Tuesday, July 8, 2025

MWENZENU N'SHAPENDWA.




 SEHEMU YA TATU   

  Shostito embu nikusimulie;
Kabla sijaingia kwenye dimba la simulizi yetu, embu ngoja nikugaie story fupi ya huyu bibie mwenzetu aliyependwa na Mwalimu mkuu mmoja wa Sekondari iliyopo huko Kinondoni. Bibi katokewa naye hakuwa na kinyongo  lakini jamani lakini upuuzi wa hawa mabibi wenye akili kisoda siku ile ile alipotongozwa yeye kamwambia Mwalimu, kamwambiaje mwaya, kawambia hivi;👂


                  “Utaezana?” Mwalimu Mkuu akajibu naye akasema,

                  “N’shindweje? Kwani mie so’ mwanaume.” Teh teh teh,🤣 nacheka mie.  Basi bibie akiwa anakenua mijinoye (meno yake) akakoleza wino, kazidisha porojo, kajitia yeye ndo’ yeye sasa ni wakati wa kumwaga seraze (sera zake), bibie kaendelea kushoboka.😉

                   “Mie sio binti wa mchezo mchezo ujue! Ninataka kula, kuvaa, kunywa kujipamba, na starehe zingine kedekede, ikiwemo kila mwisho wa mwezi un’gaie shilingi laki nne, mara ile ukipata mshahara wako, mie niende zangu shopping kusasambu sasambua viwalo, mie niende zangu Botique kuchagua chagua vikanyagio vya mchuchumio👠👡, sema babu utaezana?”


Mmh! 😐Jamoni jamoni wanawake nyie jieleweni tafadhali, jitambueni na pia jirekebisheni, yaani weye bibie kutokewa kidogotu ndo’ umgeuze babu ATM mashine, ati awe anafanya kupiga panga huo mshahara wake wa shilingi mia sita (600,000), kiasi cha silingi lamia nne kila mwisho wa mwezi bibi upewe weye kimburukutu ukaseti nywele zako saluni, (hukumbuki kuwa zama za sasa wenzako bado wanaenda kwa Wamasai kusukwa ile mitindo ya twende kilioni na mabutu,😂 hukumbuki kuwa wenzio tunanyoa vipara wembe, tena tunapakaa vichwani mawese au mafuta ya nazi ili  vichwa vyetu vya asili ving’arishwe kwa mwanga wa Jua.”)👌Naongea na wewe👉 Bibi mwanamke, mbona waninunia⁉️Teh😂 Mkorogo umedunda.


Weye uenede  huko shopping ukavae madella  mapya ya bei gharama, vimini na vitopu vinavyo uuza mwili wako kwa vijana dume waso na maadili, (Hukumbuki kuwa wenzio tulofundwa tukafundika tungali tunatikisa tikisa vyura na mizigo yetu mbele ya Babu kwa ile mivao ya kanga moko na vitenge vyetu vya asili,ili Babu apagawe hadi udenda umchuruze🤤😜 kama maji bombani, likushike Bibi likushike hadi miguuni ili ujue kuwa mjasiri hawachi asili)


              My wangu huko ndiko kuachwa solemba na huo ndio upuuzi wa mwanamke. Unaweka odda ya vitu vya bei gharama  wakati penzi bado halijachanua, mwanamke unayaonesha makucha yako yakiwa wazi wakati hata ndani ujawekwa, kumbuka bibie bado haujawekwa ndani, je ukiwekwa ndani ukamkuta Babu yu kapuku na kabwela, hoehae, hana mbele hana nyuma, kumbe ni msakatonge, mpiga miayo na mbeba mizigo pale Sokoni Buguruni, Ilala  Sokoni, Karume Sokoni au Kariakoo. Nijibu mwaya👌

 Kwa uroho wako ukafie mbali, sijui itakuwaje, Mmh! Mnuno huo si wa kitanzania, chuki hizo si za kiafrika, mmh! Teh teh teh, 🤣🤣😂roho juu juu kama kunguru mwoga. Mwaya kumbe mapenzi hauyajui, kumbe hujui kuwa mapenzi ni uvumilivu. Likushike Bibi, likushike  hilo neno likushike hadi kwenye komwe na ugokoni.

