Tuesday, September 24, 2024

MBOSSO.. sehemu ya sita



 MBOSSO

Sehemu ya sita

Lavu aliachwa mikononi mwa babu na bibiye, wakati baba na mamaye wakiwa chini ya mikono ya Polisi. Ubaya wa wazazi wake Diva tayari walikwisha panga mpango wa kumficha  Lavu hadi pale watakaposikia kuwa Diva amelivurugavuruga penzi la yeye na Mbosso. Diva anayavuruga vuruga mawazo na tena Diva anakata tamaa ya kuishi na Mbosso.  Uzuri wa mipango yao walijipa matumaini kwamba Diva angelikubali kuolewa na Msomi mwenzie mwenye kazi nzuri, mwenye maisha mazuri, mwenye cheo na sifa njema katika jamii.            

                        *****        

    Leo ni siku ya tatu, siku  ambayo Diva ametupwa ndani ya Jela ya Segerea, Mbosso naye pia ametupwa Jela, kila mmoja amewekwa ndani ya chumba chake, Diva amewekwa hapo akilalamikiwa kwa kosa la kuwaweka wazazi wake kwenye wakati mgumu mara baada ya kutoroka miaka miwili iliyopita, wakati Mbosso amewekwa hapo akilalamikiwa kwa kosa la kumtorosha Diva akijua kuwa kufanya hivyo ni kuvunja Sheria,  akakumbushwa miaka miwili iliyopita aliiba, alimwibia mkoba mwana mama mmoja Kariakoo. Mkoba ulikuwa na pesa nyingi, vito vya dhahabu pamoja na mavazi ya huyo mwanamama.    

        Itakumbukwa kwamba yule mwana mama alikwenda kuripoti Polisi ndio maana Polisi walipata nguvu ya kumshitaki kwa makosa haya mawili. Kosa la kumuibia mwanamama vito vya thamani na pesa ni kosa ambalo Mbosso aliliona kuwa laweza kutibika haraka, japo yupo hatarini. Ule mkoba wenye mali za bei gharama ulikuwepo bado ungali umehifadhiwa kwenye gari ya mkewe mpenzi bibiye Diva. Pesa walizokwisha kuzitumia hawakuwa na budi kuzirudisha  mara baada ya wao kufanya kazi kwa bidii na maarifa.    

         Kosa la kumtorosha Diva kutoka  Dar es Salaam kwenda Kijijini Lushoto lilikuwa ni mzigo kwa mbosso, japokuwa alijipa matumaini, liwalo na liwe, yote tisa kumi angelijitetea awezavyo. Mawazo juu ya Diva na mwanaye Love yalikiteka kichwa chake, alihuzunika na kusikitika. Kwa upande wa Diva angali yupo sero hataki kula wala kulala, anasikitika moyoni mwake mara baada ya yeye kufanya maamuzi ya kuja Dare es Salaam, anajilaumu na pia anailaumu nafsi yake, afanyeje basi? Hana la kufanya, anakubali kwamba amekosea japo anajipa matumaini  kwamba atatoka tu, yeye na mwanaume wake mpenzi Mbosso. Mawazo yake Diva yanatua kwenye sura ya mwanaye Lavu na mumewe mpenzi Mbosso mara anajikuta akiimba kwa hisia.      

    “Nimekumiss mpenzi wangu,

Nimekupenda mpenzi wangu,

Nitakuwa pamoja nawe, 

wakati sio muda,`      


                 Navumilia,

 matatizo yana muda wake,

Nayo yatakwisha, 

tuvumilie,

Navumilia,

Furaha ina muda wake,

 nayo itakuja,

 tuvumilie.

Kumbe wakati huo, wakati ambao Diva alikuwa bize akiimba kwa huzuni, akiimba taratibu kwa uchungu wa kutenganishwa na Mbosso pamoja na mwanaye mpenzi, ndio wakati ambao Mbosso pia alikuwa akiimba kwa uchungu ndani ya chumba cha gereza.


