Saturday, July 12, 2025

MWENZENU N'SHAPENDWA.




MIPASHO YA  MAMSAPU 


MWENZENU N’SHAPENDWA


SEHEMU YA 4



SHOGANGU PALE TULIPOISHIA.

Jiji hili kubwa sidhani kama mtu utakosa riziki, Pompo aliwaza afanye nini kujinusuru na njaa ambayo ingelimtesa, moyoni akafikiria yupo ugenini yanini kuketi barazani ashindwe  kufanya jambo lolote lile la maana, nguvu anazo, uwezo anao, nafsi inamruhusu kutafuta, pompo Moyo wangu akaingia Sokoni Buguruni huko mja hakosi riziki, riziki popote Mola atagawa.

SASA TUENDELEE MY WANGU

Mizigo inayoletwa na maroli na maroli kutoka mikoani, mizigo mingi mizito, wangu wa mapenzi akajibidisha kwa maumivu yote, akapata pata vijisenti, pesa mbili tatu naye akafanyaa uzuri wa kutafuta ‘Getto’ akalipata, akahamia kigogo mwsho kwenye makazi yake mapya, heri kidogo afadhali kidogo maana wale umbu wa kariakaoo walivyokuwa wakimtafuna Aki! wangelimmaliza wangu mie Mamsapu.


                Akajibidisha mpopo wangu, kutwa kuchwa asiharibu ratiba yake, akidamkia kazini saa kumi na moja alfajiri atarejea nyumbani saa nne usiku, akipanga amepanga asiwepo wa kuipangua, akajibidisha Mzee Baba, akajibidisha kusaka tonge, akajibidisha kwa ile kazi ya ukuli sokoni na uzuri wa mwanaume wangu akili ni mali, akili ni nywele kila mja ana zake.
Akafanya kununua nunua baadhi ya vyombo vya nyumbani, akanunua vyungu sahani, mabakuri, vikombe, vijiko na kadhalika, akanunua madishi (mabeseni), ndoo za plastic, godoro na vinginevyo vingi kwa ajili ya kijungu jiko. Sisemi ati alikuwa anazo pesa mingi, lakini ukweli ni kwamba haba na haba yajaza kibaba, ndo! Ndo! Ndo! Si chururu, maisha yataka moyo wa kujituma, ili kufikia malengo na matarajio.


              Wapenzi moyo wangu akaendelea kujituma na kujibidisha, kajifunga mbeleko ya kuvumilia shida na karaha za Dunia hii, wala asichoke kufanya lolote lile ambalo lingelimsaidia maishani. Mara leo utamkuta anauza machungwa, mara kesho utamkuta anazibua vyoo, mara leo asafishe soko la kariakoo, mara kesho auze kahawa na kashata, mara leo aokote chupa tupu akauze apate riziki wala asikae bure maana wahenga walisema, mwenda bure sio mkaa bure wenda akaokota kitu. Mgaagaa na upwa hali wali mkavu, ikawa hivyo tena wangu wa moyoni akajiwekezea pesa miaka ikaenda isirudi.


                  Miaka ikaendaa tena na tena, asiwasahau wazee wake akiwatembelea mara kwa mara apate kuwasalimu na hatimaye wangu wa rohoni akapata wazo la kuwa na wake wa kumpooza mtimani, mtima mpweke wenye nyingi hisia za ujana na kubaleghe, wazo la kutafuta mchumba na kuoa huko kijijini kwao uzaramoni lilimwingia naye akalifanyia kazi akapata jiko, jiko Maua, msichana mzuri wa kupendeza, mrembo wa kuvutia, maji ya kunde yaliyokolea ana chura mzigo huko kwenye bwobwo bwo, ukimtizama mara mbili mbili mwenyewe utapenda.

               Mtoto Maua akawekwa ndani, lakini Maua, jamani Maua mke mwenzangu kumbe ana roho ya tamaa, roho ya kupenda mali na utajiri, lakini mwaya yote hayo sio madogo, kupakwa mafuta ya ugokoni na hao wanawake wa mjini, kalishwa maneno na hao wanawake wa mjini, kutwa kuchwa waja kumtembelea na kumkagua nini anacho nyumbani au nini hana, kala nini leo? kanywa nini leo? Hapo ndipo hao mashogaze waso na heshima nyumbani  wakaanza kumnanga kwa maneno shombo mnuko.


                “Usiwe zube mwanamke, huyo mumeo hakupendi pendo la ukweli, tizama ati kutwa kuchwa mle miogo majimbi, mchicha na ugali, teeh teeh teeh” mashogaze wakaendelea kunena na kumcheka kwa dharau.

              “Wenziwako twala vitu vya bei gharama, sio kama wewe unayeishi na mume kapuku, hamna kitanda hamna sofa hamna kabati wala hamna meza ya chakula mwaya unapaswa kufanya maamuzi ya haraka, achana na huyo kidume fukara  hakufikishi mbali kimaendeleo.” Mashoga walitia neno.

                “Lakini shoga zangu, maisha kutafuta mwacheni wangu wa rohoni ajibidishe, ipo siku ataafanikiwa,” Maua alimtetea mumewe.

