Monday, September 16, 2024

MAMA ALl👿 Sehemu ya 5 (Mwisho)



MAMA ALI

Sehemu ya nne (Mwisho)


Tulipoishia

               Mie Mamsapu nikahitimisha kwa kumwambieni Babu yenu :

 “Babu uchungu, roho yaumia lakini wacha tukubali matokeo. Mioyo ya wanadamu inaficha mengi mengine mazito kutamka. Sawa mengi ni maneno machache ni matendo, matendo yanadhima kubwa sana ya kumwangamiza binadamu. Mtu akiwa makini kuyathibiti matendo yake yamkini majuto yatamwepuka.’ Twalitoka Court tukasepa Maskani, wanyonge wanyong’onyevu, tumeshindwa kumgomboa Ali wetu. 

################


Tuendelee hapa👇


          Mwenzangu miaka mitatu sio haba, ilipita taratibu pasina kupungua visa nyumbani kwa Mamie Ali, Leo kapigana na Ba’ Yah’ kesho kazozana na Mjomba bahati lakini bado tu visa na mikasa iliongezeka. Wenyewe walichokana, Mandhari waloketi ikawachoka ikatamani kuwameza na kuwatapikia mbali na Dunia ipendayo amani, iwapayo maji safi na pumzi ya bure.

          Ali alimaliza kuzitumikia Kalenda zake tatu huko Segerea akarejea nyumbani saaaa-afi takatifu, Mamaye kwa raha zake mwenyewe akamfanyia sherehe yule ampendaye. Si kwa kumbukumbu zile alimmisi mwanaye, alimmisi vilivyo. Mie Mamsapu na Babu yenu Pompo tuliketi chini na kufanya shauri: Kijana asiketi nyumbani bure akajiunga tena na makundi ya watu wa ovyo, wapotoshaji wa hali ya juu. Dunia ni pahali pazuri ila wakazi wamejaa ubaya wa kutu. Hima hima Ali akatafutiwa shuhuli (kazi) Utingo kazi yenyewe, asiketi nyumbani bure kama Happy yule kidosho mchelemchele😂😂🤣, wacha aende mjini akacheze anakochezaga arejee ameshiba mapesa ili Mamaye, Mama Yah’ amfrahie.

Shuhuli ilipamba moto, Ali aliwajibika ipasavyo, wakwanza kudamka adhuhuri wa mwisho kurejea alfajiri hoi amechoka. Gari kubwa aisimamia mlangoni afanya udeiwaka, apiga bao na kuita abiria 'Ubungo, ubungo, ubungo….' 'kariakoo kariakoo kariakoo…'  'Kongo mnazi kongo mnazi….. Manzes'”  Wendao wajazana hadi madirisha yanakosa hewa safi, wajazana kuwahi kazini, kuwachekea chekea mabosi na kurejea nyumbani kutabasamu pamoja na familia.

.................. 👌

         “Nikuelewe vipi mwanaume mtumzima? Upewe nini uridhike?  Kama ni Bahari nishakununulia, kama ni Mbingu ndogo nishakujengea. Ajabu dunia bado usiridhie! Mmh!”Ma’ Ali kajifunga mkaja kiunoni, anesanesa kama Limshangazi 🤣 pembeni ya lango, chuki amchukia Ba’ Yah’ Mzee wa tapu tapu Makvant na magongo.

        "Unielewe Vivyo hivyo unavyoweza kunielewa, au waona kiza mbele ya macho yako?" Ba’ Yah’ kamjibu Ma’ Ali mkono wake wa mashoto kaikumbata pombe ya Mnazi, kapiga mtungi mzito, miwani imemkubali, machoni kavimba kawa mlevi konki.

       "Juzi haujalala nyumbani, jana haujalala nyumbani, nisijue ni wapi walala, ajabu leo waja mikono mitupu! Babu Waswahili wasema mkono mtupu haulambwi.”

         “Sijakupa ajira ya kunichunguza👿, mie nina uhai wangu na weye pia una uhai wako. Wapi ninalala hilo halikuhusu.” Ba’ Yah’ hakumjali Ma’ Ali.

