HADITHI YA MAMSAPU
BENTEN BENITHO
Sehemu ya 1
Teh teh teh eeeh, π nacheka mie, nacheka Mamsapu nacheka mama wa Kitanga, nafurahia siku njema asubuhi Majogoloo, uhai nipewe pumzi shukrani kwake Mola, nafsi niitumie vema fursa tele bado zanisubiria. Mie niliyependwa ndani nikawekwa navuna nipandacho nala jasho langu mie mwenyewe. Mume kanipenda Moyoni haondoki anaifurahia Luba ya mahabati tena nakuambieni huyu Pompo ninamtunza kama mboni ya jicho langu, kan’torosha Peponi kan’jengea Paradiso Mbingu yangu Mbinguni.
Wahenga wanasema uzuri wa mwanamke sio sura, sio mvao wa mawigi yake kichwani wala sio maringo na madaha kama Twiga mbungani. Uzuri wa mwanamke huonekana Machoni, Macho udhiirisha uzuri au wema wa mwanamke. Kwa bahati nzuri sie wanawake tumejaliwa uzuri wa kuvumilia, kusamehe kuhurumia na kusaidia. Any way sijisifu kwa maneno na makeke!! Niwaachieni nafasi nyie wachambuzi mchambue chambue maneno yangu kama Karanga, makapi mkiyaswaga mbali na mema mkiyakusanya mkiyatunza na kuyahifadhi ili kizazi kijacho kifaudu.
Mama wa kitanga nimekujieni na simulizi moja iliyonitia machozi huzuni na majonzi makuu ninashindwa kumsahau Mwanawangu Laazizi wangu wa kufikia Benito. Mwana wa mke mwenzangu MAUA, Mwanamama niliyempokonya tonge mdomoni. Bi. Dada aliyetema pipi kwa maonjesho ya karanga. Nakumbuka nilikwisha wagea hii simulizi ya huyu Mwanadada kwenye ile simulizi yangu pendwa MWENZENU N’SHAPENDWA sioni raha ya kuyarudia matapiko niliyoyatema miaka mingi iliopita acheni nisonge mbele, mbele kuna mafanikio
Bi. Mkubwa nikampokea mwanangu wa kufikia Benito, katoka masomoni Kenya huko ndiko mwanetu kakulia, kaishi sana huko kala na kulala Hostel. Mume wangu Pompo hana shida aligharamia. Ajabu kizazi hiki kizazi cha Bongo fleva ni shida! Hakipingwi wala hakipigiwi mawe. Teh teh teh (Nacheka mie) Mtoto karejea na Satifiketi yake ya Form four ina Divisheni ziro. Mmh! Nipewe pole mie mwanamke. Mwana wa mwenzangu kakaa shule ya Bweni miaka kama yote leo hii arejee nyumbani na Divisheni ziro, niliumia.
Basi Benitho mwana wa mwanamke mwenzangu kaketi nyumbani ni mwaka wa pili sasa, hataki kwenda Chuo japo babaye ana pesa zake, kamfanyia mpango aende Chuo, mtoto wa mwenzangu hataki kusoma! Kutwa kuchwa kajifungia chumbani kwake akipigisha Muziki mzito wa Singeli, Muziki unaoniudhi mie, Muziki unanichukiza masikioni sio haba Muziki huo umejaa maneno makali ya nguoni.
Nitawachukia vibaya wale Mashuga Mamy, wale wanawake wazee waliomzidi umri mwanangu Benito, kwa waliyonifanyia Mungu anawaona, Mungu awasamehe. Wamenivuruga mie na Pompo wangu, washatutesa sana juu ya Kibenten wangu Benito kijana aliyehitimu kidato cha nne miaka miwili iliyopita sie tulitumaini mwanetu angeliibukia Bingo kunako matokeo yake ya kidato cha nne lakin mmh! Yalituchoma. Mwana karudi na FFFF, GGGG, HHHH, ZZZZ, Ziro kwenye kila mtihani alofanya
Mmmh! Makubwa haya kijana aliyeketi Hostel miaka kama yote kuanzia darasa la kwanza hadi kuhitimu kidato cha nne anafanya vibaya kwenye matokeo yake ya kuhitimu elimu ya Sekondari. Je, yule anayekaa Dei? Kulea mtoto ni kazi nzito inayotaka moyo, mie binafsi ninamlaumu Pompo Dume langu la ukweli mapungufu yetu kama wazazi yanachangia kwa kiasi kikubwa sana kufeli kwa Mtoto darasani. Kutwa kuchwa sie tulikuwa tukizisaka pesa ili mtoto asome, ale vizuri, anywe vizuri, ajisikie kwamba na yeye yupo nyumbani. Kumbe tulijisahau, tulisahau kwamba pesa pekee haitoshi kumfanya mtoto afanye bidii darasani. Tulipaswa kumfuatilia mtoto ili tuyajue maendeleo yake kitaaluma, tujue ni wapi alipopunguka tumsaidie sababu uhuru ukizidi mtoto anaharibika, tubaki tukikumbuka wahenga walisema; Samaki ukunjwa akiwa mbichi ajapokauka hakunjiki.
Kwisha kumaliza kidato cha nne Benito akatua Masikani, anataka uhuru zaidi. Yeye na Muziki, Muziki nayeye. Ndo’ uingie ndani ya Apartment yake haukosi kuvurugwa kwa sauti zile za Maspika makubwa ya Muziki yakitoa sauti nzito za nyimbo za kizazi cha leo wenyewe wanaita Bongo Fleva. Sikujisikia raha na furaha kuzisikiliza hizo nyimbo ambazo kwa asilimia kubwa hao wasanii wa kizazi cha leo haweshi kuimba utupu wa mwanamke, kumchora na kumharibu mwanamke.