              “Maua usiwe bibi jinga, hapa mjini bibiwe, mjini kuna wanaume wengi wenye pesa zao sembuse huyo mumeo mbeba Zege, teeh teeh teeh,” Mashogaze walimpaka tope na kumcheka huyu bibi mwenye kibedi chake tumboni, kina miezi michache tu tangu kingie ndani ya yai.

              “Basi uketi ufikirie ndo’ utuambie sie tukutafutie mwarabu mwenye pesa zake, akupeleke Zanzibar ukaishi kule ukale raha na starehe zako babu we!” Shogaze walimsonga.

             “ Hadi kinyaa kuishi na mwokota kopo, hana msimamao dhabiti, leo achimbue vyoo vilivyo ziba na kujifukia, kesho akauze kahawa, kesho kutwa akachimbe makaburi, mara abebe ndwika, mmmh! Shoga we una nini tunashangaa mumeo yuko ovyo, rafu rafu.” walizidi kumponda na kumpaka tope.

           “Shoga huyo sio mume huyo  mtu mzima ovyo ni tahira, chizi, kapunguka akili.” Maneno yale yalimchoma sana  Bi.Maua, mke mwenzangu.
Maua hakuweza kutafakari zaidi ya kujiona kama vile hana bahati. Basi mwaya maneno mnuko yalizidi kujazwa ndani ya nyumba ya Maua na mumewe Mpopo, Maua akapoteza furaha na amani kwa jinsi wale mashoga walivyozidi kumpaka tope ati wakidai ameolewa na mume asiyejielewa. Ndipo ule upendo kwa mumewe ukapotea yale mahaba kwa mumewe yakazimika, akawa ni Bibi mnyonge mwenye huzuni na majonzi kila wakati. Asimtake Pompo yule mwokota kopo. Mzibua vyoo na mchimba makaburi tena moyo wake akaumishia kwa huyo mwarabu wa kipemba aso mjua, sifaze tu zinauwasha mtimawe.

              “My wangu, mbona hivyo mie nirudi kazini nikute chakula hakijapikwa nyumbani, vyombo haujakosha, deki haujapuguta, nguo hazijafuliwa, Bibi umeanza lini uchafu?.”Mpopo aliongea kwa upole.


              “Kwani wewe hauwezi kupika, hauwezi kufua au kupuguta deki? Usinichoshe Mpopo ningali mjamzito.” Mwanamke aliongea.

              “Yashakuwa mazoea mwanamke, mie nifanye kazi za kijungu jiko, kazi zako weye?” Mpopo alijitetea, ukweli ni kwamba amekuwa akirudi amechoka haswa, hajiwezi kwa uzito wa kazi za kila siku, ajabu akirejea home akumbane na kazi ambazo mkewe alipaswa kuzifanya, na mkewe anagangamala kujiketisha jamvini shogaze kumpumbaa.

             “Embu niondolie maneno hapa, kama waniona mie mzigo nirudishe kwetu, n’shachoka kuishi na mume aso na msimamao,” Maua alijibu ovyo.

                “Maua wangu, mapenzi ni uvumilivu, nivumilie mie, ipo siku furaha uitakayo nitakupatia.”

                “Enyoooo! unipatie weye mwokota  kopo uso na kipato.” Bibie alijibu kama mtu mwenye mamlaka.

              “Maua wangu!” Mpopo alitia huruma kama kinda alo achwa na mamamye, huzuni ikaendelea kuitafuna ile nyumba, furaha ya ndoa ikapotea raha ya ndoa ikazimika maana Bibi tayari alikwisha panga kuondoka mara tu akiisha kujifungua mtoto wake wa kwanza.

Vibweka vikaendelea, vituko vikapamba moto, nyumba ikawa haikaliki, kila akiondoka Mzee Baba mashogaze Maua ujipweteka pale nyumbani, wamevaa vijola, madella, shedo usoni,wamezikwatua sura zao, wamekuwa wazuri wa mkorogo mawigi ya bei gharama na kila kizuri walichojaliwa kilimtamanisha Maua.  Lo! Kama Maua mke mwenzangu angelijua fika kuwa wale ni mashangingi wa Jiji kwake wana jishebedua, Aki!  Ni heri angelibaki na uzuzu wake kuliko kupumbazwa kwa maneno ya wenye Jiji.

Mashoga wale walijazana pale Gheto’ wakimkebehi na kumponda Maua ati ‘hajui kuchagua mume, kachugua mtumba uliokwisha kuchoka na kuchakaa, wakati huo huo wanaume Special wapo wengi hapa mjini.
Yalipozidi maneno Maua akaumia, yalipozidi maneno Maua yakamchoma akaafiki ni bora aachane na huyo dume suruali, bora ayabwage, bora ashike vichochoro vyake. Aende kwa huyo tajiri wa Kipemba, tajiri ambaye mashogaze wanamminia sifa kede kede wakijigamba ati atamlea vizuri  yule mtoto.