Nimekumiss Mpenzi wangu,

Nimekupenda penzi langu,

Nitakuwa pamoja nawe,

Wakati sio muda,

Navumilia, 

matatizo yana muda wake,

Nayo yatakwisha, 

tuvumilie,

Furaha ina muda wake,

Nayo itakuja,  

Tuvumilie. 

Kilikuwa ni kipindi kimoja kigumu sana kwao, kipindi cha huzuni ya kutenganishwa, hata wasijue hatima yao.       

                                         *****    

        Zilipita siku saba, Diva na Mbosso  wametupwa Gerezani, Diva hakuhitaji kula, kunywa wala kulala, vivyo hivyo kwa Mbosso aliteswa sana, alipigwa ndani ya lile Gereza, baba na mamaye Diva waliwahonga Polisi wa Gereza wamtese Mbosso, Mbosso akateswa kwa vipigo vikali akihojiwa kwanini alimtorosha binti wa Tajiri? Kwanini amemuondoa nyumbani pasipo ruhusa ya wazazi wake? Mbosso alivumilia mateso ya Gerezani.    

          Diva aliendelea kugoma kula, kunywa na kulala, wazazi wake hawakuchoka kumtembelea Gerezani na kila walipomtembelea, walimshawishi Diva aachane na Mbosso .

 Walisema Mbosso hamfai Diva, Mbosso ni Jizi la Jiji, mtu anayewavunjia heshima na hadhi yao katika jamii. Itakuwaje kwa mfano mtoto wao msomi aolewe na Jizi maarufu ndani ya Jiji? Diva hakuwasikiliza, penzi la mbosso lilimnogea, alibaki na nadhiri yake Moyoni akijisemea; ‘Mapenzi hayachagui, hayabagui, mapenzi ni kumpenda umpendaye, haijalishi ana kasoro gani kiuchumi, kijamii, kisaikolojia na kadhalika. Mapenzi maana yake “Moyo” Moyo ndio hupende, Moyo ndio uchague, Moyo una macho yanayoona mbele kwenye mapenzi ya kweli, moyo una masikio masikizi ya mapenzi yenye udhati, Moyo una Moyo ndani yake na huo Moyo ni Moyo wa wawili wapendanao.  

          “Diva.” Baba alimwita Diva, na siku ya leo mamaye Diva pamoja na Sam  mzuri wamemtembelea Gerezani wapate kumshawishi. Sam mzuri amevalia Suti yake nyeusi pamoja na Tai yake nyekundu, wote kwa pamoja wamekuja kumtembelea Diva.     

       “Abee baba.” Diva aliitika kinyonge sana, amedhoofika, mwili wake umekonda, hatamaniki, yupo chini ya sakafu anawaza, na mawazo yake yote yapo kwa mbosso.       

     “Baba na mama wanahitaji heshima, ukiwaheshimu baba na mama utaishi miaka mingi yenye paradiso, raha na furaha, lakini usipowaheshimu baba na mama utapata laana.” Baba aliendelea kunena.   

         “Diva wewe unatokana na mbegu bora iliyobarikiwa na Mwenyezi Mungu, umeandaliwa maisha bora yenye elimu na maadili. sasa kwanini Diva msomi mzuri kama wewe unafanya kuwasaliti wazazi wakio? Kwanini mwanetu? Kwanini  hautaki kutuonesha heshima kwa uchaguzi na maamuzi yetu yalio sahihi?” Baba alimuuliza Diva, lakini Diva kimya analia kwa uchungu.  

          “Diva mpenzi, maisha ni maandalizi na maandalizi hayo yana nia pamoja na malengo, ukikosea maisha  ni sawa sawa na kuharibu nia na malengo yako yote, sasa tafakari, na baada ya kutafakari fanya maamuzi. Atakupeleka wapi huyo mwanaume mwenye tabia na jina chafu katika jamii? Atakufanyia  ambacho kina heri na afadhari katika maisha yako? Diva mwanangu usikosee wala usithubutu kufanya makosa.” Mamaye Diva aliongea. 

           Samsoni yule mtumishi wa benki akafungua kinywa akanena. “Haijarishi hata kama tayari umezaa na Mbosso, mimi nipo tayari kuishi na wewe. Sikiliza maneno ya wazazi ni busara na hekima ambazo kwako ni maandalizi mema katika maisha, ninakupenda Diva, wewe ni chaguo la moyo wangu unastahili kunikubali, ninastahiri kuwa nawe katika maisha haya yote.” Kelele zote ambazo wazazi wake Diva pamoja na Samsoni walizipiga, Diva alijigeuza bubu asitake kusikia la Ae au la  Bae. 

           “Kwanini kila neno jema tunalonena kwako haulichukulii na kulikubali Diva?” Baba alimuuliza Diva kwa hasira.    

        “Unataka tukupe au tukufanyie nini Diva upate furaha, ukubaliane na kauli zetu?”  Mamaye Diva aliuliza.   

         “Je, unahitaji kuendelea masomo  ‘School of Law’? Tupo tayari kukupeleka Ulaya au Amerika ukasome kipenzi, ilimradi uachane na Mbosso, tupo tayari kukupa nusu ya utajiri wetu ili uachane naye, Diva….. Sikiliza sauti zenye hekima.” Mamaye Diva alimwaga machozi. 

           “Haujibu?” Baba alimuuliza Diva kwa hasira, Diva angali anamwaga machozi, macho yake yamevimba kwa kulia, mashavu yake yamebadilika na kuwa mekundu, yameiva kwa kilio, masikini Diva ukimtazama utamuonea huruma.  

          “Kama hautaki kutupatia jibu sahihi juu ya kuachana na Mbosso, jua fika kuwa lazima tufanye kitu kibaya kwa mwanao  Love  utajuta Diva.” Baba aliropoka ili kumtisha Diva, ajabu Diva hakutishika, alibaki kimya tuli, tulivu.   

         Mara ghafla Diva akaugua Gerezani, akawa hoi taaban sababu ya kukataa kula, kunywa na kulala, Mkuu wa Gereza akawapigia simu mama na babaye Diva, haraka haraka mama na babaye Diva wakamkimbiza Diva Hospitalini, na katika kipindi hicho, Mbosso naye akaugua vibaya sana, akakimbizwa Hospitali aliyolazwa Diva. Hali zao zikawa tete, hawawezi wala hawajiwezi, madripu ya maji mikononi, madripu ya damu mishipani, madawa na masindano tele. Mamaye Diva alikuwa taaban kwa kilio akilalama inatosha sasa, inatosha, watampoteza Diva sababu ya mapenzi, watampoteza Diva sababu ya mwanaume wasiyempenda na yule ambaye wazazi hawampendi. Mama aliendelea kulia na kumsihi babaye Diva alegeze kamba wasije kumpoteza Diva.   

         Kwa shingo upande babaye Diva alikubali Diva atolewe Gerezani, ajabu Diva alipozinduka aligoma kurudi nyumbani kwa wazazi wake akidai anamtaka Mbosso yule aupendezaye mtima wake, la, sivyo atachukua maamuzi mengine magumu zaidi. Hofu ya kumpoteza Diva ilikuwa kubwa mama alimshawishi babaye Diva Mbosso atolewe Jela ili kumnusuru Diva asije akachukua maamuzi magumu. 

           Kwa shingo upande babaye Diva akafanya kumtoa Mbosso Jela akimkanya na kumuonya asijichanganye na Familia yao, asijaribu kuwa karibu na Diva, asichokoze Nyuki asije kupatwa na masahiba asiyoyategemea. Diva akarudi nyumbani kwa baba na mamaye, akala akanywa na kulala, bado aliendelea kupambana na vikwazo vingi kutoka kwa wazazi wake wakimshawishi aolewe na Samsoni.                                    *****

Itaendelea

No comments:

Post a Comment

I promise you

   I PROMISE YOU. (NINAKUAHIDI.) SURA  YA KWANZA. UBAYA WA POMBE. “Umenizingua job, umenizingua kwa muda mrefu sana mpenzi wangu…….kwanini l...