Friday, July 18, 2025

MWENZENU N'SHAPENDWA

 


MIPASHO YA MAMSAPU 

MWENZENU N'SHAPENDWA 

Sehemu ya tano

Jina zuri kutamka, lapendeza machoni, lanivuta moyoni, nitaliweka kifuani.” Pompo kajishaua na kuchombeza maneno yaliyozidi kunifanya niweuke, n’shituke na kupandwa na hisia za kumhitaji, japo simjui lakini kanivuta macho yangu kumpenda.


                 “Shidayo nini kakangu? Je nikufungashiye matunda yepi?”

                 “Nifungashie yote na yote nitayalipia.”   

                  “Eeeh! Toba! Mwanaume we! Sijapata kufanya biashara kiwepesi kama hivyo,” nalifurahishwa na manenoye.

                   “Leo lazima upende na ukipendwa pendwa ufurahie? Pompo kaongea.

                   “Nimependa kakangu, nimependa sana tena nafurahia kwa jinsi ulivyopenda pia.” Naliongea kwa raha tele. Nikitamani kuendeleza maongezi na mwanaume huyu kijana.

                    “Kama umependa na mie pia nimependa, twaweza kuungana ili tupende zaidi.” Pompo katamka

                    “Mmmh! We mkaka una mambo, huchoki kunena.”  Ilikua ni zamu yangu mie kujishaua kwa Pompo.

                    “Naomba unielewe na pia unifikirie zaidi.” Pompo katamka.

                   “Nitakuelewa pia nitakufikiria zaidi, nipe mida mirefu, muhimu mawasiliano.” Nilikuwa mwepesi kumjibu Pompo. Akafanya kuchagua chagua matunda aliyoyataka mara ile katoa noti ya shilingi elfu kumi, kanigea, mie n’kagomea, n’kamwambia, n’kamwambiaje, n’kasema

              “Chukua hayo matunda kama zawadi yako, weye nimekupendelea.” Pompo kashangaa ule wema niliomfanyia na yeye alivyo mtani kanishika mkono wangu wa kulia kanipiga busu. Ooosh! Mie kutetemeka, jamani aibu kwa mie Bi. Dada, japo raha n’kajisikia maana yule fundi alinipendeza usoni.

              “Asante, njoo tena kesho  nitakuona Mamsapungo tuongee mengi ya maisha.” Maneno yale nilitamani yaendelee kuwepo na mie muda wote wa kukutana na yule kijana mzuri wa kunipendeza. Nilitamani nisimwache na yeye asiniwache niwe pamwe na yeye milele.

                “Nitakuja rafiki, nitakuja nikusikilizeni,"

                “Nina hadithi nyingi nyingine kwa ajili yako,” Pompo kaniambia.

                “Ninapenda sana hadithi uniwekee moja yenye umoja nipate kuburudika.” Nilimwambia Pompo kwisha kunena maneno yale mie nilijitwika kapu langu nikafanya kumuaga na yeye akaniaga akinitizama  ninavyopotea mbali na upeo wa macho yake, nisiweze kujizuia kugeuka geuka nyuma ili nimuone tena yule mwanaume kijana

##########################

               “Nina nini mie, mbona  naweweseka  weseka kitandani, ndoto nyingi nyingine juu ya huyu mwanaume kijana niliyepata kumuona mchana wa jana?” Naliongea mie na moyo wangu, ni usiku wa manane, usiku mzito ajabu ndoto nyingi nyingine juu ya huyu Pompo zilinigutusha, nimelowa jasho ajabu kama mgonjwa wa Maralia.

                 “Mkaka huyu!” Naliwaza mie Bi.dada wa kumi na 19 (19 age)

                 “Nisimpite asije kuniona mbali na peo za macho yake, nisitoweke mbali na peo za macho yake, lazima nifanye hima niwe karibu na yeye, niutue moyo pale ninapoona pafaa kutuliwa. Niridhie kwa moyo wote, moyo mmoja, nisione kinyongo  na mtima nyongo ukae mbali na mie, nahitaji furaha sihitaji sumu, sijawahi kupenda kwake huyu nitafanya maamuzi sahihi”  

Mie Mamsapu niliwaza na moyo wangu, ilikuwa ni usiku mzito, mvua sio mvua, kila tone lililodondoka lilinipa  matumaini ya kuujaza moyo wangu mafuriko, na mafuriko hayo ni mafuriko ya mapenzi.

              Hata siku ya pili tulipoonana mie na Pompo tukanena zaidi wakati huu ulikuwa ni wakati mzuri kwetu, sio tena kariakoo kule nalikomkuta pompo akijenga majumba ya watu, leo kanichukua na kunipeleka ufukweni, tena kaaga kule saiti kasema  ‘angependa kupumzika,’ ruhusa ilikubaliwa.


               “Moyo hauwezi kuishi pekee, moyo wahitaji faraja na mfariji, ujue Mamsapu maji ya moto yaliyochemka mtu hawezi kuyaoga, ila tu yakipoozwa kwa mchanganyo wa maji baridi.” Pompo aliongea tukiyatazama maji mazuri ya bahari yenye mawimbi madogo madogo.

              “Mie pia ninafahamu.” Nalimjibu Pompo kwa ufupi

              “Vizuri wafahamu, tena wajua Babu yetu Adam hakuweza kuuvumilia upweke hata Mwenyezi Mungu alipompatia mali na fahari.” Pompo alieleweka.

              “Ndio kamleta Bibi Hawa ili Adam apate furaha, mali na fahari ni vitu vya kupita tu ila wawili wenye Mapenzi walidumu.” Mie nikaongeza maneno.

