MIPASHO YA MAMSAPU.
( PASHO LA KWANZA)
“MWENZENU N’SHAPENDWA.”💕
Sehemu ya kwanza.
Bibi we! Mwenye wivu ajinyonge, mwenye wivu asage chupa, mwenye wivu ajitose baharini aliwe na Papa. Maisha haya ni ya yangu mie, mie Mama la kitanga, Tanga ni kwetu kwa asilia, Lushoto ndio nyumbani, nyumbani kule mapenzi yalipozaliwa, kule mapenzi yanamea kama maua, kule ndo’ kwetu kwetu kwa mapenzi, Huba mahabuba💕🥰
Enyoooo!😉 Unaambiwa Shoga kalichuna Buzi kulila limempiku, teeh teeh teeh!! 😂😂👌(Nacheka mie) kicheko changu mwenyewe, kicheko dawa, napenda sana kucheka, tena kucheka kwenyewe nakwambieni nacheka na mboni 👁️🗨️wangu, Tende wangu Arua wangu, wangu wa ubani, Pompolimpopo kwa kifupi mwite Pompo au ukipenda mwite Mpompo, yote haya ni majina yake, yeye ni wangu na mie ni wa wake kanipenda mwenyewe.
Shoga nakwambieni huyu nitamshikilia sana, kama ni kun’torosha kan’torosha Mbinguni na kama ni kueleka nitamshikilia hata nifike naye Peponi,🌬️🌁 simwachi hasirani, simtemi abadani, ninampenda, 😍😙ninampenda pendo la kupendeka, ninampenda ajabu sioni mfano.‼️ Tena nikuombe kitu shoga'ngu nasema hivi siku ujapomkuta Pompo anaongea ama amesimama pembeni na mwanamama mwingine usisite kuniambia. Mwaya nilivyo na gere Aki! Nitaua mtu mie, 🔪🗡️nitachoma nyumba ya mtu mie,🔥 nitakwenda kwa Babu Sangoma nyumbani Tanga ili nipate kumfanya mtu kitu mbaya.
Aki! Mapenzi ni wivu na ili mapenzi yanoge na kunogela, acheni nimshikilie wangu wa rohoni, Pompo ndio jinale, acheni nimchunguze wangu wa moyoni Mzaramo aso na mapepe, makeke, michepuko na micharuko. Ndo’ mjue kuwa yeye kazaliwa pwani 🌊🚣kule wataalamu wa kupika na kupakua.
Basi nisikilizeni nyonyo, mapenzi ustaarabu, mapenzi uungwana, mapenzi upendo wa dhaati, ndo’ maana malenga Washairi wengi wanasema, wanasemaje.
Popote penye mapenzi, 😍
Hapo pana matatuzi,😻
Mema yanifuate,🥳
Na mabaya yasinikute.🥹
Teeh teeh teeh! 😂😘Ai! N’cheke mie, 😄nimelipenda Shairi hili, mwenyewe utapenda. Mwaya nikwambie nini? Mpende akupendaye hata kama ana kilema, mpende umpendaye hata kama ana maisha ya kikabwela, ndo’ maana waswahili wanasema, mpende umpendaye simche akutendaye. Kipenda boga penda na Ua 🌺lake, kipenda moyo nyama mbichi au sio nyonyo, hupo hapo? Mapenzi kikohozi, mie n’shapendwa na mie tena n’shalipenda boga pamoja na Ua lake.
