Sunday, September 15, 2024

Mama Ali ๐Ÿ‘ฟ. Sehemu ya 4

 


Mama Ali

Sehemu ya nne

Tulipoishia:

Shoga usilie bibie, penye dhiki pana faraja, hakuna marefu yanayokosa mwisho,dawa ya deni kulipa na dawa ya matatizo kuyatatua…..” Nalimfariji Ma’ Ali’

      “Mwenzangu, mie nipo njiapanda nikizubaa mwanangu atadondoka kama tunda bovu juu mtini, nitamlilia nani mie masikini.” Mwenzangu alikonda kwa malalamiko.

“Nitakusaidia mwaya, tumgoje babu yetu pompo akuje toka kazini tumweleze shida yetu atusaidie,” Nalimpooza Shogangu Ma’Ali.#


Tuendelee hapa

Jioni kuingia Babu yenu Pompo karejea kutoka shuhulini, mie nae kwa kiroho cha huruma nikamdodosa Babu yenu naye akaelewa. Uzuri babu yenu Pompo hazingui wala hanaga magumashi. Nakwambieni yeye ni Mtu mwenye ubinadamu kaitoa shilingi laki tano mfukoni tena kawaambia polisi: “Mwana mpotevu arudishwe nyumbani.”Aruuuuuu  ilikua ni shangwe vigeregere nderemo na matabasamu. 

Mamie Ali hakukauka kumshukuru Babu yenu Pompo. Ali kwisha kutoka korokoroni karejea nyumbani tena uzuri wa yeye kurejea Pompo kamwita 

        “Embu ukuje tuyajadili tuyapambe yapambike”

       “Una umri gani mwanangu?” Babu kamuuliza Ali.

“Kumi na misaba nimetimu Babu yangu.”Ali kamjibu Babu yenu.

“Mdogo sana weye!!” Pompo kashangaa.

“Mdogo wa umri mzito wa matukio.” Ma’ Ali kapalilia makaa.

“Pia mdogo wa kuwajua watu na Dunia.” Pompo kayachokoza, Ali katazama chini aibu yamtikisa.

        “Sikiliza mwanangu.”Pompo kaanza kumwaga somo.

       “Katika umri wako kijana anahitaji kufanya bidii shuleni, bidii yako isiimezwe na tamaa za macho kutazama, tamaa zako zimalizwe na tamanio la kujifunza hekima, saburi na wema wa Dunia.”Pompo kakazia.

      “Macho hayakomi kutazama lakini kamwe usiuruhusu moyo wako kusukuma damu mbali ukaenda na maasi kuyatenda. Je, huoni maasi ni dhambi tendo chukizo kwake Mola na Dunia ituzungukayo?” Ali kaulizwa jibu asilitoe kainama chini kimya kwa aibu aloikumbata.

       “Uporaji, unyang’anyi, utumizi wa siraha zenye ncha kali, utumizi wa dawa za kulevya na mambo mengine machafu ni dhambi na hiyo dhambi uifute kuanzia leo machoni kwako.” Pompo kaweka tuo.

“Sikiliza mashauri ya Babu kazi uyatendee.” Ma’Ali kaongea.

      “Shukrani mgaie Pompo Babuyo, Pasina Babu Jela ungeliozea, ungelinuka ukaharibika na Jela kulivyo na maradhi mwana sijui kama ungelitoka salama.” Ma Ali aliendelea kunena kwa uchungu wa ndimu na maganda yake.

“Mwana umenitia aibu weye, jamii inichukie, fedhea nzito mjini sijui wapi nitaivua.” Ma Ali kwa hasira kayafufua yalokufa. “Mtazame Ba’ Yah’ babayo wa kufikia, pombe imemloga, hana mbele hana nyuma kaoza na kuharibika ajabu maji kufuata mkondo weye pia wanihujumu Ali.” Ma’Yah’ kalimwaga chozi.

     “Nisamehe mama, please forgive me kwa usumbufu na bugdha ilojitokeza ninakuapia sintarudia kamwe kukupa wasi wasi, stress hofu na mashaka.” Ali kapiga goti sakafuni kuomba msamaha.

     "Nitakunasa mabao mwana we! Embu mgeukie Babuyo Pompo na Mamie Mamsapu uombe radhi njema na kushukuru kwa mazuri kukutendea.” Ma’Ali kampigia kelele Ali, Ali kafanya hima kugeuka.

      “Ninaomba radhi Babu yangu Pompo na Mamie Mamsapu, naomba nishukuru kwa wema na mazuri mliyonitendea pasina nyie mie ningeliongeza Kalenda Jela.”Ali aliomba kwa moyo safi.

       “Hofu iondoe, matendo ya zamani uyafute, ukitubu uzaliwe upya uwe mwana mwema kwa Mamayo na kwa jamii ikuzungukayo.”Babu yenu Pompo kazipokea radhi za mjukuu.

      “Shule rejea uwachane na marafiki pamoja na makundi potofu, matunda mema utayafurahia iwapo utamshika elimu.” Mie Mamsapu nalimshauri Ali.

