Monday, September 9, 2024

MOYO WENYE MASHAKA. SEHEMU ya kwanza

 






       “Maumivu ya mapenzi, Umenisaliti,

         Kidonda cha mapenzi, umempenda mwingine,

         Japokua nimekusamehe, Lakini moyo unamashaka,

        Moyo wenye mashaka, Najua sitadumu na wewe,

        Moyo wenye mashaka,  Najua nitakutoroka.”   

 

SEHEMU YA KWANZA

NALAZIMISHA KUCHEKA

 

                 Nikalazimisha kucheka mdomoni mwangu nikitamani kicheko kinitoke, ili nionekane kwamba nina furaha, yaani sina kinyongo sina chuki sina ubaya kwa mpenzi wangu msaliti wangu mzuri wangu wa zamani, Lameck Lameking. Lameck niliyempenda si kwa maneno matupu kama wanavyopenda vijana wa siku hizi bali kwa matendo ya dhaati yaani mapenzi ya kweli, yale mapenzi ya Adam na Bibi Hawa mapenzi ya kila kitu, mapenzi ya kukubali kila kitu, mapenzi mataraamu kama pipi Looh! Haki! Wenye wivu wajinyonge  Mimi mwenyewe nilijiona, nilijiona nimepata tena nimepata nilipotaka kupapata.

               Nafanya kucheka kwa kulazimisha kucheka ingawaje moyo wangu wakataa kunifanya nicheke, basi nalazimisha kucheka pale Lameck Lameking anafanya kunichekesha unajua mpenzi msomaji, mie nalikwisha kumsamehe msaliti wangu, nikataka maisha yaendelee bila kinyongo, tatizo lipo kwenye moyo wangu, moyo wangu umejaa mashaka, Loh! Mmh!  Mawazo, nimegubikwa na mawazo.

                      Lameck anaendelea kunichekesha kwa matani yake ya kila siku, Lameck ana vituko mwanaume wangu  asikwambie mtu, kwa vituko na vibweka namfanananisha na yule mchekeshaji maarufu Duniani Mr Bean, Ananichekesha kama vile natizama zile katuni za Tom and Jerry  ana vingi vituko kama waigizaji wa kinaigeria Haki na Ukwa  Teeh teeh teeeh!🤣🤣🤣🤣😘 Nalazimisha kucheka japokua sina kicheko nafanya kutabasamu lakini mpenzi msomaji moyo wangu💗, moyo umejaa mashaka.

                    “Opamiss” Lameck ananiita japo sina furaha, labda niseme tu kwamba najaribu kuivuta taswira ya furaha, furaha ya lazima.

                    “Abee! Mpenzi” Nalimwitikia nikimtizama machoni kwake, tukayagonganisha macho yetu, haraka haraka nikayatoa macho yangu na kutizama pembeni, alikiona kile kitendo aliona namna ninavyo yakwepesha macho yangu kwake.

                     “Ninakupenda sana mpenzi wangu, nimekuweka moyoni mwangu, acha yaliyopita yapite tuwe na furaha mpenzi, mapenzi ni furaha, raha na uzima tele.” Lameck aliongea tukiwa tumeketi sebuleni kwetu wawili pekee sebule ile kubwa kwangu ilionekana kuwa ndogo, ni sebule iso na vitu vingi vya bei gharama. Kuna sofa moja kubwa lenye pande tatu  za kutosha watu watatu pia upande wa kulia kuna sofa jingine dogo lenye pande mbili za kuketi watu wawili. Kuna meza kubwa ya kioo, chini kuna zuria(kapeti) zuria nililolinunua Kariakoo pale Shule ya Sekondari Benjamini Williama Mkapa. Tv screen moja ndogo imebandikwa ukutani kuna kiyoyozi kinachotoa upepo wa ubaridi (AC) tena kuna Freezer inayofanya vyakula vyetu visiooze (inagandisha vyakula) si mnajua tena mie sie mtu wa kuketi nyumbani mie kigulu na njia kutwa kuchwa nipo kazini nipo bize na biziness zangu.                

                      Maneno aliyo nena Lameck niliyasikia vizuri masikioni mwangu, haki!  Niliyachukia, niliyaona kama upuuzi sio upuuzi tu bali pia niliyaona kuwa ni maneno yaso na maana kwangu, yanini niyaweke moyoni au niendelee kuyasikia masikioni mwangu, yamejaa upuuzi. Leo anajifanya kunipenda sana eeh! Wakati anajua fika  kuwa alinisaliti muda, bado sijasahau nina kumbukumbu tosha kwamba Lameck alinisaliti, akampenda mwanamke mwingine, akanitia kidonda,  jamani kidonda cha mapenzi kumpenda mtu mwengine wakati mie nipo, kwangu hilo ni donda tena donda moyoni mwangu. Kidonda kinachotoa usaha  nahisi ni jipu, jipu la mapenzi, lakini mh! Sio kila penye donda la usaha pana jipu, madonda mengine ndio hayo yanayotoa  usaha kwa sababu ya kuoza kwa nyama.

