SURA YA SABA
MAJUTO MJUKUU.Kila mtu ndani ya kijiji cha Kidundai alimjadili Mzee Jamali, kila mtu ndani ya kijiji cha kidundai alimlaumu Mzee Jamali kwa yale maamuzi ya pupa na yasiyo na busara, wivu wake ni kama kidonda tena kidonda kisichopona haraka, wivu wake ulimfanya ajifungie ndani ya nyumba yake akilia usiku na mchana, anajuta kwa kufanya maamuzi ya haraka haraka pasina kutumia busara. Loh! masikini mzee Jamali majuto ni mjukuu, anayajutia maamuzi yake.
Kuna tatizo jingine lililojitokeza mara baada ya Mizimu pamoja na Miungu kumpatia adhabu Mzee Jamali, choo chake kiliziba, utumbo wa tumbo lake ulifunga, ulifunga siku ile ile, aliyopewa adhabu kubwa ya kugeuzwa mnyama wa kufugwa, tabu aliyoipata wakati haja kubwa inahitaji kupita ilikua ni tabu kuu, tumbo lilimviringa viringa, chakula alichokula hakikutoka nje, maji aliyokunywa hayakutoka nje wiki nzima aligugumia maumivu makali ya tumbo.
Nduguze waliogopa kumpeleka hospitali wakihofia usalama mdogo ambao wangeliupata wakiwa ndani ya hospitali. Walimwita Dakta ambaye walimweleza hali halisi ya tatizo la Mzee Jamali. Dakta aliwaelewa naye akaanza kazi yake mara moja. Upimaji ulifanyika na vipimo vilionesha kuwa utumbo wa Mzee Jamali ulikuwa umesinyaa. Kutokana na kusinyaa kwake takataka za tumbo zilishindwa kupita kwa urahisi. Basi ukapitishwa mkono wa Dakta kunako kinyenyeo cha mzee Jamali, taka taka zikavutwa kwa nguvu zote nazo zikatolewa zikiwa tayari zimeharibika kwa kuwatoa wale wadudu waitwao funza.
Loh! Salale, msalie mtume! Ndugu yangu matatizo mengine binadamu wanajitakia wenyewe, tizama siku zilivyozidi kukatika tumbo la Mzee Jamali lilianza kuumuka umuka kama mtu aliye tafuna gunia zima la amira, tena likaumuka umuka na kutaka kupasuka,
Tunu hofu ilimjia juu ya afya ya Mzee Jamali aliogopa sana hali ya Mzee Jamali , ukitegemea hapo awali wawili hawa walilala juu ya kitanda kimoja kwa sasa Tunu alijikuta anamuachia kitanda Mzee, ampishe ili auguze hilo tumbo lake kubwa ajabu.
Kilio, majuto, maumivu na masikitiko ni baadhi ya vitu vilivyotawala kichwa cha Mzee Jamali.Tunu pamoja na mwanaye Ally walimsihi Mzee akaiombe radhi Mizimu, Miungu iliyompatia adhabu, kutokana na kutawaliwa kwa zile fikra na hisia zilizo jaa wivu, kijicho, gere na husuda. Mzee Jamali alizidi kuchelewa, tumbo lake lilizidi kuwa kubwa tena tumbo kubwa la kutisha. Hatimaye usiku mmoja akiwa amelala kwa taabu na kwa majuto makuu, tumbo lake lilizidiwa nguvu, mishipa yake ikawa dhaifu. Mishipa hiyo ilitanuka na kuumuka kwa kadri tumbo lilivyotuna na kuwa kubwa ajabu.
Masikini mzee Jamali alikua ni mtu wa kulia mbele ya mwanaye Ally na mkewe Tunu, alilia akiomba asamehewe, alilia akiiomba Mizimu ya kwao imsamehe kwa sababu Mizimu ilikasirika na kuchukizwa na hisia zake, alilia, alilia ili Miungu impatie radhi. Yote tisa kumi maombi yake hayakufua dafu mbele ya macho ya Miungu .
Tumbo lake lilianza kuchanika kadri lilivyokua likiumuka, lilichanika chanika kama nguo kuukuu inavyochanika ikilia ‘charuuu chachachacha’ lilichanika akiwa analitizama lilichanika kutokana maumivu makuu aliyoyapata pamoja nayeye kushindwa kuingia maliwatoni ili apate kutoa haja kubwa na haja ndogo. Mungu wangu we! Funza, funza walitapakaa ndani ya chumba alicholala Mzee Jamali, walitapakaa huku na huko. Mzee Jamali akiwa anawatizama, kwa macho yake yote mawili, walitapakaa mbele ya mkewe na mwanaye mpendwa Ally alipokuwa akikata roho Mzee Jamali alilia sana na kuomba msamaha.
Wazee wa mila, mila za wasambaa, wabondei, Wapare na wapogoro, waliitwa usiku ule, usiku ambao Mzee alijikuta anapoteza maisha yake. Onyo kali lilitolewa, asishikwe wala asiguswe mwili wake, wacha azikwe ndani ya kile kijumba nyasi chake alichopatwa na umauti, na hicho kijumba nyasi sharti kibomolewe chote, kitupwe kama zege linavyotupwa, kizindikwe kama zege linavyozindikwa, Kibomolewe. Hatua iliyofuata ikawa ni kukibomoa kile kijumba nyasi cha Mzee Jamali, kijumba ambacho Mzee alifia humo,
Ikapigwa mbiu, mbiu ndani ya ukoo wa Mzee jamali, ndugu hawakupaswa kugawana mali za Mzee, mali za mtu aliyetupiwa laana, laana ya Miungu, Miungu ya koo za wasambaa, Wadigo, wapogoro na wapare.
Hakuruhusiwa mtu aiguse mifugo ya Mzee Jamali,
Hakuruhusiwa mtu aziguse biashara za Mzee Jamali,
Hakuruhusiwa mtu aziguse nyumba za Mzee Jamali,
Hakuruhusiwa mtu aziguse nguo za Mzee Jamali
Tunu mkewe Jamali hakuruhusiwa,
Ally mwanae mpenzi hakurusiwa,
Tena hakuruhusiwa mtu awe karibu na Tunu au Ally,
Amguse Tunu au Ally kwa vidole vyake.
Mzee Jamali alikua ana mashamba mengi,
Nyumba nzuri, mke mrembo na mzuri,
Biashara nzuri pamoja na vitu vingine vingi vya thamani,
Hakuwa mchache wa mali.
Wazee wa mila walitoa onyo, mtu yeyote yule ambaye angelithubutu kugusa kitu chochote kile kilichoachwa na marehemu mzee Jamali basi ile laana aliyotupiwa mzee Jamali ingelishika nafsi na kupenya kisha kuingia ndani ya mwili wa huyo mtu aliyegusa au kuchukua mali za Mzee Jamali. Ndugu walitia hofu kuu juu ya usalama wao binafsi, ukitegemea tamaa zao za kurithi au kugawana mali za Mzee Jamali ziliwika ndani ya mioyo yao walijikuta wanawaendea wazee wa mila waiombe Mizimu, Miungu na Mashetani, waiombe msamaha ili maisha yao yapate kuendelea kama siku zile, siku zile kabla laana haija mkumba Mzee Jamali.
Wazee wa mila waliingia kazini, waliingia tambikoni, kuishawishi Miungu yao itoe msamaha juu ya ukoo wa Mzee Jamali pamoja na kuifuta laana iliyotua juu ya kila kitu alichomiliki Mzee Jamali.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment