Saturday, August 23, 2025

CASH MADAME



CASH MADAME.


 SEHEMU YA KWANZA


STEVEN BIKO

            Suzanna ndio jinale halisi, lakini wacha tumpatie jina la  Cash Madame, mama mwenye pesa zake, kama yeye binafsi anavyopenda kuitwa. Yeye ni mama la mapesa, hapa mjini mama kama yeye  vijana wengi utawasikia wakimwita ‘pendeshee’ yaani mama la mapesa kama nilivyo kueleza mpenzi msomaji, Suzann ana pesa mapesa, pesa nyingi kama mchanga wa bahari Suzanna hana shida kama unavyodhani weye mwenye kijicho cha ukapera yeye ni Cash madame mama mwenye pesa zake.

 Jumamosi ya leo ni wikiend moja tulivu, Suzi au tumwite kwa jina alipendalo Cash madame (Mama mwenye pesa zake) anateremka ngazi mbili tatu za hiyo Benk ya NMB tawi la Mwalimu house Ilala boma, ametoka kazini na sasa anaelekea nyumbani kwake, Magomeni mapipa huko ana mjengo wake, bonge la mjengo aliojengewa na mumewe marehemu Mheshimiwa Abdul Kadiri.

                  Suzanna aliteremka chini kwenye ngazi ya Benk ya NMB Mwalimu house, amevalia moja ya sketi fupi yenye rangi ya bluu ikionesha asilimia kubwa ya maungo yake, mapaja manono malaini ya kunenepa, yeye mwenyewe ni mweupe wa rangi ya chungwa la kitanga nakwambieni mwanamama ni mwenye mg’ao wa  dhahabu mnene wa kuridhika, wigi lake jeusi kichwani, kajipaka wanja kwenye kope zake, lipstick midomoni mwake, basi mwanamama anatembea kwa maringo na kwa madaha anaelekea kunako gari yake, gari moja zuri aina ya  Prado. Nadhani gari hiyo mwanamama kaigharamia si chini ya milioni hamsini au milioni themanini na ushee, hiyo ni kazi ya mumewe Bwana Abdul Kadiri kumfanya mkewe mrembo anapata furaha sio mdomoni pekee kunako tabasamu pia moyoni kunako hifadhi hisia za mapenzi ya dhaati

                 Suzi aliifikia gari yake, mara baaada ya kuteremka ngazi mbili tatu za ile Bank ya NMB Mwalimu house, akaingiza mkono wake wa kuume kunako moja ya pochi  zake nene zilizo jaa maburungutu ya pesa, noti mpya mpya zenye rangi nyekundu (Elfu kumi kumi) kama sikosei zilikua yapata milioni saba. Ndio tabia yake,  yeye na pesa pesa na yeye anatembea siku zote na maburungutu ya pesa mikononi mwake, hana shida yeye si ni mtumishi wa Benki na baya zaidi mumewe Marehemu Abdul kadiri hakua mtu mdogo hapa Tanzania mtu  maarufu mwenye cheo chake mwenye mshahara wake, tena mumemewe ni fisi la mafisadi, ashindwe nini? Kama ni pesa na utajiri vitu hivi havikumpa shida.

                Suzi akaitoa Remote ndani ya pochi yake ya mkononi na baada ya kuichomoa hiyo Rimoti akabinya binya vitufe fulani akiwa amesimama pembezoni mwa gari yake na hata baada ya kubinya binya vitufe hivyo gari yake ikatoa mlio wa ‘piiiiiii piiiiiii piiiiiii’ mlio wenye sauti ya chini,  mlango wa gari yake mlango wa mbele, mbele kwa dereva ukafunguka akajitoma ndani, akaingia kwa madaha akisindikizwa na macho pamoja na vimacho vya wanaume vijana wanaouza mitumba hapo soko la Ilala boma yangali yanamtizama kwa matamanio makubwa miongoni mwa macho ya hao vijana  mengine yakijisemea “nitampataje mwanamama mzuri huyu.” Suzi yupo very simple hana magumashi yaani hazingui wala hapotezei akikupenda kakaangu basi ujue kuwa amekupenda balaa, amekupenda penzi la dhaati hakuachi, au labda umuache wewe na roho yako, roho ya wivu na tamaa, roho ya……. Mmmh!  sijui utayaweza? Ushindwe mwenyewe! Teeh teeh teeh (Nacheka mie).

                  Basi ndo hivyo tena, mara baada ya Suzi kuingia ndani ya ile prado yake nyeupe, harufu nzuri ya marashi aliyoyanunua kule Pemba na Unguja yakalipamba gari lake, gari ikanukia na kupendeza zaidi Suzi akaiwasha gari yake naye akaondoka pale Ilala Boma.

