SEHEMU YA 1
MIE WADA.
Mie na kapu langu la matunda nalijibebesha kichwani nikiyanadi nadi mitaa ya nyumbani kwetu Moshi Bar. Ni kawaida yangu kupiga mbija na kelele za marudio ili kuita wateja wenye kila mioyo na mawazo yao binafsi: huyu ataniunga mkono, huyu atanikagulia kagulia kapu langu na asishindwe kunikosoa kisha ajipitishe kwa dharau utafikiri anayajua maumivu ya mie kukung’utwa na Jua la mchana,vumbi na kelele zao wenye mandinga.Yule mwenye moyo ❤ safi atayanunua bila longolongo.
“Embe, embe, embe.” Nilipigisha kelele kuita wateja na walaji wa tunda.
“Chungwa, chungwa, chungwa.” Niliita wateja kwa masauti ya juu kisha nikarudia na kurudia kuita tena pasina kufa moyo maana hiyo ndo' shuhuli inipayo ugali na tembele nyumbani.
Alright niite Wada binti Wande Mzaramo kwa kabila, mrefu kiasi mnene wa umbo, maji ya kunde ndo’rangi yangu majaliwa sina makuu mtoto wa Kizaramo. Dar es saalam ndo’ nyumbani kwetu nilikozaliwa, nilikokulia, kupata elimu na mahitaji yote ya kila wakati.
Mwenzangu sitaki kukuficha yalonikuta yasije kukukuta na wewe mtimilifu wa tabia ila kwa kifupi ujue tu shida hizi ndizo zinazotumaliza na kutuangamiza wakati mwingine sababu wewe mwenzangu unaweza kudhani umepata kumbe umepatikana mie nalidhani nimepakatwa kumbe nimekalia kuni la moto na kuni lenyewe mbona liliniunguza makalio yangu, nalijuta, we! Nisikuhadithie.
Kama kawaida yangu kupiga kite na kuita watu wangu wa kila siku, wale wapya na wale wa zamani: “Embe, embe, embe, embe. Kula embe upate afya.” Mrembo na uzuri wangu natangatanga na njia Barabara ya Moshi Bar kusaka wateja. Ngozi yanikomaa na kuupoteza uzuri wangu majaliwa sabababu ya Jua kunibananga
“Chungwa, chungwa, chungwa, chungwa. Kula Chungwa uongeze damu.” Kwani domo huchoka kupiga kelele? Kamwe! Mwili ndo’ uchoka kwa matembezi ya masafa marefu. Ninapokutana na mteja kama kawaida kwanza mteja uyaangalia matunda yenyewe kisha uyabinya binya na kuuliza bei ya tunda mie kazi yangu ni kumjibu “ Beba moja mia mbili, tatu mia tatu” kipenda roho nyama’ niambie basi niambie kama kuna mtu asiyependa kula sembuse kunywa?! Kula na kunywa utusogezea siku za uhai mbele. Kula na kunywa utufanya tupate nguvu na mauwezo ili tuweze kufanya kazi zetu za kujenga taifa.
Maana hata mimi ninashiriki kujenga taifa langu Tanzania na pia ninatoa Kodi na Billi kwa juu. Kodi ya pango langu Geto nilipopanga, chumba kimoja binti najitegemea. Billi ya maji na umeme vyote hivyo ninashiriki kikamilifu kutimiza wajibu wangu.
“Dada mbona ili Embe limeoza?” Napigwa swali na mteja wangu mpya.
“Halijaoza kaka limekolea sukari, ndo’ maana limekua tepetepe, rojo bin bokoboko.” Mie natetea biashara yangu ili nisimwangushe mteja wangu mwenyewe.
“Ok. Nitachukua matatu.” Mteja wangu baada ya kujiriidhisq ha na uzuri wa Embe langu akajichagulia ya kutosha. Nikamfungashia naye akanipa pesa yangu. Mie binti wa kizaramo nikaendelea kuinadi busness yangu.
“Embe, embe, embe! Chungwa chungwa chungwa!” Mitaa na mitaa iliyonilea niliizunguka pasina kukata tamaa. Heri mkono uende na chakula nikipite maana mgaagaa na upwa asile wali mkavu. Dakika ziliyoyoma hatimaye masaa, mara nipate mshikashika embe japo anunui, mara nipate mkosoaji ambaye atanunua baada ya kunikosoa na kunikasirisha, mara nipate asiye na kilomolomo aniunge mkono na biashara yangu iendelee.
(Tuonane kesho)
No comments:
Post a Comment