Simulizi
MBOSSO
SEHEMU ya kwanza
KIZINGITI
“Wasemaje mwana mpuuzi wewe? Hivi una akili za kutosha kichwani hata utake kuongea maneno kama hayo? Hivi una akili ubongoni hata useme unataka ……… Ati unataka kuolewa na MBOSSO?” Mamaye Diva alipiga kelele, Diva alimwaga machozi mengi sana, mengi kama maji ya Bahari, kamasi haziachi kumtoka, kichwa nacho kingali kinauma kwa sababu ya Mbosso mwanaume aliyeuteka moyo wake, mwanaume aliyeupendeza mtima wake, mwanaume kijana tena kijana wa rika lake.
Wameketi sebuleni yeye, babaye pamoja na mamaye mpenzi, ajabu wazazi wake wote wanaupigilia msumari moyoni mwake Diva, wanamkoromea na kumkataza ati kunena kwamba anampenda Mbosso, yule kijana mwizi, mhuni, kichaa wa kuokotwa na kutupwa.
“Diva wewe ni msomi, una Degree yako, kwanini hautuelewi? Kwanini haujitambui? Au tuseme kwamba kitendo cha sisi wazazi wako kugharamia elimu yako, kuhangaika wewe usome ni kitendo cha kutupa mali zetu bure, guvu zetu na akili zetu?” Babaye Diva aliongea kwa hasira.
“Hapana baba sina maana hiyo, kinachonifanya mimi nimpende Mbosso ni moyo wangu, moyo wangu ndio unaompenda Mbosso, sifichi wazazi wangu, nimekufa kwake, nimezimia kwake, siwezi na tena sijiwezi kwa sababu ya mapenzi yake kwangu, tafadhali wapenzi, mniruhusu mie mwana wenu niolewe na Mbosso.” Diva alilia.
“Diva, yawezekana mwanetu una pepo tena hilo pepo sio haba umetupiwa mama, yanini kulilia mapenzi ya yule kijana mwanaharamu wa Jiji? Mhuni wa Jiji, hana elimu, hana kazi maalumu, wala hana hadhi na heshima ya kuolewa na wewe binti kutoka katika familia ya watu wanaojiweza?” Mama alichangia hoja.
“Sina jinsi wapenzi baba na mama, sina wazo la kumpata mwanaume mwingine yeyote yule hapa duniani zaidi ya Mbosso. Moyo wangu umetua kwake, sijali kuhusu umasikini wake, sijali kuhusu elimu yake, sijali kuhusu tabia zake, ninachojali mimi ni kwamba pole pole ndio mwendo, nitafanya juu chini ili nipate kumrekebisha, nitafanya juu chini ili nipate kumfanya ajitambue.” Diva alilia tena.
“Mwana we! Usipofunzwa na mamayo utafunzwa na ulimwengu, sisi ni wazazi wako, kamwe hatuwezi kukupa wembe ujapoulilia, hatupendi upatwe na madhara maishani mwako, tusingelipenda kuona unateseka ndio maana tumehangaika ili wewe usome uje kuwa na maisha bora.” Mama aliongea kwa hasira. Baba akasimama pale alipoketi kisha akaongea kwa sauti kubwa iliyojaa hasira, wakati huo huo alikuwa anajiandaa kuondoka.
“Kiburi si maungwana, vijana wa siku hizi mnajiona kama mnaijua sana dunia kuliko sisi wazazi wenu tuliowatangulia, sasa sikiliza Diva, ukijifanya mkaidi ndani ya nyumba hii, kamwe hautafaidi siku ya Idd, ukijifanya mbishi, mgumu na mwenye uelewa mdogo, ujiandae kuondoka ndani ya nyumba hii nisikuone tena.” Baba alipadwa na hasira, naye akachukua funguo za gari yake, haraka haraka akaondoka ndani ya sebule ile nzuri yenye vitu vya bei gharama.
“Mwanangu, usibishane na wazazi wako mpenzi, sikiliza sauti ya baba na mama yako, jifunze mengi kupitia wazazi wako, kumbuka wewe ni binti mdogo mwenye umri wa miaka ishirini na mitatu, unajiandaa kwenye maisha ya kuja kuitwa mama, sio leo bali siku moja nzuri aliyokupangia Mola, kwanini ubishane na wazazi wako? Ukibishana na wazazi wako, kamwe hauwezi kuja kufanikiwa maishani. Sikiliza sauti ya wazazi wako, ukumbuke wazazi wako ni kuku na wewe ni yai.” Safari hii mama alipunguza ukali wa sauti yake, alihitaji kumbembeleza mwanaye aliyezama kwenye penzi la kijana mwizi, jambazi na mtu aliyeogopwa katika jamii.
