HADITHI YA MAMSAPUNGO
MAMA ALI(JIRANI WA MIE)
SEHEMU YA KWANZA
Basi mie Mamsapu Mama wa kitanga Lushoto ndio nyumbani kule mahabati yalikozaliwa, Mwanamke nalikua nimelala usingizi wa fofofo mfano wa Pono yule samaki mwenye usingizi mzito baharini, Nalikua usingizini pamoja na Pompo babu yenu, roho wangu, mume wangu mwenyewe. Mwanamke nikadamka sababu nalishituliwa na kelele za hao wasotutakia amani usingizini kutwa kuchwa wao ni magomvi na matukano yasoisha matanga. ‘Saa sita’ Naliitazama saa Ukutani mida ya Bundi na Popo kulizunguka Jiji la Mzizima.Masauti ya mabezo, kebehi na matukano ya nguoni yalinikera masikioni mwa mie, masauti hayo yalimgutusha Babu yenu Pompo akadamka usingizini wenge na ruweruwe usoni utadhani kaona Ghost-Mzimu. Sie tukasikia;
“Nakwambieni Ba’ Yah’ mie leo nakudunda Mwanaharamu uliyejivua roho ya utu na ubinadamu.” Mama Ali alibwata. Mama Ali ni jirani wa mie kajaliwa makinda wawili Ali mwenyewe na Yasini ambaye pia huitwa “Yah.”
“U’ndunde kama nani? Umbwa tegemezi weye, embu niwache kabla sijakutengua uno lako.” Baba Yah’ aliongea kwa sauti ya upole iso mkoromo.
“Umtengue nani Kafiri mdogo weye, dume zima ovyo yaani uzima wote ulonao hujifunzi kujitegemea na kuisaidia familia yako? Wanitegemea kula nikulishe, kuvaa nikuvishe Kodi ya Pango niitoe mie binti wa kifipa… Bili ya maji na Umeme usiitoe... Hapa mjini babuwe! Maisha mapambano, bora nikuchoke.” Ngumi nzito zililipasua shavule Baba Yah’
“Hembu niwache Bibie.” Baba Yah’ alibwata kwa maumivu makali.
“Nikuwache uende wapi? Sikuwachi hadi niridhie kukumalizeni.’Puu puu paaa. Ngumi nzito zilimvaa Baba Yah’ masikini mlevi yule alishindwa kujitetea.
“Nini cha mno Usiku huu mwanamke?” Roho wangu Pompo aliyeutema usingizi alinihoji.“Mazito mwenzangu, nyumba ya jirani haweshi vituko. Mama Ali kaliamsha dude Shwetaini amponda mumewe kama goma la kikurya."
“Mwanamama hana adabu huyu, matukano mazito, ngumi zasikika mtu wa mbali kusikia.” Pompo aliniambia.
“Maisha roho wangu, maisha yamewashinda, shida zao hazina heshima, shida zawafanya jirani zetu wapondane mfano wa kisamvu ndani ya Kinu.”
“Sie twapigana na Jua tulipate tonge laUgali wao wapigana na kiza kusaka nini?” Teh teh teh teh Pompo roho wa mie alicheka kwa kebehi mida ile sie tumeketi tandani twasikiliza kadhia na makasiriko ya wenzetu wenye hasira za mkizi.
“Ndo’ twende tuwapange na kuwapangua yasijezuka yakuzuka sie tukasikia jirani wagawana majengo ya Serikali; Mama Ali Jela na Baba Yasini kulazwa Mirembe wodi za vichaa.” Nalimshauri Pompo babu yenu.
“Si uende weye mwanamke ukautulize mpira mapepe.” Pompo alinipa shuhuli.
“Babu we! Kun’twisha zigo zito kama Mlima Kilimanjaro hunionei huruma?” Nalimtazama Pompo kwa jicho la makasiriko sikupendezwa na ushauri wake.“Wanasaikolojia wasema wanawake mnatabia ya kuelewana vizuri zaidi ya sie kuwaelewa.Tafadhali enenda uyatulize maji Ziwani.”Pompo alinituliza kisirani.
