Monday, September 23, 2024

DONDA LA WIVU.. sehemu ya tatu



KASHIKWA SHARUBU.

            Mtume! Mungu wangu we! Mzee jamali alishituka mara baada ya kufika ndani ya shamba lake  alilopanda karoti, nyanya  na kabeji. Shamba lilikua limeharibiwa vibaya sana, aliwakuta Ng’ombe wakiwa wameingia ndani ya shamba lake na kuanza kuharibu haribu. Ng’ombe wale walikua wakishambulia mazao yake kama vile nzige ashambuliavyo mara baada ya kuingia kwenye mimea.


Looh! Mama we! Mzee Jamali alichanganyikiwa, asitake kuamini kama tukio lile analoliona machoni kwake ni jambo la kweli ama la! Ni utani, asitake kuamini kuwa lile tukio alishuudialo mbele yake ni sinema au ndoto za mchana, ndoto za kufikirika.


            “Yallah! Hasara gani tena hii mbele ya macho yangu?” Muda ule ule mzee Jamali alianza kuwafukuza wale  Ng’ombe pamoja na kondoo waliokuwa bize wakiharibu mazao  shambani kwake. Hata hivyo kitendo kile cha kuwafukuza wale wanyama hakikusaidia kitu, kwani tayari wale wanyama walikwisha kuharibu haribu shamba lake. Tayari walikwisha kumtia hasara kubwa isiyo weza kuhesabika.


             “Joeli, Joeli, Joeli.” aliita mzee Jamali  aliita kwa sauti kuu.


             “Joeli we!”  Aliita tena lakini asiitikiwe.


 “Amekwenda wapi huyu mtoto mpumbavu Joeli, amewaacha wanyama wa Mzee Shemagendo wakiniharibia shamba langu, hapana, ni lazima niende kwa mzee Shemagendo nikamshitaki huyu kijana, amenitia hasara kubwa kiasi.


  Aliongea pekee  mzee Jamali, amekasirishwa na kitendo cha Joeli, kivulana kilichopewa kazi ya kuchunga na kuwongoza wanyama. Ubaya wa huyu Joeli angali bado ni mtoto mtundu na mtukutu. Wakati wote mtoto huyu hupenda kucheza mpira akiwa pamoja na watoto wenziwe, uwasahau wanyama. Basi utamkuta anapanda juu ya


anapanda juu ya miti na vilima akifukuzana na watoto wenziwe. Joeli bado ni mtoto tena mtoto wa kufurahia michezo.


            “Looh! Masikini jamani! Nilikwisha panga kuvuna mazao yangu  niwauzie wafanya biashara wanaosambaza mboga mboga ndani ya jiji la Arusha na Dar es saalam. Mpuuzi mtoto Joeli amewaacha wanyama wakiharibu haribu shamba langu……. Oooh! Masikini uzembe gani huu?”


  Hasira zilimpanda Mzee Jamali, alitamani angelikua na mbawa za ndege apate kuruka afike pale alipo Joeli. lakini atafanya nini mzee? Amevunjwa moyo,  shamba lake halitamaniki tena, limeachwa nyang’a nya’ga, Ukitegemea wiki ya kesho alitarajia kuvuna na kuwauzia wafanya biashara mazao yake.


“Tokeni!  Tokeni! Tokeni!” Mzee Jamali alijitahidi kuwafukuza wale Ng’ombe, Mbuzi na Kondoo ambao walikua wangali bize wakiharibu haribu shamba lake, shamba lake halikutamanika machoni, lilikua limeharibiwa haribiwa vibaya sana,  ndugu yangu iwapo kama ungelipata nafasi ya kulitazama haki! Ungelimuonea huruma Mzee Jamali. Mzee yule akawa mnyonge wa ghafla, masikitiko makuu moyoni,  akiyatizama tizama mazao yake yalivyoharibiwa, mategemeo yake yalikua ni kukikamata kiasi cha shilingi laki sita mkononi. Pesa ambazo tayari zilikwisha kupotelea ndani ya midomo  na matumbo ya wale wanyama waharibifu.


“Joeli, Joeli, Joeli we!” Mzee Jamali alimwita tena yule mtoto aitwaye Joeli, mtoto mwenye kadirio la umri wa miaka kumi na mitatu, kapewa dhamana ya kuwatunza wale wanyama lakini kwa utoto wake mwingi ndio hivyo sasa kaenda kucheza mpira na kupanda juu ya miti akiwaacha wanyama wale wakifanya uharibifu ndani ya shamba la Mzee Jamali.


                       “Nitamtafuta huko huko kwa mzee  Shemagendo, nipate kumshitaki kwa makosa aliyonifanyia, Mzee Jamali alishika njia  inayokwenda nyumbani kwa Mzee Shemagendo apate kumshitaki mwajiri wake. Alikwisha itambua ile mifugo, aliitambua kuwa ni ya Mzee Shemagendo, anaijua vizuri,  imewekwa alama nyuma ya migongo yao na alama zile sio ngeni machoni kwake. Basi safari yake ikaanza, akipanda Vilima na kushuka Vilima, amejaa hasira hasara anaongea pekee njia yote ni kama vile kageuka na kuwa mwendawazimu fulani aliyepoteza mwelekeo.


