Wednesday, July 2, 2025

I PROMISE YOU

 


Tendo  la mie kujiuzuru kunywa matapu tapu likawa  pia ni mwisho wa Brenda kunywa . Maji ufuata mkondo, Brenda alinifuata aliungana nami ili kumpiga vita adui pombe. Nakumbuka vizuri, naikumbuka tarehe 25 mwezi wa pili mwaka 2016  ni tarehe iliyonifanya nichukue uamuzi mgumu wa kwenda nje ya mkoa wetu Iringa, nikaelekea ndani ya jiji la Dare s saalam.


Lengo likiwa kutafuta shughuli yoyote ile ya kunitotongotongo. Sio tu kunitoa kimaisha pia kunitimizia malengo yangu mengine kama vile kumtimizia Brenda furaha ya mtima wake. Si anataka nimuoe? Yes, anataka nimuoe lakini siwezi kumuoa pasina kufuata mila na desturi za kiafrika, ni lazima nimtolee mahari, sherehe kubwa ya kupendeza na baada ya hapo nimuweke ndani ili awe wangu, wangu wa milele.

             Sikupenda kuwa mbali na walezi wangu, babu na bibi, sikupenda kuwa mbali na macho ya Brenda, ilinibidi nikubali kuwa napaswa kuondoka, napaswa kwenda mbali na mji wa Iringa, nikatafute riziki na iwapo nitafanikiwa napaswa kurejea nyumbani haraka iwezekanavyo, haraka  mara baada ya kufanikiwa nikijua fika kuwa mwenda kwao si mtoro, mjasiri aiwachi asili.
Basi mpenzi wangu Brenda akaniandalia kila kitu kwaajiri ya safari yangu na uzuri wake nauri ya kwenda jijini Brenda alinitafutia. Babu na bibi walinitafutia  pesa ya makuli na malazi mara nifikapo jijini. Sikua na jinsi ilinibidi niondoke niende ndani ya jiji nililo amini kuwa nitapata kazi. Penye wengi pana mengi, nilijiamini na pia niliamini kwa kudra za Mwenyezi Mungu kazi nitapata, kazi ya kunitoa kimaisha. Japo mie ni mvivu wa kufanya kazi sina udhoefu wa kufanya kazi yoyote ile, nilikuwa ni mzoefu wa kunywa pombe. Pombe pekee ilikuwa fani yangu sikuwa na kazi nyingine niliyoipenda kama kunywa matapu tapu.

                 Looh! Ndugu zangu pombe iliniharibu, kimwili na kisaikolojia, sikuhitaji kufanya kazi yoyote ile, nilikuwa mzoefu wa pombe na kunywa pombe ilikuwa ni kazi yangu, sikuwa na kazi yoyote ile ya kuniwezesha kimaisha, kilimo kilikua ni cha babu na bibi, walilima walipanda walivuna waliuza na kunipatia pesa ambazo kila siku ziliishia kwenye bunge la walevi, nami nikachangia pesa ya pombe, kila siku ili nipate kiburudisho cha mdomo wangu.
        *******************************
              Saa nane mchana niliingia ndani ya jiji la Dare s saalam, sikuelewa nitaanzia wapi kwenda au nitafikia kwa nani? Nimeondoka kijijini na kuja mjini ati kutafuta maisha, hivi mimi ni mpuuzi wa maisha ya aina gani? Nilijiuliza mara baada ya  kutoka Ubungo Bus terminal. kituo kikuu cha mabasi yaendayo na pia yatokayo mikoani.

             “Hivi nimefanya uamuzi gani mimi?” nilijiuliza tena safari hii moyo ulianza kunilaumu kwa uamuzi wangu wa kutoka kijijini kuja mjini kutafuta maisha, kwenye mji wa watu nisio wajua, sina undugu nao, sina ujamaa nao wala sina mahusiano nao.

              “kwanini nimeondoka kijijini, sehemu ambayo kuna kila kitu ninachohitaji haraka ningelipata, chakula cha kutosha, maji, matunda ya kutosha, pahali pazuri pa kulaza kichwa changu, marafiki wenye heshima zao, ndugu jamaa na majirani, mimea wadudu na wanyama. Mmmh!” Niliguna mimi na moyo wangu bado mawazo yalilindimaa.