        “Kama maisha yako hayanihusu ninaomba uondoke nyumbani kwangu ni bora nifuge Ng’ombe aniletee nyama na maziwa kuliko weye mavi ya kuku.🤣” Ma Ali kamjibu ovyo Ba’ Yah.

         “Kinizuiacho nini kuondoka? Nina nini hapa nyumbani? Sina kijiko sina bakuri, sina kitanda sina meza nina mwana mmoja ambaye kwangu ni jicho na mboni yake.” Ba’ Yah’kalifungua pazia la Lango aanze kuondoka.

       “Yasini sio wako ni wangu mwana, ujue hilo. Tafadhali 👌usirejee hapa nyumbani ishia huko huko kwa huyo mpumbavu mwenzio.” Ma’ Ali aliingia chumbani apate kumtolea vigagula ambwagie na kumfukuza Ba Yah’. Alipotoka chumbani alipigwa butwaa kuona Yah’ mwanaye hayupo sebuleni, Baba Yah’ pia hayupo sebuleni, akili zikamtoroka akafanya hima kutoka nje kasi ya upepo wa Tisunami kumtafuta Ba’ Yah’ aliyeondoka na mwanaye.

        “Yallah! Mola we! Mwanangu nampata wapi? Ma Ali alilia.“Jamani Ba’ Yah nirudishie mwanangu,nirejeshee tafadali.”Alipiga kelele asimwone Ba’ Yah’ wala Yah’ mwanaye.

        “Majirani, majirani nisaidieni mwenzenu, Ba’Yah’ kaitoroka nyumba na mwana kamchukua pasina hiari ya mie.”Alipiga kelele kuita majirani. Majirani pamoja na Inzi wanoko walitoka Mabomani wapate kumsikiliza Ma’ Ali aliyeeleza kisa na mkasa ulomkuta.

“Nalimfukuza Ba’Yah’ kwa ubovu wa tabia yake ya kutorejea nyumbani na kulewa kwa sana. Ajabu ile nimeingia chumbani kumtolea takataka zake yeye kamtorosha mwanangu, nisijue wapi wameeleka.”Alilia Ma Ali,

  “Makubwa! Jamani.” Majirani pamoja na Inzi wanoko walishangaa.

“Kukutia hofu, wasiwasi, presha, stress na hasara ya roho.” Walimwambia na kumwonesha hisia za huzuni.

“Hima enenda Polisi kamripoti, Jiji hili kubwa utatanga tanga usifanikiwe.” Walimshauri.

        “Jamani ina maana hamjamwona akipenya vichororo na vinjia vya ovyo?”Aliuliza.

        “Amwone nani kila mtu yupo bize na mishe za kutafuta hella mjini.” Walizidi kumchanganya. Akalia asikate tamaa ya kumtafuta mwanaye. Akaendelea kumsaka.

#####

Alienda kuripoti Polisi lakini bado tu asimpate Yah’ mwanaye, uzuri wa majirani zake wengine walimjua Ba’Yah yule mlevi koko, mlevi koma. Waliyajua machimbo yake walijua wapi kaeleka kwa nguvu ya huruma na ubinadamu walimpasha Mamie Ali aliyeanza pandwa presha ya kuchanganyikiwa.

“Acha kutanga tanga kama Kuku mtaga Yai ukaumiza Malundi  yako bibie. Sikia Ma’ Ali mumeo kawekwa ndani na kimada dogodogo alofundwa somo unyagoni. Babu afanyiwa mambo ya kitanga hadi analewa kwa huba apate kukusahau weye mwenye makucha ya Mwewe." Walimwimbia taarabu👌.........

“Kimada dogodogo amchukia mwanao hana mfano. Ndo’ maana Wa mwambao wanasema “Mama wa kambo mwogope, sio Mama.” Mipasho ile ilimshitua Ma’Ali.

      “Ungelijua mapema walahi! Usingelihangaika kulilea lile dume levilevi. Fanya hima enenda Magomeni kalianzishe varangati, dawa ya moto ni moto.” Walimpa njia. 