                    Haya sasa, nyama imeoza, nyama ya mapenzi, mie naona mzigo kuila, sijui ni nani ataila? Kuishika tu naona kinyaa ndo iwe kuitia mdomoni! Mmh! Nitatapika mie, ama ndio niwaachie hao Umbwa malaya wake, malaya ambao Lameck ametembea nao, ametembea nao siku hizo mie nikiwa bize kumtafutia pesa ya chakula, nikihakikisha baba asie na kazi  amekula ameshiba, baba asie na nguo amevaa amependeza. Siku zile  mie  mama nikitafuta hela ili  nimgaie baba asie na pesa, looh! Nalivumilia  mwenzenu.

                   Pande la  nyama limeoza, naombeni ushauri wenu wajuzi wa kushauri soga na ngano za mapenzi, si mwajua fika kuwa mapenzi ni nyama, mie sikujua hilo hata pale naliposikia malenga  Mshairi mmoja akighani  diwani yake akilalama ati;

                 'Mapenzi ni nyama,

                 Nyama tamu ya ulimi,

                 Muhimu kuitunzia heshima,

                Yanini kuiletea vichomi!?'

 

                   Tusiende mbali ebu niambieni enyi washauri wenye mashauri nasaha, hivi kama nyama imeoza na kuharibika kabisaa labda yatoa  wadudu mie niifanyaje? Niitupe au niibakishe, kama nitaitupa watasema kayatupa mapenzi, japokua wajua kua hayo mapenzi tayari yamekwisha haribika na kama sitaitupa  nitaibakisha eeeh? Si itaendelea kuoza  na kuharibika? Aash! Yanikera mie, harufu nzuri siipati nachukizwa na uozo wa hilo pande la nyama, anyway lazima niketi chini na kufikiria maamuzi yatoke moyoni mwangu. Embu subirini haraka na pupa za nini?!

                     Yale maneno aliyoyatamka Lameck kwa upande mwingine nalimwonea  huruma, aah! Kwasababu ninampenda, siwezi kumtupa. Nalimtafuta mie mwenyewe, nalimtafuta kwa udi na kwa uvumba (nalimtongoza)  sinaga aibu kama walivyo na aibu wanawake wenzangu, mie nina sifa, haiba yangu inaniambia fanya unavyotaka kufanya, japo utakacho kukifanya kiwe sahihi, haiba yangu inanisukuma, haiba yangu inanisogeza, na haiba yangu inafanya nifanye maamuzi. Sioni aibu sababu kwangu aibu ni kitu kishenzi.🔥

                       Aaahh! Mfyuuu🥴! Nafyonya nachukia moyoni, sijui kwanini nina tabia za kidume dume, ubabe kiasi fulani umenitawala, lakini kwa huyu mpenzi niliye na mashaka sijawahi kamwe kumfanyia ubabe, nilimpenda moyo mmoja, alinikaa moyoni, wakati wote sijapata kumtamani mtu mwengine. Niweke wazi, sikufanya kazi kwa amani na kwa utulivu wakati wote nalimuwaza   Lameck Lameking nalihitaji kuwa karibu karibu naye kwa mapenzi moto moto.

                   Sifa zisijae gunia, sifa zisijae hadithi hii ya kusisimua, labda nizitaje sifa chache nilizojivunia kwa huyu tende wangu wa ubani, nilimpenda yeye tu, nikajiaminisha kuwa nitakuwa pamoja nayeye pekee, milele. Iwe raha iwe karaha maisha ni muda na muda wenyewe ndio huu unao kwenda hautaki kurudi nyuma.

                 Lameck ana macho fulani madogo yaliyo jaa upole mboni za macho yake zinaonesha kuwa ana matamanio si ya kimwili pekee bali hata yale ya kutaka mali, kama wanaume wengi wanavyotamani. Nisikufiche mpenzi msomaji macho yake nayajua vema nimeyasoma sana hatimaye mwisho wa sekunde nalimfumania  akigonoka  na huyu Bibi ambaye mara baada ya Lameck kuondoka nyumbani kwangu akaenda kuishi kwake.

