Saturday, July 19, 2025

OBIMO CHETA

 



OBIMO CHETA


REMEMBER MY LOVE 💕 


Sehemu ya nne


Hakuwa na pahali pazuri pa kulala, hakuwa na maji, hakuwa na chakula, alilala kwenye majengo mabovu ambayo hayajakamilika kujengwa, alilala popote pale akitanga tanga na njia, akiomba omba chakula na maji huko Arusha Mjini, haja jinsi Derila, maisha ya wale waliokuwa pamoja naye hayapo tena, wamemkataa, oooh! Masikini, Derila hana furaha na ujauzito wake nao unakuwa kila siku, unakuwa mkubwa ajabu.


        Mbu hawachoki kumfyonza damu, chawa nao hawachoki kumtembelea, sio yule binti mweupe wa rangi ya chungwa kwa sasa, amebadilika rangi amekuwa na rangi ya kaki, ukimtazama mara mbili mbili waweza kusema kuwa yule sio Derila uliyemzoea miaka na miaka, kama unamjua basi waweza ukalia na kumuonea huruma.


                *************************

        Kuna kijana mdogo wa umri, mdogo wa umbo lakini kwa kipaji cha kuimba nyimbo yupo vizuri, tatizo alilo nalo  yule kijana ndilo tatizo alilo nalo Derila, Frank alifukuzwa nyumbani kwao kikatili, alifukuzwa mara baada ya kufeli masomo yake ya sekondari, alifeli kidato cha pili, alifeli kutokana na mapenzi yake kwenye burudani, muziki ndio burudani yake, yeye ana kipaji chake kizuri sana, anaimba japo hapewi sapport, ni kama vile Frank anaupoteza muda wake mzuri wa kujibidisha na masomo, ingawaje amefeli, tena kufeli kwake kuna nafuu, yote kwa sababu anayo nafasi nyingine ya kurudia darasa japo hataki kurudia, wazazi wake walipoona wamembembeleza bembelezo lisilozaa matunda hawakuwa na jinsi, waliamua kumfukuza, tena walimfukuza kama mbwa, mbwa mwizi, wazazi wa kipindi hiki daima hawakuwa na mashauri bali walikuwa na maamuzi, na maamuzi yao daima ni kuwafukuza watoto wao pale wanapoona hawaafikiani kabisa.

        Frank akawa omba omba la jiji, maisha yalipomtupa mkono, ugumu wa hayo maisha ndio uliomfanya Frank awe ombaomba la Jiji, uzito wa maisha ndio uliomfanya Frank ashindwe kupata mahitaji yake muhimu, chakula kwake ni kama ndoto kukipata, maji au mahali pa kulala ni taabu na taabiko, wazazi wake hawamtaki. Ndugu, jamaa na marafiki hawana cha kumpa.

        Ombaomba, Frank akaungana pamoja na ombaomba na mwenzie Derila, tena huyo Derila angali ni mwingi wa majonzi, kilio na masikitiko, analia na kuhuzunikia juu ya penzi lake, penzi alilolipenda Derila. Frank akawa faraja kwake, alimfariji kwa nyimbo nyingi zilizojaa mapenzi na kumbukumbu za kweli.

        Tendo la Frank kumuimbia Derila nyimbo, lilikuwa ni tendo lililomfariji sana Derila akawa sio mtu wa kulialia tena, sasa akawa ni mtu wa kuimba pamoja na Frank, watu wenye moyo wa kutoa chochote walitoa pale walipoburudishwa na nyimbo tamu alizoimba Frank pamoja na Derila, tuseme uzuri wad Derila alikuwa na sauti nzuri ya kuimba, sauti ya kumtoa nyoka pangoni, sauti bora kabisa, sauti ya burudani, na uzuri wa sauti hiyo ndiyo iliyowafanya watu wajitolee chochote kile kidogo walicho nacho, iwe pesa, iwe chakula, iwe nguo au ushauri, burudani iliwatosha.

        “Watu wanasema umejaliwa sauti tamu sana Derila.” Frank alimsifu Derila.

        “Ni bahati tu Frank, mimi binafsi sijui kama ninayo sauti nzuri ya kuvutia.”Derila alitabasamu, ndivyo alivyo Derila siku zote hutabasamu.

        “Je. Derila unaonaje siku moja mimi na wewe tuingie studio, tutengeneze Audio moja, wimbo wetu uwe mtamu wenye mavuto.” Frank alishauri.

        “Frank, kwa hali hii ndugu yangu kweli tunaweza kuingia studio, pesa tutapata wapi, maisha yetu yalivyo magumu, sidhani kama tunaweza.”

        “Tunaweza Derila, tunatakiwa kila siku tunapopata kidogo majaliwa tukitunze kwa sababu haba na haba hujaza kibaba, ndo, ndo, ndo sio chururu.” Frank aliongea, wapitao njia walifanya kurusha rusha vijisenti kwenye bakuri zao, kwani walijua kuwa wale wawli ni wahitaji?


        “Mmmh! Tuombe Mungu afanye wepesi Frank, mbele za Mungu yote yanawezekana.” Derila aliongea kwa imani, Frank akatabasamu, naye akafungua kinywa chake akaimba kwa hisia;

                         Milele, milele,
                         Milele, milele,
                         Mapenzi milele,
                         Milele na milele.

                         Tupendane sana,
                         Tupendane tena
                         Milele na milele
                         Mapenzi milele
                         Mi na wewe milele.


           
    ********************************

Itaendelea

No comments:

Post a Comment

OBIMO CHETA

  OBIMO CHETA REMEMBER MY LOVE 💕  Sehemu ya nne Hakuwa na pahali pazuri pa kulala, hakuwa na maji, hakuwa na chakula, alilala kwenye majeng...