Kwa mahasira Ma’ Yah’ kafunga safari kutoka Buguruni nyumbani hadi magomeni lengo kumsaka Yah’ mwanaye, ajapompata nakwambieni Ba Yah’ atakoma kuringa. 

Kafika Magomeni mwanamke kaanza kupeleleza wapi atampata yule mlevi koma Ba’Yah mwanzo mgumu, mvumilivu hula mbivu, atangaye na upwa hali wali mkavu. Alifanikiwa kumpata mlevi Ba’ Yah’ kapozi mbele ya Bibi dogodogo kutoka Tanga amkanda na kummasaji makando ya kumsahahu Mama Ali.

       “Nilikufukuza Jibwa weye sikumfukuza mwanangu.” Ma Ali alilianzisha.

        “Niliondoka na mwanangu sikuondoka na wewe Mbogo mla pilipili.”Ba’ Yah kamjibu Ma’ Ali. 

       “Sikia babu; kuzaa uchungu kulea tabu niachie mwanangu nikuache uendelee na kimburukutu chako.” Ma’Ali alipunguza jaziba.

       “Omba jingine lakini sio kunitenganisha na mwanangu Yah’.” Ba’ Yah aliongea kwa kujiamini.

       “Ba’ Yah’ nikuulize wanijua mie Mbogo mn’goa meno kwa mkono, mnyoa nywele kwa meno, mkata ulimi kwa kucha, mnyofoa macho kwa sauti ya ngurumo?” Ba’ Yasini kaulizwa.

      “Nisikujue Shetani ulozaliwa gizani? Nijue na mie vivyo hivyo.”

       “Tusipoteze muda, tafadhali nipe mwanangu.” Alimpigia kelele.

       “Sikupi ng’o”Ba’ yah’ aligoma kingangari.

        “Unipe usinipe utanipa kwa lazima.” Ma’Yah’ alibwata. Akamvamia na kumrukia Ba’ Yah’ usoni kwa kasi mfano wa ndege anyaye ghafla  juu ya mti, akalianzisha varanga, akanyesha mvua ya mapigiti, Lo! Ba’ Yah alikorogwa akakorogeka. Yule Bibi dogodogo wa kitanga alikimbilia kuita majirani na Inzi wanoko waliojazana kushangilia ile shuhuli ambayo kwao ni kiburudisho. Nakwambieni kwa yale mapigiti Ba’ Yah’ alisalimu amri akamkabidhi mwanaye Yasini kwa Mama Ali wakati huo Ba’ Yah’ kavunjwa Lundi (guu) la mashoto. Ubavu wa mashoto umelegezwa, koo lake lashindwa  kukoroma, jicho limemtoka pima mfano wa mwanamke mtafuna kungu. Lo! Mazito ya Dunia.

##########

        Ma’Ali alirejea nyumbani Buguruni. Bado kawaka hasira, lakini mmh! Kaguna. "Kuna nini nyumbani Buguruni?" Kajiuliza. Umati wa watu nje ya Boma alojipweteka bure kujiachia umejaa tele. Vilio na majonzi vyasikika, upepo haukuwa mzuri pale Bomani.

        “Nini cha mno jamani?” Kamtua Yah’, chini kutoka gongoni kwake.

       “Mazito Ma’ ali, Ali hatunaye mtu huyo.” Walimpasha majonzi.

       “Uwii! Yalah! Toba mie!” Ma’Ali aliona kizunguzungu kizito chamvamia kama Jini chokozi. Je, habari aloambiwa ni ndoto!? Mbona mabadiliko ya ghafla. Hapana jamani maisha ni fumbo binadamu kafumbiwa. Juzi juzi tu kamtoa Mwanaye Jela leo kaambiwa Ali katutoka mtu huyo! Hapana! Haikubaliki abadani. Machozi yalimbubujika

      Mie Mamsapu, Ma’ Happy pamoja na Mjomba Bahati tulimbeba Ma’ Ali na kumpeleka ndani ya Bomale maana kizungu zungu kile kingelimwangusha chini puuu! Fahamu apoteze na povu kumtoka. Huko ndani kilio cha nyongo kilipasua dali ilikua ni Bahari ya machozi na majonzi. Sie wenye uchungu viunoni tuliambiwa Ali mwana wa Mama Ali alipatwa umauti akiwa kazini. Conductor yule alikanyagwa na Roli lililobeba mchanga mauti yakamchukua roho yake ikaacha mwili😭😭😭😿😿😢 Alale pema pazuri.

