SEHEMU YA KWANZA.
HOTELINI
Ndani ya Hoteli Paradiso katikati ya Jiji la Mzizima (Dar es salaam) ZEE LAZAMANI akiwa na Mwanagenzi wake JANE wameketi wanapiga Soga, vinywaji baridi juu ya Meza vinasuuza koo zao. Zee anamshawishi Jane, Moyoni Jane anasuasua kumpatia jibu Mwalimu Zee. Ghafla BRAZA JERO akaingia ndani ya Hoteli Paradiso, aliwaona vizuri wale wawili wanaojadiliana kuhusu mapenzi. Jero akajibanza kunako kona moja ya ile Hoteli pasina kuonekana, yamkini Braza Jero anawafuatilia kwa udi na kwa vumba. Sijui kwanini? Tutajua mbele ya Safari.
“Kama ni kukupenda usiusamehe Moyo wangu Jane, Moyo haujafanya kosa kukupenda sababu kupenda sio kosa kila Mwanadamu ana Haki ya kupenda na kupenda huko Mwanadamu mwenye tamanio la mapenzi humchagua yule wa kumpenda sababu hiyo nimekupenda sana Jane.” Zee lazamani alimchombezea mtoto Jane, Kinda sawa sawa na mwanaye wa kumzaa.
“Akah! We Zee mie bado Kifaranga sihitaji kuyaharibu Maisha yangu.” Jane binti wa Kidato cha tatu Shule ya Sekondari Benjamini alijishaua mbele ya Zee lazamani.
“Waogopani? Je, waogopa ati utatimuliwa Shule? No no no, Jane hakuna wakukutimua kama vumbi pale Benjamini.Tafadhali niamini mimi, mimi ndio Zee lazamani Mwalimu mkongwe wa wakongwe, Mwalimu mkuu wa wakuu, mtetezi wako, pendo lako na Sabuni ya Moyo ukichafuka. Sidhani kama kuna mwingine zaidi ya mie.” Zee alijigamba.
“La, hasha! Siogopi kufukuzwa pale Benjamini, binafsi sina interesting ya kuendelea na masomo sababu siyapendi nafanya kulazimisha tu ilimradi kulisukuma Gurudumu liende kama vile Ng’ombe apelekwaye chinjioni. Hofu yangu ni kuingia penzini na matokeo ya kuingia penzini ninayajua mie.” Jane alijifarangua akionesha sura iliyojaa wasiwasi na woga kwa mbali.
“Mie ndiye Mlinzi wako, Malaika mwema, ninaahidi kukulinda. Sema je, wanipenda? walipokea ombi la Mtima wangu? Tuanze kuyadumisha mapenzi yakadumu na kudumika, tupendane daima.” Zee akagugumia funda mbili tatu za kinwaji chake baridi akaachia tabasamu na kufurahia.
“Moyo wangu bado haujahamasika, sioni kama umenishawishi nikashawishika au labda ningerejea tena masomoni, uniache nitulie nisiyafikirie sana mapenzi, nirejee Darasani nikajikite ndani ya dimbwi la masomo.” Jane alichanganya maneno.
“Wanipa muda tena!? Je, ninapaswa kukusubiri umalize Kidato cha Nne? Miaka miwili ni muda mrefu sana. Mmmh!” Zee aliongea kwa sauti ya deko na miguno.
“Mwalimu mpenzi, sioni baya sababu mvumilivu hula penzi bivu. Je, una shida nyingi zinazousumbua Moyo wako? Mke unaye, Bi. Mkubwa. Hawara pia unaye na mie Jane wanitaka niwe miongoni mwa wakezo? Huna haya weye, ‘mfyuuuu.’ Jane akambitulia domo Zee lazamani.
“Watakaje kwa mfano? Je, utaniruhusu nimuache Bi. Mkubwa ili nikuoe weye? Au nimteme na kumtapika Hawara wangu ili niwe na mtoto nyanya, mchele mchele kama weye? Tambua nina haja ya kuishi nawe ili nikurithishe Mali na fahari za uzee wangu. Nina Mali nyingi sidhani kama waweza kuzikadiria kwa siku moja.” Zee alitoa kiapo Jane akacheka pasina kujua kuwa Braza Jero anayasikia maongezi yale Jane akanena.
