Tulipoishia
"Mtoto tayari ametuunganisha, sidhani kama baba na mama yangu watakuwa na pingamizi juu ya hilo.” Diva alijipa tumaini.
“Tutegemee mengi, mazuri, mema na yenye kukubaliwa, pia tumtangulize Mwenyezi Mungu atakayetuwezesha na kutufanikisha katika safari yetu ya kurejea nyumbani Dar es salaam.” Mbosso alitia neno, wakaendelea na shughuli ya kilimo, kuvuna viazi vyao vingi vyenye afya na siha njema, vilivyoshiba mbolea na rutuba ya kutosha.
***
Tuendelee hapa Leo.
Safari ya Diva, Mbosso na Lavu kurejea nyumbani Dar es salaam iliiva, ndani ya ile Prado aliyoimiliki Diva, waliketi hawa wanafamilia wakiwa na furaha, raha na imani ya kwamba sasa mambo ndio yanaenda kuwa sawa sawa. Yanini kuandikia mate wino ukiwepo? Wacha waende nyumbani kwa baba na mamaye Diva japo kuyaweka mambo sawa ili sasa waishi kwa amani kwa sababu bado walijiona wamekosa baraka pale tu wazazi wao wakiwa na pingamizi.
Waliwasili salama salimini ndani ya Jiji la Dar es salaam, wamebeba zawadi tele kutoka Shambani, mikungu ya ndizi, viazi vitamu, mihogo, magimbi, kabichi na vinginevyo vingi vya bei gharama, tena uzuri wake wawili hawa hawakutumia gharama yeyote ile, bali walitumia hekima zao kupata mazao ya shambani.
#####
Baada ya kuwasili walitegemea labda wangelipokelewa kwa furaha, bashasha, raha na vicheko, lakini bila ya kutarajia walikumbana na zile sura zenye chuki kutoka kwa wazazi wa Diva, vitisho na maneno ya kuvunja moyo, japokuwa walijitahidi kuomba msamaha, walijitahidi kuomba huruma, tena waliwaeleza wazazi kwamba ni mapenzi ndio yaliyowafanya watoroke na kwenda kuishi pamoja, hilo halikusaidia, hasira za wazazi wake Diva ziliiva.
“Ulishindwa kutuheshimu pamoja na kuyaheshimu mawazo yetu, mawazo ambayo kwa uzuri wetu tulikuhelimisha tukijua kwamba yatakusaidia katika maisha yako.” Babaye Diva akiwa ni mwingi wa hasira, amefura kama mbogo aliyejeruhiwa, aliongea mate yakimtoka kwa fujo mdomoni.”
“Biblia takatifu inasema ‘Waheshimu baba na mama yako, ili siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi akupayo Mwenyezi Mungu’. Lakini Diva umetuvunjia heshima, umetudharu sie wazazi wako, umetuona sie kama takataka, umetufananisha na vyombo vibovu vilivyoharibika hata ufikie hatua ya kujikabidhi kwa mwanaume asiye wa hadhi yako.” Mamaye Diva aliongea.
“Baba na mama, tumekuja kuomba mtusamehe, yaliyotokea tunajua ya kwamba yaliwavunja mioyo yenu, lakini yote tisa kumi tunajuta na pia kwa sababu ya mapenzi tunaomba mtusamehe, tunapendana, tumepanga maisha ya pamoja milele hadi kifo.” Diva aliyatetea mapenzi yao. Wakati huo hawa wapendanao wameketi juu ya sofa moja kubwa pale sebuleni wakiwa na nyuso za huzuni, tegemeo lao ni kuyaweka mambo sawa kama walivyoyaona yanaenda kombo.
“Diva, nakumbuka kabla ya haya yote kutukia niliwahi kukuambia mwanangu, niliwahi kukuambia kuwa wewe ni msomi tena sio msomi jina bali ni msomi wa chuo kikuu, msomi mwenye Degree ya Sheria, ulishindwaje kuitumia Degree yako kumtafuta mume kijana msomi mwenzio. Tazama jinsi wazazi wako tulivyo na upendo, upendo wa dhati, tulifanya hima hima kukutafutia mapenzi tukampata kijana msomi mwenzio tukategemea mtapendana na kuishi pamoja, ajabu iliyoje Diva mwanangu umetuangusha na kukutia aibu mbele a jamii.” Mamaye Diva alitia neno.
