Saturday, July 5, 2025

MWENZENU N'SHAPENDWA.

 MIPASHO YA MAMSAPU

 

MWENZENU N'SHAPENDWA 


(PASHO LA KWANZA)


Sehemu ya pili



Nyonyo👌pale tulipokomea.

              Nshapendwa na yule anayejua kupenda, yule anayejua nini maana ya upendo mapenzi na mahaba, n’shapendwa na yule aliyenikuta hoehae sina mbele sina nyuma. Leo hii ukija Kigamboni kwenye mjumba wetu wenye horofa tatu mwaya utanikuta nimetulia tuli kama Dhahabu safi mgodini, najibidisha kusuka ukindo (mikeka) kufuma vitambaa vya mezani, kudalizi, kusoma vitabu au kuandika Hadithi, kupika na kupakua kumpeti peti wangu wa rohoni wangu anayenithamini anayejali na kunijali anajua maana ya mwanamke thamani ya mwanamke na kadharika.


Basi shogangu tuendelee.

       Yeye keishanijua na mie n’shamjua mapungufu yangu na mapungufu yake kwa pamoja tunayaweka mezani tunayatatua, sie sio watu wa kulumbana ovyo, 🧨🥵sie sio watu wa songombingo vibweka na vituko, sie sio watu wa kupishana kauli, amani yetu haipimwi kwenye mizani ⚖️au kwenye vibaba hayo ndiyo  mapenzi mapenzi kuvumiliana, mapenzi kungojeana, kusaidiana na kubebeana mizigo ndo’ maana kukwambieni mwenzenu n’shapendwa kan’penda mwenyewe. Aliyen’penda namshikilia hadi tufike Mbinguni, ya kwetu mapenzi hayadodi,hayavundi, si ya kwenu yanavunda na kuvurunda? Teeh teeh teeh😄 (Nacheka mie) 


       Babu! Hilo shombo mnuko mie wapi na wapi.
Basi mwaya maneno mengi yala vitendo, mie sio muongeaji sana, mie ni mtu wa vitendo zaidi acheni ninengue baikoko 🥁 ngoma ya kitanga, acheni nikate viuno vyangu feni kwa baikoko ngoma ya kitanga. Mie hapa sishindwi, mambo ninayaweza ndo’ maana Babu haniwachi, Babu yenu kalewa kwangu, karegea kwangu na kama ni kufa basi atafia mikononi mwangu kwa haya machezo wacha tutoke ngoma droo. Teeh teeh teeh😘🤣😂 nacheka mie niliyependwa.


         Simbagui hanibagui kama wahenga wasemavyo “Mapenzi hayabagui hayachagui, kupenda mpende yeyote hata kama ana kilema.” Basi natabasamu😋😊 moyoni, Mpopo wangu mie hajanibagua kama hao waso yajua mapenzi. Hao ambao ili wakupende sharti waijue elimu yako tena elimu yenyewe iwe ile ya Madgree, Maproffes, Madoctor na maPHD, Mmmh! (nimejishika tama) Shoga kwa hali hiyo sie ambao hata elimu ya vidudu na chekechea hatujaigusa tufanyeje sasa? Au ndo’ Mungu kaandika, ati’ “Waso na elimu wasipendwe?” Nijibu shoga hilo nalo swali. Mmmh! (naguna mie) mmmmh! Makubwa, madogo yana wadogo zake.🫣😶‍🌫️🙈

          Wapuuzi hao ili wakupende sharti wavijue vyeo na kazi yako tena iwe kazi yenye mshahara mnono mnonozi na posho nzuri, sharti waijue dini yako, sharti wakuchague kutoka kwenye kabila lao, rangi yao, lugha yao na utaifa wao baya zaidi wapuuzi hawa wanahakikisha kuwa hauna ulema au ulemavu, wowote ule, kasoro zozote zile usiwe nazo shogangu. Mmmh! Haya mapenzi ya kuremba na kurembua naona kinyaa na kutapika🫢🥱🫣, haya mapenzi ya kupotezeana muda naona kichefu chefu na kutapika.

