LA MCHONGO
Sehemu ya pili
MKAKA AITWAYE MARCUS.
Wada mie kiguu na njia ghafla Gari moja zuri aina ya Prado nyeusi ilitua miguuni kwangu, kwanza nilikereka pili nilifyonya kwa nguvu mfyuuuuu mjaa laana'. Kwanini mpuuzi mmoja anisimamie miguuni kama vile amedhamiria kuivunja miguu yangu? Nilijiuliza mtimani, hasira zangu zimejaa kifuani.
Nikaitazama ile Gari mbele kwa Dereva vioo vya Gari yake vilikuwa off tena tinted yaani vyeusi wala nisimuone Dereva mwenyewe. Sekunde mbili tatu vioo vya upande wa yule Dereva nimwitaye mpuuzi vilifunguliwa akanitazama kwa tabasamu lenye afya na mie nikamtazama kwa madharau na mbetuo wa mdomo.
“Sorry Sister, sikudhamiria kuitua Gari yangu karibu na malundi yako?” Alianza kujitetea. Mie pigo la moyo likanienda kasi ile tu naisikia sauti ya yule mkaka, sauti ambayo nilihisi ni ya kimalaika. Tulitizamana nyuso domo langu gundi nishindwe kutamka kimya namtazama huyu Malaika mwenye sauti tamu ….
“Oh, usijali!” Wada mie nalifungua kinywa gundi nikanena.
“Habari ya leo, pole na majukumu ya kila siku.” Alinisalimia. Kumbe huyu Kaka ni mstaarabu hivi angekuwa mpuuzi mwingine si tayari angenitibua mwili wangu kwa tope la tairi ya Gari kisha angelinikimbia na kuniwacha ningali mchafu mchafukoge.
“Njema Kaka, nimepoa.” Nilimjibu kwa ufupi.
"Wauza tunda.” Macho yake yalitua kwenye kapu langu lililosheheni tunda zangu.
“Ndio…Embe Mia mbili, Chungwa Mia mbili pia.” Nilijinadishia biashara yangu.
“Ok naweza kuchukua Embe tano na Chungwa tano.” Mkaka niliyemwita moyoni mpuuzi alianza kunipooza makasiriko yale ya kuisimamisha Gari yake miguuni kwangu.
“Chagua kakangu.” Mie nikatua kapu langu chini na kulisogeza karibu na dirisha la Gari yake. Yule Mkaka akachaguwa Tunda. Sasa mie kwa kimbeembee nalibaki nikimtazama tu na kuushangaa moyo wangu umeanzaje kuvutiwa na huyu Mkaka kijana. Mmh! Kuishi singo yataka moyo. Alipomaliza kujichagulia Chungwa na Embe yule Mkaka akafanya kutoa noti ya shilingi elfu kumi na baada ya kunikabidhi akatamka
“Chenji jisevie.” Waooo! Moyo ulitabasamu yaani baada ya kukata shilingi elfu mbili ya tunda naachiwa elfu nane kama zawadi. Mungu unipe nini mimi Wada! Hii bahati ni nadra kunitokea, niikatae au niikubali? Kazi kwangu. Wahenga walishatwambia bahati ni kitu nasibu hakiji mara mbilimbili. Asante ikanitoka kinywani. Nikamshukuru yule mkaka niliyemdharau na kumwita mpuuzi moyoni.
“Niite Marcus, ninaishi Chanika huku Moshi Bar nimekuja kubarizi na kuvuta hewa.” Alianza kujitambulisha Mkaka wa watu. Mie niliyenogewa na zawadi nikajipendekeza ili nisionekane sina ushirikiano.
“Wada ndo’ mie mtoto wa kizaramo, Muuza tunda lenye asali. Moshi Bar ndo’ nyumbani. Karibu Bwana Marcus.” Kwa furaha nilijibu wakati huo bado ningali nimesimama kwenye kioo cha ile Prado nyeusi.
“Samahani kama hutojali waweza nielekeza pahali ilipo Hoteli, ningehitaji kupata maakuli ya mchana huu.” Marcus aliniomba nimpe direction ya pahali ilipo Hoteli. Si mnajua tena jamani mie mwenyeji wa mji huu wa Gogolamboto, Moshi Bar basi nikanena;
“kuna Masika Pub hapo hukosi kila pochopocho nono lenye kukupa nguvu na afya tena ukichanganya na tunda ndani ya mlo, we! Mbona utakua umeiokoa siku yako nzuri .”
“Patanifaa hapo” Marcus kijana mrefu mweusi tii kama Jungu lililoungua ukokoso, kadirio la umri wa ishirini na tisa akaongea kwa furaha.
“Pasikufae tena kaka mzuri kama wewe mwenye moyo wa Dhahabu?” Nikanogesha sifa na Sifa zikapamba moto.
“Sio mbaya kama utanisindikiza, nitanunua chakula cha watu wawili mie na wewe!” Waoooo! Mungu anipe nini mie, mkaka amenyimwa mbambamba huyu. Ile kusikia tu kuna Offa ya mie kula Hoteli mbona nalitabasamu tena na tena, Ukitegemea siku yenyewe nilikua ovyo tangu asubuhi sijapitisha maji kinywani na sasa ni kama saa saba mchana tumbo ni kavu kama maganda ya karanga tena laniunguruma ‘ngroooo’. Mie nikafurahi.
