MAMA ALI
Sehemu ya pili
Hadithi ya MAMSAPUNGO.
Majogoloo yakawika ‘siku njema asubuhi.’ Mie Mamsapu na kiherehere changu nikajidamsha kivivu pale tandani baada ya usafi wa mwili nikafanya kuingia Mekoni chai kuandaa. Mwili wote machovu amani kupotea sababu purukushani la jana lilininyima usingizi. Mwanamke wa kitanga Mawazo yote juu ya gubu la Ma’ Ali hisia zikaniambia tayari keishadamka tandani mnuno domoni kamnunia Ba’ Yah’ ambaye leo hawaongei wala hawatazamani nyumba imegeuka mkuki moyoni.
Mie huyo nikajimwaga jikoni chai kuiandaeni, Taarabu domoni lanimwagika kama mwendawazimu, naliimba na kujimwambafai.
Zumbukuku wee,
zumbukuku wee.
Wanifanyia ukware,
ili nione uchungu,
Unanionea gere,
kwa iki kipaji changu,
Donge lako ni la bure,
Donge lako ni la bure,
Hutopata kitu kwangu.
Kwangu hotofua ndafu,
hujui zindiko langu,
Hapa ni maji marefu,
tokea tangu na tangu,
Hali yako ni dhaifu,
hali yako ni dhaifu,
Huviwezi Vita vyangu.
Zumbukukukeee,
zumbukukueee
Mama wa kifipa kajibebesha mtungi kichwani kafanya kwenda kuteka maji, kila mpita njia amwonaye njiani amsema na madole amnyoshea sababu ya kadhia ya jana. Ma’ Ali alikereka Keishazoea maisha ya Uswahili yenye changamoto balaa. Mwanamke kajipitisha vichochoro viwili vitatu hatimaye kisima hicho miguuni kwake lakini mbona hateki maji? Mmmh! Kayafumania mazito kutamka, kamkuta mwanaye Ali pembeni ya kisima kakumbata kademu mchele mchele jicho la huba na madenda kudendekeana. Ndo’ sababu Mamie Ali kapoteza amani kawasha kibiriti cha hasira, hasira za mbogo nakuambieni hasira hasarani.
“Wafanya nini asubuhi yote hii dakika za za kuwepo Shule, darasa, wazipoteza kwa huba la hicho Kinyago cha kimakonde? Mwana una nini weye? Makatazo yote niliyokuonya na kukataza hayazai matunda? Mwana kumbuka nalisema sitaki kukuona wasimama mbele ya kinyago hiki.” Ma Ali alibwata.
“Ma’ Samahani yawezekana njia umepotea? Huyu Beautiful Angel si kinyago, Jinale Happy ni Ua langu la thamani, Malaika mkalia moyo wamwitaje kinyago takataka Jahani?”Ali alimtetea Happy.
“Acha kunikera ewe ndege ulozaliwa jana. Niliyekunywesha uji kwa kijiko ni mie Mamio. Wawezaje kunifunda maneno, domo lenyewe lanuka maziwa utotoni. Nataka heshima, adabu na kusikilizwa. Fanya hima enda shule, elimu ni faida, elimu ni mwanga katikati ya kiza totoro.”
“Shule! Shule kitu gani Mamie? Nimeridhika kusoma, kuandika na kuhesabu sioni cha mno zaidi ya huo ujuzi Shuleni. Sina haja ya kuendelea na Shule.” Ali alimjibu Mamaye.
“Mwana embu nisikie’ elimu ni zaidi ya hayo machache ulojifunza shule, katika umri huu mdogo ulionao wasubiri kupanda madaraja lukuki. Mosi, hitimu shule ya Msingi. Pili, enda Sekondari, paa juu enda Sekondari ya upili, piga kitabu ujipenyeze Diploma na Degree. Tambua maarifa mengi bado yakungoja. Hawa watoto mchelemchele muda wakuharibia……. Ishike elimu ikushike.” Ma Ali alipunguza makasiriko akaigeuza shingoye akamtizama Happy binti mwenye nyonyo embe,uno la nyigu, sura mduara, mrefu kama ubua, shavu dodo lenye dimpozi na matabasamu.
“Binti nani kakuroga na kukutia wazimu wa huba ungali mchelemchele wa Darasa la sita? Aki! Ushajiharibu sio kwa mawazo hayo juu ya mwanangu Ali, umependa ukapitiliza.” Ma’ Yah kaendelea kunena:
“Nisikilize, ujio wako Duniani ni faida kubwa kwa Wazazi walokuleta pia kwa jamii inayokuzunguka. Ukishika mbili moja litakuchoka, waikataa nguvu ya elimu wahitaji vidume vikupapase matiti na makalio…. Kama ni mipapaso utapapaswa hadi makalio yapasuke puuuu mfano wa puto la Kihindi.”Maneno ya Ma’ Ali yalimchoma Happy aliinama chini kwa aibu.
“Happy roho wangu wachana na Mama, Mama yangu jau nifuate tusepe.” Ali alikereka akaukamata mkono wa Happy na kumtoa pale chochoroni, alihisi Mama ambughudhi na kumchosha. Wakatokomea mitini. Ma’ Ali kasimama pale kisimani hasira shingoni atamani awakimbize awakamate awameze kama Chatu ammezaye Nguruwe.
