Saturday, September 21, 2024

KIGUU NA NJIA sehemu ya tatu


 #ANNA: (Wakiwa darasani Siku liyofuata). Eeh! Shoga yangu wacha we! Unasema kuwa ulilala kitanda kimoja na yule handsome aitwaye Ben?

AMINA: Sikufichi shoga yangu, nakwambia ilinibidi nimlazimishe ku do naye, yaani kijana alionekana mgeni haswa, mara nimshike hapa, utakuta anatetemeka, mara nimpapapse pale, angelitoa mikono yangu, lakini yote tisa kumi nilimuweka pale alipopaswa kuwekwa.ANNA: Teh! Teh! Teh! Teh! Yaani shoga yangu kuku mgeni hakosi kamba, huyo keishaingia kiulaini laini, na kwa jinsi nijuavyo mie atakulilia huyo, hakuachi ng’o, atakuwaza iwe usiku iwe mchana, hawezi kula kulala, wala kusoma juu yako.

AMINA: ( Anakomboa mafuta ya ku
jipaka midomoni mwake kunako kopo dogo alilobeba kisha anajipaka paka midomo yake). Swala keishaingia mitegoni.

SUZZANA: (Alikuwa bize anajisomea somea vitabu). Lakini rafiki yangu, ukumbuke kuwa mshika mawili moja humponyoka, mdharau mwiba mguu huota tende, mapenzi na shule wapi na wapi? Yakupasa ushikilie elimu kwanza, mapenzi yapo, nawe utayapata ukiisha kuolewa, mara baada yaw ewe kumaliza chuo kikuu na kupata kazi laazizi.

ANNA: Huyu naye asitutibulie maongezi yetu, kila siku yeye anajifanya ni mshauri nasaha, kila siku yeye anajifanya ni Bingwa wa kutoa hoja kuhusu elimu, kama unaona mawazo yetu ni finyu basi ushauri wetu ni wewe kuwa mwalimu tu itatosha iwapo utakuwa mwelimishaji wa jamii.

AMINA:  Tena wengine tumeshachoka na hiyo elimu ambayo yeye anaitilia mkazo, wala hatuoni faida yoyote ile zaidi ya  kupoteza muda wetu wa kufundwa mada zile Zile za kurudiwa rudiwa. (Anajibu kwa kebehi).

ANNA: Umesikia wewe Kimburukutu!

SUZANNA: (kimya). Anaendelea kujisomea.

AMINA: Yaonekana huyu Bibiye bado ni kifaranga, hajapata kumjua mtu mume ndio maana, yupo Zubezube, haoni mbele wala nyuma, kutwa kucha anakazania elimu, elimu, elimu…Elimu ndio nini?

ANNA: Tena kwa taarifa yako kuna msemo mmoja wa Wazungu unaosema. ‘Money is everything, education is nothing…. Money is better than education” Sijui hupo hapo?

AMINA: Yupo hapo na tena yeshamshuka, anajishaua shaua bure. (Mara ile Mwalimu Grace anaingia, darasa linasimama kumsabahi, naye anawaitikia kama kawaida yake.)

MWALIMU GRACE: (Anafundisha). Leo tutaimalizia ile mada ya ugonjwa wa kipindu pindu. (Mara kwa ghafla Amina alijisikia Kichefu chefu, anatoka mbio mbio kuelekea nje kutapika).Eeeh! (Mwalimu Anashangaa). Nyie wanafunzi mbonqa ni wa ajabu sana, yaani nimewafundisha  msiende kula vyakula vichafu, tayari mmekwisha bugia. (Analalamika). Niliwakataza kunywa maji yasiyochemshwa, niliwakataza kula matunda yasiyooshwa, niliwaambia ni marufuku kunywa maji ya mitoni. Mwe! Lakini bado tu hamnisikii. (Anamwendea Amina pale alipoinama kutapika). We Amina, vipi una tatizo gani?

AMINA: Najisikia kichefu chefu madam, nahisi ndio hizo dalili za Kipindu pindu, maana tangu kizuke hapa jijini Dar es Salaam, kila mtu ana hofui na kuogopa.

MWALIMU GRACE: Oooh! (Anapumua kwa kasi kidogo). Pole sana mwanafunzi wangu, kama unajisikia vibaya waweza kwenda kulala pale kwenye bustani ya shule. Mwalimu Grace alimpatia ruhusa ya kwenda kupumzika). (Amina Alikwenda kupumzika angali ana wingi wa hofu na wasi wasi juu ya afya yake, kwasababu huu ni mwezi wa pili sasa, amekuwa akitapika tapika ovyo, mate yanamjaaa Mdomoni mwake, kuchooka kusiko kwa kawaida, mara angelitamani kula udongo, mambo kede kede yanamchanganya.

****************

Uvumilivu ulimshinda Amina, akajikuta anaelekea hospitalini kumwona Daktari, akiwa yeye na mama yake walifika hospitalini salama, walimweleza Daktari shida iliyowapeleka, naye Daktari alichukua vipimo vya damu yake Amina, mara baada ya vipimo, majibu yalitolewa.

