OBIMO CHETA
(MY LOVE 💕 REMEMBER)
Sehemu ya pili.
Usa river sokoni, ndipo alipoyaweka makazi yake, ndipo alipoona pafaa kuwa nyumbani, hana pahali pengine zaidi ya sokoni, tena keisha zoea maisha ya sokoni kuliko yale ya Cattle raid and ambush. Anayapenda maisha ya sokoni kuliko yale ya nyumbani kwao Loliondo, sokoni anapata chakula, wakati Loliondo hakupata chakula. leo anakutana ana kwa ana na huyu binti mzuri aliyependeza macho yake, walisimama pamoja, nao wakatizamana kwa muda wa sekunde chache kisha Delira akamsabahi Singa ambaye wakati wote huo amepumzika, amechoka kutokana na kazi nzito ya kubeba mizigo inayoletwa na maroli yanayotoka mikoani.
“Nzuri sana dada yangu.” Singa alijibu kwa tabasamu.
“Naitwa Derila, sijui nani mwenzangu?”
“Naitwa Singa.” Singa alijibu kwa rafudhi ya kimaasai.
“Ninashukuru kukufahamu kaka, ninao mzigo wangu mmoja sio mzito sana, naomba ufanye kunibebea.” Derila alimwomba Singa amsaidie kubeba mkungu wa ndizi alizozinunua mda si mrefu mara baada ya kununua mchele.”
“Waenda wapi kwani?” Singa alimuuliza Derila.
“Mtaa wa Leganga.”
“Oooh, hapo tu, mbona karibu na soko, wacha nikubebee Derila.”Singa aliubeba mzigo ule wa ndizi Uganda kisha wakatoweka na kuelekea mtaa wa Leganga. Njiani Derila alianza kumchokoza Singa kwa maneno yenye matani.
“Unaishi peke yako au unaishi na mtu?”
“Naishi peke yangu, wewe je?” Derila aliulizwa.
“Na wazazi wangu wakulima wa viazi na mahindi.”Derila alijitambulisha vitu ambavyo hakuulizwa, tena akaendelea kuongea.
“Mie ni mwanafunzi wa kidato cha nne, wewe una elimu gani?”
“Mimi standard Seven.”
“Kwanini haukuendelea na elimu ya Sekondari?”
“Aaah! Matatizo tu sister Derila.”
“Lakini unatamani kuendelea.”
“Sana, japo muda unaenda sina wa kunifanyia ufadhili.” Singa aliongea.
“Ufadhili sio tatizo, hata mimi naweza kukuunga mkono na kukufanyia ufadhili.”Derila aliongea, si kwa utani bali kwa mafumbo.
“Mmmh! Kweli.”
“Yes, I can.” Derila aliongea kwa kimombo.
“Mmmh! Singa aliguna.
“Mbona wewe ni mwanafunzi, utawezaje kunifanyia ufadhiri?”
“Uwanafunzi sio tatizo, hembu nipe nambari yako ya simu nami nikupe yangu tuwasiliane zaidi kwa ajiri ya mipango hii iweze kufanikiwa.”Derila aliongea, Singa bado hakumuelewa Derila, basi Singa akampatia Derila nambari ya simu, Derila naye akampatia Singa nambari ya simu yake, nao wakaendelea na maongezi yao.
“Uje nyumbani mchana wa leo tule na kufurahia sherehe ya Christmass.”Derila alimkaribisha Singa aje ale na kunywa kwenye ile Christmass.
“Asante sana kwa ukaribisho wako, lakini mimi ni mgeni sana, hapo nyumbani kwenu najua kwamba nduguzo watauliza sana juu ya uwepo wangu nyumbani kwenu.” Singa alivunga.
“Usijali Singa, nitawaambia huyu ni rafiki yangu…unajua …una…”Derila alihitaji kusema neno japo alihisi atakuwa anaharakia ukitegemea ni mapema sana kwake kunena neno alilotamani kulinena.
“Najua nini, mbona unashindwa kumalizia kauli yako?”Singa aliuliza, Derila alitabasamu akapunguza mwendo, naye akasimama watu wakipita na kuelekea sokoni kutafuta tafuta riziki.
“Naomba nikuambie, tena nisikufiche Singa”Derila alivuta mkono wa Singa, mkono wa kuume, naye akaugandamiza kiganjani mwake, wakatizamana kwa sekunde chache, kisha Derila akanena.
“Ninajisikia kuwa na haja nawe Singa, sikufichi ninakupenda, japo waweza kushangaa, lakini ndio hivyo tena, moyo wangu unakutamani sana, sijui wewe unasemaje.”Derila alizifuta aibu zake zote, akamweleza Singa yaliyo moyoni mwake, Singa alitabasamu, meno yake meupe pee yalivutia mbele za Msichana huyu anayejua kupenda.
“Asante, umewahi kunitamkia juu ya suala la mapenzi, mimi pia nilijiandaa kukutamkia juu ya suala la mapenzi, wacha nikuambie kuwa ninakupenda, nimevutiwa na wewe, ninakuhitaji pia, moyo wangu una furaha kuu, kwani umeushinda kimapenzi.” Singa aliongea kwa kutabasamu.
“Asante Singa, haya yawe mapenzi ya mimi na wewe, kwamba tupendane kufa na kupona.”Derila angali ni binti mdogo mwenye umri wa miaka 23. Hana aibu mtoto wa kike, anajitambua na pia anajielewa, yupo radhi kunena lolote lile ambalo hatarajii kunenewa.
