Saturday, September 21, 2024

JUTO sehemu ya pili


                                    JUTO

  Sehemu ya pili

             Basi nakwambieni mara baada ya Kungwi Uaridi kumaliza Semester  yake akalipwa ujira naye akaondoka akaenda zake, tayari keisha mfunda huyu Bibie Maisha ya Mjini, kamfunda mafundo yote, kamfunda uvumilivu, ustahilivu, unyenyekevu, utulivu, upendo, mahaba na vyote muhimu katika ndoa. Tayari Bibie kafundika hata Mumewe akafurahi na kujisifu kwa kuchukua hatua njema, uamuzi bora na wenye busara kumtafutia mkewe Mwalimu wa kumfunda mafundo ya Mwanamke.

Miezi miwili mitatu mara baada ya Kungwi Uaridi kuondoka pale nyumbani kwa Bwana Denis, nasema nyumbani kwa sababu Denis tayari kashajikamilisha, ana nyumba yenye kila kitu muhimu ndani, hakipungui kitu, ukitaka unga, mchele, mafuta, nazi, hoho, nyanya nakadhalika Bibie hukosi hapo, vyote hivyo huletwa na huyu Mume aliyezaliwa Pemba akalelewa Pemba na kuja kuishi Dar es salaam. Zamani, zama za utoto na utu uzima alikuwa akiitwa Ally Hassan, lakini mapenzi, mapenzi jamani yakamfanya huyu Mpemba abadili Dini kutoka kwenye U-Ally Hassan akaenda kwenye U-Denis.

Lily alijiona mpweke, mpweke aliyepungukiwa kitu kimoja muhimu maishani mwake, Mtu wa kuongea naye, mtu wa kucheka naye, mtu wa kubadilishana naye mawazo. Nyumba yao ni kubwa ina vyumba sita, Sebule (Sitting room) Jiko, Choo na Bafu ndani kwa ndani, pasina kusahau chumba cha stoo na chumba cha faragha (maongezi). Miezi mitatu aliyoitumia kufundwa na huyu binti (kungwi) aitwaye Uaridi tayari ilikwishafikia tamati, alimzoea sana Kungwi Uaridi ajabu leo hamwoni mtu wa kumzoea. Masikini, unyonge, upweke na mawazo yalimtibua Lily.

Kama nilivyokwambieni hapo awali, mumewe ni mtu wa ‘Mishe mishe’ (Mizunguko ya hapa na pale) hana muda wa kutulia nyumbani ili apate kuzungumza na Mkewe, hata siku za Jumamosi na Jumapili Mwanaume yupo bize kutafuta pesa. Kwa bahati nzuri pesa anazipata, Bosi anamlipa kitita chake, ndio maana amejenga nyumba yake mwenyewe, kilichobaki ni kuwekeza haba na haba ili anunue Coster yake mwenyewe aimiliki na kuizungusha ndani ya Jiji. Upweke! Upweke binti aliuona ni kama sumu, hajazoea upweke, alizoea kuketi Pahali na watoto wenziwe zama zile bado hajaolewa akicheza cheza rede, akiruka boi, akifukuzana na mabinti wenziwe. Wakicheza kombolela, wakienda kisimani kuchota maji au kufua nguo mtoni, tena wakikata kata kuni Mwituni wakiokota okota Mayai ya Ndege na matunda Mtini. Loh! Hajazoea upweke japo ndani ya nyumba yake kuna Televisheni, hata hiyo Televisheni anaona haimbadilishi fikra zake. Televisheni inazungumza na kujijibu yenyewe, yeye ana maswali kedekede ambayo Televisheni haiwezi kumjawabia. 

‘Aaagh’ alijichukia, yanini kukaa kibubu wakati Dunia sio ndogo, Dunia ina watu wengi ajabu. Basi Mwanamke akatoka ndani mchana wa siku moja Jumapili tulivu, siku hiyo Soko la Ilala hufurika watu wenye hitaji la mahitaji mbali mbali ya kimaisha, hajatoka ndani muda mrefu tangu Kungwi Uaridi aondoke hivyo leo ameona acha atoke kidogo akanyooshe nyooshe miguu na mikono yake , akaangaze angaze apate kinachoangaza.

        “Hi” Kashikwa bega lake la mashoto, ile anageuka tu uso kwa uso kakutana na mabinti watatu warembo haswa, warembo ajabu, wamejikoroga usoni wakakorogeka, kwa mapambo, kwa marashi, kwa manukato na kwa mavazi. Lily aliwatazama ashindwe kujifananisha nao, kwanza wao ni watoto wazuri wa Mjini, weupe wa mapodozi, wazuri wa maumbo. Tena maumbo yenyewe hawakosei wanatumia madawa ya kuyaongeza hayo maumbo. Embu tizama makalio yao yalivyo makubwa ya nesanesa, hembu tizama macho yao, macho kungu  na hayo matiti yao? Loh! Sitaki kusema kwamba yanafanana na mto wa kulalia. Ni makubwa balaa.

