MBOSSO
SEHEMU ya nne
Tulipoishia
.
"Ni hivi Mbosso, mimi na wewe tunahitaji kuondoka hapa Kigogo haraka sana iwezekanavyo.” Diva aliongea.
“Kuondoka! Kwenda wapi?” Mbosso aliuliza.
“Tutande popote pale duniani ilimradi tu huko tuendako kuwe tofauti na Mjini yaani Kijijini.”
“Kwanini tuondoke? Kwanini tusiendelee kuishi mjini? Twafata nini kijijini?” Mbosso alidadisi.
“My love.” Diva alimdondoshea Mbosso juu ya kitanda kile kikuukuu chumbani kwa Mbosso. Kama tutakumbuka kuwa Diva na Mbosso walikuwa wangali wamekaa juu ya kile kitanda kikuu kuu chumbani.
“Ninahitaji tuyabadilishe mazingira, maisha yetu sio lazima tuyatumie tukiwa Mjini, Kijijini pia ni kuzuri, kuna nafasi kubwa kwa ajiri ya mimi na wewe. Kumbuka kwamba nimetoroka nyumbani, nimetoroka kwa ajiri yako, sitaki wala nisingelipenda kuona kwamba penzi letu linasongwa songwa na wazazi wetu.” Diva aliendelea kuongea.
“Nipo radhi kuikataa elimu niliyonayo ilimradi tu niwe na wewe. Nipo radhi kuukataa utajiri wa baba na mama ili mradi tu niwe na wewe I love you, I love you baby.” Diva alimbusu Mbosso kunako mdomo wake wakati huo Mbosso akimpapasa papasa Diva kimahaba.
“Tutaenda wapi sasa my? Pia hujaniambia huko tunakotaka kwenda tutakwenda kufanya nini?” Mbosso alihitaji kujua zaidi.
“My love, mbona tayari nimekwisha kukuambia kwamba tutakwenda popote pale Kijijini na pia tunaenda kuyabadilisha maisha yetu tunayoishi sasa. Maisha yapo popote kijijini pia.”Diva aliongea angali bado anamtia mabusu mfululizo mdomoni .
"Sawa na hilo Gari lako ulilokuja nalo utaliacha wapi? Au ndio tunaondoka nalo?” Mbosso alimuuliza Diva.
“Hiyo Prado tunaondoka nayo ni mali yangu, baba na mama walinipa kama zawadi siku ya birthday yangu miaka miwili iliyopita.”Diva aliongea, wakati huo huo wawili wale walianza kuvuana nguo zao moja baada ya nyingine, hamu ya kulaliana iliwajaa, ajabu muda si mrefu walikwisha lewa kwa mahaba, walikwisha tupana juu ya kile kigodoro alaliacho Mbosso, wakawa bize wanashughulika.
###
Endelea
Siku iliyofuata, Diva na Mbosso walianza Safari, Safari ya kulihama Jiji zuri la Dar es Salaam. Walipanga kwenda Lushoto Tanga. Safari yao ilinoga, ikanogelea na kwa mapenzi ya Mungu walifika Lushoto Tanga mchana kweupe nao hawakutaka kuupoteza muda, waliingia ndani ya Kijiji cha Magamba huku mvua ikiwa inanyesha taratibu, ubaridi ukiwa unavuma taratibu, tena uzuri wa Lushoto, ardhi ya kilimo ipo ya kutosha.
Diva alifuata kilimo?
Ndio Diva alifuata kilimo, Diva hakutaka awe mwana Sheria yeye alitaka awe mkulima, ingawaje hajapata kuwa na wazo la kuja kuendesha kazi za kilimo maisha yake yote. Amelelewa katika familia ya watu wanaojiweza hawana shida, kila kitu kilicho kizuri kinapatikana hapo. Ajabu iliyoje kwa sababu ya mapenzi Diva amekuwa radhi kuviacha hivyo vyote vizuri vya anasa.Tena Diva amefuata mabadiliko ana nia na lengo la kumbadilisha yule chizi Mbosso, ati yeye anafikiria njia bora ya kumbadilisha yule chizi ni kuketi pamoja kujadiliana, kupanga na kupangua. Kutekeleza na kutimiza. Uzuri wake Diva ameona njia ya kutimiza hayo yote ni kuyahama makazi ambayo wangali wamekulia na kulelewa huko kwenye anasa nyingi, vurugu na vurumai.
................