“Wewe nae, hayo ni mawazo yenu wanaume, hamtujui vizuri sie wenye roho za makasiriko, wivu, chuki, tamaa na husda.”Naliongea mwanamke nikateremka pale tandani tenge langu kiunoni, kanga yangu begani nieleke kwa shoga yangu na jirani wa mie Mamie Ali.
“Wanawake mmejaliwa roho za kusaidiana.” Babu yenu Pompo aliongea tena. Sikujishuhulisha kwa maneno yake nikafanya kujiteremsha kutoka juu ya Floor apartment Horofa ya tatu nikamwita Jose mlinzi wa lango kuu anitoe na kunisindikiza nyumbani kwa Ma’ Ali Mama mgomvi kama Beast mnyama pori asichoke kumponda mumewe mlevi aloshindikana.Kidogo kabla hatujafika kwao wenyewe mie Mamsapu nikayanasa maongezi ya Mjomba Bahati na Mkewe Mama Happy dirishani walisikika wakichati;
“Ba’ Happy naomba udamke uelekee kwa Ma’ Ali kuuzima moto wenye makali kuwili, mwanaume mwenzio apondwa vibaya wenye wajilaza hapa asijeuawa bure.” Ma’ Happy aliongea.
“We! Usinichoshe, aeleke nani? Fujo za ovyo kama zile hazinipi faida.” Mjomba bahati alimjibu Ma’ Happy.
“We naye wakitoana roho je? We huogopi! madhambi hayo mdomoni” Ma' Happy aliongea kwa huzuni.
'Teh teh teh teh.' Mjomba Bahati alicheka, akanena; “Bora wauane roho yangu itulie. Jinsi nimchukiavyo Ma’ Ali sioni mfano Duniani.”
“Chuki zako ni za bure Ba’ Happy kila siku nakwambieni wape Notis wahame ajabu ya kuzubaa kama Kunguru mgonjwa.” Twalimsikia Ma’ Happy akinena.
“Hisia zilinambia Mwanamke yule kaniroga maana Wafipa si mchezo! Wanazo dawa kali na hatari. Kila nikitaka kumtimua yule mwanamke na mumewe najikuta mnyonge mnyong’onyevu nasuuzika na kulainika.” Mjomba Bahati alijitetea
“Usinambie ndo’ ushafia mazima kwake mie nionekane takataka.” Ma happy alitania.
“Kamata adabu, nani akafie mbele ya kinyago cha kifipa? Namchukia mwanamke yule.” Mjomba alimjibu Ma’ Happy. Mie na Jose tulichoka kusikiliza ule Umbea tukaondoka pale dirishani, dirisha la pango aketilo mjomba Bahati na mkewe Ma’ Happy.
“Hodi wenyewe.”Naligonga Mlango wa kijumba cha Ba’ Yah na Mama Ali bahada ya Kuwai yale majanga
“Pita Mamsapu pita ndani Bi. Mkubwa ukuje kunisaidia tuliponde hili dume suruali, yaani kero lanikera kama uchafu Jahani.” Ma Ali alibwata kwa dharau na makasiriko. Mie nikaufungua mlango wa kile kijumba chenye kuta zenye nyufa lukuki ukilitupa jicho lako juu ya paa mwenzangu! Utashuudia mbavu za Umbwa zatamani kudondoka si kwa kuliwa na mchwa kule! Nikajitoma ndani pamoja na Mlinzi Jose akanifuata nyuma mfano wa Umbwa mtumwa amfuataye bwanaake.Uwii! Yangu mie macho niyazibe kwa pazia, Niloyaona si madogo kuhadithia, nikafanya hima kumtoa Inje Jose Mlinzi wangu asiyaone nisopenda kuhadithia. Aibu Jamani Ma’ Ali alikuwa utupuni utupu wa mnyama wa porini. Maziwa kule! Makalio kule, Paja kule! Gongo wazi yaani mtupu kama mtoto alozaliwa. Kamkalia Ba’ Yah’ kiunoni juu ya tanda kamkwida shatile, amtukana na kumponda mumewe.
Si kwa manguvu yale mwanamke kamponda mumewe damu zamtoka puani na masikioni, mfano wa bomba limwagalo maji. Bichwa la Ba’ Yah’ nundu zimesheheni aona vinyota nyota na vimulimuli, kalainika kawa denda la mlenda.