Lily Cheusi mangara, tena cheusi Chungu ni mrefu kama alivyo Mumewe Denis, nywele zake asilia hajapata kuzipaka dawa, azionapo hizo nywele za hao wadada wampao ‘hai’ mwenyewe anazitamani, japo tuseme mwenyewe hajui wala hajazoea kuvaa mawigi marefu kama mkia wa Farasi. “Hi.” Lily aliitikia ile salamu.“Naitwa Elizabeth.” Yule mkubwa kuliko wote mwenye kadirio la miaka Ishirini na mitano alijitambulisha. Ajabu hata hajaombwa afanye hivyo, papara tu ndio zamsumbua.  “Huyu ni Shoga yangu anaitwa Lisa na huyu mwenye kidoti puani ni Shoga yetu anaitwa Anjelina.” Elizabeth aliwatambulisha Shogaze wakati wote huo Lily alikuwa amesimama pembeni ya Barabara hao Dada watatu walikuwa wakimfuatilia pale walipomwona. Kumbe ni zube, zube la Jiji. Teh teh teh. (Nacheka mie) Hachoki kuangaza angaza huku na kule kama Tochi kizani, tembea yake yenyewe binti bado ana mguu wa Kijiji japo amefundwa kafundika, amefundwa na Kungwi Uaridi, Kungwi aliyevumilia yote.

“Asanteni sana kwa utambulisho wenu, mie ni Liliani watu wengi hupenda kuniita kwa kifupi Lily, nimeolewa ninaishi Buguruni Malapa.” Lily alijitambulisha kwa ufupi. “Oooh! Unakaa Malapa, wacha we! Hata sie twatoka huko Shosti.” Anjelina binti mwenye kidoti puani alionge amejaa tabasamu, meno yake mema yaonekana.

        “Sie tungependa uwe Shosti wetu, tumekupenda sana tumependa jinsi ulivyo mpole mwenye huruma tele machoni.” Anjelina aliomba urafiki.

“Hakuna tatizo nipo tayari nawakaribisha nyumbani, nimefurahi kujuana nanyi mmekuja kipindi kizuri kwangu.” Lily alichekelea, furaha ya kupata marafiki ni moja ya mambo anayoyapenda Maishani.

“Asante sana Shosti, tutakuja hata kesho, hembu chukua Nambari zetu za rununu  nawe utupe Nambari yako ili kurahisisha Mawasiliano.” Lisa aliyeketi kimya muda wote alitia neno.

“Hamna shida Shosti, hembu ngoja niwape,” Lily alitoa rununu yake aina ya NOKIA, akaandika andika hizo Nambari za Marafiki waliokuwa wakitumia hizo simu zinazoitwa SAMSUNG GALAX-6, IPAD na INlFIX. Mmh! Vitu vya bei gharama. Basi huo ndio ukawa mwanzo wa urafiki mwema kati ya hawa Mashosti wanne, Elizabeth, Lisa, Anjelina, na Lily, kutwa kuchwa hao wakina Elizabeth, Lisa na Anjelina, walikesha wakila na kunywa nyumbanmi kwake Lily, muda mzuri ambao Mumewe hayupo. Kutwa kuchwa wakipiga simulizi za hapa na pale, simulizi zimejaa umbea, zinachosha na kuumiza vichwa kuzisikiliza, kutwa kuchwa kumtoa Lily Out na kwenda kumtembeza sehemu mbali mbali za Jiji. Lily akainjoi kula Bata na raha. Pesa zipo, zile Pesa alizoachiwa na Mumewe yeye alizitumia na hao Mabesti wake. Akajisikia Mtoto Lily, akajisikia raha kuwa na Mabesti wanaompunguzia mawazo, upweke na unyonge. 

Kumbe! Kumbe binti hakujua kuwa wenzie wapo kazini, pale wanamchota akili, kilichofunikwa binti anaona kimefunuliwa na kilicho funuliwa anaona bora kifunikwe ni kama Mazingaombwe, yeye mwenyewe haelewi nia na malengo ya hawa Mashosti, Mabesti na Mashoga zake.

Hakushtuka wala hakushtukia kuwa hao wenziwe anaowaona kuwa ni wafariji wake kimawazo wamemtamani Mumewe Denis, maana Denis mwenyewe hatulii nyumbani ni kiguu na njia, yupo bize kusaka pesa, kutwa kuchwa yupo ndani ya Coster anasaka hella ya Bosi ili apate kidogo dogo ambacho ni haki kwake. 

Au labda hawa Mashosti walimuona Denisi hapo Malapa? Labda, maana Denis ni Dereva na Dereva lazima akutane na makumi ya watu kila siku iitwayo leo. Jamani hisi na hisia hazitoshi, tusilolijua litatusumbua, tusilolijua lipo kizani.

Itaendelea  



No comments:

Post a Comment

I promise you

   I PROMISE YOU. (NINAKUAHIDI.) SURA  YA KWANZA. UBAYA WA POMBE. “Umenizingua job, umenizingua kwa muda mrefu sana mpenzi wangu…….kwanini l...