             Ndani ya dakika harobaini na tano Mzee Jamali alikwisha kufika nyumbani kwa mzee Shemagendo, alikaribishwa vizuri kama kawaida ya mgeni yeyote yule aendaye ugenini. Uzuri wa siku ile alimkuta Mzee Shemagendo akiwa ametulia tuli, ametulia kama maji  mtungini, anavuta makambo kambo, kiko mdomoni, moshi unafuka na kutoka kwa raha zake zote. Pembeni ya eneo aliloketi  amewekewa pombe ya asili inayotengenezwa kwa kutumia Miwa. Mzee yule alifurahia kuvuta mikenge miwili mitatu pamoja na moshi utokao puani na mdomoni kwake kwa kutumia Kiko yake.


Walisalimiana na baada ya salamu mzee Jamali aliyatoa maumivu yake yaliyotulia moyoni, akayasambaza masikioni kwa Mzee mwenzie aliyejiweka bize akijiburudisha kwa yale matamanio ya pua na mdomo.


               “Ndio hivyo mzee mwenzangu, N’gombe wako wamekula na kuharibu haribu shamba langu, wamenitia hasara kubwa sana hasara ambayo sikuitarajia, sikuitarajia kama ningeliiona, machoni, amini, kama hauamini maneno yangu kuwa ni maneno thabiti wacha tuongozane, tufike shambani kwangu ili ukajionee wewe  mwenyewe uharibifu uliofanywa na mifugo yako.” Mzee Jamali aliihitimisha akiwa na hasira shingoni.


                    “Mmmh! Maneno uyanenayo yana ukweli, ama! Waileta kesi isiyo nihusu mie na mifugo yangu?” Mzee Shemagendo alimuuliza mzee Jamali.


            “Ndio maana nimekwambi itakua vizuri iwapo tutakwenda pamoja ukashuhudie uharibifu uliofanywa na mifugo yako, hapo ndipo utakapo niambia dhariri kama  mifugo tutakayoikuta shambani kwangu ni ya kwako au la!”


             “Nitayaaminije maneno yako mzee Jamali? Ama, wewe utaniaminije iwapo nitakuchukua na kukupeleka ndani ya Zizi la mifugo yangu? Utaiona ilivyo tulia tuli, haijapata kutoka nje siku nzima ya leo.”



              “Tangu asubuhi ya leo hadi mchana huu mifugo yangu imetulia tuli haijapata kutoka, Joel unaye niambia amefanya uzembe wa kuiwacha mifugo yangu ndani ya shamba lako mbona yupo ndani, ametulia tuli siku nzima ya leo, hajapata kwenda malishoni zaidi ya kupumzisha mwili na akili zake.”


             “Umesema?” Mzee jamali aliongea kwa mshituko.


“Umesema ati Joeli hajaenda malishoni? Mzee mwenzangu muda huu ninaoongea na wewe twaweza kwenda chini ya kilima cha Kidundai kutizama mifugo ilivyoharibu haribu Shamba langu nawe utaniambia ukweli wa shuhuda za macho yako, utaniambia kama Joeli anahusika au hausiki katika  uzembe huo.” Mzee Jamali hakuitaji kutoa maelezo mengi juu ya uharibifu uliofanywa na na Joeli mtumishi wa Mzee Shemagendo.


“Hupaswi kuandikia mate wino ungalipo Mzee wangu tizama kundi langu lote la Ng’ombe Mbuzi na Kondoo hawajapata kutoka ndani ya banda, sababu Joeli mtunzaji wa mifugo yangu ni mgonjwa, tangu usiku wa jana amekamatwa na Maralia.” Shemagendo aliongea. Wakati huo huo Jamali tayari wamekwisha kufika ndani ya  Zizi la Mzee Shemagendo kundi lake limetulia tuli kama maji ya mtungini. Kundi limeshiba limetuna tuna na kuwa na afya bora, hali ambayo inazidi kumstaajabisha Mzee Jamali, ni kama vile Mzee Jamali alikuwa ndotoni, ndoto ya mchana, ndoto isiyo mletea picha, picha halisi ya kile anachokiona. Nusu saa iliyopita mifugo ile ile ambayo anaiona   ndani ya banda la Mzee Shemagendo ndio ile ile mifugo iliyolisafisha shamba lake la nyanya, karoti na kabeji. Mifugo hiyo imelisafisha shamba na kulifanya liwe jeupe kama saruji.


                     “Je, ni halali kuileta kesi ya visingizio nyumbani kwangu? Joeli unayedai kuwa ameiwacha mifugo yangu shambani kwako ndie huyu huyu unayemwona amelala ndani ya kijumba nyasi changu, yu mgonjwa wa Maralia iliyomkamata usiku wa kuamkia jana.” Shemagendo aliongea pasina hofu wala wasi wasi, wakati huo tayari amekwisha kumvuta Mzee  Jamali ndani ya kijumba nyasi alicholala mtumishi wake Joeli.


