Thursday, September 12, 2024

JUTO

 JUTO




1

“Mume si ni wake?”

“Ndio, tena kaolewa yupo kwenye ndoa ya fahari, raha na karaha.”

“Sasa kama Mume ni wake si ndiye anayemjua vizuri sana zaidi ya hao Shogaze wanaompa taarifa nyingi ambazo hajui ipo siku zitamfirisi?”

“Mwenzangu, Dunia hadaa elimu shujaa. Kama angelijua hao wakina Elizabeth, Lisa na Anjelina (Majina mazuri kutamka) ni matapeli, waongo na wenye nia mbaya kwake asingelithubutu kuanzisha Ushosti nao. Wamemlia taimu, alizubaa na hatimaye yamemkuta yale asotarajia.”

“Katoka Kijijini, sorry! Katolewa Kijijini guu limejaa sagamba hadi kwenye visigino, hajui kulitumia jiko la Mchina  sembuse kulitumia Jokofu tu mbona ilikuwa shuhuli! Yaani Bibie anaweka viatu kwenye Fridge akijua hilo ndo’ Kabati, Teh teh teh (Nacheka mie) Ushamba mtupu, Mumewe Denis kachukua jukumu, jukumu la kumfunda akafundika. 

Lily akatafutiwa Mwalimu, binti mdogo wa kumfunda kazi mbalimbali za pale nyumbani. Kungwi akamfunda akafundika. Akamfunda kupika Wali uliokoozwa tui la nazi na mchanganyo wa maziwa, si unajua tena Lily hajui kupika Wali, akipika basi tegemea kula boko boko, kwao washaazoea kula ugali na hiyo mboga ya mrenda, kisamvu, bamia na nyanya chungu. 

Kungwi akamfunda jinsi ya kupiga pasi nguo za Mumewe, kufua tu alikuwa hajui. akafundwa jinsi ya kupuguta deki, si unajua kuwa huko Kijijini kwao Lukozi hawapigi deki zaidi ya kufagia? Kungwi akamfunda mengi hayo machache yabaki kuwa mfano. Na uzuri wa huyu Kungwi aliyemjua kwa jinale ‘Uaridi’, hakuwa msiri, mtoto akafundwa namna ya kumpeti peti Babu wawapo chumbani, wawapo Sebuleni na hata bafu kukoga. Any way Mahaba popote, popote pana Mahaba.

“Kungwi Uaridi alikuwa na umri gani?”

“Kumi na minane kashafundwa mambo ya Kizaramo kafundika, binti mcheshi, muongeaji mzuri, mpole usoni, mzuri machoni utampenda rohoni, humwachi hasirani.”

“Tuseme Lily alikuwa na umri gani?”

“Bado mdogo kinda kindaki si zaidi ya kumi na sita japo si unajua tena Mwaya watoto wa siku hizi wanakua haraka, wanatanuka na kuongezeka haswa, sura zao zinang’ara kama Lulu, maumbo yanawatamnisha hata Malaika, sauti tu hapo baasi mwenzangu usiongee.”

“Bado sijajua kuhusu Denis, hembu nitobolie nile nifaidi.”

“Punguza uroho Bibie, Mume wa mtu umjue kwa faida gani?  Kwa ufupi yeye ni Dereva, Dereva wa Magari yazungukayo Jiji, route zake ni Vingunguti, Mnazi Mmoja, Ubungo, Gongo la Mboto, Temeke na Kawe. Yaani ni Safari tupu, Safari za mara kwa mara, Safari za kuchosha mwili na akili, Safari za kumdamsha  Alfajiri na kumlaza saa sita usiku manane. Loh! Mwanaume kazi, lakini afanyeje? Hana jinsi, wacha apigike ili avune apandacho.

“Umri  wake vipi?”

 “Bibie mbona wamchunguza sana Mume wa mtu? Wivu kidonda ukiushiriki utakonda.”

“Eeeh! Nawe sina nia hiyo, mtu mwenyewe simjui wala sijamwona,  ndiwe unisimuliye Story hii tamu Mashallah!”

“Basi tulia nikupe vitu, vitu hadimu japo Dunia ina mengi ya kujifunza, mengi ya hayo watu huyaficha na kuyafanya yawe siri, siri za ndani, siri zao wenyewe, siri haina siri, siri ni ya wawili, watatu siri imefichuka.”

“Mmmh! Mwenzangu, maneno mengi kama Chiriku.”

“Wacha niseme tu nina haki ya kuongea, nilivyo Mbea nina kila kitu cha kukueleza, tena ujue kuwa Denis ni mtu mzima, Jibaba lenye miaka 30 hivi, uzuri wa Denis hana papara, ametulia baada ya kumpata Lily, lakini Lily masikini binti huyu kama angelijua kuwa Mjini shule wala asingeliujenga Ushosti na hawa Wahuni wa Jiji.”

“Sijui  Hadhira yangu tupo pamoko? Au ndo’ mawazo ya kumpata Denis Mume wa mwenzio?”

“Ni pamoja nawe Fanani, lakini wanitia kichefu chefu unaponitokezesha kwa mtu nisiyemjua nisiyemwona, jaribu kuacha kusisitiza juu ya mtu hewa mbele yangu. Kama ni kupenda naweza kumpenda yeyote japo nimjue au nimwone, sio mtu kapa, huko ni kujisumbua tu. Ok, nisimulie wangu.”


(Ngoja niketi kitako nikuburudishe)

No comments:

Post a Comment

ZEE LA ZAMANI

  SEHEMU YA KWANZA. HOTELINI Ndani ya Hoteli Paradiso katikati ya Jiji la Mzizima (Dar es salaam) ZEE LAZAMANI akiwa na Mwanagenzi wake JAN...