                 Bibi, mwanamke ni kujielewa, mali na utajiri, Mola mgawaji, wawili kutafuta ni haki yenu, usiwe tegemezi sana, ukumbuke bibi ukumbuke kuwa mtegemea cha nduguye ufa masikini. Maisha ni haya haya si mafupi si marefu, hakuna marefu yaso na ncha. Hata baada ya Harusi na starehe nyingi kwenye sherehe ya Harusi bado kuna maisha ya baadaye, kuna mengi ya nyie wawili kujadiliana ikiwemo; mle nini? Mnywe nini? Mvae nini? Haya ni mambo madogo madogo kuyamaliza,  mgali bado hamjanunua kiwanja hamjajenga hata tuvyumba tuwili, bado mmepanga wakati huohuo kodi ya pango mnadaiwa, bili ya umeme hamjalipia, bili ya maji hamjalipia, na hayo madeni dukani kwa Mangi? Mmh! Shogangu Dua jamani Dua,🤲 ombeni Mungu. Mpemba asije akawatoa roho kwa wingi wa madeni mliyoyaacha dukani kwake, mmh! Mwenzangu ndo’ usiseme,kwa hali hii mie nashika tama.🥺🙂‍↕️🤭😱


              Teh teeh teh! 😂Nacheka vizuri, nacheka mie, nakwambie mwaya yule Mwalimu mkuu aliketi  jamvini akafikiria “Maisha ni haya haya, mengine yako wapi?” hatimaye ‘at the end of time’ akaweka Conclusion liwalo na liwe sio mbaya kubwaga manyanga, akamtema yule Bibi  mpenda huduma, akamwomba  Allah Subahhana 🤲mwingi wa rehema na neema, mgawa kidogo na kikubwa, mpaji wa mema na mwondoaji wa mabaya, ampaye ampendaye na kunyima amtakaye.



Mwalimu akampata wake wa moyoni, akamuweka ndani huu ni mwaka wa kumi ndoani na wamekwisha kujaliwa watoto watatu (Aruuuuuuu… Vigere gere shoga'ngu,  makofi, nderemo na vifijo). Yule Bibi mwenye taama ya Fisi mpaka leo hii hajaolewa, huu ni mwaka wake wa kumi  sasa bado angali anasaka mume tajiri  wala asimpate. (Alie tu, si anajifanya yeye ni Bibi Mpenda huduma, akome shoga zangu, akome akomae.)


         Bibi ndo’ maana kukwambieni waogopeni waja hawa, waja wasoyajua mapenzi, wao daima udai na kuvitanguliza vitu vya bei gharama, wakati huo huo wao wenyewe hawawezi kuvitoa, ni wajinga wenye mikono na mioyo ya kupokea, wakati huo huo wenyewe kutoa hawatoi, ndo’maana hawa mabibi kwetu wanaitwaga ‘Mafyangu fyosa’ yaani 'wataka pupa,' ni watu wa vitu vya bei gharama, ni wenye porojo na malalamiko tele pale  usipowatimizia haja zao. Ati shogangu wanafaaa hawa. ⁉️ Kungwi napita.🚶‍♀️👢

             Mwanamke umependwa mara ile ati utamke nawe useme; “Kama unanipenda kweli ninunulie vocha, kama unanipenda kweli ninunulie della, nitumie shilling elfu kumi, nifanyie hiki nifanyie kile.” Teh teh teh! (Nacheka mie) shoga huo ni ulimbukeni na ujinga uliopitwa na wakati. Tena ni ujinga wa kujipendekeza, kujikokongoza, kujishaua na kujishebedua, kumbe weye shostito bado upo kwenye Analojia wakati wenzio tupo mbali kwenye Digitali. Ujue tu ujue kuwa mapenzi hayapimwi kwa hizo kauli zako, kauli za kusema  “Ati kama unanipenda………” “Nifanyie hiki nifanyie kile” Mmh! (Naguna mie)🤭

 
Je, nyonyo bado una imani haba?  Humwamini Babu? Haumaini kuwa Babu anakupenda? Kaganda kwako, wataka ayeyuke? ameguke au adondoke kwako? Watakani shogangu mbona hauna moyo wa kuridhia na kuridhika?