“kulikoni mwanamke wamponda mumeo pasina huruma.” Nalilizoa zoa shuka lililobwagazwa chini sakafuni nikamvika Ma’ Ali nipate kumsitiri ule utupu wa kuzaliwa kwa aibu ile hakika lnzi wanoko na kadamnasi ndebendebe ingelifaudu umbea kuusambaza.
“Nina haki ya kuliponda hili goma zembe lililochoka na kuzeeka. Ma Ali alinena usoni kaiva kawa mwekundu wa mkorogo, kawa mbaya kama embe lililooza , ngozi yake ishakuwa ngumu mfano wa tofaa lisonunulika Sokoni, Mwenzangu dunia ina mambo.
“Kaniudhi huyu we acha tu! Mie nalikuwa Mbezi kunako shuhuli (Sharehe) yeye kenda Buguruni Bar kunywa na kulewa Madabo kiki na makeivant yake. Shuhuli kwisha kumalizika nikampigieni simu ‘Babu we fanya kunirushia Wekundu wa Msimbazi, Rusha Tigo pesa nijisevie nauri, ukame umenipurunya na kunipukutisha.” Ma’ Ali alipumua kwa hasira akaendelea kunena.
“Mwanaume pasina haya kagoma kunitumia Pesa, kanizimiaSimu nisimpate tena, kama sio huruma za Wapambe mie bila kupenda ningelilala shuhulini. Wacha nimponde na kumfunda ajue kumlea mkewe kama Yai. Hakunioa bure ajue hilo, ajue mwanamke ni kama mtoto ataka matunzo.’ Puu poo Ma’ Ali alimtwisha ngumi nzito Ba’ Yasini.
“Bibie utammaliza mumeo kwa kisa na mkasa usoeleweka.” Nalijaribu kumwondoa Ma’Ali juu ya kifua cha mumewe. Kamkalia mumewe kama jiwe zito juu ya Mlima, amtesa kwa mapigiti na matukano ya nguoni.
“Mwekundu wa msimbazi, Shilingi elf kumi!? Wadhani Pesa hiyo yaokotwa, eh? Au yatolewa bure msaada kanisani? Kama yachimbwa kisimani ningelikuchimbia lakini thubutu kamwe sichezei pesa za mie kukupa Malaya Umbwa mwenye kijicho tamaa.” Ba’ Yah’ alimjibu Ma’ Ali. Nilivyomtizama Ba’ Yah nalimuonea huruma, hayo Ma K-vant, Madabo kiki, Gongo na Konyagi Spirt yatamuua jamani, yatamuua angali bado ni kijana mwenye familia.
“Kunizalisha unizalishe, kuhudumia familia waona mzigo, wacha nikutwange utwangike, ujifunde kumlea mkeo kwa nguvu ya upendo wa hali ya juu. Ma’ Ali alibwabwaja.
“Shoga manguvu yote hayo wayatoa wapi? Mwanamke kumponda babu kama gunia la mahindi! Sikia bibi ndoa yataka heshima, ketini chini mjadiliane myamalize kiutu uzima sababu kupigana na kutukanana kamwe hakutakusaidieni.” Nalitoa ushauri.
“Dawa ya huyu ishachemka nakuinywa ainywe kwa lazima.” Shoga’ngu Ma’Ali hakutulia , Kwa hasira alimvaa Ba’Yah’ akamponda kwa mangumi na mateke. Mie msuruhishi nalikuwa njia panda. Nikamwita Jose mlinzi wangu anisaidie kulivuruga lile janaba. Nyie! Yasijezuka yakuzuka wenyewe watoane majino, majicho na akili ubongoni. Wenyewe watoane viungo mwilini, waharibu na kuvipangua pangua vyombo ndani ya nyumba, Hapana jamani hasira uzaa hasara. Jose mlinzi wa mie aliingia kulisuruhisha lile varangati, zogo mzogoe, baada ya purukushani za hapa na pale tulifanikiwa kumnyuka Ma’ Ali akatuliza maji mtungini.
(Tuendelee kesho Shogangu)
No comments:
Post a Comment