“Mama naomba nirudie kusema yote niliyoyatenda niliyatenda kwa sababu ya mapenzi yangu kwa huyu mwanaume niliyempenda, moyo ndio unaoanza kupenda sababu hiyo moyo wangu ulitua kwa Mbosso acha niseme ukweli kwamba ningali bado ninampenda, Mwenyezi Mungu ametujalia Binti mzuri huyu hapa mbele zenu, matokeo ya mapenzi na kupendana naomba yaliyopita wazazi mtusamehe mtupatie Baraka zenu ili tuishi kwa nguvu za haya mapenzi.” Diva aliyatetea mapenzi yake.
“Wazazi tambueni kuwa tumependana na kuachana kamwe isiwezekane.” Mbosso aliyekuwa kimya sasa alitoa neno.
“Diva ni mwanamke mwenye hekima , hekima nyingi za kisomi, mimi nilikuwa ninatabia nyingi mbaya kuzitamka katika jamii, leo hii Diva amenibadilisha nami leo ni mwingi wa utulivu, amani na mipango mizuri katika maisha. Pasina Diva mimi leo hii ningeliharibika ningeliuawa na wananchi wenye hasira, ningelifungwa Jela kwa sababu ya tabia zangu chafu zisizofaa katika jamii.” Mbosso alinena.
“Ukweli Diva ni mwanamke mwenye hekima, tizama ndie yeye aliyenishawishi mie niingie kwenye Kilimo na uzuri wa Kilimo tumevuna tulichopanda, tumejenga nyumba nzuri huko Lushoto,Tanga. Tumenunua Mashamba mengi makubwa kwa ajiri ya mazao yetu. Tumefuga mifugo mingi, tungali bado tuna mipango mingi ya kimaendeleo, wazazi tafadhali mtusamehe na pia mtubariki ili tuyadumishe mapenzi yetu.” Mbosso aliongea akiwatizama wazazi wake Diva, wazazi ambao bado wamefura kwa hasira.
“Kama mnataka Baraka zetu mtazipata…… Lakini poleni.”Babaye Diva aliongea, wakati huo alitoka pale Sebuleni na kuelekea chumbani kwake, mkewe (mamaye Diva) alimfuata. Sebuleni pale walibaki Diva, Mbosso na Lavu mwanawao kipenzi.
*****
“Tupige simu Polisi ili waje wamkamate huyu mshenzi mpuuzi Diva na hiki Kimburukutu chake Mbosso.” Mamaye Diva aliongea wakiwa chumbani yeye na mumewe.
“Wazo zuri sana hilo my wife, umenikumbusha tulikwisha ripoti Polisi juu ya kutoroka kwa Diva miaka miwili iliyopita, wazo hili litatusaidia kuwaweka ndani ili walione joto la Jiwe.” Babaye Diva aliongea.
“Sharti tuyavunje mapenzi yao.”
“Uzuri Samsoni kijana anayefanya kazi Benki ya CRDB angali bado hajaoa, lazima amchukue Diva, haijalishi hata kama Diva amekwisha zaa mtoto.” Baba alinena.
“Tufanye juu chini kulivunja penzi lao Diva.” Mama aliongea tena.
“Hembu nipe simu yako ya kiganjani niwapigie Polisi, niwataarifu juu ya uwepo wa hawa haramia ndani ya nyumba yetu.”Babaye Diva aliomba simu, mamaye Diva akampatia, na baada ya kumpatia simu ilipigwa Polisi, Polisi waliahidi kufika nyumbani kwa babaye Diva haraka sana iwezekanavyo.
Nusu saa baadaye, polisi walikwisha kufika nyumbani kwao Diva (nyumba ya babaye Diva bwana Zine), Diva na mumewe wakiwa hawana hili wala lile wanajipa tumaini la kupewa msamaha kwa kadri ya juhudi zao. Walishtuka kuwaona Polisi wawili wakiwatia pingu mikononi mwao. Babaye Diva na mamaye Diva walifurahia lile tendo. Diva na Mbosso wakapelekwa kituo cha Polisi kwa kosa la kutoroka miaka miwili iliyopita.