Akuu! Mtoto wa kitanga nisiyajue mambo? Mbona kichekesho, n’shafundwa Bibie, n’shafundwa jinsi gani nimkande kande Babu, namna gani nimpeti peti na kumfariji, 😽kutwa kuchwa namwimbieni nyimbo za mapenzi. Nisikufiche Bibie nshafundwa mie nshafundwa namna gani niiamshe mizuka iliyo lala, ile mizuka ya kwenye sita kwa sita, pale kwenye mastyle kama yote, pale penye uturi na upepo mwanana wa kizanzibari. Bibi! mwenzenu n’shapendwa kanipenda mwenyewe. Anafurahia pochopocho nimpalo, kazidi kunenepa, kaboreka, kanawili nae katanuka, afya hiyo si mchezo!! Yeye menyewe akili kwa kusema “Mambo ninayaweza.”👌👏 Shoga weye si wamlisha mumeo madikodiko, Nyonyo kumbe kuivisha mahanjumati hauwezi?😱🥹 .Aibu🙈🙊
Kumbe wewe bado ni wa rojorojo, bokoboko, dikodiko na mitori yenye maji mengi, mmmh! Shoga mbona una haraka kama upepo wa kisulisuli, 💨wan’fanya nahisi kutapika. Utangoja👌😂
Nisikilize nyonyo👂 some time mwanamke mabadiliko, kwanza kabisa kabla haujawekwa ndani muhimu upitie unyagoni, ukafundwe huko Tanga, ukafundwe usafi sio wa nyumba pekee hata mwili bibie ili ukiwa ndani usimpe kero babu kwa huo mnuko wa kikwapa,🙀 mmmh! Yaani bibi kwapalo linuke kama panya alofia ndani, 🙊hapana, hapana jamani Babu atakutorokeni, aibu nyonyo!!
Tena shoga'ngu ukiisha kuwekwa ndani, uaminifu mia kwa mia, 💯💝hao vijibwakoko wenye tamaa za Fisi waambie wapite kushoto, wakafie mbali, vibudu hao, vinyamkera hao, waone sura zao kama Popobawa, washachelewa, wewe ushapendwa yanini tena upendwe na hao viroboto, hao kunguni, hao chawa, hao kupe, papasi na funza, waeleze Bibi waambie mwenzenu n’shapendwa kanipenda mwenyewe👌
Muhimu, tena muhimu nyonyo, nisikilize mwenzio, mie ndie kungwi, kungwi la kitanga, nakufunda, nakufunda shoga, uwe na heshima Bibie, vaa mavazi yenye stara, 🥻usiuoneshe utupu wako kwa hao waso na hekima. Jifunze kupika ama ikiwezekana niite mie kungwi la kitanga, niite nikufunde namna ya kumpikia babu, kumpikia wali wa nazi na manjonjonjo mengine kibao hapa siyataji hapa sio pahali pake labi tukutane mekoni, huko ndo’ utanijua kuwa mie ndie kungwi la mapishi, mie ndo ticha mwalimu na mwalimu n’shapendwa.
Bibi, kumbuka wako wa rohoni sharti abaki kuwa wa rohoni umuwazie yeye, umlilie yeye, stress zako zote ziwe kwa ajili yake yeye. Bibi tena ujue namna ya kukaa na mashoga maana mashoga wengine nuksi mikosi, wanaweza kukupotosha pasina wewe kujua kuwa wanakuharibia, watakuvuruga kama ungelijua kuwa wanakuzunguka mbuyu wala usingelipata shida kujua kuwa habari zingine zinafirisi ndoa. Basi shoga'ngu uwe na jicho la tatu kuwasikiliza mashoga, maana mashoga wengine hawana dogo dogo watajifanya kama wanakuja kuomba chumvi mekoni kwako, kumbe wanakuja kumkoroga mumeo na mumeo akikorogeka basi ujiandae kuachwa solemba🥹, utaliwa kasumba, shanga zote zitakupwerepweta. Ai! we! Mwenzako n'shapendwa.
Nshapendwa na yule anayejua kupenda, yule anayejua nini maana ya upendo mapenzi na mahaba, n’shapendwa na yule aliyenikuta hoehae sina mbele sina nyuma. Leo hii ukija Kigamboni kwenye mjumba wetu wenye horofa 🏢tatu mwaya utanikuta nimetulia tuli kama dhahabu,💛 najibidisha kusuka ukindo (mikeka) kufuma vitambaa vya mezani,kudalizi, kusoma vitabu au kuandika Hadithi, kupika na kupakua kumpeti peti wangu wa rohoni wangu anayenithamini anayejali na kunijali anajua maana ya mwanamke thamani ya mwanamke na kadharika.
No comments:
Post a Comment