“Ninakupenda sana Mbosso, ninahitaji uje kuwa baba bora kwa huyu mwenetu ajaye, sihitaji uje kuwa baba ambaye jamii inakuchukia na pia jamii inayachukia matendo yako. Mimi na wewe muhimu tujibidishe katika shughuli za kilimo, ufugaji na biashara. Chochote tutakachokipata tutatumia vema, tutahifadhi kwa ajiri ya akiba na pia tutamtunzia ‘kijacho’ wetu. Diva aliongea wakiwa shamba wanapalilia viazi vyao, wanamiliki hekali nyingi juu ya milima ya Wasambaa, huu ni mwezi wa sita tangu wamekuja Lushoto Tanga.Uzuri wa kuja Kijijini Diva ameuona; Mbosso amebadilika sana, amekuwa karibu karibu na Diva, hana tena zile tabia zake za wizi. Amekuwa mtulivu sana, Diva anafurahi sana kumwona Mbosso akiwacha kabisa ile tabia ya kuvuta ‘Dawa’ hata hivyo kitu kimoja ambacho bado kinamchukiza Diva ni ile tabia ya Mbosso kunywa Pombe ya mataputapu, tabia ambayo Mbosso anaonesha kuwa ameikomalia.
Mbosso analewa nakwambieni analewa hadi aibu, analewa nyakati za usiku, analewa nyumbani kwake yeye na Diva analewa na tena analewa. Diva hapendezwi na tabia hiyo, ndio maana anafikiria namna ya kuibadilisha hiyo tabia ya Mbosso, kama ameweza kumshawishi aachane na wizi, uporaji na utumizi wa dawa, je, ashindwa kumzuia Mbosso aachane na ulevi wa kupindukia? La, hasha, Diva angali bado anafikiria ‘pilipili’ ya kumfanya Mbosso aachane na ulevi ili hapo baadaye awe baba bora anayefaa kuigwa na jamii.
MIAKA MIWILI BAADAYE.
Diva na Mbosso tayari wamejaliwa kuwa na mtoto mzuri mdogo wa kike, waliyempatia jina lake ‘Lavu’. Lavu ni mtoto mtundu, amekopi sura nzuri kutoka kwa mama yake lakini macho Nyusi na kope ni za babaye, midomo ni ya babaye. Uzuri wa mtoto Lavu, yungali bado mdogo lakini anaonesha matamanio ya kwenda Shule kusoma pamoja na watoto wenziwe. Diva na Mbosso wakafanya juu chini kumpeleka Lavu ‘Nursery’ (Shule ya chekechea), na kwa bahati nzuri uelewa wake ni mkubwa darasani.
Siku moja Diva akiwa ameketi barazani anamfunda bintiye Lavu kusoma na kuandika, Mbosso alirejea kutoka shamba amebeba jembe, panga na fimbo. Juu ya bega lake amejitwika zigo la viazi ulaya, vile viazi vya chipsi. Mara baada ya kuingia uwanjani alilibwaga lile zigo chini ‘puuu’ akiwa anapumua kwa uchovu, Diva aliamka pale alipoketi akamsabahi mumewe.
“Pole na kazi mume wangu.”
“Asante sana my dear wife.”
“Loh! Umechoka kweli.” Diva aliongea akimfuta jasho mumewe kwa kitenge alichojifunga kiunoni.
“Nimepowa Sweet, yote maisha tayari nimekwisha yazoea kama ulivyoyazoea wewe, na kwa kiasi kikubwa tunayafurahia haya maisha mema ambayo pesa ipo nje nje, vyakula si haba, ni vingi ni vya kumwaga, akiba haiozi bali inazidi maradufu.” Mbosso aliongea.
“Nafurahi kusikia mneno hayo my husband, umeona eeh! Kubadili mazingira katika maisha ni jambo lenye heri, mipango tuliyoipanga tizama imezaa matunda. Kilimo kimekubali, mifugo inazidi kuongezeka na kunawiri, tayari tumejenga nyumba yetu na uzur iwake tunaye mtoto Lavu, tunamuwekea akiba ya pesa Benki ili maisha yake yaje kuwa mazuri hapo baadaye.” Diva aliongea.