DAKTARI: Umesema upo kidato cha ngapi vile? (Dakta aliuliza).

AMINA: Nipo kidato cha tatu Dakta.

DAKTARI: Na huyu ni mama yako mzazi au mwalimu wako.

AMINA: Mmmh! Daktari nawe una maswali mengi kama Polisi, huyu ni mama yangu mzazi.

DAKTARI: Ok, kuuliza sio ujinga bali ni kutaka kujua. Ni hivi binti, vipimo vinaonesha kuwa wewe ni m…aaah!, wewe ni mjamzito, na tena huu ujauzito wako ni wenye miezi miwili hivi. (Dakta aliongea).

MAMA AMINA: Yallah! Toba! (Alipigwa na mshangao).

AMINA: Mimi nina mimba Daktari? (Bado amebaki anashangaa, kinywa wazi, haamini yale yasemwayo na Dakta).

DAKTARI: Ndio mdogo wangu, wewe ni mjamzito, tena ujauzito wako ni wa miezi miwili, mimi binafsi nashangaa kwanini unajihusisha na suala la mapenzi katika umri huu mdogo ulionao!

MAMAYE AMINA: Au umekosea kupima bwana Daktari, mwanangu yungali bado mwanafunzi, atawezaje kushika mimba akiwa shuleni?

DAKTARI: Suala la yeye kushika mimba akiwa shuleni sio tatizo, tatizo ni yeye kujihusisha na suala la mapenzi akiwa shuleni.

AMINA: (Akilia machozi). Jamani Daktari, nitafanya nini mimi, bado shule naipenda, ninataka kusoma, elimu ndio ufunguo na ukombozi wangu.

DAKTARI: Sina chas kukushauri mdogo wangu, cha muhimu ni wewe kwenda kuongea na walimu wako, labda watakushauri vema na pia watajua jinsi ya kukusaidia.

AMINA NA MAMAYE: Machozi yaliwafunika, wakalia kama vile wamepatwa na msiba.

************

Amina pamoja na mamaye walikwenda Shuleni kwao Amina ili wapate kuomba ushauri wa mwalimu kuhusu tatizo la Amina. Walipokelewa vizuri, mwalimu Grace aliwasikiliza kwa upole zaidi.

MWALIMU GRACE:Ulikuwani mtoto mwenye tamaa kiasi hicho, daima nilikuona ukiwa mtiifu na mwenye uvumilivu darasani, ajabu leo umeshika ujauzito, hembu nieleze huo ujauzito ni nani aliyekupatia. (Amina kimya kwa aibu.) Nakuuliza tena Amina, unieleze huo Ujauzito  ulionao ni nani aliyekupatia ili nayeye achukuliwe sheria na hatua kali kwa  uharibifu huu uliofanyika.

AMINA: (Kimya).

 MAMAYE AMINA: Usijitie ububu shuleni, umesikia mwana we! Mpatie jibu mwalimu wako naye ataweza kutoa ushauri wake.

AMINA: (Anajibu kwa hofu.)Yawezekana ni Ben.

MWALIMUI GRACE: Ben yupi tena huyo.

AMINA: Yupo kidato cha nne B.

MWALIMU GRACE: Ok, vema, suala hili sio la kitoto, mimi kama  Mwalimu wa nidhamu nitalichukua hili suala na kulipeleka kwa mkuu wa shule, yeye ndiye mwenye uamuzi wa mwisho, nadhani atajua nini atakachoamua na kukushauri. (Mwalimu Grace alimruhusu Amina aende darasani, mamaye Amina alirudi nyumbani kwake, Mwalimu Grace tayari alikwenda Ofisini kwa mkuu wa shule ili kutoa taarifa juu ya lile jambo.)

******************

Amina akiwa darasani ameketi pamoja na shogaze wawili Anna na Suzanna, ilimbidi awatobolee ile siri ya yeye kuwa mjamzito).

ANNA: Eeeh! Mwaya, unasema kweli?

AMINA: Yamenikuta mwenzenu.

SUZANNA: Yaani kutaopika kote kule, kichefu chefu cha mara kwa mara, kulala lala ovyo darasani, Kupenda maji na udongo, nani asijue kuwa tayari mwenzetu umekwisha nasa? nilikwambia mimi cheza na elimu, uisicheze na pesa ama mapenzi, hivyo ni vitu hatari katika masomo.

ANNA: Eh! Eh! Bibiye, huu sio muda wa kumlaumu shosti wetu, huu ni wakati wa kumfariji, maana tatizo alilonalo sio dogo ni zito kama Mlima. 

SUZANNA: TEH! Teh! Teh! Teh! (Anacheka kwa dharau) nicheke mie, ni bora angelifeli mitihani, mie ningelikuwa mstari wa mbele kumfariji, kumtia moyo na kumtakia ajibidishe zaidi, lakini kwa hilo suala la ujauzito nasema siliwezi, nitajifariji kwenye elimu, elimu ndio msingi wa maisha yangu, mbona wahenga walisema kama unaona elimu ni gharama basi jaribu ujinga ili uione hasara yake.