                  “Dah! Sijui niende wapi siku ya leo nikajirushe?” Suzi aliwaza yeye na moyo wake yungali yupo round about, kati kati ya makutano ya  barabara ya Uhuru na  Kawawa, gari yake imesimama taa zimeruhusu gari zinazoenda Kawe, Kigogo ya Mburahati, Mabibo, Manzese na Makumbusho.

               “Aaah! Wacha niende beach, nikaangaze angaze macho yangu leo.” Suzi alihitimisha matamanio yake, sasa amebadiri nia badala ya kwenda nyumbani kwake Magomeni ameona wacha aende beach kupunguza mawazo pamoja na kupepewa na upepo mzuri wa baharini.

                      “Beach!” Suzi aliwaza tena, taa za kuruhusu magari, zilimruhusu apite.

                      “Magogoni beach, Kawe beach, Mahaba beach, Kunduchi beach, Kigamboni beach……. Ooooh beach…beach…beach….!!!’ Suzi aliongea kama mwendawazimu, gari yake iliendelea kutembea, mara jicho lake likatua juu ya uso na mwili wa kijana mmoja aliyekua akitembea pembeni ya bara bara, mtaa wa Congo, moyo wa Suzanna ulishituka na kudunda kwa kasi ya ajabu, ndu ndu ndu ndu moyo wake ukaendelea kwenda kasi, hakutaka kwendelea mbele.

 Akaisimamisha gari yake pembeni ya bara bara ya ule mtaa wa Congo, macho yake yalitua kwa yule mwanaume kijana mweusi hivi, mrefu kiasi, sio mrefu sana, ana mwili wa mazoezi,(body bulder) mwili wake umejengeka vizuri, amevalia singled inayo onesha wazi misuri ya mikono yake, misuri mizito minene ana kifua kipana kinachovutia, ana sura nyamvuto yaani sura inayovutia mwanamke, ukimwona mwenyewe utampenda, labda utakubaliana na mie kuwa asilimia kubwa ya wanawake wanaona aibu ndio maana wanashindwa kumtongoza japo wanamtamani sana.

                  Baada ya Suzanna kuisimamisha gari yake hakutaka macho yake yazibwe kwa pazia, kama wasemavyo wahenga bahati haiji mara mbili mbili, chelewa chelewa mwana sio wako, hakutaka apitwe na wakati ndio maana alikuwa macho kodo ili kujua wapi na wapi yule kijana hand some ana elekea.

                 “Ooooh!” Cash madame alivuta pumzi ndefu iliyotaka kumtoa kijasho, kiyoyozi kilicho ndani ya gari yake kilimpooza naye akalainika na kuregea kijike jike, yule kijana alivuka bara bara, kutoka kushoto kuelekea kulia sehemu ambayo gari ya madame imeegeshwa. Kijana yule mwenye body builder alitembea kwa nguvu zake zote wakati huo huo Cash madame alikua akitizama ujio wa yule kijana kupitia kioo cha gari yake, moyoni asitake kuona yule kijana anampita kama gari bovu.

                “Holla! Hallow brother!” Suzanna alimwita yule mwanaume kijana mwenye macho makubwa kama mayai ya bata, makubwa kama mfano wa mwanamke aliyetafuna kungu manga, ana nywele nyingi za kichotara wa kipemba, ni mzuri sio wa sura pekee, jinsi anavyotembea, anavyosimama na anavyomtizama Cash madame. je akifungua kinywa chake apate kuongea? Mmmh! Hiyo sauti yake tamu nakwambieni madame atachanganyikiwa, hiyo sauti yake tamu itampooza madame, italipooza joto alilo nalo, haki ya Mungu! Madame atazimia kwa furaha, presha, presha, presha ya kupanda na kushuka itampalia madame, mama mwenye pesa mapesa.

                  “Yeah madame.” Yule kijana aliitikia, macho ya hawa wawili yakatazamana.

                  “Unaelekea wapi nikupe lift?” Suzi aliongea kwa kujiamini, Keisha toka ndani ya gari yake yupo ‘out’ kisiketi chake kidogo, kilaini, kimepanda juu kinayaacha mapaja yake yakiwa wazi yanaonekana, meupeee pee, si mkorogo wala si mchina ( sio yale ya kutengeneza kwa madawa na makemikali) ni yale ya asili.