      Mie nazidi kujiuliza ndani mtimani, hivi hadi weye shogangu kufikia hapa ulipofika wapuuzi hawa wamekuwezesha wapi? Wamekusaidia kwa lipi mwaya?⁉️  Wamelikupigania weye hadi upate elimu vyeo na mshahara mnono? Mwaya mbona wanakupangia masharti kwenye maisha yako weye? Ajabu shosti! Kumbe hawajui kuwa weye shogangu umetaabika sana kufika hapo ulipofika, kumbe hawajui kuwa ni Mungu tu ndiye aliyekufikisha hapo ulipofika. Aki! Nyonyo kama wangelijua kwamba umepitia magumu maishani mwako kamwe wasingelikuwa mstari wa mbele kukupangia majukumu uso weza kuyabeba. Teeh teeh teeh 😂😂Shogangu watemeni watu hao wakanyageni na tena msiwape mioyo yenu.

Waangalieni watu hao kwa jicho la tatu wangalieni mbele na nyuma, msijaribu kuanzisha uhusiano wa malove pamoja nao. Mwaya watakufirisi hao, mwaya watakutesa hao, mwaya watakunyanyasa hadi unikumbuke mie shogako Mamsapu, mie kungwi la makungwi, mie Mama la kitanga, mie niliyependwa na aliyenipenda kan’penda kweli kweli, kwangu hameguki kwangu habanduki. Aloo!👌

             Kwa kifupi shoga ukiisha kuwajua firauni hawa, Bedui na makafiri hawa , hauna haja ya kuwasoma mara mbili mbili, weye waambieni kwa kifupi, “Pita kushoto, Babu we! Mnikome.” Wapotezee mwaya, watakuharibia time zako, hawa waja waso na akili timamu akili zao zimepalalayizi, kwetu tunawaita vichuna, vichuna Mbuzi, wakati huo huo kumbe hawajui kuchuna, hawajui kumchuna Babu kisomisomi, wapo vile vile “primitive mode of production,” kutwa kuchwa kumwomba Babu pesa za mapodozi, pesa za manukato, pesa za vitu lakshari, ati hereni, bangiri, shedo, mawigi, sendo, vitopu na vimini, teeh teeh teeh 👌😂mwaya nacheka mie.

Ngoja nikupe somo shogangu, hivi umewahi kumsikia khadija Kopa yule mtunzi na mwimbaji wa nyimbo za taarabu, Khadija anatuambia “kalichuna buzi kulila limemshinda.” Ndo’ hapo sasa!! Ndo’ hapo shogangu, mie nakwambieni weye ulichune buzi kisomisomi. Shogangu ukishampata Babu ambaye hana malengo ya kukuoa, we chunia tu, chuna pambee😂👌 ubavuni(mtimani) mwako japo asijue kuwa huna malengo naye.

               Fanya hivi shogangu, mpe Babu mapenzi moto moto yeye mwenyewe apagawe, mwimbie nyimbo za taarabu mwenyewe achanganyikiwe ujue kumbembeleza mwaya, Babu ubembelezwa kama anavyobembelezwa mtoto, kama hujui shauri yako, haya ndo yetu sie watoto wa kitanga, tunajua kubembeleza hadi Babu akabembeleka, tunajua kupuliza hadi moto ukawaka, tunajua kushika pale panaposhikika nakwambieni shoga sie watoto wa kitanga tukipenda tushapenda, hatumeguki hapo, hapo ndo’ safari, kufika kimoja, kurudi ‘never,’ kama ni kuhamia tushahamia na kuweka mji hapo.

              Waambie shogangu, waambieni hao wanaopenda kukuru kakara, hawatulii kama kijogoo tamaa.