Sasa fanya kumuudhi Babu muudhi kwa kumwambia huo ujinga wako ambao haujapitia kisomo.📚



     
Nyonyo mie najisikia aibu sana pale tunapowatwisha waume zetu  mizigo mingine ambayo hawapaswi kubebeshwa, tujue na tutambuwe kuwa waume zetu  waliumbwa kutupendezesha sie wanawake ambao tunawapenda hao waume zetu, waume zetu kwa asilimia 90 wao ndio wabebaji wakuu wa majukumu ya  familiana sie wanawake asilimia kumi ndio baki yetu katika familia.

             Wao ndio watafutaji wakuu wao ndio wahangaikaji wakuu ili sie wakina nyonyo tule tunywe na  tufanye yote katika familia. Sikiliza nyonyo, umasikini na utajiri ni mapenzi yake  Mola, usimwache Babu ati kwa sababu ana kilema, hapana kila mja ana kilema chake, ndio maana  likazuka neno “Binadamu hatujakamilika  ni Mungu  tu ndie mkamilifu”

Sasa mie Mamsapu Mama la kitanga wacha nikupe simulizi yangu, jinsi nilivyotokea kupendwa na huyu roho wangu, mtima wangu mboni na jicho langu, ninampenda nayeye ananipenda, sijui weye mwenzangu  upo  hapo?  Aliye na masikio asikie, aliye na macho atazame,kama huwezi kusoma basi picha angalia shoga, Babu we! kantangaze. Biashara ni matangazo, mwenye macho usimwambie tazama, kama hujui kusoma basi shoga tazama picha.


                Shoga kwa mtindo huu Mangi anakwambia  ni bora nyumba yake ishike moto lakini sio Daftari yake ya madeni kuliwa na panya, Mpemba anakwambiaje anasema kama kukopa mkope sana lakini uwe umekwisha weka Rehani nyumba yako, mke na watoto wako(na ujaposhindwa kulipa, halali yake. Atapiga bei kila kilicho chako)😭 Huzuni. Muhindi na Mwarabu hawana neno wao wana kwambia Hewala haigombi na mie nakwambia shogangu ogopa kubeti kucheza kamari na kubashiri. Hiyo michezo ya watani wa Jadi Simba na Yanga sio ya kwako mwanamke, mazito yatakukuta mwaya kama haujaenda kuchota pesa zako Benki ili ulipie kamari na kubashiri mwaya ukifirisika sijui kama haujavuta bangi mwaka huu?  Teeh teeh teeh! 😂 Nakuona stress na mawazo yamekupanda kichwani, presha presha hadi utalazwa ICU. Ndo’kukwambieni hayo mambo ya wanaume ya nini wewe mwanamke?⁉️


             Wewe mwanamke fahamu wajibu wako kama Bi.Mkubwa, Bi.Mdogo, Bi.Dada au binti katika familia. Kijungu jiko kinaitaji chumvi, mtoto anahitaji kukogeshwa, kuni na maji haujateka kisimani na porini, nguo za babu hazijafuliwa wala kupigwa pasi,bustani ya mboga mboga na maua inahitaji maji na mbolea, mwanamke bado haujapuguta deki, bado hujakwenda mashine kusaga na kukoboa, bado haujakwenda soko kununua mahitaji ya nyumbani, bado Bibi bado haujawalisha Mbuzi n’gombe kuku na nguruwe, lakini kwa hicho kiguu chako unatanga tanga na kudanga kama mwendawazimu, mwaya kwa huo uhayawani wako nasema hivi hilo ni Pepo na hilo Pepo likemewe katika jina la Bwana Yesu“EMENI.”
 