“Baba yako akirejea kutoka kazini mpenzi mwanangu, umjie na kumwomba msamaha, umpigie magoti asikugawie radhi, kikubwa unachopaswa kuzingatia ni kukaa chini na kufikiria uachane na huyo Mbosso hakufai mwanangu, tena hatupendezi machoni mwetu mtu Jambazi na mwizi kuolewa na wewe binti msomi kutoka katika familia za watu wa daraja la juu, watu wanaojiweza, watu wenye fedha zao ni aibu mwanangu.” Mamaye Diva aliongea.
“Mama nihurumieni moyo wangu hautaki kuyaondoa mapenzi niliyoyavundika kwa Mbosso, ni heri nife lakini sio kumuacha yule ambaye moyo wangu umezama kwake.” Diva alikuwa mgumu na mwenye msimamo thabiti, wala asitake kuubatilisha msimamo wake.
“Mmmh!” Mamaye Diva aliguna akakosa maneno ya kuongea mara baada ya kumwona mwanaye king’ang’anizi, mgumu na mwenye msimamo.
**** Siku iliyofuata asubuhi Diva alitembelewa na Shogaze wawili, Shoga wa damu damu, hao Shogaze amesoma nao chuo kikuu cha Makumira Arusha, wote wamechukulia masomo ya Sheria tena wangali wanatarajia kuendelea ‘School of law’ kwani hawajatosheka na Degree moja waliyoipata.
“Teh teh teh, Ai mwaya mbona watuchekesha!” Atu Shogaye Diva alicheka, hadi meno yake yale ya chumbani yakachungulia.
“Loh! Umesema ati umempenda Mbosso, ai! Loh! Jamani loh! Putuuu.” Atu akatema mate ndani ya chumba alalacho Diva.
“Eeh! Bibie, ndio ufikie hatua ya kutema mkoromo ndani ya chumba cha mwenzio?” Siha aliongea, wakati huo huo Diva alikuwa kimya, mnyonge asiyejua afanye nini kujiokoa ndani ya penzi ambalo si wazazi wake pekee wanaompinga, majirani, marafiki na wengi wamjuao Mbosso hawakomi kumpigia kelele. ‘Hakufai huyo, hakufai huyo, hakufai huyo.’
“Wacha niteme jamani aibu tena bonge la aibu na fedheha, mwe! Yaani Diva Shogangu umeshindwaje kupendwa na wanaume wazuri watanashati walio Chuo, walio Maofisini, walio kwenye kazi zao nzuri ziwaleteazo pesa, vipato, mali, raha na furaha ufikie hatua ya kumpenda yule kichaa mwendawazimu?” Atu alimponda Shogaye Diva, wakati huo huo Diva ni mwingi wa mawazo ameketi juu ya kitanda chake, kichwa chake kakiinamisha chini kwa huzuni iliyo kuu.
“Atu.” Siha alimwita Atu kisha akaendelea kuongea.
“Kupenda waweza kumpenda yeyote, haijalishi ni mwenye mali nyingi, cheo, kazi nzuri au Status katika jamii. Mimi ninafikiri Diva ana sababu za kwanini anampenda Mbosso, kwa hisia zangu ninahisi ni moyo wake ndio unaomsukuma kumpenda Mbosso sababu moyo ndio huanza kwanza kupenda.”
“Mmh! Hongera kwa kumuunga mkono Diva bibie Siha, nadhani wote mmepotoka na wote mmepotea. Duh! Mie naona ni bora nipendwe na Nyani kuliko kupendwa na mwizi, mhuni, mkabaji, mtumizi wa dawa za kulevya kama Mbosso .”Atu alitia neno, wakati maongezi yao yakipamba moto, mamaye Diva alijibanza Kona ya nje ya mlango wa Bintiye apate kusikiliza maneno mawili matatu ambayo wale Mashoga walikuwa wakiongea.
“Atu, usiseme hivyo tena usiingize elimu ya darasani katika mapenzi kwa sababu elimu ya darasani na mapenzi ni vitu viwili tofauti. Elimu ina sababu zake, mapenzi pia yana sababu zake tena ukumbuke kuwa mapenzi yana nguvu, nguvu za kuvunja vunja milima. Mapenzi yana nguvu, nguvu za kuondoa chuki, uhasama na ugomvi.” Diva alitia neno kisha akaendelea.
“Najua kinachowafanya wengi wanipinge juu ya mapenzi yangu kwa huyu mpenzi wangu niliyempenda mwenyewe sababu ya tabia zake, tabia ambazo jamii inayomzunguka haipendezwi nazo, hata hivyo mie ninatoa ahadi kwamba nitafanya kila njia kila sababu na kila hatua ya kumbadilisha Mbosso wangu, nitafanya kila niwezalo akubalike katika jami. Najua na pia natambua kwamba wanume wengi hupenda kuoa mwanamke mtulivu mwenye tabia njema lakini hao hao wanaume wanajikuta wanasahau kufikiria iwapo mwanamke ana tabia zisizopendeza inawapasa wao kama wao kuchukua jukumu au hatua ya kumbadilisha mwanamke.” Diva aliongea mengi.
