JUTO
Tulipoishia
Kumbe! Kumbe binti hakujua kuwa wenzie wapo kazini, pale wanamchota akili, kilichofunikwa binti anaona kimefunuliwa na kilicho funuliwa anaona bora kifunikwe ni kama Mazingaombwe, yeye mwenyewe haelewi nia na malengo ya hawa Mashosti, Mabesti na Mashoga zake.
Hakushtuka wala hakushtukia kuwa hao wenziwe anaowaona kuwa ni wafariji wake kimawazo wamemtamani Mumewe Denis, maana Denis mwenyewe hatulii nyumbani ni kiguu na njia, yupo bize kusaka pesa, kutwa kuchwa yupo ndani ya Coster anasaka hella ya Bosi ili apate kidogo dogo ambacho ni haki kwake. Au labda hawa Mashosti walimuonaDenisi hapo Malapa? Labda, maana Denis ni Dereva na Dereva lazima akutane na makumi ya watu kila siku iitwayo leo. Jamani hisi na hisia hazitoshi, tusilolijua litatusumbua, tusilolijua lipo kizani.
Endelea hapa
“Hembu tuwekewazi Shoga yetu, Mumeo kakuachia kiasi gani cha Pesa ili zikuwezeshe kupata mboga mboga na viungo vingine?” Leo Elizabeth alimuuliza Lily, wamekuwa wakimuuliza maswali kibao yanayomhusu yeye na Mumewe hata asijue kuwa hao Shagaze ni wajanja tena ni wajanja wa Jiji.
“Yeye huacha kila siku Elfu Ishirini juu ya Meza, hizo zatosha kununulia vitu vidogo vidogo ilihali nyumbani kwangu hapakosekani mboga, viungo, mchele, unga, mafuta nakadhalika.” Lily aliwajibu wale rafikize.
“Mmmh! Shosti huoni kwamba Mumeo hakutendei haki? Yaani uachiwe Shilingi elfu Ishirini? Jamani Dereva huyu anakutesa sie wenzio waume zetu huacha Mezani Shilingi laki moja na nusu kwa ajili ya matumizi ya mboga mboga na pengine zinapobaki ni kwa matumizi yetu binafsi, si unajua tena kila mtu ana Mume wake, kila mtu Mumewe anamjali Mkewe.” Anjelina alitia neno. Lily aliachia domo wazi akishangaa.
“Jamani kweli au utani? Siamini, pesa yote hiyo ya kazi gani kwangu wakati kila kitu kipo nyumbani hata hiyo Elfu ishirini ni kama zawadi anipayo Mume wangu maana kuna sikuhiyo pesa haitumiki yote sababu nina kila kitu ndani.” Lily alijitetea. “Shoga sio hivyo, tusikilize sisi Mumeo hakupendi, kama angelikuwa anakupenda angelikudekeza kama Mtoto mchanga. Ajabu anakutendea kama sio Mtoto mchanga, alipaswa kukuachia Pesa nyingi kila siku kuanziaShilingi laki moja na kuendelea.”Mashosti walitia neno, neno ambalo liliuchanganya sana Mtima wake Lily akijiuliza Mumewe ambaye mwisho wa mwezi hupokea Shilingi laki tatu, ataweza kweli kumpatia shilingi laki moja kila siku? Mmmh! Vigumu, haiwezekani, hiyo Elfu ishirini pekee Mumewe hupewa na Bosi ili imtoshe kwa mahitaji ya nyumbani. Je, hiyo laki moja au laki mbili Mumewe atapewa na nani?
“Tena Shogangu keshokutwa unikopeshe Shilingi Elfu hamsini nina shida nayo, nina shida kweli kweli nitakapopewa na Mfalme wa moyo wangu sitachelewesha nitakulipa, si unajua tena ukame ni kitu cha lazima? Acha basi chako kula na wenzako” Lisa ambaye ndiye aliyemsuta Lily kwa kumwambia Mumewe hamtendei haki anapompatia pesa ndogo ya mahitaji ya nyumbani ajabu ndiye aliyekuwa akiazima pesa akidai atairudisha pale Mumewe akimgea.
“Kweli Shoga zangu au ni utani haya maneno yawatokayo vinywani?” Lily alitia neno.
“Uongo ushindwe, uongo hauna nafasi kwetu, sababu msema kweli ni Mpenzi wa Mungu, Shosti umewekwa hapa kama Sanamu, huelewi wala hujielewi, tunakushangaa sana yaani Mwaka mmoja wa kuishi na Mumeo hajawahi kukutoa Out ukapate Dinner au kukupeleka Sinema mkacheki Muvi, Mwaya ujisikie kuwa hupo kwenye ndoa ujisikie kupedwa, jamani lo! Masikini.” Mashosti waliongea zaidi na zaidi.
