaweka ndani ya kipima joto changu (kimkoba) tena siku hiyo nikatupia mwilini mwangu kitopu flani hivi kinacho yabana maungo yangu, viatu vizuri vyenye kanyagio la chini chini, nikachukua kofia yangu ya kichina, kofia moja pana hivi. kwisha kumaliza kuvaa nikatoka ndani ya chumba kile, nikaubamiza mlango, ule mlango ambao ndani yake kuna godoro ninalo lichukia, sio godoro pekee hata mashuka yenyewe kwangu ni kero.

                    Lameck alikua akinisubiria, alipo hakikisha kuwa tayari nimeweka mambo sawa, akanyanyuka pale alipoketi akanishika kiuno changu nikajifanya kutabasamu, ile mikono yake, mikono aliyonigusa siku zile nalihisi joto kali ajabu lakini leo mie nahisi baridi yanitetemesha. sikupendezwa, nikatamani kumwambia, “Bwana we! Niwache mie.” Ila sikuthubutu kunena hivyo sababu moyo wangu ulijaa unafki na sababu ya hayo yote ni yale maumivu ya mapenzi, Lameck amempenda mtu mwengine mie anifanya bwege, eeeh! Mh! kweli kupendwa kazi.

       Gari yangu Tax,  ipo wazi juu ya bodi yake, ni gari moja ya fahari, sijainunua muda mrefu ina mwaka na ushee mara chache siku za jumamosi namezoea kutoka out pamoja na Lameck msaliti wangu, najaribu kuupoteza muda kwa kumfunda funda namna gani anaweza kuiendesha hiyo gari, kafanya juhudi ndani ya miezi mitatu tayari alikwisha kujua namna ya kuicontro hiyo gari sioni tabu kumuachia aiendeshe yeye mwenyewe lakini leo sitamwachia nitaiendesha mie mwenyewe nitaicontro hadi tufike beach.

           Baada ya mwendo wa safari yetu tulifika Mbezi beach, aah hapana hatukwenda Mbezi, tulikwenda kunduchi, mahaba beach ๐Ÿ–️ ni kutulivu sana, kuna faa kwa ajiri ya wapendanao, kunafaa  kwa ajiri ya wenye kupunguza mawazo yao, kunafaa sana. Upepo mwanana ni uturi wa mapenzi. Basi mie Opamiss pamoja na Lameck tukayachezea sana maji ya bahari, maji yenye chumvi chumvi, japo yanaburudisha kuoga, tukala pamoja na kuusikiliza Muziki wa ngoma za asili. Tulikutana na wasanii wanaoimba na kuburudisha wageni wanao kwea kule.


       Muda wetu mzuri ukayumba yumba na kupotea, basi tukachoka tukahitaji kuondoka. Lameck anaudhi moyo wangu, sio kama zamani, zama zile nalizompenda ajabu, kwa sasa kila anachonena nakiona kama kibaya lakini acheni niseme hakuna marefu yasiyo na ncha, kila kitu kina muda wake, nalijua hilo najua muda ukifika nitaweka mambo yote yawe safi yanyoke yanipendeze.

           Ati nimpeleke shopping, sikukataa japo kwa kinyongo nilikubali, mie mwenyewe sijui kwanini moyo wangu unasukumwa na unafki? Kwanini moyo wangu una mashaka? Unajua mpenzi msomaji hapo kale, kale kabla Lameck hajanitia maumivu ya mapenzi kile chochote alichotamani, kile chochote alichoomba, kile chochote alichotamka mie nalikua chapuchapu namtimizia, nilimpatia, nilimuhudumia, nilimfanyia bila kinyongo yaani nilikuwa tayari kwa ajiri yake.

             Wakati huu mapenzi yamegeuka nyama iliyooza, nayachukia haya mapenzi, yanitia harufu mbaya puani kwangu, nahisi kinyaa na kutapika, sijui niitapike, lakini wacha mie nivumilie, japo nahisi kuutesa moyo, moyo unahangaika mahangaiko makuu. Naificha hiyo nyama iliyooza ili watu wasijue fika kuwa mie mwenzao ninatembea na la kuvunda, nisingependa wajue sababu mie pia ni binadamu ninaipenda siri yangu ibaki kuwa siri yangu.

          Nikaigeuza ile gari yangu iliyo wazi juu, tukaelekea barabara iendayo Ubungo, njiani tukipiga story mbili tatu za hapa na pale mambo ya maisha, kawaida mbona! Hatuwezi kuizuia midomo yetu iwache kunena.

           Ndani ya Mlimani city Lameck  alikuwa huru kuchagua chagua nguo viatu na saa ya mkononi, alipanga na kupangua, alichagua na kuingia chumba cha kubadili nguo, akabadili atakavyo. Mie nilimwangalia tu akinilazimisha nimwambie kama hizo suti alizovaa zimempendeza ama la! Hazijampendeza? Sikutaka kuongea zaidi ya kumnyoshea dole gumba kama ishara ya kwamba nguo zile alizovaa ziko poa na kama hazikuwa poa nalilidondosha dole gumba langu  (naliligeuzia chini) kama ishara ya kwamba hizo  haziko poa. Akachagua chagua viwalo alivyoridhia mie  nikalipia gharama zote.