“Kweli kabisa uongeayo Shogangu, kama Mbosso ni mwizi jukumu unalo tena sio tu kusema unalo hata sisi tulio wema kwako tunaokupenda Shoga yetu tuna haki ya kumbadilisha kwa maneno na kwa vitendo.” Siha alitia wazo. Wakati huo huo mamaye Diva aliyekuwa bize akisikiliza mazungumzo ya wale rafiki, alichukizwa na maneno aongeayo Siha, alihisi kwamba Siha anaelekea kumpotosha mwanaye. Basi mamaye Diva akajisemea moyoni, “Lazima nimbadilishe Diva, na nitambadilisha haraka sana iwezekanavyo.”
“Diva shogangu maamuzi unayo wewe.” Siha aliongea.
“Panga na kuchagua kwa umakini zaidi, kama kweli Mbosso amekupenda na wewe umempenda basi mapenzi ni yenu, uwanja ni wenu.”
“Sidhani kama mapenzi yenu yatadumu.” Atu bado alikuwa mpingaji.
“Kesho na kesho kutwa tutakuja kuambiwa kwamba Mbosso katiwa polisi, kaiba, kabaka, kachoma nyumba, kafanya mabaya na maasi. Kaivunja amani ya nchi na kwa jinsi alivyokuwa jizi la kutisha, wallah! Nakwambia Diva shogangu na wewe utakwenda kulala Jela, utalala Jela kwa sababu unamhifadhi mwizi ungali unajua kwamba ni mwizi, tena mwizi aliyeshindikana.” Atu hakuchoka kumponda Diva.
“Ajabu Mwanasheria tarajiwa kama wewe leo hii unang’ang’ania mapenzi ya mtu avunjaye sheria, au ndio kumtetea mwizi huko? Ama umejipanga kumtetea mwizi kwa kisingizio cha mapenzi?”Atu alivyokuwa na domo chafu alizidi kumponda Diva ambaye hata hivyo alikuwa hana neno la kusema zaidi ya kulia na kumwaga machozi.
****
Mamaye Diva aliongea na babaye Diva jioni ya leo mara baada ya babaye Diva kurudi kutoka kazini kwake. Aliongelea mipango ya kumtafutia mume Diva, kikao hiki kilikuwa ni cha watu wawili tu, mamaye Diva na babaye Diva. Diva hakujua jambo lolote linaloendelea, yeye wakati wote anamuwaza Mbosso wake mwanaume wake mrefu kiasi, mweusi kiasi, mzuri wa sura ya kumpendeza Diva.
“Huo ndio mpango wangu baba Diva, mwaenetu anapaswa kutafutiwa mume, tena haraka sana iwezekanavyo, akipatikana mume mwenye elimu, fedha na heshima zake angarau huyo mume atafanya kumbadilisha Diva ajitahidi kumsahau huyo kichaa ampendaye.”
“Ni aibu mke wangu, ni aibu kwa mwaenetu kuolewa na mwizi, jambazi. Tutaficha wapi nyuso zetu sisi? Aah! Tutakuwa wageni wa nani sisi haswa pale binti yetu ajapopatwa na maswahiba? Tena hayo maswahiba yasababishwe na huyo mwizi njemba.”
“Ndio maana nimetoa ushauri tufanye hima hima tuliokoe jahazi kabla halijazama. Kadri tutakavyombadilisha Diva, ndivyo tutakavyo ona matokeo yake. kadri mumewe Diva atakavyombadilisha Diva, ndivyo Diva atakavyoyaona matokeo mema. Mpenzi, tusimwache mwanetu ateseke.” Mama na babaye Diva walijadiliana kwa marefu na mapana usiku huo.
“Ngoja nifanye juu chini kumtafuta kijana wa rika lake pale ofisini kwetu Bank ya CRDB, nitamshawishi amuoe mwanetu hata ikiwa bure pasipo kulipia mahari. Au unasemaje mpaka hapo mke wangu?” Babaye Diva aliongea.
“Mume wangu, wazo lako ni bora, kwa sababu tunapaswa kufanya hima hima ili maji yasije fika shingoni, kama ujuavyo tena hofu yetu ni kutapa tapa, muhimu tushirikiane ili tuokoe jahazi lisizame.” Mamaye Diva aliongea akimtaka mumewe washirikiane wakati ule ulio mgumu kwao, wakati ambao Diva aliwaweka wao kwenye kipindi kigumu sana.”
Itaendelea.
No comments:
Post a Comment