“Nina  nini mimi?je hakuna kazi yoyote ile ya kuniwezesha nitoke vema kimaisha nikiwa kijijini? Mbona wapo wasusi wanasuka mikeka , makapu, kofia na nyungo? Mbona wapo wafinyanzi? Wasanii wa vikundi mbali mbali vya ngoma wanatumbuiza na kuvuna fedha zao? Wawindaji hawakosi nyama, matunda, mayai na asali ya kuleta nyumbani. Wakulima ni wengi wenye faida, wanailisha dunia  matunda ya aina mbali mbali; mafenesi machungwa mapeasi, mabohora, matango, matikiti maji mapera ndizi na mananasi. Kilimo cha mahindi, viazi mtama, uwele, ulezi, mpunga, maharagwe, kunde na mbaazi.” Vyote hivyo mie goi goi nilikuwa msindikizaji tu, nikiwasindikiza wakulima wajibidishe katika shughuli za kilimo japo mie mzembe na mvivu kazi yangu kula, kunywa na kulala.

                 “Je kijijini hakuna ulinzi? Nilishindwa kujiunga na jeshi la wana mgambo? Je kijijini hakuna biashara? Mbona zipo nyingi zile za masokoni, zile za madukani, zile za kuingiza na kutoa mali ndani na nje ya kijiji. Kuna uvuvi, kuna ufundi uwashi, kuna mengi ya kujivunia, nimeshindwaje kujibidisha katika hayo, nimefanya maamuzi ya kuushangaza mtima wangu, maamuzi ya kuondoka  kijijini na kuja mjini kutafuta maisha. Nimekuja kutafuta maisha gani ikiwa ningali ninajua kuwa hata kijijini maisha ambayo nimekuja kuyatafuta mjini yapo. Tena yapo fresh tu.” Niliwaza sana siku ile.
                 ‘Piiiiiiiiiiii…..Pooooooo………Piiiiiiiii!’ ilikua ni sauti ya gari, Mitisubish pajero kama sikosei, ilifunga breki karibu karibu na miguu yangu, wakati huo huo mshamba mie  nilikua najiandaa kuvuka barabara kuu ya lile eneo la ubungo.

               “Yallah! Toba! Nimepona mie.” Niliongea mie na mtima wangu mara baada ya kuiona ile gari ikiwa imesimama pembeni ya miguu yangu dereva aliyekuwa ndani ya ile gari alinitizama kwa chuki na kwa hasira. Aliugundua uzembe wangu uzembe barabarani, nilivuka barabara pasina kuzingatia sheria za brabarani, nilivuka tu kama mwendawazimu, nilivuka pasina kujielewa elewa, nilivuka pasina kutazama wapi  utokao wa yale magari na wapi uendao wa yale magari pamoja na motokaa zilizoongozana kama farasi.

                “Una nini wewe kijana?” Mwanaume mtu mzima aliyeonekana kushiba vya kutosha, alichomoka ndani ya gari yake mara baada ya kuiegesha ile pajero  pembeni ya barabara. Ana nywele nadhifu nyeusi  zilizonawili amevalia shati ya blue tai nyeusi na koti moja yenye rangi nyeusi,, ni mnene kiasi,  katupia miwani machoni.
                Ukimtazama mara mbili mbili waweza sema moyoni mwako mwanaume yule ni mwenye pesa zake anajiweza kiuchumi, ni kibosile fulani ndani na nje ya serikali kama sio kibosile basi ni kigogo fulani hivi ndani ya nchi. Any way hisia hazijengi sikuhitaji kuziruhusu hisia za moyo wangu kutawala fikra na mawazo yaliyojaa moyoni mwangu kama ni kupona nimepona, nisije nikapoteza miguu na viungo vyangu vingine nikiwa ugenini, nipo salama salimini, kwanini nisimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniepusha na majanga yale.

Aki! mbona ningeteseka ugenini kama ningelipoteza miguu yangu au kama nigelipoteza jicho langu la kushoto, wakati huo huo nimekwisha poteza jicho la upande wa kuume mmh! Nilipoteze na hili lililobaki kwa bahati nasibu? Mmmh! Janaba,mmmh!  Huruma jamani.

                “Samahani Bwana mkubwa nina upofu jicho langu la kulia hili lililosalia halioni vema, ndio maana nimevuka pasina kuwa mwangalifu.” Nilijitetea ili kupunguza hasira za yule Bwana mkubwa macho ya wengi yalinitazama , macho ya wengi yalitamani kujua mwisho wa ile sinema yetu.

                “Aaahh! Kumbe una upofu wa macho, ooh! Pole sana kijana.”  Yule kibosile alinipatia mkono  wa faraja mara baada ya kumueleza matatizo yangu.