“Oooh! Nami nafurahi kuwa nawe mpenzi, tena nafurahi kuishi na mwanamke mwenye kujua namna ya kupanga mipango ya kimaisha nayo ikatimia. Tizama Diva kama sio wewe ningelikuwa wapi mimi? Umenitengeneza nami nimekuwa mpya, zamani nilikuwa mvivu tegemezi, mzembe, mwizi na mdokozi. Leo hii mimi nadamka pamoja na wewe twaelekea shamba huko hatukosi cha kutusogezea siku.” Mbosso aliongea.
“Mpenzi, kitu kizuri ambacho moyo wangu umekuwa na furaha zaidi ni jinsi ulivyobadilika, sikuipenda ile tabia yako ya kunywa pombe nawe ukalewa, sikupenda ile tabia yako ya kuvuta moshi wa Sigareti. Sina budi kusema asante Mwenyezi Mungu mume wangu umebadilika, sasa haunywi pombe, hauvuti moshi wa Sigareti, unakunywa juisi na maji, unakuwa karibu karibu na familia yako, yaani mpenzi moyoni ninafurahia.” Diva aliongea kwa furaha.
“Aaaah! Hayo mambo madogo madogo na wewe….” Mbosso aliongea kisha akendelea.
“Wewe ni mke wangu, mumeo ndio mie, napaswa kukusikiliza unachotaka nisifuate, unachonisihi nifanye nami nafanya.” Mbosso akambusu Diva mdomoni.
“Mimi ni mkeo, wewe ni mume wangu, ninapaswa kukusikiliza unachotaka nifuate, unachokataza nisifuate, unachonisihi nifanye nami nitafanya.” Diva aliongea kisha akarudisha Busu mdomoni kwa Mbosso mumewe.
“Ninahitaji maji, Lavu nenda kachote maji ninywe babayo.” Mbosso alimwambia mwanaye mdogo.
“Acha nikachote mie baba, mtoto anasoma hembu nisaidie kumfunda hizo herufi A, E, I, O, U.” Diva aliongea kisha akaamka pale alipoketi na kuelekea sebuleni kumchotea mumewe maji ya kunywa. Wakati huo huo Mbosso na Lavu waliketi pale barazani, Mbosso akimfunda bintiye herufi na Silabi.
*HASIRA
Wakiwa shambani wanavuna viazi vikuu, Diva na Mbosso walisaidiwa na jirani zao watatu, jirani hao wamejitolea kuwa wasaidizi wao katika shughuli za kilimo, ufugaji na biashara ya mazao ya shambani. Diva alianzisha maongezi.
“Vipi mume wangu, hiyo gari letu Truck ya kubebea mazao shambani dalali amesema lini litaingia Lushoto?”
“Nimepigiwa simu, Dalali ananiambia siku tatu zijazo tutarajie furaha yetu kuongezeka, sasa tutakuwa na gari yetu wenyewe, gari ya kubebea mazao shambani pamoja na mizigo mingine inayopelekwa Jiji la Dar es salaam, Arusha, Tanga mjini, Pwani na Dodoma.” Mbosso aliongea, wakati huo vijana wake wale vijana watatu walikuwa bize shambani wakivuna viazi vilivyozaliana kwa wingi kama mchanga wa bahari.
“Vema mume wangu, tukiwa na Gari tutapunguza hasara ya kutumia usafiri wa watu wengine na pia sisi kama sisi tutakuwa msaada kwa wengine.” Diva alikuwa ni mwingi wa furaha, aliongeza tabasamu.
“Na vipi kuhusu safari yetu ya kurejea Jijini Dar es salaam, je, bado ungali unaifikiria mpenzi?” Diva alimuuliza mumewe.
“Nimeafiki mpenzi mke wangu, wacha turejee nyumbani kwa wazazi wetu tukaombe pale tulipokosea watusamehe, tukaombe waridhie na wakubalie ili tuishi pamoja, watubariki tuyaendeleze mapenzi yetu.” Mbosso alionge.
“Mtoto tayari ametuunganisha, sidhani kama baba na mama yangu watakuwa na pingamizi juu ya hilo.” Diva alijipa tumaini.
“Tutegemee mengi, mazuri, mema na yenye kukubaliwa, pia tumtangulize Mwenyezi Mungu atakayetuwezesha na kutufanikisha katika safari yetu ya kurejea nyumbani Dar es salaam.” Mbosso alitia neno, wakaendelea na shughuli ya kuvuna viazi vyao vingi vyenye afya na siha njema, vilivyoshiba mbolea na rutuba ya kutosha.
****
Itaendelea
No comments:
Post a Comment