               Mmh! Mwaya ukweli mchungu mie roho yaniuma kuona au kusikia mashoga zangu mnafanya kubeti, kucheza kamari karata🃏 na kubashiri, hapana jamani, hapana! Acheni niseme, msema kweli mpenzi. Bado naumia mie. Naumia na wale mashoga ambao kutwa kuchwa wapo kubeti na kutazama mpira mara ati utawasikia wakibishana
 
              “Leo  Man united itakipiga na Chelsea, Juventus na Genk,” Mara ooh!

               “Nakwambia mzee Mama leo ni Mess, Pogba, Samatta na Chirstiano Leonardo wataibuka kidedea.”
 
                “Tufinge, tufinge, mzee Mama nakwambieni Taifa stars itagongwa na Burudi, Burundi ni chuma cha reli kile,” 
 
                “Ah wapi! We shombe shombe tu, Simba hawana chochote wale, points zote  mechi za ndani ndo’ wanafanya vizuri, mbona wakienda ughaibuni wanapigwa mimba.” 
 
                “Ah shoga mimi Mzize na Azizi kidamu damu hao ndio Baba lao, lazima leo wanipe mabao ya kufa mtu, kifo cha mende mbele kwa mbele, Mwendo wa chuma tembele” 
 
Jamoni shoga kutwa kuchwa wajipweteka matanga yako kushabikia Mpira baada ya kushabikia mambo ya kimaendeleo. Jamoni ndo’ maana nimesema ‘Nyani hakioni kibamia chake bali anakiona cha mwenzake,’ teeh teeeh teeh mie nayaona makovu yenu lakini nyie hamyaoni, kamwe sina muda wa kuyakalia kimya, lazima niwasute ili mjue fika kuwa damu ni nzito kuliko maji.
                 #########################

Sikiliza nyonyo, dhiki uvumiliwa, palo na dhiki hapakosi faraja mvumilivu hula mbivu, mbivu nono zenye mafuta. Mie mwenzenu nimepitia mengi, bila Pompo sijui kama leo hii ningelikuwapo hapa nikikuandikieni 'MIPASHO YA MAMSAPU. Pompo wangu pia kapitia mengi sana lakini acheni Mungu aitwe Mungu, lenye mwanzo halikosi mwisho, lenye mwisho lilikua na mwanzo ndo’ maana kusema hakuna marefu yaso na ncha.

               Pompo mume wangu alizaliwa uzaramoni, huko kwenye hali ngumu ya maisha, huko kuyapata maji safi na salama ni ndoto, huko kwenye giza la utusi tusi vibatari na mishumaa ndio mwanga wao, ama kweli Mungu ni upendo mwanga wa mwezi na Jua kuwamulika.


Huko kupata chakula bora chenye afya na virutubisho ni mtihani, huduma za Hosptali au Dispensary ni shida ndo’ maana Pompo wangu hakuwa na nasibu ya kupata elimu hata ile ya darasa la kwanza. Lakini leo hii, leo wangu wa moyoni anakula matunda yake utajiri na mafao yake.

 
            Mpopo roho wangu, mpenzi wa moyo wangu alikitumikia kilimo cha mkono wa Jembe kwa muda mrefu sana, alipalilia palilia mboga mboga matunda na minazi, iliyomletea Nazi, dafu pamoja na pombe ya minazi, miaka nenda miaka rudi Pompo wangu wa rohoni akaipata baleghe yake akaiva kwa upole uzuri wa sura uchapakazi na pia kupendwa na kila mwenye upendo kijijini.