“Sijataka Mali zako Mwalimu, sijakushauri unipe Mali, hayo ni maamuzi ya ghafla. Ningependa nikuombe uniache kwanza ili nitulie masomoni niitafute elimu na mafanikio yanifuate.”
“Ninakusikiliza lakini ninaomba wewe pia unisikilize tulianzishe penzi haba haba, ndo! Ndo! Ndo! Mdogo mdogo taratibu tutafika.” Zee alijaribu tena kuitupa Karata yake kwa huyu Binti wa kumi na saba.
“Ni bora niyaogope mapema Zee langu. Nijuavyo mie Mwonja Asali haonji mara moja ataonja tena na matokeo ya lamba lamba ni kulichonga Gogo la Asali. Mie ninaisikiliza vema sauti yako lakini nawe pia yaheshimu sana mawazo yangu.” Jane aliongea Zee alishindwa kuendelea kunena, aliyapima maneno ya Jane yakapimika. Kwanza maneno ya Jane yana msimamo legelege pili maneno ya Jane yanayumbayumba, hapo ndipo Zee aligundua Jane anafeli. Mtimani Zee alikuwa akiyatengeneza maneno ambayo kwake binafsi alihisi yatamchochea na kumshawishi Jane aingie kwenye Hamsini zake.
Kama ni suala la uharibifu Zee amewaharibu sana Mabinti wa Shule, amewarubuni na kutumia kila aina ya vishawishi, vizawadi na pesa zake za Posho. Kwa muda ule mfupi aliweza kumsoma Jane, alimsoma kama Binti aliyekubali ingawaje anayachanganya maneno. Anadhiirisha kuwa amekubali ombi lake na wakati huo huo anakataa kwa visingizio kedekede viso na nguvu ya kuyashinda maneno ya Zee.
Braza Jero akiwa amejibanza Koridoni asionekane na Mtu akaiwasha Kamera ya Simu yake, Samsung Galax 7 akapiga Picha mbili tatu, Moyo wenye wivu ukamfunika, akajisika gere. Je, atafurahia vipi akimuona Jane wa Moyo wake akipangiwa mipango dhalimu na ya kulichuja penzi lao? Jero akachukizwa na yale maongezi aliyoyanyaka. Naam, Jero alifanikiwa kupata picha halisi ya kila kinachoendelea miongoni mwa Mwanafunzi na Mwalimu wake. mmoja akishawishi ili apate yale anayotamani wakati mwingine akiyakataa mashawishi ingawaje anaonesha dalili za kuyatamani hayo mashawishi. Basi Jero akalitega sikio lake asipitwe na maneno.
“Utanifurahia nikileta Posa nyumbani kwa Baba na Mamayo?” Zee aliuliza.
“Jamani Mwalimu, mbona papara!? Wamaanisha umedhamiria kunioa kabisa!?” Jane aliuliza kwa mshituko kidogo.
“Sikutanii mtoto nimekupenda, uzuri wa umbo lako na mabadiliko ya mwili wako ni moja ya vitu vinavyo nishawishi na kunihamasisha nikupende.Wacha nifanye hima nisichelewe sababu Waswahili wanasema chelewa chelewa wakuta Kuku sio wako.” Zee aliongea na kucheka.
“Mmmh!” Jane aliguna akanyanyua Bilauri pale mezani akagugumia funda moja taratibu kwa madaha, akaitwaa Tishu akafanya kuyafuta mabaki ya ile Sharubati mdomoni.
“Katika mapenzi umbo la nje na mwonekano wake ni vitu ambavyo vinaushawishi mkubwa kuliko umbo la ndani ambalo ni Moyo.” Zee aliongea kipuuzi.
“Sio kweli Zee wan’danganya.”Jane alimkosoa Zee.
“Nakudanganyaje? Embu nieleze nikuelewe ili nami nipate kufafanua maana ya kauli yangu.” Zee alimpa Jane nafasi ya kujieleza.
“Moyo ndio wenye nguvu na ushawishi mkubwa mapenzini, mwili umejaliwa tamaa. Kwa maana hiyo Moyo huanza kupenda mwili hufuata matakwa ya Moyo. Je, umenipenda Moyoni au umenitamani mwilini?” Jane hakumpa nafasi Zee ajieleze badala yake akamuachia swali ambalo Zee hakulipatia jawabu stahiki.