                Babu! Pompo akukubali nakwambieni, alimpenda Maua hakuna mfano. Alihitaji Maua awe karibu karibu naye, iwe kufa  iwe kupona, lakini ndo’ hivyo tena, mashoga haweshi kuzidisha chumvi. Maua akajaliwa mtoto jinale Benito, kwisha kujifungua akaeleka kijijini kupumzika rikizo ya uzazi.


             #################

Shoga zangu hivi mnadhani mara baada ya kuisha kwa rikizo ya uzazi wa Maua alirejea nyumbani kwa mumewe pompo? Ile Nyota ya mapenzi yao, mapenzi ya pompo na Maua ikazimika na kupotea. Maua kawadanganya wazaziwe kuwa angelitoka kidogo asingelichelewa kurudi. Kumbe! Kumbe ndo’ kimoja, ‘imekwenda hiyo ikirudi pancha,’  Maua alikuwa kama Ndege iliyopotelea juu angani, hakurejea tena, alikwisha kuelekea kwa huyo mwarabu wake aliyembadirisha diniye akamfanya awe Mwislamu na ndoa ikafungwa kimya kimya asijue mtu kwamba Maua kaolewa tena.


               Pompo akapewa taarifa na wazazi wa Maua huko kjijini, wakalalama tabia ya mkewe  kumtelekeza  Benito. Lo!Pompo akawa njia panda asijue mkewe kendapi? Asijue mwanaye Benito ataishije bila Mama, ikawa hivyo tena Maua kamtelekeza mtoto, juhudi za kumsaka kila kona hazikuzaa matunda hatimaye Benito akachukuliwa na Bibi Mama mkwe akalelewa Uzaramoni, mtoto akakua mtu sasa, mtoto wa babaye na babaye akafanya hima kumtafutia shule ili mtoto asome.


                    ###          ####        #####

Pompo hakuwa na furaha, yale mapenzi aliyo yazoea sasa yakawa ni mapenzi kukosa, mke aliyempenda leo hii hamwoni hasirani. Pompo akajibidisha sana akafanya juhudi zake zote apate kuyaboresha maisha. Hakukoma kuwekeza haba na haba ajaze kibaba, na hatimaye mwanaume yule mzibua vyoo akanunua kiwanja chake huko Kigamboni matarajio yake yalikuwa ni kujenga tena kujenga nyumba aipendayo.


             Mwaya mie siku moja napita pita na kapu langu la maembe ndizi machungwa na maparachichi. Hiyo ndio biashara yangu hapa mjini, mjini maisha magumu asikwambie binadamu tunaganga njaa mjini hadi miayo ya kufa kufa inatusaliti, tufanyeje sasa bora kujibidisha riziki popote Mola atagawa.


                Sikutarajia kuguswa bega langu la mashoto na huyu mwanaume kijana niliyemtazama usoni akanipendeza, ni fundi, fundi mwashi, mjenzi anajenga mahorofa ya wakazi wa Jiji, alionekana kwa yale mavazi yake makuukuu, kofia ya kujihami na uzito wa mawe, makatambuga yake miguuni, ndio mara yangu ya kwanza kumuona, lakini mbona kanipendeza mie, sijawahi kupenda ila huyu  kwake nitazimia, sijiwezi tepetepe, regerege hata nisijue kwanini jamani? Nashangaa!

             “Habari ya wewe Dadangu?” Fundi kanisalimia, mie kapu langu la matunda juu ya kichwa, kichwa kinachoteswa kwa uzito wa makapu, makapu ya mbogamboga, nyanya, vitunguu, matunda na vitafuno ambavyo kutwa kuchwa mie nazunguka kiguu na njia kusaka soko.

                “Njema Kakangu, karibu.”nilimwambia huyu mkaka anitiaye presha ya moyo.


           
   “Jina langu Pompo, mie fundi ujenzi, wewe je?” Fundi kajitambulisha kwangu.


               “Ewe vipi? Biashara matangazo, jinalo lanihusu nini mie? Jina langu likupe nini weye?” nilimletea nyodo yule fundi.

                 “Sio poa Dadangu, nina nia njema sina mautani kama hao vijana mapuuzo.” Pompo kaongea, nikaipenda sauti yake imtoayo nyoka pangoni, mie tena nikatabasamu.

                “Ok. Niite Mamsapungo, toto la kitanga, kule mapenzi yalikozaliwa kule wajuzi wa kutwanga na kupepeta, hupo hapo babu!?”  nikajipendekeza kwa huyu Fundi, wakati huo huo moyo waniwashawasha kumpenda mwanaume kijana  HB.

              “Jina zuri kutamka, lapendeza machoni, lanivuta moyoni, nitaliweka kifuani.” Pompo kajishaua na kuchombeza maneno yaliyozidi kunifanya niweuke, n’shituke na kupandwa na hisia za kumhitaji, japo simjui lakini kanivuta macho yangu kumpenda.


             “Shidayo nini kakangu? 


Tukutane kesho Majaliwa, Pompo anambie shidaye.

No comments:

Post a Comment

OBIMO CHETA

  OBIMO CHETA REMEMBER MY LOVE 💕  Sehemu ya nne Hakuwa na pahali pazuri pa kulala, hakuwa na maji, hakuwa na chakula, alilala kwenye majeng...