              “Pole sana kijana wangu, embu nieleze ni wapi unaelekea ndani ya jiji ?” Bwana mkubwa aliniuliza.

              “Sina pahali pa kwenda bwana mkubwa, mimi ni mgeni ndani ya jiji, nimetokea Iringa kijijini nimekuja jijini japo kubahatisha  labda nitapata kazi itakayo niwezesha na  itakayonibadirisha kimaisha.” Niliongea kwa kirefu, nilitia huruma kama kondoo mwenye kuhitaji maji na chakula,  nikiwa nimeshikilia kibegi changuo chenye nguo mbili tatu pamoja na fedha za kujikimu.
                

“Oooh! Pole sana mdogo wangu, embu tuokoe muda kidogo, ingia ndani ya Gari yangu tutoke eneo hili, niko bize kidogo ninaelekea Kariakoo kwenye mishe mishe zangu? Yule bosi aliongea.

Je, niingie au nisiingie ndani ya ile Gari ya huyu kibosile? Nilijiuliza. Swali lililonijia ghafla ndani ya kichwa changu.

Wacha niingie tu, yawezekana ikawa ni zari la mentari. Nilijisemea mimi na moyo wangu kisha nikaingia ndani ya gari ya yule Bwana mkubwa. Nilipotaka kuketi nyuma ya siti ya ile gari Bwana mkubwa alinikataza nisikae nyuma akaniruhusu nikae mbele ya Gari.

               Harufu nzuri ya marashi pamoja na manukato yalipamba pua zangu, nilijisikia aibu  kidogo sababu mnuko wa mavazi yangu niliyotoka nayo kijijini uliingia ndani ya ile Gari na kutibua hali ya hewa, japo yule bwana mkubwa hakujali  kuhusu hali yangu ya kutibua hewa alikwisha kufungua vioo vyote vya ile Gari ili hewa nzuri ipite na kuingia au kutoka ndani na nje ya ile Gari na uzuri wake yule Bosi aliwasha kiyoyozi (AC) kilichofungwa ndani ya Gari yake kikatuperuzi peruzi kwa ubaridi wake na kutumiminia hewa safi ya kupendeza.

                “Niite Bwana Steven Biko, ni meneja wa kiwanda cha kutengeneza, kusambaza na kuuza bia ndani na nje ya Tanzania.” Yule Bwana alijitambulisha kwangu.

               “Je wewe ni nani mwenzangu? Ningependa kukujua zaidi.” Aliongea yule bosi akiendelea kuiendesha Gari yake, wakati huo huo nilijua kuwa tunaelekea kariakoo, kama alivyonieleza.”

                “Asante sana kwa utambulisho wako Bwana mkubwa.” Nilimshukuru yule bosi nikimtizama kwa kutumia kile kijicho changu kimoja kilicho hai, ukitegemea jicho langu moja lilikwisha kupoteza uzuri wa kutazama.     

              “Mie naitwa  Bwana Job Mkwawa, ni mzaliwa wa Iringa kijijini, kabila langu mhehe umri wangu miaka ishirini na mitano, sina mwenyeji hapa mjini, kama nilivyokueleza , nimekuja mjini kutafuta maisha nitafurahi kama nitafanikiwa kupata nafasi ya kazi, sijali ni aina gani ya kazi, yoyote ile nipotayari kuifanya Bwana wangu niliongea kwa matumaini ya kusaidiwa,

               “Ah! Kumbe Bwana Job wewe ni mwenyeji wa Iringa?” yule bosi aliyejitambulisha kwa jina la Steven Biko aliniuliza akiwa na kiasi kikubwa cha tabasamu mdomoni mwake.

                   “Ndio Bwana  Steven Biko .” nilimjibu yule bosi, wakati huo huo jicho langu moja linalofanya kazi lilikua likishangaa shangaa umati mkubwa wa watu waliokuwa bize wakielekea kwenye miangaiko yao.


                    “Waooo! Kumbe nimekutana na mtani wangu, mimi ni Mnyakyusa nyumbani kwetu Tukuyu Mbeya, nilizaliwa huko nikapewa elimu yangu na baada ya kumaliza chuo nilipata ajira ndani ya kampuni ya Bia.” Steven Biko aliongea, mie nikajawa na furaha mara baada ya kugundua kumbe nina mwenyeji wangu amabaye ni mtani wangu na uzuri wa yule mtani anatokea mkoa ulio karibu karibu na nyumbani Iringa.