 Ni nani aliyetazamia kuzipata habari hizi zilizoshitua moyo? Sio mie Mamsapu, Babu yenu Pompo, Ma Happy, mjomba bahati au Dalali Deo. Hatukutegemea zaidi ya kukubali kuwa kifo ni fumbo uhai ni zawadi. Masikini! Ali😭.

,...........

Tukiwa tungali bado matangani machozi yetu machoni, maumivu yetu moyoni tukaja kusikia sauti nzito, Gari ya matangazo kelele ikibwata.

        “TANGAZO! TANGAZO! TANGAZO. UDUGU WAKAZI MKETIO BONDE LA MSIMBAZI MPISHENI MWEKEZAJI VIWANDA ATUJENGEE, AJIRA ATUPATIE, MAENDELEO ATULETEE, UCHUMI ATUKUZIE.”

 Tangazo lilijirudia rudia sie tulio msibani tusielewe dhima tuloisikia. Jumbe ilitutia mashaka. Inzi wakaanzisha mabishano.

       “Tumpishe vipi? Tumpishe wapi? Tumpishe lini? Mbona kizungumkuti, sababu ya kumpisha?”

“Tukiisha mpisha twen’zetu wapi?” Inzi walizoza.

“Jamani akuje mtu Jumbe atufafanulie.” Hofu ilitanda.

“Imeisha hiyo.” Wahuni na Panya road waliimba. Dakika chache baadaye sie wenye roho za mbegu ya aladali tulishuudia yale Mabulidoza makubwa yaitwayo Vijiko yakivamia makazi ya sie hoehae na makabwela. Sijui niseme……… Naona mfadhaiko 😭 naogopa maskini! Ilikuwa ni vurugu, mshike mshike. 

       Nyie! Serikali vipi😳🤯🥶🙆, mbona Udikiteta?Demokrasia iko wapi? Vijiko kuvamia na kuyabomoa Maboma na Mapagara ya wenzetu?Tena kwa fujo!!Pasina amani na patano.

Mmh! Tugune sie na tama kushika shavuni. Dunia inakoelekea ni kubaya. Waja hatujapangwa wala kuandaliwa ila mvurugo huo! Vumbi balaa, mshike mshike, akibisha mponde mtupe kwenye Difenda na Jela akaozee.

 Basi nakuambieni vurugu zikapamba moto.Bomoa bomoa haikumuacha salama Mamie Ali, Mjomba Bahati, Ma’ Happy na Dalali Deo. Maboma yao yalisombwa na mafuliko ya bomoabomoa.

 Afadhali mie Mamsapu na Babu yenu pompo. Mie Mama mpenda amani naliponea chupuchupu kumpisha huyo mwekezaji 'kwiooo' 👌😹😹 uchumi atukuzie maendeleo atuletee. uchumi wenyewe kwioooo😹😹😹😹😹 ! (Mwaya mie Mamsapu mama wa kitanga Nacheka kwa dharau) Ndo’ wenzetu wabomolewe Maboma kisa ati wanaketi Mabondeni? Sio haki. Vurugu zikapamba moto mie Mamsapu na Babu yenu Pompo tusiamini mwisho mbaya ulompata Mamie Ali, Mamie Happy, Mjomba Bahati na Dalali Deo.


Tchao👋👋


Tuonane kesho kwenye kisa Cha Mjukuu wangu Swahili

 

No comments:

Post a Comment

I promise you

   I PROMISE YOU. (NINAKUAHIDI.) SURA  YA KWANZA. UBAYA WA POMBE. “Umenizingua job, umenizingua kwa muda mrefu sana mpenzi wangu…….kwanini l...