LEO MCHANA.
“Ni lazima niitishe kikao cha wazee wa Mila, ni lazima nipange siku moja maalumu kuwakomoa firauni hawa, wajinga na wapuuzi wanao yachezea maisha yangu ………… Nakwambieni Ally mpuuzi wewe nitakukomesha. Mwaka huu nitakukomoa ili uione dunia chungu, kama uchungu wa nyanya chungu, Ng’ombe we!” Mzee Jamali aliwaza yeye na moyo wake, amekasirika sana siku ya leo, hajapata kuwa na hasira kama alizonazo leo, kamwe hajapata kukasirika kama alivyokasirika leo, leo Shetani kamwingia, tena huyo Shetani kamshawishi afanye hima hima apate kumkomoa Ally mwanawe wa kumzaa.
“Ninatamani kumwaga damu, damu ya makafiri wapuuzi, wajinga, mafirauni nyie mnanihujumu mapenzi yangu.” Macho ya mzee Jamali yaliiva kwa hasira. kujibanza kwake nyuma ya kijumba nyasi haikutosha kuipunguza jaziba aliyokua nayo, hasira zilimpanda pale akimuona mkewe mpenzi Tunu binti mashallah! Amesimama na Ally mwanawe wa kumzaa, kila ikiwa leo hawana jambo la muhimu kujadili zaidi ya kutizamana machoni kama Ndege wawili mapenzini.
Hawana jambo lolote lile muhimu zaidi ya kunena nena vijimaneno ambavyo Mzee Jamali Mzee mwenye umri wa miaka sabini na ushee anahisi ndani ya fikara zake kuwa wawili hawa wanaongea juu ya mapenzi, mapenzi yao wenyewe, japo kwa usiri mkubwa ambao si Tunu wala si Ally aliyekua tayari kumweleza Mzee Jamali
“Tunu nilikutoa Kijijini kwenu ukiwa umeoza, unanuka, umeharibika. Miguu yako yote miwili ilikua imeoza na kuharibiwa na Funza, ambao kwa mikono yangu hii miwili nilikua radhi kuwachezea chezea hao Funza na kuwatoa miguuni kwako, ulikuja kijijini kwangu ukiwa umekonda haswa, umekonda kama gofu lililoachwa na Mkoloni, umekonda na kudhoofika, umekonda mifupa mifupa, umekonda kama Mnazi uliokosa mbolea ya Samadi. Macho yamejaa tongo tongo kama usaha,” Aliwaza.
“Nikachukua jukumu la kukulisha, kukupaka mafuta ya kukunenepesha na kunawilisha mwili wako. Leo hii unang’ara kama Jua, leo hii umenenepa kama Tembo, leo hii umeukacha ule ushamba wako wa Porini, ajabu! Taaratibu taaratibu unanisusa kisiri siri, umeona wacha unisaliti, umeona sio mbaya kuwa na mtu mwingine pembeni, umefikia hatua ya kunitema mfano wa bigi ji inayotemwa kwa maonjesho ya utamu wa karanga,”
“No way, sikubali wala sikubaliani na matendo ambayo umefikia hatua ya kunifanyia. Kwa pupa zako wataka mie niamini maneno ya wahenga waliposema heri kumfadhiri mbuzi atakupa nyama, kuliko kumfadhiri binadamu atakaye kutia aibu na fedhea. Sawa, Sina mengi ya kuongeza nilazima nitawakomesha ili mjue kuwa sihitaji michezo iliyopitwa na wakati.”
Mawazo yalimsumbua Mzee wa watu, mawazo yalimsumbua usiku na mchana, yalimsumbua asitake kumwambia Tunu au mwanae Ally juu ya donda linalo muumiza, donda linalo geuza geuza akili zake, akachomoka kutoka kwenye pembe ya kijumba nyasi chake, ameshikilia mkongojo, Koti lake lenye rangi nyeusi ametupia juu ya mabega, kanzu yake chakavu mwilini imeambatana na baraka shea yake chakavu kichwani, akajikongoja kongoja, akawapita hawa wawili waliokua ndani ya bustani ya mboga mboga, wamesimama wana ongea kwa raha zao .
Tunu na Ally walimwona Mzee Jamali akichomoza pale alipojibanza akielekea ndani ya kijumba nyasi chao.Tunu alieleka kumpokea mumewe riziki aliyokuja nayo siku ile, Ally kijana wa pekee kwa Mzee Jamali, aliendelea kupalilia mboga mboga bustanini.
Ally ana umri wa miaka ishirini na mitano, wakati Tunu ambaye kwa sasa ndie mamae Ally, mama wakufikia, mama wa kambo. Anakaribiana kidogo na umri wa Ally, yeye ana umri wa miaka ishirini na mitatu bado angali ni binti mdogo mwenye wingi wa furaha na tabasamu, tabasamu lake zuri kama Mauaridi, macho yake makubwa mazuri kama mtoto mdogo mwenye umri wa miaka mitano, nywele za huyu binti ni nywele za asili ndefu, nzuri, zimechanua mfano wa Ua Jasimini.
“Habari za kazi mume wangu?” Tunu alimsabahi Mzee Jamali, tayari Keisha kumpokea ile riziki ya siku ile.
“Salama mama Ally, nina furaha kubwa kuwakuta mkiwa salama salimini.” Mzee Jamali alijibu akilazimisha tabasamu la kinafiki limtoke mdomoni mwake akijua kwamba bado ni mwenye hasira juu ya ule uhusiano ambao yeye anahisi kuwa Tunu na mwanae Ally wameujenga.
“Pole sana baba Ally, pole mume wangu, pole kwa majukumu mazito ya kila siku.” Tunu alimfariji mumewe wakati huo huo Tunu amekwisha kuchukua kitenge chake alichojifunika kiunoni akalifuta jasho lililokuwa limesheheni juu ya paji la uso wa mumewe kwisha kumaliza kumfuta jasho lilosheheni juu ya paji la uso wa mumewe Tunu akaikamata miguu ya mumewe akaifuta futa vumbi kwa kile kitenge chake, kwisha kuhakikisha kuwa mumewe ni safi Tunu akalichukua koti la mumewe kwa lengo la kwenda kulihifadhi chumbani kwao kwa heshima zote Tunu alilitundika lile koti juu ya Msumari uliopo ndani ya chumba cha yeye na mumewe.
Akaelekea Jikoni, akakitwaa kibuyu kidogo kilicho jaa asali, tena akakitwaa kingine kilicho na maziwa fresh, akaeleka pale alipoketi mumewe. Tunu akafanya kumimina ile asali juu ya miguu ya mumewe, kulikua na beseni ambalo limemiminiwa maziwa. Basi Tunu akaanza kuiosha miguu ya mumewe kwa kuchanganya changanya ile asali na maziwa, kwisha kumaliza ile kazi Tunu alimfuta futa miguu mumewe, alimfuta futa kwa kile kitenge chake. Alihakikisha kuwa mumewe ni safi salama, Tunu alilitoa lile beseni akaenenda jahani kuumwaga ule mchanganyo wa maziwa na asali na baada ya hayo yote Tunu akaeleka Mekoni kumwandalia mumewe mlo wa mchana ule.
Maana yake nini matendo haya yote aliyoyatenda Tunu? Mpenzi msomaji acha kujiuliza, usijiulize nawe ukapasuka kichwa chako. B asi sikia ni hivi; Mapenzi ni kukubali kila kilicho kizuri na chema machoni, mapenzi yanajali na wewe pia wapaswa kuyajali. Kwenye mapenzi wapenzi hawapaswi kusikitikia gharama kubwa ya kuyaendesha mapenzi. Tunu hasikitikii hizo gharama za kuyaboresha mapenzi ya yeye na mumewe mume Mzee, Mzee aliyemzidi umri. Uzuri wa mapenzi aliyonayo Tunu ni kwamba; Tunu hayalazimishi mapenzi yaonekane kwa mumewe, anafanya jambo la kweli, anatumia vile vitu vya asili ili kuyapamba mapenzi aliyo nayo kwa mumewe.
Ndivyo walivyofundwa watoto wa Tanga, wamefundwa nao wakafundika, wamefundwa namna ya kuyapamba mapenzi, kuyalea na kuyaboresha, kufanya mambo na vijimambo tofauti tofauti ambavyo walio wengi katika ulimwengu wa sasa hawawezi na tena hawajui kufanya mambo matamu ya kale, wanasahau fika kuwa ya kale yananukia wanaziogopa gharama, wanaziepuka na kuzikimbia.