Gari iliendelea kuchanja mbuga mie mshamba na mgeni ndani ya Jiji hili nilikuwa mtazamaji, nikitizama uzuri na urembo wa lile Jiji, lililopangiliwa na kupangika kwa wingi wa mahorofa, balabala zenye ubora na uzuri wake, wafanyabiashara ni wengi pomoni kila mtu yuko bize na shughuli zake, shughuli  za kujitafutia riziki na bahati ya kila siku.

                 “Tupo wapi hapa mtani wangu?” nilimuuliza Biko mtani wangu.

“Hapa ni katikati ya jiji panaitwa Kariakoo, mbele kidogo njia ilee (akainyoshea mkono) ni barlabala ya kwenda Posta. Posta ni sehemu wanayoishi watu wenye fedha zao, wazito wa ndani na nje ya nchi, kule kuna maofisi ya viongozi wa serikali mabalozi wa mataifa mbali mbali wapo kule, kule ni paradise ndogo yenye kuvutia.”

               “Kumbe Jiji hili ni lenye fahari kubwa sana?”

                “Yes, huu mji ni johari ya watalii na wgeni wengine wengi, wanaokuja kwa ajiri ya shughuli zao za kila siku.”

                “Dah! Nitafurahia sana iwapo siku moja nikipata nafasi ya kulizunguka jiji.” Niliongea kama vile tayari nimekwisha kulizoea hilo jiji.

                 “Ondoa hofu mtani wangu, ipo siku nitakupeleka baharini ukazione meli, si unazijua meli au unazisikia tu?”
                 “Nazisikia tu wala sijapata kuziona.”

                  “Hilo sio tatizo kikubwa ni kumwomba Mwenyezi Mungu uhai na uzima ili siku moja tupate kwenda kufurahia raha za jiji.” Biko aliongea.

                 “Pesa pekee ndiyo inayoongea kijana wangu, hili ni Jiji la raha na starehe. Raha na starehe pasina pesa ni kazi bure.” Biko aliongea kama vile mie na yeye tumejuana muda mrefu sasa kumbe tumefahamiana dakika chache zilizopita, tena kufahamiana kwetu ni kwa bahati tu.”

               “Shukrani mtani wangu, siku nitakayotembezwa ndani ya Jiji itakuwa ni siku ya furaha kubwa kwangu,” niliongea kwa furaha.

                “Bwana Job nina swali nahitaji kukuuliza” Biko alinishitua kidogo, nikamuitikia kwa kutingisha kichwa kumuashiria kuwa ruhusa ya kuuliza imekubaliwa.

                “Vipi kuhusu elimu yako, umesoma hadi kufika levo gani?”wakati huu Gari ya bwana Biko ilikua ikingia ndani ya kiwanda cha BIA, nilikitambua kiwanda kile kuwa ni cha BIA kwa sababu kilikua na bango lililoandikwa Tanzania Brew company limited (TBL)

                “Kidato cha nne ndio kiwango changu cha elimu,” Niliongea

                 “Oooh! Safi sana, kijana unaonekana unanguvu za kutosha kufanya kazi, kwa juhudi kwa maarifa na kwa ufanisi mkubwa pamoja na moyo wa kujituma.” Biko aliongea maneno ya kutia matumaini nami nikakoleza chumvi.

                “Yes l can do so soninaweza.” Nilimjibu kwa kimombo kilichochanganyikana na Kiswahili. Bosi aliipaki Gari yake karibu na Ua kubwa lililiopo ndani ya kiwanda kile.
                “Safi……Good.”  Biko aliongea , tukatelemka kwenye Gari yake, nikamfuata kule anakoelekea, nikiwa nyuma nyuma kama umbwa amfuataye Bwana wake, mikononi nalikua nimekumbatia  Begi langu kuukuu lenye nguo kuukuu.

                 “Wacha nikwambie kwa kifupi bwana Job, wewe una bahati kubwa sana kuonana na pia kujuana na mimi, kampuni imepungukiwa wafanyakazi, kwa hiyo tunahitaji wafanyakazi wa kutosha, jihesabie kuwa ni mtu mwenye bahati, kazi tayari ipo mikononi mwako, wewe utakuwa ni miongoni mwa wafanya kazi wa kampuni yetu. Usijiulize moyoni kwanini nimekupatia nafasi hii ni kwa sababu ninajua kuwa wewe unahitaji kazi na kazi tayari umekwishaipata.

