Sunday, October 6, 2024

Madanganyo (Black mail). Sehemu ya tano

 


SURA YA TANO

YUPO JELA.

Cheppe alipelekwa kituo cha polisi, ili sheria ichukue mkondo wake, wakati wote huo yungali mahututi kwa kipondo cha Umbwa mwizi, mapigo mazito aliyopigwa na wale wanaume wenye hasira hasara, walitaka kumuua kabisaa, labda apige magoti chini na kumshukuru Mungu wake aliye mnusuru na kifo kile. maana mapigo yale sio ya kuadithia. Bila ujio wa polisi waliopewa taarifa juu ya unyama aliotenda basi leo hii tusingelimsikia tena Cheppe, tusingelimuona wala tusingelipata fununu zozote zinazomhusu yeye, nakwambieni tayari mafuta ya Petroleum yalikwisha andaliwa kwa ajiri yake, matairi ya gari pamoja na zana zingine za maangamizi ziliandaliwa kwa ajiri yake. Duh! Kweli wananchi wana hasira, hawakujari kama wanajichukulia sheria mkononi.

                 Joseph alikimbizwa Mkuranga hospitali, haraka haraka huduma zilitolewa, ile sehemu yake nyeti, sehemu iliyokatwa kwa ukatiri wa roho ya bwana Cheppe ilishonwa vizuri, ikarudi katika hali yake. Mungu ashukuriwe uhai na uzima wa Joseph ulirejea tena. Maumivu yake yalikuwa ni maumivu makari na makubwa hajapata kuyaona maishani mwake mwote.

                  Miezi mitatu baadae Cheppe akiwa bado yupo mahabusu akisubiria kesi yake ianze kuunguruma, alitembelewa na Dakta John, yule Dakta aliyemshauri bwana Cheppe asiamini imani na mambo ya kishirikina bali awekeze nguvu zake zote katika kujua sababu zilizopelekea mkewe apate ugonjwa wa UKIMWI baada ya hapo Dakta john angelijua namna ya kumsaidia na kumshauri bwana Cheppe.

                   Siku hiyo Dakta John hakuja pekee bali alikuja na James mwanaye Cheppe ili apate kumsabahi babaye. Mikononi mwake Dakta  John alikua na kipande cha barua  ambayo Cheusi alimwandikia mumew aliyepo mahabusu akisubiria kesi yake ianze kuunguruma.

2018/ March/ 04,

MKURANGA.

PWANI.

Mpenzi Cheppe,

Saalamu mume wangu, Natumaini upo mzima.

Nimesikia habari juu ya yote yaliyokukuta, pole sana mpenzi. Najua ulikua ukinipigania, ulikua ukijipigania na pia ulikua unapigania maisha ya mwanetu James. Mpenzi mimi sina uhai tena, niliumbwa kwenye udongo ninarudi kwenye udongo, tena ninarudi na mazambi yangu tele. Nisamehe mpenzi.

              Mpenzi daima ukuchoka kuniuliza nini sababu iliyopelekea mimi kuugua ugonjwa wa UKIMWI? Nilikuficha mpenzi, lakini nitaficha hadi lini wakati mimi ni maiti iliyokwisha oza? Sina budi nikueleze, sababu maji yakimwagika hayazoleki, asosikia la mkuu guu uvunjika. Sikua mwaminifu kwako, nilipenda sana zinaa, baya zaidi zinaa yenyewe ni ile zinaa zembe, na sasa nimepurukutika sitamaniki tena. Nisamehe mpenzi, nisamehe mume wangu, nisamehe mimi muuaji,  nisamehe sana.

             Accha nikutakieni kwaheri ya kuonana.

                              Ndimi mkeo, Cheusi Mangara.

                  ****************************************

               Cheppe alikisoma kile kipande cha barua iliyo andikwa na mkewe mpenzi yule aliyempenda sana maishani mwake, yule aliyemuweka moyoni mwake, yule aliyempigania iwe kufa iwe kupona. Machozi yakambubujika.

                   “Vipi anaendeleaje mke wangu bwana Dakta?” Cheppe alimuuliza Dakta John akiwa tayari amekwisha soma kile kipande cha barua.

                   “Hatunaye tena duniani, ndugu yangu.”  Dakta aliongea, akakitibua kidonda  chenye maumivu ndani ya moyo wa bwana cheppe, machozi yakambubujika bwana Cheppe yakamtoka machoni, yakatambaa mashavuni yalikua ni mengi kama bahari.

Alimpenda sana Cheusi ajabu leo anaambiwa “Hatunaye tena duniani” hili neno lin maanisha nini? Je lina maanisha kwamba Cheusi ameaga dunia? Amekwisha tangulia mbele za hukumu? Oooh! Masikini Cheppe alimkumbatia mwanaye James. Machozi kama mvua yalimtoka alilia na kusikitika, alilia na kumlilia mkewe aliyejaribu kumpigania kwa kila imani hata akajikuta yupo tayari kumwaga damu ya mwanadamu mwenziwe mara baada ya kudanganywa na mganga wa jadi, Sangoma Mbeleko. Looh! Majuto mjukuu.


******* Machozi yalimtoka Cheppe ********


Mwisho

No comments:

Post a Comment

I promise you

   I PROMISE YOU. (NINAKUAHIDI.) SURA  YA KWANZA. UBAYA WA POMBE. “Umenizingua job, umenizingua kwa muda mrefu sana mpenzi wangu…….kwanini l...