MIPASHO YA MAMSAPU
MWENZENU N'SHAPENDWA
Tulipoishia
Sasa shoga zangu ikawa siku moja mie nipo barazani nachambua chambua mboga ya harage kwetu twaiita Nguniani , nikitwanga twanga kipome au kwa kifupi karaga za kuchanganya kwenye Nguniani, nikatembelewa na ugeni nyumbani. kanijia huyu mwanamke anitishaye surani, mmh! kwa mwonekano wake si ningelimwita chizi mwenda wazimu, lakini aka! yatanikuta mie, nizibe mdomo wangu, sio kila neno kuropoka.
SEHEMU YA SABA
Mgeni huyo kakonda na kudhoofika, kaja na manywele tipwatipwa, yamekosa dawa ya nywele, yana rangi ya udongo na kipilipili si ni heri na mie Mama la kitanga ninayezisuka nywele zangu zisipoteze uzuri wake. Si ni heri na mie Mama la kitanga ninaye nenepa na sasa nina kibedi tumboni,🤰 basi mwaya huyu mgeni asiyetamanika kanivalia nguo kuukuu na kandambili zilizokwisha na kuchanika kisiginoni, mavazi yake machakavu kama tambala la dekio, kabeba kirago chake kichwani kufika tu naye kakitua hicho kiragoche pembeni ya mlango wa nyumba yetu mie na wangu wa rohoni💕 pompo.
“Mgeni karibu,” nilimkaribisha nikijua fika kuwa huyu ni mhitaji ana shidaze, anahitaji msaada kusaidiwa.
“Asante mke mwenzangu,”
“Mmmh!” Mie kuguna. Kanishitua kwa kaurize amabazo nalishindwa kumwelewa, mie nikatamka,
“Mbona sikuelewi mgeni kwa lako tamko?”
“Utanielewa tu, kwanini usinielewe, wakati mie nimefuata mali yangu.” yule bibie mnuka domo, vundo kwapani, na ukurutu mwilini kanijibu kwa nyodo za mwanamke
“Bibi, unashida gani nikusaidieni?” Niliongea kwa ukali kidogo, nikatamka tena,
“Nisikuelewe Kiswahili unijibucho!” Nikamwambia, nikimshangaa yule bibi mwenye sura mkomavu ambaye hata salamu hajanigea.
“Mbona ninaeleweka, au unataka kunielewa kwa manati” Alinijibu, kisha kaendelea kuongea.
“Kwanza kabisa Pompo nampata?” Alinishitua kulitaja jina la roho wangu.
“Wamjua?” Niliharakia kumuuliza
“Vema sana, tangu zama za kale za mawe, kabla weye kumjua.” Alinijibu, bahati mbaya moyo wangu Pompo hakuwepo nyumbani, nalikuwa mpweke mbele ya huyu mgeni mwenye komwe kitisho, anitishaye kwa manenoye.
“Wamjuaje, eeh!⁉️ Mwanamke?”Nilihoji tena,
“Bibie nielewe mie nasema wewe kwangu ni mke mwenza, labda Pompo hajakueleza kuhusu mkewe wa kwanza Maua ndo’ mie hajapatikana mwingine zaidiye.” Yule Bibi mwenye sura mkomavu aliongea.
‘kumbe huyu ndo’ bibie Maua, Yule msaliti aliyelewa maneno ya mashoga na mashangingi wa Jiji’ Nalijisemea mie na moyo wangu.
“kwa hiyo umefuata nini kwenye nyumba ya yule aliye kwisha kupendwa?” Nalimuuliza Maua.
“Mashallah! Nimemfuata yule nimpendaye, tena nasema hivi bibie usiyempenda kaja, Kaja na gia zake, hapa siondoki hapa namwaga mafuriko.” Yule bibi mwenye sura mkomavu, alijaribu kunitisha. Aki! kweli anasura mkomavu nasema Shoga hata akipaka Rosheni itamkataa. Mmh! Kababuka kawa majivu majivu, podali imemkataa. Teeh teehteeh!🤣🫢 Ai! nicheke mie.
