SURA YA NNE
HISIA HAZIJENGI.
Ni mwezi mmoja sasa, mwezi mmoja umepita tangu kipindi kile Mzee Jamali ashikwe sharubu, alambe Joker, azidiwe kete na Mzee mwenziwe mzee Shemagendo, rafiki yake mkubwa japo mnafiki. Ndani ya mwezi huu furaha ya Mzee Jamali imekuwa haba na haba iso jaza kibaba, anahuzuni na masikitiko amepoteza amani yake, yale mapenzi aliyo jivunia yameyeyuka na kupotelea mbali, sio mcheshi wala sio mchangamfu kama zamani. Amekua na mawazo chungu nzima, mawazo yake hayana kikomo.
Mara atawaza juu ya hasara kubwa aliyoipata baada ya kuzidiwa kete, jitihada zake za kutaka kumshitaki Mzee mwenzie mbele ya Baraza la Wazee hazimpi matumaini, tena hazijazaa matunda, zimegonga mwamba, sababu yeye binafsi amepoteza ushahidi.
Si hilo tu bali kuna hili jingine, hili linalomtibulia kichwa na ubongo wake juu ya hawa wawili wanao mnyima raha na usingizi. Hawa wawili wanaomfanya aione dunia kama vile inamuonea, japo kimoyo moyo anaumia haoni haja ya kuyaonesha maumivu ya moyo wake, haoni haja ya kukionesha kidonda cha moyo wake, haoni haja ya kuwakemea wabaya wake, amejaa wivu, wivu kidonda, kidonda kinachomuuma sana.
“Ndio adha ya kuoa dogo dogo.” Mzee Jamali anawaza yeye na mtima wake, leo yupo Lushoto Sokoni, anafanyia biashara zake, biashara ya kuuza nyanya, vitunguu, mboga mboga na matunda. Analo genge lake, biashara kwa kiasi fulani inamtoa kimaisha ndio maana kamwe hajapata kulala njaa yeye na mkewe Tunu pamoja na mwanaye Ally. Mbali na biashara kilimo na ufugaji kwake ni utukufu analima sana, analima pasina kuchoka, analima kama Mwendawazimu, tangu zile siku za ujana wake hata sasa uzee bado haujamtupa. Kilimo ni utii wa mgongo, kilimo kwake ni kila kitu hawezi kukikacha na kamwe hategemei kukikacha hadi mwisho wa dunia.
“Ninakuona hauko sawa ndani ya siku hizi mbili tatu Mzee mwenzangu.” Mzee Shemagendo hasimu wake mkuu aliongea. Amekuja kumtembelea Mzee mwenzake gengeni ndani ya soko kuu la lushoto. Amekuja japo kumtania tania ili apate kuyapunguza mawazo yatokanayo na ile hasara aliyovuna mara baada ya mifugo ya Mzee Shemagendo kutibua shughuli iliyokua tayari imekamilika kuingizwa Sokoni na kupelekwa ndani ya majiji makubwa Tanzania, avune faida aliyotarajia.
“Nipo sawa,” Mzee Jamali alijaribu kujitetea ili apate kuficha hisia juu ya chuki yake, chuki juu ya mapenzi aliyonayo kutoka kwa mkewe Tunu na mwanaye Ally.
“Sio kawaida kukukuta katika hali uliyonayo.” Shemagendo aliendelea kunena.
“Ninakujua vema Mzee, ninakujua tangu zile zama zetu utotoni, zama zile tulicheza pamoja, tuliogelea pamoja Mtoni, tulicheza mchezo wa kako na komborela, tuliruka kamba na kufukuzia panzi mijusi na vipepeo, tuliingia ndani ya misitu iliyosheheni majani na vichaka vilivyo jaa kiza na giza totoro.” Shemagendo alijaribu kumkumbusha Mzee mwenzie zile zama za ujana wao.
“Nipo safi sana bwana mdogo,” Mzee Jamali alijaribu kuzificha tena hisia zake, ingawaje moyoni alijisuta na kujiumiza kwa jinsi anavyo ficha uchi. Alitamani amweleze Mzee Shemagendo yale yote yamsumbuayo moyo. Anajua fika kuwa mficha donda aibu umuumbua. Moyo wake uliendelea kupingana na hisia zinazoutesa Mtima.
