MAMA ALI
SEH EMU YA TATU
Ma’ Ali aliondoka nyumbani kwa mie Mamsapu na Babu yenu Pompo akaeleka nyumbani kwake, alipofika nyumbani kwake kabla hajalitua tungile bichwani alishituka kumkuta Mjomba Bahati kasimama Langoni na lango hilo kakokomea kwa bonge la kufuli yaani kufuli jibaba😂.
Mjomba kajaa kisirani, 👿mahasira kifuani, kakunja paji la uso sie tusijue tatizo nini jamani!?Mjomba kumuona Ma Ali kaanza kunena kwa jaziba;🔊
“Nimekuvumilia sana Ma’ Ali nimekuvumilia hatimaye nimefeli. Leo nimeona wacha nifanye maamuzi na maamuzi yangu kamwe sirudi nyuma, sitetereki nikinena nimenena.” Mjomba hakumpa nafasi Ma’ Ali atue tungi la maji chini sakafuni.
“Makubwa madogo nisiyasikie, univumilie lipi? Usinivumilie lipi? Tamka tuyachambe na kuyachambua.” Ma’ Ali katua tungi la maji chini, ajifunga kanga kiunoni ambetulia Mjomba domo la dharau. 'Mfyuuuu'”
“Huu ni mwaka wa ngapi sasa umeketi ndani ya Pango hili pasina kulipa kodi ya Boma?” Mjomba kauliza kisha kajibu mwenyewe‘Imepita miaka saba sasa Mwanamke wajiburudisha kama Malkia, watupigishia kelele nyingi usiku, wamgeuza mumeo Punda mtumwa, matukano na mapigiti wamgaia. Ma’Ali embu tupishe tupite ruhusu wapangaji wengineo waingie.” Mjomba alitua nukta.
“Ati nikupishe upite wengineo waingie! We uogopi! Mjomba Shetwaini mwenye tamaa kakuvuruga na mvurugo huo nasema Babu niondolee kimbunga kabla sijayapandisha yakapanda Mashweitaini.” Ma Ali alikasirika.👿
“Umpandishie nani? Uliijenga weye hii nyumba?” Mjomba kauliza.
“Nikuulize weye mwenzangu ulisaidia kuchomeka fito pembeni ya hili Boma? Umewahi ezeka makuti na mbavu za umbwa juu ya hili pango? Mwenzangu umewahi kokomea lango hili lililoliwa na mchwa likaketi na kusimama vema?" Mjomba aliulizwa maswali magumu kuyajibu.
“Babu, wajimwambafai wakati weye mwenyewe ni kama mie mpangaji, hukushiriki kuijenga nyumba hii utanifukuzaje kwa mfano? Umeketi miaka saba kuilinda nyumba. Je, weye mlinzi utanifukuzaje na kuniondoa? Punguza shobo na domo tamaa.” Ma Ali alimsukuma Mjomba Bahati pale langoni Mjomba akapepesuka na kudondoka chini puuuu haraka akafanya hima kujisimamisha maana alijua aibu itamjaa iwapo Inzi (Majirani wanoko) watamkuta chini kajaa tope.
“Walifunga lango eh!” Ma Ali alimkemea Mjomba.
“Bibi eeh! Nakwambia hama nyumba hii nimekuchoka.” Ma’ Ali akamsogelea Mjomba Bahati pale aliposimama, akamvaa na kulikamata shati la Mjomba akalikunja kwa nguvu.
“Wanijua mie au wanisikia? Embu nipe ufunguo mpya wa hilo kufuli ulilolikokomea langoni.” Ma’ Ali alimkemea Mjomba Bahati.
“Sikupi ng’o Ulie tu!’Mjomba alitia madoido na nyodo.
“Nitayapandisha yakapanda, embu nipe ufunguo.” Ma’ Ali hakutania.“Sikupi embu niwache mie sio mumeo.” Mjomba aliongea kwa kutetema.Nguuuuu Ma’ ali alimrukia kwa kasi Mjomba akajipigisha kichwa juu ya komwe la mjomba, Mjomba alilegea na kuona maruweruwe pamoja na nyota nyota machoni.
“Sema, utanigea ufunguo au haunigei? Ma’ Ali alimuuliza Mjomba ambaye Safari hii damu zilimchuruza puani, mkojo ulinuka ndani ya suruali. Alitetemeka na kuogopa kufa.
“Ichukue Umbwa weye, nakwambieni kama kuhama utahama kwa lazima.” Mjomba aliuchomoa ufunguo wa kufuli jipya akampatia Ma’ Ali. Aliogopa asijeendelea kuchezea kichapo.