                  Macho yake yanaficha mambo, macho yake yanaficha siri, hataki kuniambia, tena hataki kuniambia kuwa anaye mwingine pembeni, anampenda kama ninavyompenda yeye, anamfanyia kila kitu anachokitaka kama ninavyomfanyia mmi hataki mie nijue, kwa hiyo nisilolijua ni kama usiku wa giza, nisilolijua litanisumbua, nisilolijua litanikwaza.

                  Ok. Sifa ya pili aliyonayo Lameck ana moyo uso taka kufanya ushirikiano, japokua anajaribu jaribu kuonesha yupo na mimi anajaribu kunifariji pale ninapohitaji faraja, lakini hafanyi juhudi yoyote ile ya kunifanya nifurahi na kufarijika (ingawaje ananifariji). Niliwai pata kuugua Maralia, nilizidiwa, almanusura  kufa, alikua karibu na mimi  lakini hakutaka kunipeleka Hosptali, hakutaka nitumie dawa, hakutaka kunipa pesa, ajabu kila siku alinifariji faraja nyingi Inshallah! Ya Mungu mengi nilipona kwa juhudi zangu mie mwenyewe.

                        Mbona hata yeye amepata kuugua, mara kwa mara zile siku  alizonitegemea, aliniweka wazi na mie nikamsaidia, mara nyingi tu, ajabu siku hizo alizompata huyu bibi muuza pombe ya kienyeji aliwacha kuniambia shidaze, aliacha kuniambia matatizo yake, aliwacha kunitegemea, akamtegemea bibi muuza pombe, akaeleza shida zote alizonazo kwa huyu bibi muuza pombe, tabu zake, malalamiko yake na baya zaidi alihamia kwa huyu bibi muuza pombe, nilijisikia  vibaya niliumia pia sikupenda Lameck  wangu amtegemee mtu mwingine zaidi ya mimi, mimi ni wake na yeye ni wangu, ndimi faraja yake, ndimi tunda lake wengineo mapaka shume.🐾🙀🐈

                      Lameck kijana mrefu hivi ana sura na macho makubwa meupee, nywele nyingi kichwani mwake, midomo yake mikubwa pia, shingo yake pana, mwili wake ni mwili wa mazoezi bado angali kiijana kama nilivyo mie Opa miss, msichana wa kimakonde, mrefu kiasi sio mnene, sio mwembamba, nina figa bomba  Mashallah! hips na miguu ya bia, macho maregevu nywele nzuri za asili, mdomo wangu una meno meupeeee peeee kama maziwa fresh, ninavutia lakina hata hivyo mie siko simple kihivyo kama unavyo dhani, waweza kunipenda kama unavyo dhani sababu napendeka, ndo maana kukwambia waweza kunipenda kama unavyo wapenda wanawake wengine, ajabu nikikukataa kama nilivyo wakataa wengi yote kwa sababu nilikua nae  Lameck alinitosha nilimpenda mie mwenyewe nikatulia kwake, sikuwataka wengineo, nikamuweka mtimani, nikatulia kwake, mapenzi mapenzi, mapenzi kunoga kunogela, mapenzi wakati wote mapenzi matamu kama pipi.

                     Opa mie ni mwanamke lakini wapenzi acheni nijisifu, acheni niseme ninajua kupenda, acheni nijivune na kujivunia kwa kusema najua kuchagua, niacheni niichekelee riziki yangu majaliwa, kama ni kuitafuta nimeitafuta mie mwenyewe wala sijatafutiwa, kama ni kupenda nimependa mie mwenyewe wala sikuwaza kupendwa na hata baada ya kupenda mie nikauona upendo wa Lameck, mwanaume kijana akiwa angali tope tope, masikini wa kuketi vijiweni apate kupiga soga, iwe mchana, iwe usiku hakuna maendeleo zaidi ya kuupoteza muda mzuri duniani.

 

      Basi mie Opa nikalazimisha kucheka kicheko cha kinafki nikichekeshwa chekeshwa  na Lameck msaliti wangu, nikitaniwa taniwa na Lameck yule niliyempenda sana hapo kale, hapo mapenzi yalivyokuwa matamu kama pipi, ajabu leo mapenzi yamekua kama nyama iliyooza wala nisiitamani.


(


Itaendelea SEHEMU ya pili)



No comments:

Post a Comment

I promise you

   I PROMISE YOU. (NINAKUAHIDI.) SURA  YA KWANZA. UBAYA WA POMBE. “Umenizingua job, umenizingua kwa muda mrefu sana mpenzi wangu…….kwanini l...