        Tukamaliza manunuzi yetu, tukaondoka zetu kwa moyo wote nikampeleka Serena Hoteli, moja ya Hoteli za kimataifa, Hoteli za wenye pesa zao. Watu wenye vyeo vyao, watu binafsi wale wenye hadhi serikalini. Hawana shida, wacha waburudike na kufurahia kama ujuavyo tena mpenzi msomaji maisha ni mimi na wewe.

Zamani naliyafanya maisha yangu yawe ya mimi na Lameck, lakini kwa sasa sidhani kama naweza kuyafanya yaendelee kuwa ya mimi na Lameck, ninaujua moyo wangu, ninajua fika kuwa moyo wangu una mashaka, ipo siku moyo ukitulia nitajua vizuri maisha yangu yatakuwa ya mie na nani? Sina shida ya pesa, pesa kwangu sio  big problem. Ninaisimamia kampuni ya Marehemu babangu, sio kampuni kubwa kiivyo ni ndogo kiasi, kampuni ya kuingiza mizigo, nguo za mitumba kutoka nje ya Tanzania. Kazi yangu mie ni kuisambaza hiyo mizigo kwa wateja waliopo mikoani. Any way nisingelipenda kuongelea sana kuhusu kampuni au kazi yangu binafsi sababu hiyo sio dhima na kusudio la simulizi yangu.

               Tulikula tulikunywa mie na Lameck Lameking yule fukara mwokota kopo na chupa tupu. Jamani msinikosoe ndio kupenda huko, kupenda waweza kupenda yeyote, haijalishi hata kama ni fukara namna gani utapenda tu, hata akiwa mlemavu aso na miguu au mapaja  mwenzangu utapenda tu, ndio maana moyo wangu ulimpenda Lameck, moyo wangu ulimvuta Lameck mie nikamfungulia moyo wangu nikampatia kila kitu atakacho.

         Ni mlevi, anapenda kunywa, japokua hana kawaida ya kunywa zile pombe za kisasa, kazoea kunywa pombe za kienyeji (matapu tapu) nikambeza na kumwambia aachane na pombe za kienyeji, lakini mh! Sasa naanza kuamini mjasiri aiwachi asili. Hajawacha asili yake, hajawacha mbachao kwa msala upitao, anajua fika kuwa kila mtu ana kwao kuzuri kwenye matunzio.

           Nimeona eeh! Macho hayana pazia, moyo hauna pazia, kapenda boga na ua lake, wahenga wanasema kipenda moyo hula nyama mbichi mwenyewe karudi kwenye mji wake (vilabuni) kairudia asili yake, anakunywa matapu tapu, japo kwa siri sana, kama macho yake yanavyoonesha. Lakini hata hivyo Dunia haina siri, pombe ukiinywa utajulikana tu utajulikana kwa harufu na kwa madoidoi yake. 

Lameck alirejea kwenye asili yake, sikumkataza sababu nalikua dhaifu kumkemea au kumuonya wangu niliyempenda na matokeo yake mie leo najuuuta, mie leo nasikitika, mie leo nachukia, mambo yamekuwa ovyo, Lameck kutembea na muuza matapu tapu, mh jamani mwe!   

        Haya mapenzi kuchaguana, mie nalimchagua Lameck miongoni mwa wengi naliowaona Duniani, yeye hakuridhia kuwa na mie sababu ana macho ya kuficha siri. Ndo’ maana kumtafuta huyo Bibie  muuza pombe.

Nisimsute sana, labda ndio pombe zilizo haribu mambo, labda ndio pombe zilizotibua mambo, labda mh!  Nimebaki na labda.

       Tukiwa tungali bado pale pale Hoteli, mie na Lameck tukacheza  muziki wa blues, muziki mwororo, muziki wa kizungu, muziki wa mapenzi, muziki wa kuzungurushana zungurushana, muziki wa kushikana shikana viuno na kunyanyua mikono miwili iliyoshikana na kupanda juu chini, kulia ama kushoto, muziki wa kutazamana machoni, shingoni na kadhalika, teeh teeh teeh (nacheka mie).

Nacheka moyoni nikikumbuka zama zile, mpenzi wangu msaliti wangu, Lameck alikua hajui kucheza muziki wa blues na mie nikachukua muda wa kuwa mwalimu wake, nikamfunda akafundika,wallah! Akaboreka na kuwa mjuzi wa kuzunguruka zunguruka kwa miondoko, miondoko ya blues,teeh teeh teeh aaash! Nimefurahi mie, muhimu kukumbuka pale unapokutana na kitu ambacho zamani kilikua kipya machoni, kigumu moyoni, chavunja moyo, leo hii mtu unakuwa nguli wa kucheza blues!


(Tukutane sehemu ya tatu)




No comments:

Post a Comment

I promise you

   I PROMISE YOU. (NINAKUAHIDI.) SURA  YA KWANZA. UBAYA WA POMBE. “Umenizingua job, umenizingua kwa muda mrefu sana mpenzi wangu…….kwanini l...