             Kama tujuavyo Nyonyo baleghe ni kipindi cha mabadiliko, mabadiliko hayo sio madogo ni mabadiliko makubwa ambayo upelekea kijana atambue nafsi yake inataka nini? Basi nyonyo wangu wa mapenzi alichoka kuishi kijijini alichoka kulima na kuvuna, alichoka kuchunga Ng’ombe, alichoka kuishi uzaramoni, Mwanaume aelekee Mjini akajaribu nasibu yake, mwaya Pompo akawaambia wazazi wake (Wakwe wangu) akawaambia nia yake, lengo lake na tumaini lake, japokua ilikuwa ni ngumu kwa wazazi wake kumpatia ruhusa ya kuja mjini hata hivyo ilibidi awe king’ang’anizi ilibidi aombe sana kuruhusiwa aondoke.


                  “Mwana we basi utukumbuke huko wendako”Bibi mama mkwe Mamaye Pompo aliongea.

                 “Nikusahau tena weye Mamangu! Mola anilaani.”Pompo alitoa kiapo.

               “Sie twakuombea mafanikio mema, uzima tele na baraka milele.” Babu Baba mkwe Babaye Pompo alinena.

               “Mungu anitangulie katika Safari yangu,” Pompo alinena.

               “Maombi yenu wazazi wangu, maombi yenu tafadhali.” Pompo aliwasihi wazazi wake maombi na Dua jambo jema kumtanguliza Mola.

              “Inshallah.” Ba. Mkwe na Bibi Mama mkwe walimtia moyo na kumfariji. Safari yake Safari ya kuingia Jiji la Mzizima (Dar es salaam) ikapamba moto, kafungashiwa kila kilicho muhimu kubebeka, pesa za kutosha, chakula cha kutosha Safarini, mavazi pia na uzuri wake Pompo kazibeba picha mbili za wazazi wake, Baba na Mamae, apate kuwa miss huko ugenini.

Alifika ndani ya jiji la Mzizima (Dar es salaam), alifika wangu Pompo, hana mwenyeji wa kumpokea hana pahali pa kwenda, hana chakula cha kula, Oooh! Jamani huruma kuhadithia, pesa alizokuwa nazo mfukoni hazikutosha kutumika kama tafuto la chumba cha kupanga, pesa zile zilitosha kwa ajili ya milo ya siku mbili tatu.

              Pompo wangu hakua na jinsi alilaza kichwa chake pale K
ariakoo, alilaza kichwa chake stand ya mabasi, alilaza kichwa chake kwenye malango ya maduka ya wafanyao biashara, aliilaza kichwa chake popote pale, yaani masikini pompo wangu alivumilia ming’ato ya umbu, baridi la usiku joto kali la usiku, mvua na mara nyingine vibaka wa Jiji la Mzizima.

Jiji hili kubwa sidhani kama mtu utakosa riziki, Pompo aliwaza afanye nini kujinusuru na njaa ambayo ingelimtesa, moyoni akafikiria yupo ugenini yanini kuketi barazani ashindwe kufanya jambo lolote lile la maana, nguvu anazo, uwezo anao, nafsi inamruhusu kutafuta, pompo Moyo wangu akaingia Sokoni Buguruni huko mja hakosi riziki, riziki popote Mola atagawa.     
    
      Basi mwaya Mpopo akaanza kubeba ‘ndwika’ au kwa Kiswahili fasaha kubeba mizigo, mizigo ya wanunuzi wa bidhaa mbali bali pale Buguruni Sokoni.

             
(Itaendelea.) 


 “Shogangu niunge mkono mwaya ujaposoma hii hadithi yangu mie Mamsapu Mama la kitanga usipite bila kulike na kukoment, palo na mapungufu tusaidiane kutatua, huo ndo’ ujamaa Bi. mkubwa, ujamaa kusaidiana shost. Nyonyo ujue wan’tia moyo mie unapo like na kukoment hii post, basi fanya hivyo mwaya. ”💕
 

No comments:

Post a Comment

OBIMO CHETA

  OBIMO CHETA REMEMBER MY LOVE 💕  Sehemu ya nne Hakuwa na pahali pazuri pa kulala, hakuwa na maji, hakuwa na chakula, alilala kwenye majeng...