Somo embu nitegee sikio nisikilizeni,

              Mwaka wa kwanza mapenzini, shoga punguza deko na utoto, acha utoto shoga, usithubutu kumuomba Babu vitu vya kijinga jinga kama nilivyotaja hapo juu, ati “Nataka hela nikanunue chupi, nataka hela nikanunue wigi, nataka hela nikanunue sendo, my kuna della jipya lishatoka, my mchango wa harusi, my mama anataka kusafiri , my …..” Mmmh! Shoga kwa madai hayo Babu atakuchoka, wenzio hawachuni hivyo. Yote hayo madogo madogo sio ya kumtesa Babu sababu hata weye unaweza kuyagharamia, japo kwa kudunduliza dunduliza kwenye kibubu, kuweka akiba kwenye makundi ya mashoga wanao weka upatu, au ikiwezekana fanya juu chini ukibana bana matumizi angarau upate hivyo vidogo vidogo unavyomsumbulia Babu.

N'do kukwambieni lichune buzi lako kisomi somi, si weye wajua kumpetipeti Babu, si weye wajua kumbembeleza si weye wajua kumpa malavidavi, si weye wayajua mambo yakitanga, ai! Shoga mambo ya sita kwa sita yataka mastaili, ukizubaa shauri yako, watakuibia mabinti wa kitanga, ndo’ kukwambia usiwe regerege kitandani, mperekeshe Babu hadi afie mgongoni kwako, kwa hayo mastaili shoga ai! Babu Hakuachi, au bado hujanisoma? Kama haujanisoma kawaulize wale vimburukutu shombo minuko kwanini wameachwaa solemba? Watakujibu mwaya, watakujibu kuwa mambo yamewashinda, mastaili hawayawezi muziki mzito shoga, hawawezi kukata uno, hawana vyura hawana mizigo! Teeh teeh. Lichune buzi lako kisomisomi, lichune buzi lako kimipango , usilichune kizembe.

                Shost, narudia tena kukwambieni kama ushagundua Babu hana malengo na weye, weye chunia tu au sio, weye bania , jifanye kuzuga lakini usizingue Babu asitake kujua, mpe mahaba niue, mpe mahaba nikekete, mpe mahaba niangamize, mpe mahaba ninogeshe, mpe mahaba kilio, mpe mahaba nizike, mpe mahaba nisikuache. Mwaka wa kwanza huo, kwisha mwaka wa kwanza ndo uanze kudai haki yako! Upo hapo shosti, najua bado haunisomi, embu ngoja kungwi nikupe somo. 

Maisha ni gharama usithubutu kuona unapoteza muda na mtu aso na malengo na weye, mpeleke kigamboni mwambie “My kiwanja kile kinauzwa ninunulie pesa si nyingi milioni mbili na nusu,” Teeh teeh teeh! Najua Babu lazima atakununulia tu, najua Babu lazima atakutafutia hiyo milioni mbili na nusu, najua Babu lazima ataanza kukujengea nyumba hapo Kigamboni, penzi lishanoga lishanogela, weye mwenyewe usiwe msumbufu, lichune buzi kimipango. Andaa maisha yako shoga, Maisha haya ni yako ushakuwa mtu mzima ujue. Hizo shedo, hizo lipstick, hayo mawigi hayo madelIa, ni mapito shogangu, ni vitu vya muda na kupurukutika, ni anasa na starehe za kisuIi suIi (kama ujuavyo shogangu upepo wa kisulisuli ni upepo unaovuma kwa ghafla na kutoweka, aka! Shoga usiuruhusu upepo wa kisuli suli ukutawale, hautadumu nao huo upepo utapata hasara na madhara makubwa, majuto ni mjukuu, utajuta mwaya.)


                Shoga,ukiisha kununuliwa kiwanja chako huko kigamboni hakikisha ushajengewa na weye endeleza makamuzi, mpe mpe mpe mpe mpe mpe mpe mapenzi, mpe huyo Mtumishi wa umma, mpe huyo bosi mwenye pesa zake, mpe huyo meneja wa benki, mpe huyo pendeshee mwenye pesa zake,mpe huyo papa mwenye miradi na makampuni yake mpe shogangu mpe si kwa uandunje (uchoyo) na kwa ubahiri, mpe japo hana malengo na weye lakini weye chunia tu ukiweka moyoni mwako ujumbe unaosomeka hivi, “Lazima nikuchune kisomi hadi ubakie mifupa.”