“Weye gogo utashindana vipi na jike la shoka? Hata uende Polisi nakwambieni Pango hili sihami, kama ni kuhama utaanza weye kuhama.” Ma’Ali aliongea akamwacha Mjomba aondoka Pua yatema damu asijue wapi aeleka si kwa kizunguzungu kilichotamani kumdondosha Mjomba chini Puuuu azime mazima.
.........
“Kama ni suala la kuhama babu tuhame wote, sio jitu linakuja kunipangia Maisha ati nilipishe lipite.” Ma Ali alilalama mara baada ya kumponda Mjomba bahati.
“Mpuuzi, atanishurutishaje nihame wakati ajua Boma hili sote twakaa bure, hatulipii! Baba mwenye boma hajishuhulishi na Bomale kalibwaga na kutuwachia sie hoehae tuketi bure. Hujuma hizi aah!” Ma Ali aliongea, kasimama langoni kwake kutazama mbele ajitikisa mfano wa tanda la mneso kawaona Polisi wawili waja usawa wake. Kwani alitishika? Aanze tu!
“Kaona haitoshi ndo kaniletea Polisi? Ili iweje? Namwambia hivi mie ni chuma kisichotoa kutu nitapambana nao Bingo kuibuka” kimya kilitawala, kasimama kama ubua, mikono kiunoni macho yake yameiva wekundu wa pilipili kichaa.
“Hodi hodi Mamalao!” Polisi mfupi mnene mwenye mustachi wa Kihindi kabisha hodi.
“Karibuni. Niwasaidie nini cha mno ndugu Polisi.” Kabla ya salamu Ma' Ali kakimbilia kutoa msaada.
“Sie ni Polisi kutoka Kigogo ya Mburahati, twambie mwanao yupo?” Polisi mfupi mnene katikisa kirugu na kuuliza.
“Mazito jamani! Ali mwanangu kawafanyia nini Polisi hadi kumtafuta?” Pozi lilimkauka Mamaye Ali. Alibaki kuduwaa na kushangaa.
“Hatumjui mwanao lakini ujue tu Keisha haribika na uharibifu wake ipo siku majuto mjukuu.” Polisi mrefu mwembamba aliyeshika Mgobore aliongea.
“Tujibie yu wapi Ali Mwanao?” kaulizwa tena.
“Nisijue mie! Labi Shule kaeleka.” Ma’ Ali alijichanganya.
“Usijuwe weye wapi kaeleka tena utujibie Shule kaeleka ina maana mwanao ni Mwanafunzi? Polisi mrefu kauliza.
“Hilo nalo jibu.” Ma’ Ali kajibu nyodo na vidole vya taarabu👌 kawabinulia.
“Mkanye mwanao, mfunde kwa adhabu na mapigiti, mwambie Jela sio pahali pake.”Polisi mrefu aliongea na kushauri.
"Kisa nini? Waja kuniweka mie roho juu ya kitanzi? Nisiujue ubovu wa Ali.” Ma’ alitamani kujua kisa chenyewe.
“Sikia Ma’, mwanao atamani uteja na uteja ataupata, awacha kuenenda shule awaza biashara ya dawa za kulevya. Hilo twalijua, tafadhali mkanye mwambie Jela sio pahali pake.” Polisi mfupi aliongea kwa hasira.
“Eh! Mola wangu niambie ni wapi nakosea kumlea Ali mwanangu!!? Chakula nampa ala asaza, mavazi namvisha, pahali pa kulala nampa akiugua gharama nagharamia. kwanini aikataa elimu ya darasa? Aibu yangu kuambiwa dawa za kulevya atumia na kuuza. Nitaificha wapi aibu ya mie?” Chozi lilimdondoka Mamie Ali Polisi waliondoka pasina kuaga walimwacha Ma’ Ali kapooza mapozi na hasira kumyeyuka mfano wa barafu Juani.
Basi mwaya Ma’ Ali ujasiri wote ulimdondoka, manguvu yake mbele ya Polisi kitu haba, hana ae wala bae, kageuka Buuu shuzi licha ya kuimba kumbe kucheza hawezi. Haki! Wahenga walisema uchungu wa mwana Mama aujua. Hapo Buguruni Rozana kuna Bonde, kuna Bonde kubwa la mto Msimbazi pamoja na mfereji wa maji taka yatokayo bafu na choo. Nakwambieni Vurugu ilochimba pahali hapo mwenzangu! Utaogopa. Mama aliyetambulika kwa jina la Ma’ Dimoso kamletea vurugu Dalali Deo amdai chake na chake lazima alipwe.