                   “Naelekea Posta ya zamani, asante kwa lift.” Yule kijana akaelekea lango la mbele kushoto, akajifungulia na kuingia, sijui kwanini hakusita sita? Yeye mwenyewe alijishanga shangaa na kujikuta tayari amejitoma ndani ya ile gari ya yule mwanamama mrembo aitwaye Suzanna. Wawili wale hawakukumbuka hata salamu zaidi ya kutizamana tizamana kama vile misukule isiyojua nini kinachoendelea.

                  “Namie naelekea Posta,” Suzi alijishaua shaua, akimtizama yule kijana aliyeketi, mbele ya gari yake.

                  “Niite Suzanna, watu wengi upendelea kufupisha Suzi.” Suzi alijitambulisha.

                  “Oooh jina zuri kulitamka lapendeza machoni, lavutia moyoni.” Yule kijana mwenye kifua kipana na mikono ya mazoezi pamoja na mwili ulio jengeka kisawa sawa aliongea, madame alifurahi kusifiwa na yule mwanaume kijana hand some.

                 “Mie ninaitwa Steven Biko lakini watu wengi wanapenda kuniita Steven power, body builder, kwa sababu ya mwili nilionao, mwili wa mazoezi.” Steven alijitambulisha wakati huo huo bado Cash madame angali ni mwingi wa tabasamu, tabasamu pana kama mlango wa pango la kale.

              “Vip umeoa Steven power?” Madame aliuliza.

              “La! Asha, sijaoa.” Steven hakushangazwa na lile swali aliloulizwa na yule mwana mama mtu mzima.

             “Na wewe je umeolewa, una mtu pembeni?” Steven power alimuuliza Madame.

           “Sijaolewa bado.” Madame alimjawabia yule kijana mwenye mwili wa mazoezi.

           “Mmmh!” Steven aliguna mguno ambao Cash madame aliusikia.

                     “Mbona waguna?” Suzi alimtwanga swali Steven Biko.

                   “Siamini kama kweli haujaolewa, kwa uzuri ulio nao utakosaje mwanaume hapa Dar es saalam.” Steven alionesha wasi wasi wake.

                   Teeh teeh teeh teeh! Madame alicheka kicheko cha maringo na madaha.

                  “Kuolewa ni bahati Steven au unataka kunioa wewe?” Madame aliropoka, Steven aliishia kutabasamu, hakutaka kulijibu lile swali la Madame haraka namna ile. Gari ya Madame iliendelea kukata mitaa.

                 “Vipi je tunaweza kupitia Hoteli tukapate Lunch?” Suzi aliongea wakiwa karibu karibu na Serena Hoteli, moja ya Hoteli za kifahari ndani ya jiji la Dar es salaam.

                  “No problems, hakuna matata, binafsi nina njaa kali.” Steven aliongea, gari ilisogea mbele na kwa bahati nzuri wawili wale walifika Serena Hoteli wakaingia wakaketi mbele ya moja ya meza za Hoteli ile, wakimsubiria mhudumu afike awahudumie mahitaji yao. Ala za muziki zilisikika masikioni mwao, magitaa pamoja na vinanda viliwaburudisha wageni waingiao na wale watokao ndani ya ile Hoteli wasijisikie wapweke wajisikie wapo nyumbani wankaribishwa tena na tena

                  Mhudumu aliitwa na kujongea pale walipoketi wale wawili, mhudumu huyu alikua ni msichana mmoja mzuri, mzuri wa kumtosha Steven Biko, waliendana kiujana ujana, yule msichana hakuling’oa jicho lake mbele ya yule mtanashati aitwaye Biko hali ile ilimpa kero na kumtia gere Cash madame, lakini hata hivyo hakujari alihitaji kupotezea, hana shida, kama ni pesa anazo, na kama ni kumpata Steven power sidhani kama atashindwa.

                  “Karibuni wapendwa hapa ndio Serena Hoteli, kuna kila aina ya vyakula na manywaji mtakayo.” Mhudumu aliongea wakati huo huo akaitoa Menyu yenye lundo la vyakula vya bei gharama akawapatia wale wageni Hotelini.

                  “Mie nipe samaki wa kukaanga wakubwa wawili, nyama iliyopigwa rosti, kuku mzima wa kunitosha pamoja na supu ya mbuzi, mtori wake uwe mwingi bakurini.” Steven Biko aliagiza mara baada ya kuisoma Menyu.

                  “Mie niletewe kuku rost wa kunitosha, maziwa mtindi pamoja na wali maini tena unijazie maini bakurini nile nishibe.” Madame alitoa oda yake. Mhudumu aliondoka na kwenda kuwachukulia, hakukawia alirejea na vile vyote alivyo agizwa, mapocho pocho kamili, manywaji ya bei ghari kutoka Ulaya na South Africa.