“Nimefurahi sana, waonekana ni msichana jasiri, sio rahisi kwa msichana kuutoa moyo wke kwa mvulana, hadi pale mvulana ajapoanza yeye kuutoa moyo wake kwake, huu umekuwa utamaduni wa Kiafrika miaka nenda miaka rudi.” Singa aliongea. Nao wakaendelea na safari yao.
“Sijisifu wala sijigambi, labda nikwambie kuwa hii yote inatokana na elimu niliyopewa huko Sekondari, tunafundwa kujitambua, tunafundwa tujue nafasi zetu, tusionewe, tusidhurumiwe, tusinyanyaswe au kutendewa ndivyo sivyo, sisi ni watu, watu kama watu wengine japo tuna jinsia tofauti, tuna haki ya kuongea au kuongelea lile litokalo mioyoni mwetu.” Deria aliongea.
“Niahidi kwamba leo utakuja kula Christmass nyumbani kwetu,” Derila aliongea tena.
“Mbona sijajua nyumbani kwenu Derila?”
“Naelekea kukuonesha, sio mbali sana.”
“Ok, nitakuja japo kwa kujificha ficha.”
“Usijali, hata ukijificha nitakufuata hapo ulipojificha, nitakupa chakula, tutakula kwa furaha na raha, ninakupenda, moyo wangu unasema hivyo.” Derila amejaa maneno, Singa ni mpole kiasi, hana maneno mengi, yeye ni kutabasamu tu na kufurahi zaidi. Leo amefurahi zaidi, yote kwa sababu anajiona kama ameokota Almasi katikati ya mchanga.
******************************
Mapenzi, ndio mapenzi yameanza, yameanza kama vile mbuyu unavyoanza, yaani unaanza kama vile mchicha na baadaye unakuja kuwa bonge la mti, mti wa mbuyu, mti mkubwa, ajabu ya kushangaza wengi kusikia au kuona kwamba mti wa mbuyu ulianza kama mchicha.Derila alikubali kufanya mapenzi, amekubali kufanya na Singa, kumbe Derila alikuwa yungali bikra, ndio Singa alifanya kuitoa, kumbe Derila alikuwa mgeni katika mapenzi ya kimwili ndio Singa alimzoesha, lakini pia sio siri, hata Singa hakuwa mjuzi na mzoefu kwenye pilikapilika za kupendana.
Ajabu ya mapenzi, kumbe kuna wakati ambao mapenzi hufilisi, mapenzi huharibu mambo, mapenzi hubomoa mipango, yes, mapenzi ni kitu hatari, naongelea mapenzi ya kimwili kwa sababu mapenzi yamegawanyika katika makundi mengi. Mapenzi hubomoa na kuharibu pale tu ufa ujapojitokeza, kwa sababu, usipoziba ufa utajenga ukuta. Na usipojenga ukuta, ufa utaonekana dhalili., miezi mitatu ya mahusiano yao, wazazi wake Derila baba na mama yake waliletewa ripoti juu ya udhaifu alio nao Derila kuhudhuria masomo. Darasani Derila alionywa tena na tena, lakini hakuonesha dalili za kukoma, mapenzi yalimnogelea, Singa aliingia moyoni mwake, walipendana pendo la kupendwa, yaani saree sare maaua. Miezi saba mbeleni kabla Derila hajaingia ndani ya chumba cha mtihani wa kumaliza shule ya Sekondari aligundulika kuwa na ujauzito, naye akaitwa ndani ya ofisi ya mkuu wa Shule apate kujieleza kwanini amevunja sheria? Sheria inayomkataza binti kujihusisha na mapenzi akiwa shuleni, ukitegemea yeye (Derila) bado ni mwanafunzi.
Alishindwa kujieleza zaidi ya kuomba radhi asamehewe, yeye binafsi hakujua kama ipo siku hayo yaliyozuka yangelikuja kuzuka. Mkuu wa shule hakumuonea huruma zaidi ya kumpa barua ya kufukuzwa shuleni. Ooh! Masikini Derila, machozi na majuto na masikitiko pia yalimwandama, alilia masikini, alilia Derila.
Nyumbani kwa babaye na mamaye hapakukalika zaidi ya matukano na mapigo yaliyotolewa na wazazi wake, wakimlaumu Derila kwa mapungufu yake na madhaifu.
Hata hivyo Derila anatambua na kujilaumu kwa kukatisha masomo yake mara baada ya kukolea kwenye penzi alilolipenda, penzi lililompenda, mapenzi yalimfanya awe anatoroka Sekondari kila siku anakimbilia sokoni kumtafuta Singa, mapenzi yalimfanya Derila asilale nyumbani kwao, akawatia hofu na wasiwasi wazazi wake wasijue mwana wao analala wapi, kumbe mwana wao analala kwa Singa, mapenzi yalimfanya Derila azozane na kugombana na wazazi wake, lakini yote tisa kumi, Derila alikuwa sikio la kufa halisikii dawa, Derila aliyaziba masikio yake asipate kusikia neno, Derila alijipofua macho asipate kumwona mwanaume mwingine zaidi ya Singa,ndio maana Waswahili walisema mapenzi upofu, mapenzi kikohozi, kamwe hayafichiki.
No comments:
Post a Comment