Thursday, July 17, 2025

l PROMISE YOU



 SURA YA TANO

SIACHI MBACHAO.
Najua fika kuwa Brenda ana mwana wangu pembeni lakini hilo halikomi kuniumiza mtima wangu, hilo haliachi kunichoma na kunifanya niwe na msongo wa mawazo bado ninamuwaza Brenda wangu, bado ninayawaza yale maneno mazuri ya kimomboo niliyotamka siku zile za ulevi wangu.
“Ipromise you brenda, Iwill fulfill all of your wants, you just have to wait, time and moment will come.”
             “Ninamapungufu gani hata nishindwe kufullfill all of  Brenda needs and wants.” Ninasikitika nimezidiwa kete, nimezidiwa ujanja, ujanja wa Fisi, sio ule wa Sungura na huyo Fisi tayari alikwisha poromosha bonge la harusi, harusi ambayo mie Job nilikuja kusikia nikiwa Pretoria, nakitumikia kifungo kilicho sababishwa  na Biko.
               Nimeumia, nimeumia moyoni kwa sababu ya mapenzi yangu kwa yule niliyempenda yule niliye amini kuwa amenipenda kwa dhaati lakini ajabu amenibwaga na kunitelekeza.
Msongo wa mawazo umepelekea kurudia tena asili yangu, nimerudi bungeni, nimerudi bunge la walevi, mwanzo nilikuwa mpwke na mnyonge walevi wenzangu walinionea huruma sana, wakanirejeshea amani yangu, amani iliyopotea, taratibu ndio mwendo pole pole tutafika, nikachepuka mie niliyekuwa meneja wa kiwanda cha TBL , leo hii nimekuwa  mnywaji wa matapu tapu, haki muda ni wakati, wakati ni muda, hakuna marefu yaso na ncha. Basi nikawa supa supa furaha ikarejea, japo sio ile furaha niliyokuwa nayo kipindi kile nikiwa na Brenda wangu.
             Teeh teeh teeh ai! Nacheka mie,nacheka hadi meno therathini na mawili yamenitoka, nikiwa nagugumia lita ya matapu tapu, ati walevi wenzangu wanadai kuwa ifikapo kesho watanivika ufalme, niwe Raisi wa chama cha walevi Tanzania, teeh teeh teeh, vichekesho vingine vyaniacha hoi mie chongo.
Kwa kiasi fulani bado nina majonzi na machozi mazito moyoni mwangu, Nikiwa ningali bado gerezani, babu yangu  aliugua vidonda tumbo, nikapata fununu babu yangu amekwisha twaliwa ameuwacha mwili na roho yake pema peponi.
                Bado nina kidonda moyoni mwangu, kidonda kibichi, bado hakijapata kupona sawa sawa, miezi miwili tena mara baada ya  babu yangu kuaga dunia bibi alipatwa na mshituko wa moyo, akadondokea kwenye moto wa mafiga matatu, siku hiyo alikua akipika ugali mekoni. Vifo vyao viliwasikitisha sana wanakijiji walioomboleza pasina uwepo wangu, sasa mambo yote yamebadirika nimempoteza wangu wa moyoni Brenda, nimewapoteza walezi wangu babu na bibi, nimeachana na  cheo changu ndani ya TBL, nimekuwa mpweke mwenye msongo wa mawazo. Mazuri yaliyonifuata yamekua mazito mtimani. Sio mbaya sana nipo na mwanangu Ayubu wacha adeke deke kwa babaye, mamaye amekwisha pendwa na mwanaume aliyenionesha ukarimu  na ili kumpata mama Ayubu ilibidi atumie mbinu mbadala, ndo’ sababu za mie kulala jera.
                   Ukarimu wa bwana Biko umekua shubiri mtimani mwangu, nimekubaliana na matokea kwamba nilichelewa kutimiza ahadi ya kumpatia Brenda maisha bora, nilichelewa japo nilikua na nia ya kufanya hivyo sababu nilimpatia promise, nikamwambia I promise you……..Ah! ninatizama majira ninagundua kuwa muda umekwenda sana ni saa tisa, ni usiku wa manane, nipo bado napiga mitungi ndani ya bunge letu, bunge la walevi wa kiafrika. Nina cheka cheka pekee yangu, nina cheka cheka kama mwendawazimu, ninafurahia hiyo nafasi ambayo  walevi wenzangu wameniambia ati kesho ndo’ siku yenyewe kesho ndo’ siku ya mie chongo kuvishwa ufalme, ili niwe mfalme wa chama cha walevi Tanzania.  Lakini mmmh! Msema kesho mwongo, lakini……. Lakini…. Lakini…….. Subira yavuta heri.
                 ###############################################
                                              MWISHO 

No comments:

Post a Comment

OBIMO CHETA

  OBIMO CHETA REMEMBER MY LOVE 💕  Sehemu ya nne Hakuwa na pahali pazuri pa kulala, hakuwa na maji, hakuwa na chakula, alilala kwenye majeng...