“Kinachotuumiza sie ni kitendo cha Mumeo kushindwa kukujali, anajifanya anajali sana kazi kuliko kumjali mkewe, adamke alfajiri mapema arejee usiku wa manane, hajui unavyoendelea, hajui unavyommiss, hajui unavyotamani awe karibu karibu nawe. Hivi je, ukipatwa na tatizo lolote lile linalohitaji Emergence utafanyaje Shosti? Masikini tunakuonea huruma.”
“Shosti, mnenacho chaniingia moyoni japo sijui nifanye nini mie mwenzenu mwaniacha njia panda.” Lily aliongea, akiamini maneno ya Mashosti ni ya kweli.
“Shosti, sie tunakupenda, pendo la kupendeka, utambue na pia ujue kwamba rafiki mzuri ni yule anayekushauri. Hatujakukataza kuwa na Mumeo, hatujakushauri uachane na Mumeo lakini sie tunakushauri…..umtafute mwanaume kijana wa umri wako, huyo awe karibu karibu na wewe, akupooze mawazo yanayoendelea kulindimaa, akuondolee upweke wa kutokuongea na Mwanaume japo awe mfariji wako.” Elizabeth alimshtua Lily kwa yale maneno.
“Itakuwa siri yetu Mwaya, hatutamweleza mtu, kikubwa ni kuona mwenzetu hauteseki, umesikia wapi na wapi kwamba binadamu tuliumbwa kuteseka? Hata vitabu vya Dini vinapinga kuhusu hilo, hata vitabu vya Dini vinasisitiza kusema kuwa binadamu tuliumbwa tuishi kwa raha mustarehe.” Anjelina alinena.
“Mmmh! Shoga zangu nimsaliti Denis nitoke nje ya ndoa wakati nimefundwa uvumilivu na ustahilivu, wakati nimefundwa upendo usio na kikomo.” Lily aliongea.
“Mwaya, kama hautaki kutusikiliza basi ni bora tukuachie huo ‘Upunda na Ukondoo wako, wenzio tumeona jinsi unavyoteseka, tunakuhurumia wewe mwenyewe lakini wewe hautusikilizi wala haujali mashauri yetu.” Elizabeth aliongea, Safari hii hana furaha, amenuna, domo halimpendezi, kumbe anafanya makusudi ili kumteka yule binti.
“Wenzio tunapoona waume zetu waenda njia tusozitaka tunawaonya na tujapoona hawaonyeki tunawaacha na kufuata Uhuru wetu wewe pia unapaswa kuwa huru pale unapoona Mumeo haendani sawa na wewe mkalie kimya wala usijivute vute kwake, jitafutie njia zako.”Aliongea Anjelina, muda sio mrefu walihitaji kuondoka wakamuacha Lily yu ndani ya dimbwi la mawazo
********************
Lily alikubaliana na mawazo ya wale Shosti zake mara baada ya kutafakari kwa kina pasipo kupata jawabu sahihi. Alihisi kama Mumewe hamtendei haki, japokuwa sio kweli kusema ati Mumewe hamtendei haki, uwezo wake finyu wa kukaa na kufikiri ulimfanya anasishwe kwa kijana mmoja mitaa ya Buguruni Malapa, Geofrey, ndio jinale labda hupenda aitwe Geo, ambalo ni kifupisho cha jina Geofrey.
Mapendo yakawa ni ya siri sana pasipo Mumewe Lily kugundua wakati huu pendo la Lily na Geo mbona lilinoga, Geo alimfanyia Lily mambo mengi ambayo Mumewe mpenzi Bwana Denis hajapata kumfanyia. Kumtoa Outing kula Dinner, kwenda Beach, kwenda Shopping, kumtembeza tembeza kwenye kumbi za raha na starehe, kumfanyia suprisment za mara kwa mara. Hayo ni baadhi ya mambo ambayo Denis hajawahi pata kumfanyia Lily, Lily akakolea naye, akazidiwa kwenye Pendo la huyu kijana aitwaye Geo.
“Safari hii Mtoto alianza kujilaumu kwanini aliolewa na Mwanaume asiyemjali? Kwanini anaishi na Mwanaume asiyempa raha na starehe za Duniani? Ooh! Jamani dharau alianzisha, binti akawa anadai matumizi makubwa ya Pesa, na akinyimwa hana furaha, binti akawa mkali mwenye hasira kwa Mumewe. Mume arudipo makaripio ndio salamu kwake. Akamuona Mumewe kama bwege lisojitambua, hakukumbuka kwamba ndiye Mumewe aliyemtoa Kijijini, hakukumbuka kwamba ndiye Mumewe aliyemtafutia Kungwi ili amfunde kazi za nyumbani, matumizi ya zana zinazotumia Umeme nakadhalika. Alisahau kuwa sio yeye yule mwenye ngozi ya asili, nywele za asili na mwili wa asili.