                    “Wallah! Hii ni miujiza sasa, ninashindwa kuelewa vizuri, mbona mifugo niliyoiona ikilitafuna shamba langu, ndio hii  mbele ya macho yangu, ajabu! Imetulia tuli kama vile sio hii niliyoiacha muda si mrefu ndani ya shamba langu.” Mzee Jamali aliongea kwa kuchanganyikiwa.


                   “kama una ushahidi wa kutosha, ni vema ungeliileta hiyo kesi nyumbani kwangu, lakini sio kufanya maamuzi yasiyo na vithibitisho. Utaushangaza sana ulimwengu Mzee mwenzangu pale unaposhindwa kuwa na vithibitisho kamili. Kwanini usiikamate mifugo iliyotafuna mazao yako? Kwanini usimkamate Joeli ambaye wewe binafsi unadai kuwa anahusika katika uharibifu wa mazao yako?”


                      Mzee Shemagendo  alinena, amemwacha mzee Jamali hana neno la kunena, ni mwingi wa wa hisia anahisi labda amechezewa akili zake sababu jambo kama hili linaupumbaza  moyo na akili zake, asitake kuamini au kuelewa kama huu mchezo ni wa sihiri au ni madanganyo, yeye anazidi kujiuliza kichwani kwake, kwanini iwe hivyo?  Basi  Mzee Jamali akarejea Shambani kwake apate kutazama tazama hali halisi aliyoachana nayo.


                                     ########################


Allah! Kumbe Mzee Jamali alizidiwa kete, kazidiwa nguvu, kazidiwa ujanja, tena kazidiwa na mtoto mdogo aitwaye Joeli, kapigwa chenga. Kapigwa changa la machokalamba jokerkapitishwa njia za panya. Joeli kaiswaga swaga ile mifugo  aliyoachiwa aitunze ile ishibe, inywe  itosheke. Wakati Joeli  alikwisha kumuona Mzee Jamali , alimwona  akija, akija Shambani kwake akajificha pahali pembezoni mwa miti mingi iliyopo pale shambani kwa Mzee Jamali. Alijua ile ishakua kesi, alijua ile ishakua balaa, maji shingoni na iwapo ile kesi ingelimfikia Mzee Shemagendo basi Joeli ategemee kibarua chake kuota Unyasi. Ategemee  mshahara wake wote, ule mshahara anao tunziwa na Mzee Shemagendo  ungelitumika kulipia uzembe alioufanya.


            Joeli     hakukubali, Presha ilimpanda, akamwona Mzee Jamali akipanda juu ya kilima cha Kidundai, akielekea nyumbani kwa Mzee Shemagendo moyo ulizidi kumdunda ‘ndu ndu ndu ndu!’  Pasina kuchelewa alihakikisha kuwa  anawaondoa 


wale wanyama katika eneo lile akawaswaga faster faster akaelekea nyumbani kwa Mzee Shemagendo kwa kupitia njia nyingine, njia za panya.


Mara baada ya Joeli kuwafikisha nyumbani wale wanyama  akawaingiza Zizini, akawalazimisha kulala nao wakamtii kwa lazima,kama wanavyomtii siku zote. Akamwendea Mzee wake Mzee Shemagendo, akamkuta akiwa bize anavuta vuta makambo, akiwa bize anavuta vuta mikenge kwenye mtungi wake wenye pombe ya asili. Joeli akamsimulia Mzee Shemagendo, akamsimulia juu ya kesi inayomkabili. Ujanja ujanja  pekee ulitosha kwa Mzee Shemagendo kulinusuru lile jahazi ambalo muda si mrefu lingelizama. Tayari alikwisha kumuelewa mtumishi wake Joeli, tayari alikwisha elewa hasara ambayo mzee Shemagendo angeli gharamia.


        Shilingi laki sita sio pesa ndogo ni pesa mingi sana, kuzitafuta hizo pesa na kuziweka kibindoni yataka moyo, ni kazi nzito na ngumu sana. Yataka moyo, yataka moyo wa kuzitafuta, la sivyo mambo yangelikua mshike mshike  mambo yangelikua mabaya iwapo ile kesi ingelifika Barazani kwa wazee.


              “Jifanye kuwa unaumwa, jifanye hujui chochote kinachoendelea, mimi nitafanya juu chini  kuhakikisha kuwa mambo yanakua sawa, wala usitie shaka, enenda ukalale umefanya vema kuwakimbiza hawa wendawazimu ndani ya mabanda yao, hawana uelewa, hawatambui chochote kile wanachoambiwa, daima hawa ukiwakokota wankokoteka, ukiwafukuza wanafukuzika ni wajinga wenda wazimu.” Alionga Mzee Shemagendo, akiikosoa na kuizodoa ile mifugo yake.


 

Itaendelea









No comments:

Post a Comment

I promise you

   I PROMISE YOU. (NINAKUAHIDI.) SURA  YA KWANZA. UBAYA WA POMBE. “Umenizingua job, umenizingua kwa muda mrefu sana mpenzi wangu…….kwanini l...