“Mmmh! Sijui nimweleze Mzee mwenzangu juu ya hali halisi ya mahusiano ya mwanangu Ally na mke wangu Tunu?” Leo hii Mzee Jamali anajaribu kupingana na siri aliyoificha moyoni. Wakati huo huo tayari ule moyo wake, moyo mgumu kama jiwe umekwisha anza kulainika sasa anafikiria ajipange namna gani amweleze Mzee mwenzake juu ya tatizo linalo hutibua moyo.
################################
“Ndio hivyo Mzee mwenzangu, ndio hivyo chungu kimoja mapishi mbali mbali, ndio adha ya kuoa watoto wadogo wadogo.” Aliongea Mzee Jamali mara baada ya kumhadthia Mzee Shemagendo mwanzo hadi mwisho wa simulizi inayomtia wivu.
“Yote niliyonena sijayaficha wala sijakuficha neno, mwenzio nipo njia panda, sielewi nifanye nini kama ni kumpenda huyu binti tayari nalikwisha kumpenda lakini sasa moyo wangu umekua mashine, sina raha, sina furaha sina amani nina hasira na kisirani juu ya mapenzi waliyoyajenga wawili hawa waninyanyasao.” Mzee Jamali aliongea kwa kirefu.
“Mzee mwenzangu, kumbuka wahenga wanasema chako ni chako hata kama ni kibaya namna gani,”
“Ninakumbuka na pia ninajua kuhusu hilo.” Jamali alimjibu Mzee mwenzie.
“Cha mtu mavi anakipenda yeye mwenyewe.” Aliongeza maneno Mzee yule.
“Shaabashi! Embu nieleze Mzee wewe kama wewe umechukua hatua gani muhimu kuidhibiti hali hiyo isiendelee? Je, umewapiga onyo? Je, umewataadharisha kujiadhari kabla ya hatari?” Shemagendo aliuliza.
“Hilo sijalitia moyoni, sijatilia maanani kuchukua hatua na taadhari, sioni haja ya kuwapiga onyo ati wajiadhari kabla bahari kuwa shari,” Aliongea Mzee Jamali wakati huo wawili wale walikua wameketi pembeni ya biashara anayoiendesha Mzee Jamali. Wametulia tuli kama maji mtungini, wametulia kuyajadili mapenzi yaliyopo kati ya Tunu mke wa Mzee Jamali pamoja na Ally mwana wa Mzee Jamali.
“Mmmmh! Hapana Mzee, itakua vema kama utawataadharisha mapema juu ya suala hili, wapige onyo kali ukitumia maneno yaliyo jaa mafumbo methali nahau na majigambo. Hisia tu hazitoshi, hisia juu ya mapenzi uyaonayo kwa Ally mwanao na Tunu mkeo.” Shemagendo alijaribu kumshauri Mzee jamali.
“Lakini mbona nimekwambia wawili hawa wana kila darili za kunipoka na kuyamiliki mapenzi yangu, wawili hawa wananiibia mapenzi. Je, kuna haja gani kuwapiga onyo juu ya yote haya? Yote niyaonayo mbele ya macho yangu, ninayaona live, hayana kificho na ubaya wa haya wayatendayo wanayatenda kwa uhuru zaidi,” Mzee jamali alijitahidi kujitetea.
“Hata kama Mzee mwenzangu, hata kama macho yako yanatizama na hisia zako zina hisi, mie ninakushauri ufanye juu chini uwaketishe Barazani hawa wawili, uwaeleze kinagaubaga juu ya chuki uliyonayo kuhusu mausiano yao. Ukiwaeleza matumaini makubwa utayaona kwani utapata amani, hautasikitika tena. Hisia pekee hazitoshi sababu hisia hazijengi, tena hisi kamwe haziwezi kukusaidia kuurejesha upendo uliopotea .” Shemagendo alihitimisha ingawaje Mzee Jamali bado alikua kichwa ngumu
Itaendelea.
No comments:
Post a Comment