    “Wayasikia maneno Dhahabu wayanenayo Pompo na Mamie Mamsapu? Uyatekeleze upate kuishi vema na watu. Ma Ali alimuuliza Ali na kumshauri.

       “Ma’ kusikia nimesikia, kurudia sintarudia mabaya kuyaendeleza, elimu Dunia nitaifuata ili faida niivune, Marafiki na makundi ya ovyo yatanipeleka wapi mie kinda wa kumi na saba? Ali kaitoa ahadi.#################


Kuna aheri na uzuri mwana kumuonya na mashauri kuyashika, Ali alionesha mabadiliko, Shule alieleka, ile roho mbaya ya kujifupishia maisha kwa matendo ya wizi, uporaji na unyang’anyi ilimpokonyoka. Ndani ya miezi mitatu mbele Ali aligeuka na kuwa kijana swaafi takatifu. Mbona wenyewe tulimpenda, wenyewe tuliweka tumaini ipo siku Ali atakuja kuwa mtu mbele za watu. Kumuacha Ali wetu aaibike mbele ya makucha ya wale wasojua maana ya ubinadamu kwetu ilikuwa ni sawa na kuumiza moyo. Tukajipa matumaini ni lazima tumpiganie Ali hadi tone la mwisho, lazima Ali wetu abadilike.

Lakini yalaah!  Tabia ni kama ngozi, moyo ugeuka na kutazama nyuma kule mtu alikotoka kule kwenye asili ya kiza na macho ya Ibilisi shwetaini. Mjukuu wa Pompo alikamatwa tena alikamatwa na makucha ya Shwetaini safari hii aliyoyatafuta yalikuwa ni mazito kukuambieni. Sijui niseme…. Naona mfadhaiko!Mwana wa mwenzangu mwana wangu pia. Katupwa Korokoroni kwa kesi nzito ya mauaji, ati Ali kashiriki mauaji akiwa na kundi la Panyarodi, vijana Wahuni walioshindikana mjini, vijana wenye roho ndogo ya kutoa msamaha, roho kubwa ya kujeruhi watu, kupiga, kupora mali, kuiba usiku majumbani, kuvunja Ofisi na makampuni, kuingilia mwili kwa lazima, unajisi na fedhea. Mmmh! Tulishituka sie.Kesi ya Ali ilianza kulia na kuunguruma, mie Mamsapu, Babu yenu Pompo na Mamie Ali kutwa kuchwa kiguu kueleka Court, kila juhudi na hamsha hamsha tuliyoitoa kwao Askari ili Ali wetu aachwe huru haikuzaa matunda bado tu Askari walibwata  “ALI KASHIRIKI MAUAJI’ ‘NI NGUMU KUMUACHILIA MTUHUMIWA.’ ‘ACHA SHERIA ING’ATE PANAPONG’ATWA’  Sie tukachoka  kuyasikia hayo mabwato ya Mabwana Polisi mioyo yetu ikapooza, tukawa ni wale wajawa huruma mfano wa yatima wasodeka.Tufanye nini kipya ikiwa yote mapya kila siku twayaibua lakini mbele ya Sheria yalionekana yamepitwa na wakati? Basi sie wanadamu wenye huruma zetu tukaiacha Sheria iitwe Sheria.


Mwana akakutwa na hatia ‘Kashiriki mauaji usiku wa bundi na popo alipoeleka kumwibia kizito mmoja hivi mwenye pesa chafu.’  Miaka mitatu Jela ilimuhusu akamuachia chozi Mamaye aliyegaragara kwenye tope akilia na kumlilia mwanaye.Roho wangu, Babu yenu Pompo akaniambia: 

       “Sio mwisho, bado tumaini lipo hai, mafundo tulompa hakushiba Serikali itatusaidia kumjenga na kumrekebisha. Akitoka hapo mwana atatoka na nuru usoni, atajua nini apaswa kufanya, nini hapaswi kufanya, Hayo ndio maisha yetu sie wenye macho..”Mie Mamsapu nikahitimisha kwa kumwambieni Babu yenu : 

      “Babu uchungu, roho yaumia lakini wacha tukubali matokeo. Mioyo ya wanadamu inaficha mengi mengine mazito kutamka. Sawa mengi ni maneno machache ni matendo, matendo yanadhima kubwa sana ya kumwangamiza binadamu.Mtu akiwa makini kuyathibiti matendo yake yamkini majuto yatamwepuka.’ Twalitoka Court tukasepa Maskani, wanyonge wanyong’onyevu, tumeshindwa kumgomboa Ali wetu sie

##

(Embu ngoja tufike nyumbani vinono kuandaa na mazuri kuwapikieni)

Itaendelea

No comments:

Post a Comment

I promise you

   I PROMISE YOU. (NINAKUAHIDI.) SURA  YA KWANZA. UBAYA WA POMBE. “Umenizingua job, umenizingua kwa muda mrefu sana mpenzi wangu…….kwanini l...