Alichokumbuka sasa ni kuvaa mavazi ya bei gharama, kununua mawigi ya kila rangi, kujipodoa ili mtoto apodoke. Loh! Walisema wahenga Kuku mgeni asikose kamba mguuni, mwacha asili si mjasili. Matukano, malalamiko, mabezo na maneno mengine makali yalimtoka mdomoni, sijui ni nani alimfunda kuwa na mdomo mchafu? Au hao Shogaze? Mmmh! Tizama Mumewe akishindwa kumtimizia yale ayapendayo basi asitegemee kupata upendo wa Mke na mume.
Masikini Denisi alisumbuka, alitaabika na kuchanganyikiwa. Kama ni kumpenda Mkewe jamani alimpenda, alimpenda kuliko kitu chochote kile.
*********************
Basi wale Mashosti walipoona huko nyumbani kwao Lily moto unawaka, furaha iliwajaa wakaona sasa mambo yapo smart, Dawa ya Lily bado kidogo kuchemka, ameyataka yeye mwenyewe sasa wacha wamtengenezee, wamlipue kabla hajalipuka. Unajua walichofanya Mabeduni hawa? Unajua walichofanya hawa mabaradhuri, hujui eeh! Ndio hujui, basi wakamtengenezea Bomu, Lily alipuke na akiishalipuka ndio uwe mwisho wake.
Fumanizi halikugonga mwamba, si walishamtonya Mumewe Lily kwamba ‘Mkeo anachepuka’ tena anachepuka na kijana mdogo wa umri wake, ni kijana mdogo lakini kwa maujanja ni mtu mzima. Bomu lililotegwa likalipuka, fumanizi likazua Talaka tatu, tena Talaka kama tujuavyo hazimtaki mtu kurejea tena kwa Mtaliki wake.
Loh! Masikini Jamani kilio, majonzi na huzuni, Lily akawa hana pahali pakwenda zaidi ya kukimbilia kwa Geo, Geo naye akamtimua akamwambia hataki Mwanamke wa kuishi naye, anahitaji kuwa Singo boi. Geo kwa ubaya wake akahama Mji hata asijulikane ni wapi alikohamia. Lily akawakumbuka wale Mashostize Elizabeth, Lisa na Anjelina, kutwa kuchwa ikawa ni kuwatafuta hapa na pale Buguruni hata asiwapate, masikini. Majuto mjukuu, msaliti hujuta. Lily akajuta na kuumia.
Siku sio nyingi alikuja kupata fununu ati huyo Shogaye mkubwa aitwaye Elizabeth, amewekwa kinyumba na Mumewe, mtoto anakula raha na starehe. Nyie! Masikini roho ilimuuma sana yule binti, kumbe porojo zote zile ni utapeli, ametapeliwa Mume, ameibiwa mchana kweupe, machozi na majuto yalimjaa Lily. Amekosea yeye mwenyewe, amekosea mara baada ya kuruhusu rafiki zake waingize machombezo yao, ajabu machombezo hayo yamefanya aachwe na kisha mwenziwe aingie ndani.
“Ushamba umemponza, alifundwa awe mvumilivu, alifundwa awe mstahimilivu, alifundwa awe na upendo kwa Mumewe, tizama marafiki wamemharibia, tizama marafiki wamempotosha, amelijisahau kama yeye tayari yupo ndani ya ndoa. Sasa amevuliwa nguo, amepokonywa tonge mdomoni , amedanganywa na hao waliodai ati wanaishi maisha bora wakati sio kweli ni waongo wapandikiza chuki, migogoro na uvunjifu wa ndoa za wengine.
Aliyachukulia yale maneno ya Mashosti kama kweli tupu kumbe Bibie hakutafakari kwa kutumia elimu, pupa zimemponza, ameachwa na Mwanaume mwenye pesa zake, ameachwa na Mwanaume mwenye nia na malengo, Mwanaume mwenye muonekano(Handsome) Mume amekamilika, yaani kwa kifupi ni Mwanaume wa nguvu, sijui vijana wa kileo wangelimwita ‘Dume la Mbegu’, Ajabu alipotoshwa na kuingizwa Mjini, leo hana mbele, hana nyuma, maji yamemwagika hawezi kuyazoa, anajuta juto juu ya juto na majuto mjukuu, msaliti lazima atajuta tu.
Mwisho
No comments:
Post a Comment