               “Ninapata raha kusikia hivyo.” Kidogo Pompo aliona aibu kuendelea kuongea, muuza vinywaji alipita Pompo akaagiza soda mbili , Fanta orange baridi. Tukaendelea kunywa taratibu.

               “Rangi nyekundu yamaanishani Mmsapungo?” Pompo aliitazama ile rangi ya Fanta orange.

               “Hiyo ni rangi ya moyo Pompo.” Mie nilijibu.


              “Umejibu vema, kwa hiyo moyo wangu na moyo wako ni mwekundu eti eeh? Ok. Niambie na moyo nini?” Pompo kwa maswali ni mtu mbele za watu.

               “Moyo ni mapenzi, tena mapenzi ya dhaati yale yasiyochuja, yale mapenzi ya kumpenda akupendaye kumvumilia kwa hali zote iwe shida iwe raha na mola atajalia.”

               “Napenda unavyo jibu kwa ufasaha, acha nikuambie mie niliwahi kupenda, lakini sikubahatika kupendwa pendo la dhati kwa yule niliyempenda. Maneno ya mashoga wambea na majirani yalipozidi nguvu za moyo wake akanifanyia vibweka vituko na mikasa, hatimaye mara baada ya kunizalia mtoto mmoja wangu niliyempenda akatoweka kama upepo nisijue ni wapi alipokimbilia . Pompo aliongea kwa huzuni.

              “Je, ungali bado wamsubiria?” Mie nilihoji.

              “Sidhani kama itakuwa fair kumsubiria.” Pompo alisikitika

               “Na ikiwa hivyo?” Nikamtwaga swali jipya.

               “Maua amenitesa, Maua atanitesa yule ni msaliti na msaliti nimfayie nini Mamsapu?” Pompo aliniuliza nikacheka kidogo kisha nikamjibu.

               “Huyo ni sumu, mteme, mfute tena mtupe, usimuweke moyoni.”

               “Na baada ya hayo yote?” Pompo alinitega.

               “Tulia, mwombe Mola, fanya ibada, maisha kutafuta, umempata mwengine.” Nikajitongozesha.

                “Teh teh teh! Mamsapungo wanichekesha,” Oh! Kumbe Pompo anapenda kucheka.

                “Ongea nisikie tena,” Nilihitaji kumsikiliza.

                “Nimemwomba  sana Mola, nimetulia huu ni mwaka wa saba sasa tangu yule niliyempenda nimfute, nimteme, nimtupe nisimtake tena, nikafanya ibada za mara kwa mara na Mungu amenionesha mwanamke mzuri ninampenda.”Pompo aliongea.

               “Hongera, tayari ushampata.”

                 “Nimkose tena Mamsapu, sidhani kama hiyo bahati ni ya kunipita, ninakupenda sana Mamsapu, nimekuweka moyoni.” Akaendelea kunena.

                “Nina kuhitaji, ninahitaji kuishi na wewe.” Mie nalijifanya kushtuka.

                “Simwoni mwingine, wewe ndiwe, tulia kwangu, nitulie kwako tutulizane.”Pompo aliongea.

                “Teeh teeh teeeh,” Nikacheka na kumeza mafunda mawili matatu, moyoni nikawaza “ Asinipite mwanaume huyu, asipotee mbali na peo za macho yangu, ambatane na mie tu. Aki! Sijawahi kupenda, acheni nipendwe nami nipende na kupendeka.”

              “Mmmh! Wasema kweli  Pompo?”Nalijifanya kuuliza.

              “Mia mia, sina mizinguo, mtu mzima kama mie nidanganye tena, wallah! Nipigwe kwa moto wa Mungu.” Alitoa kiapo.

              “Nakuamini Pompo, imani yangu ipo kwako, nisiwe mwingi wa kusita sita, ninajua umenipenda na mie nimekupenda pia, tusipoteze Muda  mambo kuyajadili, tupeane nafsi mapenzi yetu machanga yaanze kuota mizizi .” Naliongea vizuri Pompo akanisogelea karibu na mie nikamkumbatia, akanipiga mabusu elfu na mie nikamrudishia mabusu elfu.

                “Asante sana Mamsapungo, asante kwa kunielewa, acha mapenzi yaote mizizi, mizizi itazaa  shina, shina litazaa matawi na matawi yatazaa maua na maua yatazaa matunda.” Pompo aliongea.

              “Asante nawe pia, asante kwa kunipenda penzi la kupendeka, basi unipe penzi la dhati, usiniwache angani, uniweke moyoni mwako.” Nalimjibu Pompo, akaniomba tufanye kuogelea kwenye maji ya bahari ya Hindi nikamkubalia.tukaeleka kujimwaga hapo Coco beach, hapo mapenzi yetu yalipozaliwa, hapo ngoma za mapenzi zilipodundwa, hapo raha na furaha kunoga.

Basi mwaya penzi letu lilizaliwa mtoni, kwenye asali na maziwa yashukayo milimani, hapo mapenzi yetu yalianza kuogelea, Pompo akanipenda sana asiweze kunitema na mie Mamsapu nikamuweka moyoni nisiweze kumtoa rohoni. Hapo sie tukakumbukana kwa yale mapenzi ya kadi na maua, zawadi tele, SMS za mahaba na mapenzi, kutembeleana mara kwa mara na kufurahia pamoja. Mie nikampenda Pompo nikampenda wangu wa mapenzi

Itaendelea kesho.

No comments:

Post a Comment

OBIMO CHETA

  OBIMO CHETA REMEMBER MY LOVE 💕  Sehemu ya nne Hakuwa na pahali pazuri pa kulala, hakuwa na maji, hakuwa na chakula, alilala kwenye majeng...