“Naliikimbia na kuikataa elimu ya Dunia, jamani mtoto wa Nyoka ni nyoka nifanye nini kuliepusha jahazi hili lisizame? Hofu yangu kuachwa upwekeni kwa toweko la Ali.” Ma Ali alijiuliza mtimani asipate jibu tosha, akafanya pupa kuteka maji kisimani wazo la haraka likamwambia ‘Mtembelee Shogayo Mamsapu kuna mazuri atakudodosa.’
##############
Nalimkaribisha vizuri Mwanamke mwenzangu naliandaa kahawa safi mezani, vitafuno vya kila namna mezani tukajumuika pamoja, Mie Mamsapu, Pompo babu yenu na mwenyewe Mama Ali. Tukayakaribisha mazuri tukayajenga na kuyajadili tusitake kukumbushana visa na vituko vya usiku wa jana maana wahenga walisema yaache yalolala yalale, ukiyaamsha yatakushinda babu, ushindwe kuyamaliza.
“Yaani sijui nianzie wapi kukuelezeni jirani wa mie, mume amenishinda na mtoto anishinde kweli? Walimu shuleni nimewaelezeni shida za mwanangu ameadhibiwa hadi huruma! Wanasaikolojia wamemshauri kwa vitabu na majalida lakini wapi! Mwana hayataki mema ayataka yale moyo wamtuma kufuata” Ma’Ali aliongea na sie, Huzuni yake si haba.
“Tatizo uhuru Mwanamke. Wamwachia uhuru mwingi mwanao wakati huo huo washindwa kumkanya kwa maonyo na mafundo ayawache mabaya aloyazoea.” Mie mamsapu naliongea.“Ali mwanao Keisha jiunga na makundi ya vijana wenye utovu wa nidhamu watumizi wa dawa za kulevya, wezi, laghai, waporaji, wanyanganyi na wenye kutumia zana zenye ncha kali kuwaumiza waja waso hatia. Ndo’ kukuambia uhuru mwingi ulomwachia wamrubuni na kumharibu mwanao.” Mie Mamsapu naliongea tena.
“Nieleze Babaye Yah’ amsaidiaje Ali?” Popo Babu yenu kauliza.
“Amsaidie nini cha mno Umbwa yule? Mwana sio wake amwona takataka zisotamanika machoni.” Mama Yah’ alimjibu Babu yenu Pompo, kidogo makasiriko usoni.
“Lo! Akosea Mzee mwenzangu sababu waswahili wasema mwana wa mwenzio ni mwanao pia. Watoto ni Taifa la kesho wahitaji kulindwa kwa nguvu ya elimu ili baadaye wayatafune matunda ya Edeni.” Pompo kahubiri.
“Yaani Babu yangu Pompo bora weye wasema mie nimechoka kupigizana kelele na yule mwana mwendawazimu.” Ma Ali kaongea,
“Ataka nini mbali na elimu ya Dunia?” Pompo Babu yenu kauliza.
“Atake nini zaidi ya wizi, uporaji,Unyang’anyi na kumthamini Demu wake Happy.” Ma Ali alijibu kwa huzuni.“Mie nalijua ataka kudili na kazi ya maana impatie pato nami nifanye juu chini kuisaka kwa ajili yake.” Pompo katoa wazo.
“Unenayo matamu kuyasikia Babu yangu Pompo, lakini Ali mwana yule hataki kufanya kazi yoyote ile imwingizie pato, mawazo yake yote ni pombe kali, sigareti na mabangi.” Ma’ Yah’ kaongea.
“Mwana kaharibika udogoni.” Mie Mamsapu naliongea tama shavuni.
“Ombi langu kwenu Babu yangu Pompo na Mamie Mamsapu naomba nisaidieni....... nisaidieni nisije mpoteza nimpendaye, tamanio langu kumwona Ali afanikiwa maishani sababu mafanikio yake ni uzima wangu, aribiko lake ni pigo kwangu Mamaye, tafadhali nawategemea.” Ma’Ali alilengwa lengwa chozi.
‘Twatamani kukusaidia lakini Mamie wacha Dunia ishike bakora kumchapa mwanao sababu baada ya kisa mkasa, ipo siku Ali atabadili tabia.” Pompo katoa wazo.
“Jamani!! Naumia kusikia hivyo roho wangu Pompo, sie wanawake tumejifungasha uchungu viunoni. Dunia kumwadhibu Ali ni uchungu kwa Mamie.” Mie Mamsapu naliongea kwa uchungu.
“Muda haugandi moyo wangu Mamsapu tufanye nini iwapo juhudi na hatua zote kuchukuliwa ajabu Ali asibadilike! Maonyo na marekebisho yote kutendeka Mwana kawa mgumu mfano wa jiwe. Wacha apate fundo baadae atarejea kuomba ushauri.” Babu yenu Pompo aliongea sie Wanawake twalimkalia kimya Mioyoni tukiumia.
[Basi mwaya mie Mamsapu nakome hapa Leo, kesho majaliwa tukutane barazani, Kuna kombe la kahawa na kapu la kashata nimekuandalieni]
No comments:
Post a Comment