                “Waoooo! Moyo wangu uliliripuka kwa shangwe japokuwa bado sikujua ni nafasi gani ya kazi ambayo napaswa kuishughulikia hilo halikunitia wasiwasi nilihitaji kuwa na subira subira yavuta heri, nitaambiwa hapo baadaye ninapaswa kufanya nini?

               “Bwana Job nitakupatia nafasi ya kuingia kwenye utengenezaji wa kilevi hiki kinachopendwa na  watu wengi ndani na nje ya Afrika mashariki. Kwanza kabisa utafundwa namna ya kutengeneza Bia na baada ya  sisi kuridhia uelewa wako katika utengenezaji wa Bia ndipo utaingia jikoni kuuchochea moto ili tengenezo lako likamilike na uzuri wa kazi yako  hautakuwa pekee utaambatana na wenzi  wako wengi  mtagawana majukumu mbali mbali ya jikoni.” Aliongea Steven Biko ameniacha mdomo wazi nisitake kuamini bahati kubwa kama hii , yaani leo hii hii ninaingia ndani ya Jiji  ninabahatika kupata nafasi ya kazi hata kabla ya kutanga tanga na njia.

              Bwana Steven biko aliniingiza ndani ya  Ofisi yake, Ofisi moja nzuri ya kitalii, ofisi ile ina mvuto, sio wa kuhadithia kwa maneno matupu yatokayo mdomoni mwa watu, bali ni kwa matendo thabiti kwamba imeboreka na kuboreshwa. Imepambwa kwa tunu na medali mbali mbali ambazo kampuni hiyo ilizitwaa baada ya ushindi mnono uliotokana na ushindani wa makampuni.
      
        “Nitakupeleka kinyerezi, nje kidogo ya mji wa tabata ninamiliki nyumba yangu moja huko, ipo ipo tu hakuna mkaaji wewe ndiye utakaye kuwa mkaaji hapo,” Biko aliongea moyo wangu ulifulumia kwa furaha na shangwe isiyo na kifani. Kitendo cha Biko kuniamini namna ile kilinishangaza,  bado ni mgeni kwenye macho yake hanijui wala simjui vizuri. Jambo hili ni lenye heri na fanaka ni Baraka tele  kwangu, nikajiona na kujisikia kuwa ninapendwa pendo ndani ya pendo.

  Muda si mrefu alikuja binti mmoja mrefu mwembamba, ana macho  yenye mboni za paka, ngozi yake ya kiaribino nywele zake zina rangi ya kaki, haijakolea sana. Biko alinitambulisha kwangu kuwa huyo ni Secretary wake. Jinale Riziki. Riziki akatuburudisha kwa kutuandalia vinywaji  soft, matunda na  vitafuno vya kuburudisha midomo yetu. Sikupenda mtoto riziki apite zake na kuondoka kabla sijajitambulisha.

 nikajitambulisha kwake  Riziki alifurahishwa na uwepo wangu akanikaribisha kwa moyo wote mimi kama mfanyakazi wa pale.

                  Hatukukaa sana pale kiwandani Steven biko alihitji nikapumzike kwenye nyumba aliyo niandalia, nilikuwa na shauku ya kutaka kuiona hiyo nyumba aliyonieleza Steve.
                     ################################
                  Looh! Kumbe Dar es salaam ni Jiji zuri machoni kwa wengi wanao ingia na kutoka, kweli macho hayana pazia mtu usikubali kuambiwa  njoo ujionee wewe mwenyewe.  Juma mosi ya leo Bosi wangu alimuomba Secretary wake Riziki anitoe out. Nikaangaze angaze macho yangu huku na huko, nikapoteze ushamba wangu wa kihehe, nikafurahie mandhari ya waswahili,  wapemba, wazaramo na waruguru. Nikajionee fukwe za bahari ya Hindi, majumba ya kisanaa pamoja na mitaa mbali mbali iliyopo ndani ya jiji lililobarikiwa na Mwenyezi Mungu kwa kuwa na kila kizuri majaliwa. Kwa kifupi Dar es salaam ni mbingu moja nzuri yenye paradise ndani ya dunia.