“Babu ungenipasha ukweli majanga nisiyapate.” Ma’Dimoso kamkwida roba Dalali Deo Inzi kibao zapiga kelele za shangwe kama mazuri yaoneka.
“kwani Nilijua? Nilijua pembeni ya Mto Msimbazi kuna Majanga? Bibi sometimes ni wewe kujiongeza sio kunifanyia vituko nyumbani kwangu, tambua mie nimeoa na watoto ninao.” Deo alijitetea.
“Mie pia nina mume na familia ninayo wadhani najipendekeza kwako un’tongoze? Deo ukitaka haya yaishe tafadhali nirudishie Mapesa yangu.”
“Kiendacho kwa Sangoma hakirudi, Mama cha msingi ni wewe kumtafuta Baba mwenye Nyumba myapangue yaishe.”
“Baba mwenye nyumba kaukimbia Mji na kuutoroka nisijue wapi kaeleka baada ya mafuriko kuisomba nyumba yake. Kila chema nilichojaliwa kimesombwa na mafuriko: Tv yangu, Masofa ya bei gharama, Feni, fridge, Mtungi wa gesi vimeharibika ilihali hata mwezi sijaumaliza .Sema wataka nikamdai nani Laki tatu zangu ikiwa mwenye nyumba kajitorosha makusudi?” Mama Dimoso aliongea kwa huzuni.
“Ndo’ Uje kunidai mie? Kwani mie nilikusaidia kuuandika mkataba? Bibi hapa mjini Bana jiongeze ukishindwa kuhama Bondeni ukuje tuishi na mie mke wa pili nijiongezee.” Dalali alimjibu jeuri Mama Dimonso.
“Wasema nini Dalali!?”🥴😡Mama Dimonso aliwaka kama kifuu cha Nazi.
Ghafla upande wa pili ilisikika sauti ya kilio cha kuomba msaada.
“Nasema achia, achia mkoba huu.” Ali Alipiga kelele.. Mama Dimonso, Dalali Deo na Inzi wengine waligeuza shingo kueleka kule sauti yapigwa.
“Sitaki Ali, sitaki kuuwacha mkoba wa mie.’ Maimuna binti aliyechezwa ngoma majuzi hapo, alipigisha kelele, kaushikilia mkobawe kwa manguvu yote, manukato yote alojifukiza yalimpwaya sio kwa kutetemeka kule.
“Usinizingue.” Ali kaukunja mkono shoto wa Maimuna kaushika kwa nguvu mkoba wa Maimuna Maimuna vivyo hivyo asitakekuuwacha mkoba wake wenye Pesa lukuki pamoja na simu ya bei gharama alopewa kunako kigoma chake, kigoma cha Mwali tumfunde. Ali akafanya kumpiga ngumi nzito Maimuna, Mai aliona wenge na nyotanyota kichwani, pigo lile zito lilimfanya Mai apoteze nguvu na kuwacha mkoba uliotua mikononi mwa Ali. Ali yule mwana mpumbavu akafanya tendo ovu haraka akamzoazoa Maimuna na kumbwagaza Mtaroni, Mtaro ule wenye maji taka. Inzi wote walipigwa na butwaa kumwona Ali akimtendea tendo jambo ovu Maimuna.
“Mwana kalaaniwa yule!” Deo aliongea.
“kaharibika jamani, mbali na utumizi wa dawa za kulevya afanya uporaji.” Ma’ Dimoso alichangiza. Safari hii kamuachia Deo, huruma zote juu ya Maimuna aliyetupwa ndani ya tope na uchafu wa chooni.
“Tusionekane tumeshindwa kulea, wizi watendeka mchana kweupe kadamnasi yaangalia. Jamani bangi mbaya.” Deo aliongea.
“Embu tujishuhulishe kumtoa Maimuna ndani ya dimbwi lenye tope binti asije dhulika. Twamtazama kama manyani yasotoa msaada.” Mama Dimoso alishauri.