“Teeh teeh teeh,” 😂Mie nikacheka kwa uzuri zaidi, kwa cheko la kimapozi na kebehi, nikimrembulia jicho langu, jicho kungu babu we!, nikimpasha ajue fika kuwa mie n’shapendwa.
“Nadhani umeruka njia bibie, umeruka ukuta, upofu umekutafuna,” Nikaendelea kumchamba.👌
“Labda niseme ushachelewa, ndege ishakuacha na hata ikirudi tena bibie lazima ikukatae maana weye jasusi mtu mbaya uso na mapenzi hufai kuigwa,” Maua alinisikiliza, domo kunuka hiyo ni ishara ya njaa kumkamata.
“Pompo kanieleza kisa chako chote,baada ya kisa mkasa uliyataka weye na roho yako, ulichagua kudanga na kutanga tanga na njia sasa yamekushinda eeh, ya kwetu utayaweza” Nili mnanga ka vile n’shamzoea kitambo.
“Bibi uso yajua yatakusumbua, hivi weye walijua penzi la mie na Pompo lilivyokuwa?” Maua kaniuliza.
“Halikuwa, bali kwa umbea, kwa magubu na masimango ya shogazo ndo’ ukamfanyia yaya huyu muuza kahawa, leo umesikia ati katajirika na weye ushaona heri umrejee?” nikamsuta yule bibi mwenye sura mkomavu, nikamchamba tena.
“Si ulisusa wenzio twala, bibi hapa umefika kula huli utishia kunawa, tena uniondokie haraka kabla Ibilisi wangu hajapanda” Nikamfokea Yule bibi aliyekuwa akinitizama kwa matamanio ya kunipoka roho wangu.
“Wanijua mie weye?” Maua kapandisha shetani, hasira zishamjaa.
“Nikujue kwa faida gani? Mbovu weye, mbovu uso na akili za kupenda, miaka mitisa yote hiyo ulo mtelekeza kampata ampendaye tena enenda ukawasimulie na hao shogazo walo kupotosha na kukuacha ‘dillema’, njia panda, kawaambie ulomkata kampata alomkubali” Naliongea kumthibiti shwetaini wake.
“Sema nini hunijui miye mtoto wa kizaramo, umbwa weye nitakufanyizia kitu mbaya, kwa taarifayo Pompo atarejea mikononi mwangu.”
“Una wazimu nini weye? Au ushalewa na kupagawa, atinikujue mtoto wa kizaramo, enyooo! Weye ndo’utanijua miye mtoto wa kitanga, kamwe Pompo hawezi kuwa tayari kuyarudia matapiko alokwisha kuyatapika, teh teeh teeh (nikacheka kimadoido), bibi umeruka mkojo na kuyakanyaga mavi, teeh teeh teeh (nikamcheka kwa dharau, na kejeli nikiubetua mdomo wangu kumfyonya.) Ushaingia choo cha kiume sasa subiri wanaume wakuchangamkie, punga weye, bwabwa ulokosa soko.” Nikamkejeli nisitake anitie machoni,
‘Piiiiiiii piiiii piiii’ Ilikua ni sauti ya Tax ya roho wangu Pompo Keisha kuja , yupo mlangoni anapiga honi apate kufunguliwa, Jose mlinzi wangu, mtoto wa miaka kumi na mitano kamfungulia Pompo Pompo kaingia na kuipaki gari yake pale alipozoea kuipaki kwisha kufanya hivyo akaja pale naliposimama na huyu bibi mwenye sura mkomavu.
Maua kumwona Pompo akalitupa begile kuukuu chini, akamkimbilia Pompo, kwisha kumfikia akamparamia mwilini, Pompo Kamshangaa mwanamke huyu, akamtoa haraka haraka na kumtupa chini kama zigo la taka taka, alikwisha kumtambua kuwa yule ni Maua kaja kumchefua.