“Lavu aliachwa mikononi mwa babu na bibiye, wakati baba na mamaye wakiwa chini ya mikono ya Polisi. Ubaya wa wazazi wake Diva tayari walikwisha panga mpango wa kumficha Lavu hadi pale watakaposikia kuwa Diva amelivurugavuruga penzi la yeye na Mvosso.Diva anayavurugavuruga mawazo na tena Diva anakata tamaa ya kuishi na Mbosso.
Uzuri wa mipango yao walijipa matumaini kwamba Diva angelikubali kuolewa na Msomi mwenzie mwenye kazi nzuri, mwenye maisha mazuri, mwenye cheo na sifa njema katika jamii.
*****
Leo ni siku ya tatu, siku ambayo Diva ametupwa ndani ya Jela ya Segerea, Mbosso naye pia ametupwa Jela, kila mmoja amewekwa ndani ya chumba chake, Diva amewekwa hapo akilalamikiwa kwa kosa la kuwaweka wazazi wake kwenye wakati mgumu mara baada ya kutoroka miaka miwili iliyopita, wakati Mbosso amewekwa hapo akilalamikiwa kwa kosa la kumtorosha Diva akijua kuwa kufanya hivyo ni kuvunja Sheria, akakumbushwa miaka miwili iliyopita aliiba, alimwibia mkoba mwana mama mmoja Kariakoo. Mkoba ulikuwa na pesa nyingi, vito vya dhahabu pamoja na mavazi ya huyo mwanamama.
Itakumbukwa kwamba yule mwana mama alikwenda kuripoti Polisi ndio maana Polisi walipata nguvu ya kumshitaki kwa makosa haya mawili. Kosa la kumuibia mwanamama vito vya thamani na pesa ni kosa ambalo Mbosso aliliona kuwa laweza kutibika haraka, japo yupo hatarini. Ule mkoba wenye mali za bei gharama ulikuwepo bado ungali umehifadhiwa kwenye gari ya mkewe mpenzi bibiye Diva. Pesa walizokwisha kuzitumia hawakuwa na budi kuzirudisha mara baada ya wao kufanya kazi kwa bidii na maarifa.
Kosa la kumtorosha Diva kutoka Dar es Salaam kwenda Kijijini Lushoto lilikuwa ni mzigo kwa Mbosso, japokuwa alijipa matumaini, liwalo na liwe, yote tisa kumi angelijitetea awezavyo. Mawazo juu ya Diva na mwanaye Love yalikiteka kichwa chake, alihuzunika na kusikitika. Kwa upande wa Diva angali yupo selo hataki kula wala kulala, anasikitika moyoni mwake mara baada ya yeye kufanya maamuzi ya kuja Dare es Salaam, anajilaumu na pia anailaumu nafsi yake, afanyeje basi? Hana la kufanya, anakubali kwamba amekosea japo anajipa matumaini kwamba atatoka tu, yeye na mwanaume wake mpenzi Mbosso. Mawazo yake Diva yanatua kwenye sura ya mwanaye Lavu na mumewe mpenzi Mbosso, mara anajikuta akiimba kwa hisia.
“Nimekumiss mpenzi wangu,
Nimekupenda mpenzi wangu,
Nitakuwa pamoja nawe,
wakati sio muda,`
Navumilia,
matatizo yana muda wake,
Nayo yatakwisha,
tuvumilie,
Navumilia,
Furaha ina muda wake,
nayo itakuja,
tuvumilie.
Kumbe wakati huo, wakati ambao Diva alikuwa bize akiimba kwa huzuni, akiimba taratibu kwa uchungu wa kutenganishwa na Mbosso pamoja na mwanaye mpenzi, ndio wakati ambao Mbosso pia alikuwa akiimba kwa uchungu ndani ya chumba cha gereza.
Nimekumisss Mpenzi wangu,
Nimekupenda penzi langu,
Nitakuwa pamoja nawe,
Wakati sio muda,
Navumilia,
matatizo yana muda wake,
Nayo yatakwisha,
tuvumilie,
Furaha ina muda wake,
Nayo itakuja,
Tuvumilie.
Kilikuwa ni kipindi kimoja kigumu sana kwao, kipindi cha huzuni ya kutenganishwa, hata wasijue hatima yao.
*****
Itaendelea
No comments:
Post a Comment