“Ali kakimbia, aitwe Polisi, Jela yamuhusu sio kwa ubovu ule.” Deo aliongea kwa hasira.Wawili wale wakazama topeni kumtoa Maimuna aliyelia kwa uchungu. Maimuna kashauriwa aeleke Polisi kumshitaki Ali. Jamani shilingi laki tatu sio pesa mtoto, mkobani kulikuwa na simu janja (Smart phone) ambayo Maimuna aliinunuliwa kwa bei ya kutupwa, bei gharama vitu vyote hivyo vimeliwa kiboga? Hapana! Roho ilimchoma maimuna uchungu ulimvaa binti yule haraka akaeleka Kigogo Polisi lazima Ali akamatwe.
Siku mbili baadaye Polisi mfupi mwenye kirungu na Polisi mrefu mwenye Mgobole walimkamata Ali wakamtia ndani na jalada wakamwandikia kesi ilianza kucheka. Nyie! Uchungu wa mwana usikie tu Mie Mamsapu nalikuwa Mekoni natwanga na kupeta karanga nijipikie kisamvute ghafla nalishtuliwa na kilio cha mwanamke mwenzangu akilia kama mwana mdogo alopigwa, akilia kwa machungu, maumivu moyoni, jamani! Naliumia mie.
“Kulikoni mwenzangu walia kama Ngoma ya Kigodoro inopigwa mtaani, Machozi yako ya thamani wayapoteza, nini cha mno Shoga’ngu?” Nilimuuliza Ma’Ali.
“We acha tu Mamsapu mazito yamemkuta Ali mwanangu.” Ma Ali aliongea kwa machozi.
“Ali huyu huyu mkataa shule? Kayazoa yapi tena huko atutie hofu sie tumpendao?”
“Kuzaa uchungu, kulea kazi Shoga’ngu naumia mie.” Ma Ali alilia mie kazi yangu kumtuliza nikijua fika kilio kinaukomo wake.
“Tusionekane tumeshindwa kulea mchana kweupe wizi watendeka, kadamnasi yashangaa, jamani! Bangi hizi!” Mama Ali alilia sana mie kazi yangu kumtuliza kilio chenye kikomo. Kwisha kulia na kunyamaza nikamwazima masikio Mwanamke mwenzangu dodoso anidodose.“Nalimshauri Ali kuishika elimu, Bahari iso na mwisho, Bahari inayozoa makosa, uchafu na Madhambi yote ya walimwengu, Bahari inayosafisha panapochafuka, inayowapa faida wengi na kuufuta umasikini lakini Ali mwanangu haitaki elimu Bahari.” Mwanamke mwenzangu alilia akanena tena:
“Juzi kati Polisi wamenitembelea na kunionya juu ya tabia mbovu aikumbatiayo Ali sikuamini kama ni kweli mwanangu Ali kaoza na kuharibikia Dawa za kulevya ajabu leo kuambiwa katiwa pingu Korokoroni! Nalia shoga’ngu, nalia mie mwanangu Ali.” Mie Mamsapu naligeuka msikilizaji nalimsikiliza Ma’Ali.
“Jela, Jela yamsubiri mwanangu nifanye nini mie?”alijiuliza.
“Ushaenda Polisi kunena nao?” Nalimhoji.
“Nishafika shoga’ngu, nishaambiwa Ali kamtendea ubaya Maimuna Mwali Mzaramo alovunja ungo juzi kati.”
“Kamtendani?”
“Mwenzangu baada ya kisa mkasa, baada ya chanzo kitendo. Hata nisijue nianzie wapi kukuelezeni. Polisi nimeambiwa Ali kayakumbata makosa lukuki:Kujerui, kuuza dawa za kulevya, kupora, kunyang’anya, na kuiba kwa kutumia silaha zenye ncha kali.. Nameambiwa Maimuna kaporwa simu ya bei gharama Pesa mingi zaidi ya laki tatu.”
“Uwiii! Mazito kusikia.”
“Yaani!” Ma ‘Ali aliagua tena kilio.
“Shoga usilie bibie, penye dhiki pana faraja, hakuna marefu yanayokosa mwisho,dawa ya deni kulipa na dawa ya matatizo kuyatatua…..”Nalimfariji Ma’ Ali’
“Mwenzangu, mie nipo njiapanda nikizubaa mwanangu atadondoka kama tunda bovu juu mtini, nitamlilia nani mie Masikini.” Mwenzangu alikonda kwa malalamiko.
“Nitakusaidia mwaya, tumgoje Babu yetu pompo akuje toka kazini tumweleze shida yetu atusaidie,” Nalimpooza Shogangu Ma’Ali.#
(Mmh! Mazito! Mambo yasije kumpwerepweta Ma'Ali. Embu ngoja tumgojie Babu yenu Pompo akuje mazito tumdodose).
No comments:
Post a Comment