Ni utundu kiasi ni ubunifu na ujuzi. Tunu anajua fika kuwa ili kumtoa nyoka pangoni sio tu kwa kuitumia sauti yenye mahaba bali pia zatakiwa mbinu mbali mbali kuhakikisha kuwa huyo nyoka lazima atatoka iwe au isiwe atake au asitake lazima atoke tena lazima atoke kwa mikiki mikiki papala papala, liwalo na liwe.
Mchana ule Mzee Jamali alipata chakula alichoandaliwa na mkewe, Ugali mzito, nyama tamu, mtori pamoja na maziwa ya mgando, Mzee akala akashiba na kusaza japokua bado moyoni mwake hakumwamini mkewe, bado mawazo machafu juu ya mkewe Tunu na mwanae Ally yalimvuruga akili, hakutaka kuonesha hisia juu ya chuki aliyohifadhi ndani ya mtima wake chuki juu ya hawa walio kwenye mihimiri yake. Aliendelea kuuonesha upendo wake kwa Ally mwanae na Tunu mkewe wakati huo huo angali anawajengea visa na vituko moyoni.
Je, amepata kumfumania Ally na mamaye wa kufikia wakiwa ‘very closer?’ hapana hajapata kuwafumania wawili hawa wakiwa very closer. kinacho muuma yeye ni jinsi anavyo waona hawa wawili wakiwa Beneti kwa kila kitu ambacho anaona mbele ya macho yake.
Anachukia mara akisikia Ally na mamaye wakigongeana milango, ni mapema mno, mapema hata kabla Jimbi hajawika ‘kokorikoo ‘ Ally atagonga gonga mlago wa chumba cha babaye na mamaye Tunu, Ally atamwamsha mamae Tunu ili waende kuteka maji mtoni, siku nyingine Tunu ataugonga mlango wa mwanae Ally watoke kwenda msituni kuteba kuni. Yamekua ni mazoea ya kujirudia rudia hali ambayo kwa miaka miwili sasa mzee Jamali anajitahidi kuivumilia tangu kipindi kile Babu alipomuoa huyu Mrembo anayemtilia mashaka, anautilia mashaka mwenendo wake yeye na mwanae Ally
Mchana wa leo mzee atandaliwa vyakula vinono vinono vilivyopikwa na mkewe lakini ajabu mara ile atajisikia kichefu chefu na kutaka kutapika kwa sababu macho yake hayana pazia, anamwona mwanae Ally akiongozana na Tunu wanaelekea Mekoni wakifika huko wanashirikiana kuandaa makuli, mara ile wote kwa pamoja watamenya menya na kukata kata nyanya vitunguru, karoti, pili pili hoho pamoja na mboga mboga za majani, watakata kata kuni, watawasha moto, watainjika safuria ya Ugali, wataanza kuusonga huo Ugali, ajabu! watapokezana kuusonga Ugali.
Mzee Jamali anachukizwa na tabia ya mwanae Ally mara akimwona anakosha vyombo, anafua nguo za za mamaye Tunu wakati huo huo Tunu naye anajiweka bize kufua fua Nguo za Ally. Tabia ni mazoea na mazoea yanampa tabu Mzee Jamali, tabu ya kuwaona wawili hawa wakipuguta deki kwa pamoja, wakifwagia mandhari ya nyumba yake, wakiwalisha ndama waliopo nyumbani, wakienenda malishoni kuwaswaga Ng’ombe, Mbuzi na Kondoo, watahudumia bustani ajabu watachezea chezea maji, watamwagiana maji, watakimbizana na kucheza kama watoto wendawazimu, watafanya fujo, wakati wote huo mzee Jamali anawatizama jicho la chuki, anavumilia japo hana la kunena.
Usiku nao unakua mzito kwa huyu Mzee wa watu japokua anapata nafasi njema ya kujadiliana mambo mbali mbali ya kimaisha pamoja na mkewe lakini pia hapendezwi kwa ile tabia iso na kikomo, tabia ya Ally na mamaye Tunu kuketi pamoja pembeni ya moto wakijadiliana mambo mbali mbali ya kimaisha, lamkera jambo hilo, lamkera mzee Jamali, lakini afanyaje? Hana la kufanya zaidi ya kuvumilia na kuyaficha maumivu moyoni mwake.
####################
Itaendelea
No comments:
Post a Comment