               Mwaya, mwaka wa pili mapenzini, nadhani tayari ushawekewa mradi wako mwenyewe, nyumba tayari isha simama, pesa zipo Benki Account, una gari yako weye mwenyewe kutembelea, una mashamba yao huko Kyera Mbeya ukilima mpunga mtamu unaonukia, una kibedi tumboni, basi linogeshe penzi, linogeshe hadi akupende, hayo ndo maisha mwaya, kungwi nakufunda, acha utoto wa kulilia lilia madella wakati wenzio wana nyumba wana magari wana miradi wanapesa nyingi Benki, washa jirahisishia maisha yao, maisha yao yamekuwa simple na uzuri wa akili zao tayari wana bima za afya, weye je? Weye uliyekalia anasa na starehe za kulilia kwenda kwenye makasino, kwenye mabar, kwenye makumbi ya starehe kwenye disco na muziki wa uchi utupu, mmmh! Ama kweli wahenga walisema fuja mali kufa kwaja. Mmmh! Shauri yako shoga utanikumbuka mwaya, utakumbuka kuwa Mamsapungo alisema:

                   “Umekalia kuti kavu, bado kidogo kudondoka, muda ni wakati na wakati ni muda, utumie muda vizuri kupanga mipango ya kiamendeleo, utumie muda vizuri kujijengea maisha ya baadaye, utumie muda ili muda ukufaidishe, usiwe nyuma nyuma shoga, usiwe nyuma nyuma kama mkia wa nguruwe, usiwe nyuma nyuma kama ng’ombe apelekwaye machinjioni, usiwe nyuma nyuma kama umbwa amfataye tajiri wake, usiwe nyuma nyuma kama bendera fata upepo, huku upo na kule upo, japo wahenga walisema njia mbili zikimshinda fisi msamba atachana. Watakucheka, watakucheka hadi Nyani na viumbe viso na akili, watakucheka mwaya.”

               Shoga tuendelee na mada yetu, tuliishia wapi….? Ok tuliishia pale tulipo wasuta hawa mashosti wabaguzi na wachaguzi, hawa wanaoangalia elimu kama kigenzo cha kuyajenga mapenzi, hawa wanao angalia vyeo, lugha, utaifa ukabila na udini,

                   Ndio maana hawoi wala hawaolewi, kutwa kuchwa kupodoa sura zao zile sura za majivu na masizi ati wanataka ziwe sura za Dhahabu au machungwa yaliyoiva balaaa!! Kutwa kuchwa kwenda saluni kuseti nywele zao na kuvaa mawigi, kwanza hizo nywele zenyewe haziwapendezi ni nywele mbaya kama vile wamezipaka mavi. Jamoni!! Waogopeni watu hawa hawaoi wala hawaolewi, wanaringia uzuri wakati uzuri wenyewe hawanaga, wanasaka na kutafuta wazuri huko kwenye mitandao ya kijamii (Google, Face book, Wasp na Insta.) wakati wenyewe ni wenye sura za Mazombi na mazumbukuku, wenye mioyo yenye tufani majanga na majonzi. Teeh teeh teeh, my wangu (Shogangu) mpende akupendae yule ajuaye thamani yako yule anayejua kuwa duniani kupendana.

               Tena shogangu, usipende mapito maana mapito ni yale mapenzi ya kukurupuka kurupuka kama myama aso na akili weye shogangu uwe na moyo wenye akili usibwabwatuke bure, usijipendekeze bure mbele ya wanamume, uwe makini na wanamume, maana wanamume wengine ni waongo malengo yao kukugeuza chapati kisha wakiisha kukutafuna wakuteme mkavu kama vipeke vya ubuyu na machungwa.

Shogangu Leo nimenena sana kesho nitakupa mfano.

No comments:

Post a Comment

OBIMO CHETA

 OBIMO CHETA (MY LOVE REMEMBER). Siku Derila alipokutana na Singa, ilikuwa ni siku nzuri, siku ya kusheherekea sikukuu ya Christmass,🌲🎄⛪...