              Kizuri, hakikosi kasoro, jiji la Dare s saalam sawa ni Jiji zuri linalopendeza machoni, lakini pia hata hivyo Jiji lina mapungufu yake kwa mfano mitaa ya kariakoo kama vile Faya, Big bone, na Mnazi mmoja Sekondary ni maeneo yaliyo jaa vibaka, mateja na wahuni wengine wengi. Mitaa ya Buguruni haswa  haswa Buguruni sokoni uchafu umerindimaa ni rahisi sana kwa magonjwa kupenya.
Nenda kigogo  ya mburahati, nenda jangwani, maisha ya watu wa huko ni ya chini sana umasikini uliopo maeneo hayo ni umasikini wa kuogopesha ni kama vile hawana serikali waungwana hawa ni kama vile Serikali haiwasaidii waja wa Mwenyezi Mungu, majanga mbali mbali kama vile magonjwa ya milipuko (kipindu pindu) na mafuliko ni moja ya taabu zinazo watesa waja hawa.
Kwa kifupi mtoto Riziki alinionesha uzuri na ubaya wa Jiji lenye mamilioni ya watu, jiji lenye maelfu ya Magari majumba ya fahari na biashara za kila aina. Binafsi nilihisi kukaribishwa, binafsi nilijiona nipo nyumbani, ukarimu na mapenzi niliyopewa ulinihamasisha na kunitia moyo wa kutafuta yale maendeleo ambayo ndiyo nimekuja kuyatafuta ndani ya jiji la Bongo land.

Hazikupita siku nyingi nilianza kazi ndani ya  kile kiwanda cha BIA, nilifunzwa  nini ninachopaswa kufanya mimi kama mimi ndani   ya ilekampuni, nilifunzwa nikafunzika, upishi wa pombe  ndio ulikuwa wajibu wangu niliwajibika ipasavyo. Nikikumbuka kuwa hapo awali kabla ya kuja ndani ya jiji nilikuwa mlevi wa kutupwa mlevi mwenye cheo ndani ya Bunge la walevi, Spika wa Bunge la walevi. ajabu iliyoje mara baada ya kulihama Bunge la walevi cheo changu kimeshuka kwa asilimia 95 kutoka kwenye uspika wa Bunge la walevi hadi kuwa mpishi wa pombe ya walevi mmmh! Mengine makubwa, madogo yana nafsi zake, sio mbaya yajayo yanafurahisha.

                    Any way nisiache mbachao kwa msala upitao, mcheza kwao utunzwa, mjasiri  aiwachi asili, kila ndege ana kwao kuzuri kwenye matunzo, na mimi ninaye mama, mama yangu  hakukwama kunilea na mama yangu si mwingine zaidi ya Bibi mlezi wangu, yule aliyenipatia deko na madekezo. Na mimi ninaye Baba na Baba yangu si mwingine ni yule yule Babu yangu aliyenilea nami nikaleleka kwa deko na madekezo. Upendeleo wao ni upendeleo mkuu, malezi yao ni malezi ya kuku na yai, hawakunipiga, hawakunifokea, hawakunikemea na kunikwaza kwa jambo lolote lile.
                ##########################
Miezi sita ndani ya kile kiwanda cha bia, nilibadilika sana, tabia ni mazoea, mjasiri aiwachi asili. Ule ulevi wangu wa kutupa ulinivamia tena ulinivamia kwa kasi ya ajabu, muda mwingi niliutumia kunywa pombe na uzuri wa hiyo pombe naliipishi mie mwenyewe, nilikua huru kunywa pombe mara baada ya kumaliza kazi yangu ya upishi. ‘Mie ndie mpishi, muda mwingi nipo mekoni, wacha niitumie hiyo fursa kuuburudisha mtima wangu kwa pombe,’ Naliwaza.

                Ndio maana kusema mazoea yana tabu,mtu kuzoea kitu, Aki! kukiwacha ni vigumu ajabu, muda wote uwaza jinsi gani lile pendo alilolipenda liingie moyoni mwake tena. Bosi wangu, Bwana Steven Biko hakuwa na longolongo juu ya ulevi wangu, aliniachia uhuru wa kuamua nilitawale Jiko nililo achiwa ili nipike na kupakua.
Mshahara wangu, marupu rupu pamoja na posho za mara kwa mara, bosi wangu Steven Biko alinipatia tena alinizidishia mara mbili zaidi, akinitaka niendelee kuchapa kazi pasina longolongo, pasina matata uvivu na uzembe, nilikua mtiifu kwenye ile mishe(kazi) nilikuwa siriasi japo ulevi kwangu ilikuwa ni vigumu kuukataa.

Itaendelea



No comments:

Post a Comment

OBIMO CHETA

 OBIMO CHETA (MY LOVE REMEMBER). Siku Derila alipokutana na Singa, ilikuwa ni siku nzuri, siku ya kusheherekea sikukuu ya Christmass,🌲🎄⛪...