Basi Madame na yule Kibeni teni wake (dogo dogo) aitwaye Steven Biko, mwanaume mwenye mwili wa mazoezi, aliyejazia, aliye shiba, mzuri wa sura chotara wa kipemba na kiarabu. Waliendelea kula taaratibu taaratibu wakinyofoa nyofoa na kutafuna vipande vya nyama walizoagiza. Malaji pamoja na manywaji ya Bei gharama.

                 “Je, unakunywa Pombe?” Suzi alianza kumchokoza chokoza handsome wake aliyemuokota mtaa wa Congo.

                 “Yeah, niko safi katika unywaji wa pombe kari za kisasa.” Biko alideka.

                 “Good, nitakununulia siku ya leo, unywe utosheke, hata ukipenda agiza kreti mia, nipo tayari kukununulia.” Suzi aliongea.

                  “Waooo! Napenda sana bia pamoja na mizinga ya konyagi.” Biko aliona sasa ni fursa ya kuagiza kila atakacho. Wakati wote ule wangali bado wananyofoa nyofoa minofu ya kuku na samaki.

                   “Biko.” Suzi alimwita Biko.

                   “Naam Madame,” Biko aliitikia, Suzi akiwa ni mwingi wa tabasamu akanena.

                   “I love you so much Biko, nimetokea kukupenda sana, naomba uniamini tena unielewe mie moyo mpweke.” Suzi aliongea akimaanisha.

                   “I love you too Suzi, nimekupenda my.” Biko pasina kupepesa macho, aliongea na kujishaua.

                   “It’s true, ni kweli love?” Suzi alihitaji uhakika kutoka kwa Biko.

                    “Yes my,I mean it…..nina maanisha.” Biko hakuchelewesha jawabu.

“Waitress! Leta bia hapa.” Steven Biko alimpigia kelele mhudumu yule aliye wapokea, yule mhudumu mrembo ambaye mara kwa mara hachoki kumtazama Steven Biko kwa matamanio makuu, japo anashindwa kuelewa atampataje pataje, maana anajua fika kuwa mwanaume yule ana mtu wake, na mtu huyo ni mwanamama mwenye pesa zake.

                  Bia zililetwa, kreti zima, pamoja na konyagi mizinga, meza yao ikasheheni chupa kibao za pombe. Biko hakulaza damu aliendeleza makamuzi, alizishambulia zile bia kwa pupa ni kama vile hajapata kunywa pombe miaka na miaka mingi iliyopita.

                   “Duh! Kumbe yupo konki, konki liquid, konki master. Mnywaji mzuri wa pombe.” Suzi aliongea yeye na moyo wake mara alipomwona Steven Biko akigugumia bia mbili tatu kwa pupa.

                   “Mbona wewe haujinafsi kwa bia mbili tatu?” Biko alimuuliza Madame ambaye wakati wote huo alikua kinywa mvinyo,

                   “Aaah! Love mie tena sio mtumiaji wa kileo chochote kile, mie ni wa vinywaji baridi, soft drink,” Suzi alimjibu Biko.

                    “Jaribu kidogo sweet heart.” Biko alianza kmshawishi Suzi.

                    “Asante, nitajaribu siku nyingine, si unajua fika kuwa mwenzio ninaendesha gari.” Suzi alijitetea. Biko hakuwa na neno zaidi ya kuendelea kunywa kwa mapozi yake yote, vilevi vilipopungua hakusita kuongeza, aliagiza, aliagiza, aliagiza, aliagizaaaa, hadi alipotosheka, akawa bwii’ amelewa chakari.

                     “Mhudumu.” Suzi alimwita yule mhudumu wa ile Hoteli ya kimataifa.

                     “Abee Madame.” Mhudumu alikuja haraka haraka pale alipo Suzi.

                      “Je tunaweza kupata chumba cha kulala?” Suzi alimuuliza yule mhudumu.

                      “Ndio Madame, chumba kizuri kipo horofa ya tano, mlango nambari 25.” Mhudumu alimjibu Suzi

                      “Ok. Kamata hii shilingi laki tatu ni zawadi yako, asante kwa kutuhudumia.” Suzi alimpatia fedha yule mhudumu, mhudumu alizipokea hakukosa shukrani, tabasamu pana lilimpanuka alikenua na kuchekelea moyoni kwa furaha, ile shilingi laki tatu ni pesa nyingi kwake, ni nani mwingine aliye wahi kumpa hiyo zawadi? Mmmh! Hakuna, leo kapokea bahati, bahati kubwa kweli kweli.