“Nisikilize Jane umbo la nje ni zaidi ya matamanio ya Moyo, umbo la nje linabeba na kukumbata Sura nzuri yenye umbo la Yai ling’aaro kama Taa, Ngozi nyororo yenye rangi ya Dodo lililoiva, Macho ya Kungu yanayomvuta Mwanaume tamaa. Ujaponitazama ninayaona mapenzi mazito yenye rangi ya Dhahabu iliyokooza. Umejaaliwa kinywa chenye maneno yanayomtoa Chatu Pangoni, Shingo ndefu ya Twiga mbungani kiuno bila mfupa hicho ni kiuno cha Nyingu jike, tumbo jema bichi lisilochoka na kuchosha, mapaja mazito yaliyonona na kutononoka kama nyama nono ya Nguruwe bado sijakusifia Makalio yako yanesanesa kama Tanda la Banko, haki! Mbona Mtoto wanitamanisha Mie…… Uwii! Nimesahau kukusifia chuchu zako bora kama Zabibu na Divai. Basi Mrembo usinipe tabu nikachoka, fanya kuniruhusu niingie Mtimani nitalii vigeni vilivyo ndani.” Zee alimmwagia sifa Jane, Jane akacheka na kuchoka.
“Ungali bado haujanijibu swali langu. Je, umenipendea mwili au umenipenda pendo la Moyo wa dhati? Zee akaona isiwe tabu ngoja amjibu mtoto Jane.
“Wataka nirudie kunena? Nipo tayari. Basi nikueleze, mie nimekupendea pendo la nje, penzi la mwili na matamanio ya raha za kimwili ndiyo shida yangu kuu. Macho hayana pazia kionekanacho wazi ndicho kinizuzuacho Machoni hata nishindwe kula au kulala. Ninasema kweli siwezi kupenda visoonekana sababu mie sio Jini mie ni Binadamu mwenye mapungufu na madhaifu yangu.”
“Mmmh! Sawa nimeilewa nia yako Mwalimu Zee hauna haja ya kunipenda mimi wataka penzi la kunichezea na kuniacha kapa mwenye hasara isiyoweza kubebeka.” Jane alionesha wazi kuchukizwa na kukasirishwa na yale maneno ya Mwalimu wake akanyanyuka Kitini na kutaka kuondoka.
“Umewaza tofauti Jane.”
“How come? Kivipi?”
“Uhalisia wa mapenzi ni kuchunguzana ili hapo baadae wawili turidhiane. Hivi je, bado haujaona ninavyokuchunguza mwendo na mwenendo wako? Acha niseme tayari nimeridhia ndio maana matamanio yangu ni kuleta Posa nyumbani kwa Baba na Mamayo haraka iwezekanavyo ili ukimaliza Kidato cha Nne nikuweke ndani, niwatimue wale Wanawake Wazee na wachovu Mahabani, nikupe miliki na urithi wa wanangu, nikupe raha na fahari zote unazozitamani.” Maneno yale yalimfurahisha sana Jane akatabasamu tabasamu lake zuri kama Uaridi likampendeza Zee.
“Nayafurahia maneno yako basi acha niondoke, Jumamosi ya Leo imekuwa ni siku njema kwangu yamkini nitalala na kuamka vema. Maneno yako yameanza kupooza hisia zangu mbaya juu yako.”
“Usinichukie Mtoto Jane, basi niambie ni lini tena tutatapata nafasi ya kunena mazuri kama haya? Je, waniacha upwekeni nilikose busu lako shavuni ili mie nijisikie kweli wanipenda?” Zee alimbembeleza Jane, Jane akatabasamu.
“Jumamosi twaweza kukutana Mikadi Beach, Kigamboni. Busu langu kamwe sikupi hadi siku utakaponitolea Posa, hatua itakayofuata ni kufunga ndoa na Sherehe kubwa ya bei gharama itadondoshwa, tule, tunywe, tusaze Majogoloo.” Maneno ya Jane yakamfurahisha Zee, Zee akamshuhudia yule Tausi mwenye maringo na madaha akijongea na kupotea mbali na peo za Macho yake. Zee akaendelea kunywa kinywaji chake kwa taratibu, Moyoni akijipongeza sababu Ndege mzembe hunasa mtegoni.
Itaendelea
No comments:
Post a Comment