“Utakua umefanya la maana sana kaka yangu, embu ngoja nikupeleke.” Kimbeembee nikakimbilia upande wa siti ya Dereva kule mbele kabisa. Jamani mie mshamba wa kupanda Gari nzuri yenye kiyoyozi kinachotoa ubaridi wa barafu na manukato ya Arabuni niburudike kidogo, Nijione angarau nimeanza kupendwa nikapendeka. Gari ya Bwana Marcus ikashika moto, mwendo mdogo mdogo tulifika Masika Pub wawili tukakaribishwa kama Mfalme na Malkia wake. Eeeh! Wakati mie ni Bibi muuza tunda na mwenzangu ni mtu mwenye pesa zake. Muda kitambo Mhudumu alituletea maagizo yetu: Kuku rost, wawili wazima, pilau na chips kavu pamoja na Sharubati baridi kupooza koo zilokauka kama karatasi.
“Kumbe mwenzangu wewe ni mtulivu, mpole na mwenye moyo wa kujali.” Wada mie nikaanza kumsifu yule Mkaka aitwaye Marcus.
“Utulivu na upole ni Jadi yangu bibie. moyo wa kujali uniongezea maisha na matamanio ya kuliona Jua.” Marcus aliongea, tuliendelea kukata nyama kwa meno ya shoka.
“Bibi anakufurahia nyumbani, raha anajisikia kupata mwanaume kijana anayejali. Ni nadra ujue.” Niliendelea kulikoroga hata nisijue huo ujasiri wa kulikoroga naliupataga wapi? Maana hata maneno yaliyonitoka kinywani niliropokwa bila speed.
“Bibi!? Bibi gani!? Mie nipo moyo mpweke labda mwenzangu weye unaye wa kukuinjoisha.” Safari hii Marcus aliacha kula akakimbilia manywaji. Eeeh 🤭eeeh eeh! Nikajichekesha kishambenga.
"Nakutania tu Marcus, tuliza amani kula kaka yangu, kula upate afya, kula tunda, kula uongeze Namba na Callenda” Marcus akacheka pia kisha akatulia akiniangalia kwa sekunde kadhaa na kunena;
“Ninakuhitaji, nina haja nawe usiku wa leo, naomba unielewe.” Yalimtoka maneno.
“Mie!?” kusikia vile nikapaliwa chakula, haraka nikashushia maji kooni nisije aibika nionekane mlafi.
“Yes, weye niliyesimamisha Gari yangu miguuni kwako, umenipendeza sana. Kwa usiku mmoja wa leo nitakugeia shilingi laki mbili ili kesho asubuhi upate kifungua kinywa na mambo mengine yaendelee.
'Jamani nyie! Makubwa Mkaka huyu.' Moyoni nilijisemea.
“Laki mbili kwa kazi gani haswa? Nipewe shilingi laki mbili ya kunywea chai asubuhi? Ukarimu ulonitendea sasa watosha.” Moyoni niilitamani hiyo laki mbili ambayo sijaiona lakini njia ya kuipata sasa ilinishangaza.
“Kwani meneja wa Benki ni mgumu kutoa pesa?” alinihoji
“Wafanyia Bank!!?’ Niliuliza kwa mshangao, Macho pima kama jusi lilobanwa mlangoni.
“Mbona hukusema” Mshamba mie nilijishaua na kuropokwa tena.
“Mdogo mdogo ndio mwendo.
”Marcus alichombeza kisha akasema tena.
“Hapo vip tumeendana?! Umenielewa ombi la moyo wangu?”
“Mmh mbona mapema kutamka!” nilijing’ata ng’ata domo“Sawa basi nitakuachia shilingi laki tatu” Alitanguliza pesa baada ya maneno, mie moyoni kuguna sasa, mgeni huyu !!! iiihiii! Au ndio nimepata pa kupatikana. Kimya nikijirembua rembua macho. Mawazo yote juu ya pesa. Wala sikutafakari zaidi ya kutamani matamanio ya macho kuona, moyo kupata, ubongo kuhisi na kufikiri.
“Ok love nimeridhia kwa Offa uloahidi kunipa yamkini itanisaidia kuboresha maisha yangu na kunipa faraja katika biashara zangu” Mie Wada nikamshukuru.
“Ni bahati sana kwako Wada kukutana na mimi yaani hata biashara ya kuuza tunda leo ndo tamati yake, tukiisha zoeana na mapenzi kukorea nitakufungilia biashara kubwa ya kuuza duka lako mwenyewe. Small super Market.” Maneno yalimtoka mwanaume kijana. Mbona nilivutiwa na sauti yake, moyo uliweweseka kwa utamu wa ile sauti tu!.
“Jamani! Jamani! Mie wada mbona nina bahati” Niliongea kwa furaha chakula kingali mdomoni nakitafuna kwa pupa tena ovyo bila ustaarabu😂😂😂 Mzaramo mie.
(Itaendelea)
No comments:
Post a Comment