ANNA: Kwenda zako huko, unajiona wewe ndiye  mwenye akili sana ndani ya darasa hili,  kumbe bichwa zero, huna huruma msichana wewe, lakini ukae ukijua matatizo ni sehemu ya maisha ya kila siku, hatuyakaribishi matatizo bali matatizo ndio yanatuvamia.

SUZANNA: Aaah! (Anacheka kidogo). Ati hatuyakaribishi matatizo bali  yenyewe ndio yanatuvamia. Napingana na wazo lako kwa sababu asiyesikia la mkuu huvunjika guu, asiyefundwa na mamaye hufundwa na ulimwengu. Amina amelilia wembe ameshapewa, tangu mwanzo nilitoa ushauri wangu tujihadhari kabla ya kuzuka kiwa hatari lakini sikio la kufa kamwe halisikii dawa. Ndio hivyo sasa, leo mmenikumbusha usemi mmoja wa Wahenga waliposema Masikio hayazidi kichwa. (Suzanna aliongea kwa kirefu).

ANNA: Nitakuponda vibaya wewe binti wa kilokole tena ni heri ungelihama pahali hapa tulipotulia, unazidi kutuharibia ishu na mishe zetu, mchawi mkubwa we! (Anna anataka kumpiga Suzanna, lakini  Amina aliyeketi katikati ya dawati alizuia yasitendeke).

SUZANNA: Usipoziba ufa utajenga ukuta, maji yakimwagika hayazoleki, mfa maji haachi kutapa tapa. Pokea huo ujumbe bibie Anna, zubaa uchekwe, hapa ndio mjini bibie. Ukijipendekeza kidogo tu tayari na wewe unaondoka na huo mzigo wa mwenzio, mie nakushauri acha kabisa hayo mambo ya kupenda penda wanaume watu wazima pamojqa na wanafunzi wenzio, watakuharibia maisha yako bure, utashindwa kutimiza ndoto na malengo uliyojipangia, itakuwa ni sawa sawa na kuupanda muda hatimaye ukavuna upepo, mbona walisema wenye hekima, cheka na Nyani uvune mabua. (Leo Suzanna aligeuka mhubiri)

AMINA: (Machozi yanamtoka). Yote ayasemayo Suzanna ni ukweli mtupu, Anna rafiki yangu, majuto ni mjukuu, kila mtu hujuta, tufuate ushauri alioutoa Suzanna, Suzanna ni rafiki bora aliyefaa kuigwa katika jamii, amefundwa akafundika, anaelewa nini kinachoendelea, anajua pia matokeo ya kile kinachoendelea. (Analia).-Looh! Tamaa mbele mauti nyuma, sijuik hatima yangu itakuwaje, jamani kile kipindi cha raha na furaha sikuipenda elimu lakini wakati huu wa shida, tabu na misukosuko ndio roho yangu imeanza kuipenda Elimu, hembu tizameni daftari zangu zote, tangu naanza kidato cha kwanza hadi hiki cha tatu, sijapata kuandika neno na ukitegemea walimu wetu walivyo wazembe hawafuatilii, hawachunguzi, hawasahishi wala hawatoi tamko la ukusanyaji wa haya madaftari yetu wapate kukagua kagua mienendo yetu ya kimasomo. (Aliongea akilia zaidi na zaidi).

ANNA: (Anamfuta machozi Amina kwa kutumia kitambaa chake). Usilie sana Amina, acha yaliyopita si ndwele tuuyagange yajayo lakini si unamjuua alieyekugeia huo ujauzito?

AMINA: Mwaya, nipo njia panda, kutwa kuchwa kutembea na mijibaba mijitu mizima kama Zeee la PutaPuta. Kutwa kucha kutembea na wanafunzi wenzangu kama vile Ben, utadhani hapo nitamtaja nani aliyenisababishia huu ujauzito…Yaani nipo Njia panda.sina mbele, sina nyuma, sina ae wala bae). Mara wakasikia monitor wa darasa akimwita Amina aliyehitajika Ofinini kwa mkuu wa shule. Huko nako akakutana na macho yake Ben aliyekuwa akilia kwa uchungu ati asifukuzwe  shule kwa kosa la kumtia Mimba Amina. Mkuu wa shule alikuwa mkali kama Pili pili,. Hatimaye Amina alipewa barua ambayo aliambiwa aipeleke nyumbani kwa wazazi wake naye akafanya kama alivyoambiwa)

###

Itaendelea

No comments:

Post a Comment

I promise you

   I PROMISE YOU. (NINAKUAHIDI.) SURA  YA KWANZA. UBAYA WA POMBE. “Umenizingua job, umenizingua kwa muda mrefu sana mpenzi wangu…….kwanini l...