“Nisamehe Pompo, nisamehe mume wangu,” Maua alilia Machozi ya uchungu, mie nikamsogelea Pompo nikatua ubavuni kwake tukimshangaa yule mwendawazimu.
“Nikusamehe kwa lipi baya au lipi zuri Maua? weye si ulichagua njia zako na sasa uzirudie hizo njia ulizojiendea.”
“Pompo ni Ibilisi ndiye aliyenipitia,tafadhari rudisha moyo wako kwangu.” Maua aliongea Mie kimya nayasikiliza maongezi ya hawa wawili waliopotezana miaka na miaka.
“Nawe enenda ukampitie huyo Ibilisi aliyekupitia. Sikia Maua n’shampata wangu wa mapenzi, yeye ni huba langu, moyo wangu, roho na nafsi yangu. Yeye ni mahaba na mapenzi yangu, huyu hapa ubavuni kwangu, ninampenda sana nisitarajie kumuumiza na kumuacha.” Pompo akanikumbata na kunipiga mabusu niliyoyapokea kwa dhaati yakamchoma yule msaliti yakamuuma na kumtia kijicho.
“Najuta Pompo,najuta kwanini niliwasikiliza mashoga zangu, sikujua kuwa wale ni wanafki, wabaya wenye nia mbaya kwangu.” Machozi yalimtoka Maua angali pale chini ni mwenye huzuni.
“ Sasa ushajua kuwa wale shogazo ni wanafki wabaya wenye nia mbaya kwako?” Pompo alimuuliza Maua.
“ vemaa kama utawafuata, hao hao uliowasikiliza sana kuliko mie niliekupenda. Maji ushayamwaga ushindwe kuyazoa, tena ondoka hapa nyumbani kwangu, usiniletee mizigo nisiyoweza kuibeba.”Pompo alimjibu Maua, wakati huo huo akimnyanyua pale sakafuni apate kumwondoa aende zake huko alikotoka
“ Usinitese Pompo, usinitese uliyekuwa wangu, nipe tena nafasi moyoni mwqako nirejee.”
“Huna akili mwanamke, siwezi kupenda wawili, siwezi kuyarejea matapshi niliyoyatapika, tafadhali nifute na pia nisahau moyoni mwako, wewe ndiye uliyenitesa, umetanga tanga sana na sasa umeona heri urejee baada ya kupata dhiki za dunia.” Pompo alifanya kumsukuma Yule mpuuzi.
“Ondoka ondoka nyumbani kwangu.” Pompo aliongea kwa sauti kuu.
“Usinifukuze Pompo dunia imenifunda, sina mbele sina nyuma, sina pa kulaza kichwa change sina chakula change,” maua aliongea . Pompo hakujali kuhusu matatizo ya Maua akamwita mlizi Jose mlinzi wa lango kuu la kuingilia nyumba ile, akamwambia amwondoe Yule msaliti, Jose akafanya kama alivyo agizwa.
“Please Pompo please nipokee tena.” Maua aliongea.
“ Rejea kwa hao waliokupokea hapo awali, watakupokea tena.” Pompo alimjibu Maua.
“Nimekataliwa, nimekataliwa na ndugu ,jamaa na marafiki, NITAKWENDA WAPI MIE Pompo? Nina kutegemea wewe pekee. “ Maua alilia kwa sauti kuu.
“Na mimi ninakukataa nisikutake tena, ulipenda sana starehe hukunipenda mie sasa wanidai nini kingine? Sina unidaiacho, nimeridhika na huyu niliyemwomba Mola anipatie.” Pompo aliongea akanikumbata kwa mapenzi yote.
“Pompo…Pompo… Pompo… please.” Maua alikwisha kutolewa nje ya lango kuu la kuingilia nyumba ile. Ni mwingi wa huzuni na kilio, anaijutia roho yake, anayajutia maamuzi yake, maamuzi aliyokwisha kuyachukua hapo awali yana muumiza, haki majuto ni mjukuu na sasa leo anajuta.
Itaendelea
###################
No comments:
Post a Comment