Friday, September 20, 2024

DONDA LA WIVU sehemu ya pili.

 


SURA YA PILI

TUNU.
                 Kwisha kupata mlo wa mchana, mzee Jamali akapata nguvu, afya na uzima, mkewe mdogo ni mjuzi wa kuyapika mahanjumanti, madikodiko, mapochopocho manono manonozi, mlo ule ulimpatia sio nguvu pekee bali pia matumaini ya kuishi kwa raha na furaha , yote haya ni mapenzi apewayo na mkewe Tunu mke wa pili mara baada ya mke wake wa kwanza kuaga dunia.

                 Mzee Jamali alifanya uamuzi wa kuoa mke wa pili ili kujiondolea mawazo na uchovu, Tunu alimpendeza machoni, basi  mzee Jamali akamuweka ndani, akampamba, akamremba na kumkwatua, kabla ya kuwa hivi alivyo sasa mzuri  wa kunenepa binti alikua yu dhaifu, amekonda na kukondeana. Amekonda na kuchakaa kama gofu lililoachwa na Mkoloni. Haki! Huko nyumbani kwao Lukozi Tunu aliiishi maisha ya kifukara sana. Nikwambieni mpenzi msomaji kwa mara ya kwanza kama ungelipata nafasi ya kumuona, jamani! Usingeli mtamani, mmmh! Kukonda huko sio haba, maisha magumu Vijijini.

                 Kwa juhudi za mumewe, Mzee Jamali Tunu alianza kuboreka kimwili, afya yake iliyoporomoka kwa sasa ilianza kuimarika na kujengeka yote sababu Tunu hakupata kulala njaa hata siku moja ndani ya nyumba ya Mzee Jamali kila kitu alichokihitaji Tunu alikipata, hakuna  alichoomba Tunu akakikosa. Uzuri wa nyumba ya Mzee Jamali kuna bustani ya mboga mboga na matunda ambayo yamekuwa msaada  mkubwa katika kuiboresha afya ya Tunu.

                 Lukozi kijijini kwa babaye na mamaye shida ziliwatafuna, umasikini uliwameza, tabu ziliota mizizi, mahangaiko yaliota mashina masumbuko yalichipua na kumea Maua, mara leo wangelibahatika kupata mlo, mara kesho wangelikosa, leo wanywe kesho wasinywe, leo waumwe kesho wapone, leo wavae kesho je? Tabu juu ya tabu, pesa ngumu kupatikana,  mahitaji yao muhimu ngumu kuyapata, umasikini nao tayari umekwisha gonga hodi na kuingia kwa lazima.

                  Looh! Umasikini mbaya, yaani umeamua kugonga hodi hadi kwenye kijumba nyasi chao Tunu, kijumba nyasi kilicho shikiliwa na makuti pamoja na mbavu za Umbwa, dhiki tupu. Ingawaje wazazi wake Tunu walimshukuru Mwenyenzi Mungu muweza wa yote mara baada ya Mzee Jamali kujitokeza kumposa yule binti.

                     Kuolewa kwa Tunu kuliyapooza yale machungu ya umasikini wa familia ya baba na mama Tunu, kuolewa kwa Tunu ilikua ni  kupunguza mzigo wa kumlea Tunu ambaye wazazi wake waliokumbwa na umasikini ulio wakalia hadi visiginoni sasa waliutua ule mzigo mzito wa kumwangaikia Malaika wao.

                     Ndio maana ninasema walimshukuru sana Mwenyezi Mungu maana baada ya dhiki faraja tabu na shida ni jambo la mapito. Wanadamu hawakuumbiwa maumivu ya milele. Uzuri wake  mara baada ya Tunu kuolewa amekua ni msaada mkubwa sana  kwa wazazi wake, akihitaji chochote kile cha kuwapelekea wazazi wake huko Kijijini kwao Lukozi binti hanyimwi,  binti anapewa tena anazidishiwa mara mbili zaidi ya kile alichoomba. Anapewa pesa, anapewa nafaka, anapewa zana za kilimo, anapewa zawadi nyingine nyingi  za kuwapelekea wazazi wake, baba na mamaye, huko kwao kijijini Lukozi kijiji kilicho ndani ya mji mzuri wa Lushoto Tanga.

                     Kwisha kupata mlo mchana wa leo, mzee Jamali alitoka ndani ya chumba chake cha kupumzikia. Alikua amejilaza kwa zaidi ya masaa mawili alipata wazo la kwenda kulitizama shamba lake, shamba alilopanda karoti nyanya na kabeji, ana hamu ya kuliona shamba lake, ana hamu ya kuona namna gani shamba lake linavyomea na kupendeza, yeye ni mkulima kilimo kwake ni utukufu anajua tena anatambua kuwa kilimo ni uti wa mgongo, asiefanya kazi asile, jembe halimtupi mkulima, asie na shamba kwake kuna njaa.

                     Keisha ukosha mwili wake kwa maji safi salama maji yenye umoto moto, kapambwa kwa kanzu nzuri yenye rangi ya kijivu tena uzuri wa Bi. Mdogo Tunu kampamba mumewe kwa kumvisha koti  jeusi alilo linyosha vizuri  kwa pasi ya makaa, ajabu hata kulipiga pasi lile koti la mumewe Tunu kashirikiana na Ally mwanae.

                    Karibu njia yote Mzee Jamali aliyawaza mapenzi manono apewayo na yule binti aitwaye Tunu binti aliyefundwa kafundika kwenye unono wa mahaba. Kati kati ya mawazo yake mzee wa watu anabadirika na kumshuku kimoyo moyo mkewe Tunu anamshuku kuwa Tunu anamsaliti tena anamsaliti kwa kutembea na mwanae  wa kumzaa Ally.

                   Akawaza na kuwaza tena Mzee Jamali, usiku wa jana, usiku wa mahaba yao, Tunu alikua akimpepea pepea Mzee Jamali, akimpepea kwa kutumia ungo mzuri safi wa kupepetea mchele ili Mzee apate usingizi alale unono.. ….Leo tena kabla hajaondoka kwenda kulitizama shamba lake Mzee Jamali anakumbuka heshima na adabu ya huyu binti, ile anamvisha Baraka shea yake, binti alipiga goti chini akamsihii mumewe waende pamoja huko kwenye bonde la Kidundai lilipo shamba la Mzee Jamali, ajabu Mzee Jamali hakutaka kuongozana na mkewe, akamweleza Tunu akamwambia, sio mbaya kama atabaki nyumbani apumzike, hatochelewa kurejea.

                   “Lakini binti anaonekana kuyajua mapenzi kwangu mie, nilie mtoa Kijijini kwao kwenye umasikini wa kutupwa?” Yalimjaa mawazo Mzee Jamali, akachanganywa changanywa  na hayo mawazo hatimae akachanganyikiwa.

                  “Mmh! Hivi ndivyo walivyo mabinti wa siku hizi? Yawezekana Tunu analazimisha mapenzi kwangu, ajifanya kunipenda wakati huo huo  hataki kuonesha darili za kunitema. Je, Tunu ananipenda kweli  au anampenda Ally? Mmmh! Hapana sikubali kuona hali inavyoendelea lazima niwakomeshe wawili hawa wanao nipumbaza akili zangu.”  Aliwaza Mzee jamali , aliwaza akiendelea kupanda na kuteremka kilima cha Kidundai.

Itaendelea 

No comments:

Post a Comment

I promise you

   I PROMISE YOU. (NINAKUAHIDI.) SURA  YA KWANZA. UBAYA WA POMBE. “Umenizingua job, umenizingua kwa muda mrefu sana mpenzi wangu…….kwanini l...