                      Steven Biko alikua bwiii amelewa hajielewi, yupo juu ya meza anapepesuka pepesuka macho yake yameregea regea, mwili umeregea hawezi wala hajiwezi, Cash madame akamzoa zoa pale alipoketi na kumpeleka kwenye lift iliyowatua horofa ya tano, wakajitoma ndani ya chumba nambari 25, kufika huko, Suzi akambwaga Steven Biko juu ya kitanda kimoja nadhifu, bora kiloichoboreshwa, na baada ya Suzi kumbwaga Biko juu ya kitanda Madame alianza kumchojoa chojoa viwalo vyote ndani ya mwili wa steven Biko alimchojoa kama vile kuku anaye nyonyolewa manyoya, na baada ya kumaliza kumnyonyoa nyonyoa nguo zake, sijui nini kilicho endelea, sie hatujui, wanajua wao wenyewe kile kilichoendelea.

                              #####################

                     Mapenzi ni ua chanua, mapenzi kikohozi, hayana siri mapenzi wala hayafichiki, ndio hivyo tena ikawa hivyo lile penzi la Cash madame pamoja na Steven Biko yule kijana mwenye mwili wa mazoezi, penzi lao likachanua na kupendeza, tizama leo Cash madame anamtoa Out steven Biko anampeleka Mlimani City anaenda kumfanyia Shopping moja ya nguvu, nguo si nguo bali ni nguo za bei gharama, mashati mawili ya bei gharama, suruali tatu za bei gharama, viatu vya bei ya juu hata ile saa anayoivaa Steven Biko ni saa ya bei gharama, haki! Steven Biko kwa sasa ameanza kujiona tayari amefika pale anapotarajia kufika.

                     Ule umasikini wake wote tayari umekwisha kuyeyuka, tena sasa body builder anaishi kwenye raha na starehe, awali alikua akifanya kazi ya kubeba ‘ndwika’ (mizigo) magunia na mizigo mingine ya wachuuzi soko kuu la Ilala boma, leo kama zari ameangukiwa na bahati nasibu, yeye binafsi anajiuliza aiwache au? Mmmmh! Never, impossible, acheni ajilie vyake vimekuja kama Mana ndani ya jangwa lenye njaa na kiu.

                     Miezi miwili mbele, penzi kunoga, penzi kunogela, mama mwenye pesa zake akamfanyia suprizement yule kijana mzuri mwenye mwili wa mazoezi, akamnunulia bonge la gari Land cruser pajero gari moja jeusi la kupendeza, haki! Steven Biko aliruka ruka kama mwendawazimu kwa yeye kupewa ile gari haijatokea maishani mwake, ni kama ndoto japo ni kweli. Msela akajiona sasa hapo amefika, patamu hapo, hameguki wala hadondoki, hapo panamtosha sana, hapo amefika pengine hapaoni.

                   Basi Steven Biko akaanza kudeka na yeye akadekezwa, Steven Biko akaringa na kujiona yeye ni bora zaidi ya rafiki zake wale wabeba ndwika, wale aliotoka nao mbali kimaisha, wale wasakatonge, wale alioumia pamoja nao alio hangaika nao, haki! Mbona alijiona na tena alijigamba.

                   Miezi miwili mbele, akanunuliwa kiwanja apate kujenga nyumba yake binafsi, maeneo ya kigamboni, ramani ya nyumba yake ikachorwa, haraka haraka nyumba yake ikasimama, nzuri ajabu, nzuri mfano wa zile nyumba zilizojengwa Mbagara kama unaelekea Chamanzi, uzuri wa nyumba hizo zipo ndani ndani, zinapendeza, zimejengwa kisasa, ni za wenye pesa zao matajiri wafanyao biashara zao.

                 Mpenzi yao yakanoga na kunogela, kila alichokitaka Biko alikipata, alikipata haraka pasina kuchelewa, pesa mingi alipewa, zawadi mingi aliletewa, maeneo mengi yenye fahari alipelekwa, Steven Biko alijiona kweli kweli, alijiona tayari amefika, tena amefika pale alipotarajia kufika na ule umasikini uliomkumbata hapo awali ulianza kujimegua megua wenyewe ulijimegua kama gamba la nyoka linavyojivua. Umasikini ule ulikiri kumuacha na kumtema kabisa.

ITAENDELEA 

No comments:

Post a Comment

BEKA

 SURAYA TATU                        “AKIPITA ATAJIPITISHA.” Beka akawa member wa kampuni ya SIGA, akipelekwa hapa na pale kulinda mali za ma...