Nyimbo zingine zinamdharilisha Mwanamke, hizo nyimbo za Singeli hazifuati ubora wa Lugha fasaha ya Kiswahili embu tuone mfano mmoja ambao msanii wa Muziki kama kioo cha
jamii anavyowadharilisha wanawake.
Michirizi ya kwenye Nyonga,
Shanga juu ya uno,
Matiti kama mto wa kulalia,
Nipe nikupe raha tupate.
Leta huo mzigo, Mashine nitakugea .
Mmmh! Ashakum si matusi siwezi endelea kusikiliza hizo nyimbo ziso adilifu. Serikali inawajibu wa kutoa elimu kwa kizazi hiki cha sanaa ya Muziki. Kwanza kwa kuanzisha Chuo kitakachowafunda Vijana Muzik na utamaduni wake. Vijana wetu watajua namna ya kuandika mashairi yenye vina na mizani. Nyimbo zenye maneno yenye hekima na adili. La, sio hizi ambazo Maudhui yake hayafai kusikilizwa na watoto wadogo, wazazi na jamii kwa ujumla.
Kwa hasira nikateremka juu ya Horofa ya tatu nikafika chini ya flow Apartment nikafanya kuvamia chumba cha Mwanangu Benito, nikaubamiza mlango wa chumba chake ukafunguka. Hasira zikanifanya nimpigie kelele Beni mwanangu wa kufikia.
“Mwana we! Hembu nizimie hiyo Radio Spika, aina gani ya nyimbo unazosikiliza? Nyimbo ziso na heshima wala adili. Washindwaje kusikiliza nyimbo za dini upate kujifunza neno la Mungu nawe ubarikiwe.” Nilimkemea.
“Mama wanizingua.” Kijana wangu aliongea kwa sauti kuu, sauti ya ujana wake sio nzito kuibeba, nyepesi, sio laini kama zile za videmu. Akah! Babu we, ninaogopa mwanangu akiwa na sauti za videmu mie nitaambiwa mwanao nyota yake si riziki. Ninamshukuru Mungu kampendelea Mtoto wangu mrefu kiasi, mweusi wa rangi, mwili wake ni mwili wa mazoezi ‘Body builder.’
“Sikiliza Beni ushakuwa mtu mzima na uzima wako una maana yake muhimu kuutunza ukutunze. Kumbuka ujana ni kipindi kifupi sana cha wakati, ujapouchezea ujana uzee utashika hatamu. Kwanini wasikiliza nyimbo ziso na maadili mema? Nyimbo zinazokupotosha na kukuharibia njia ya maisha yako.” Nilimkemea tena mwanangu.
“Oyah Mamangu kama hauna Idea fresh si useme tu, mie nipo na stress kibao naomba uniache nijitulize.” Beni alinijibu kihuni huni nikamtizama akaichukua paketi ya Sigareti juu ya meza, akaiwasha, akaweka domoni akaanza kuivuta mikupuo miwili mitatu.
“Mmmh!” Niliguna, moyoni nikijiuliza ameanza lini kuvuta Sigareti mwana wangu wa kufikia? Hapana. nilikereka. Nikamsogelea usawa wake nikampoka ile pisi ya Sigareti domoni nikaitupa sakafuni nikaikanyaga kanyaga na kuhakikisha haitoi moshi tena.
“Wanifanyaje Mamangu? Mbona wanipoka uhuru? Je, nimefanya vibaya kurejea nyumbani? Beni aliuliza maswali mfululizo.
“Uhuru mbaya huo mwana we! Wajua kuwa wewe ni msomi miongoni mwa wasomi tegemezi katika taifa letu? Hembu sikia. Kupata Divisheni Ziro haimaanishi ati umefeli maisha. Hapana, kuna maisha mengine baada ya kufeli Mitihani Darasani. Pale ulipoanguka amka tena endelea kukimbia, pale ulipokosea usiliwache kosa libaki kuwa kosa, jaribu kusaka ufumbuzi ili kulitatua kosa.” Niliongea kama mlevi, nisijue niliupata wapi ujasiri wa kumfokea mwanangu. Beni akafanya kutoka ndani ya chumba chake nisijue wapi anakwea, nikakitazama chumba chake kilkikuwa nyang’a nyang’a, shagalabagala, ovyo hakitamaniki kwa uchafu wa vikorokoro na vikorombwezo kibao vilivyozagaa chumbani.
Kijana kabandika ukutani picha za utupu, tupu ya wanawake wa Kizungu, picha zingine zikionesha faragha ya mume na mke. Mmh! Nilikereka nikajiuliza Mtimani ni nani anayemharibu Beni wangu? Je, ni Shule aliyosoma? Ni marafiki na makundi ya marafiki? Mmh! Nilibaki na Labda.
Njiiiiiii…..mmmmmuuu. Mlio wa gari ikiondoka ulisikika Beni alikuwa anaelekea pahali, sikutia shaka uhuru wa kuitumia gari anao, tushamuachia aitumie gari popote pale atakapo kuenenda.
Nitamwita Haika mtumishi wangu wa ndani, azinyofoe hizi picha za utupu na kuzibwaga jahani kisha azitie kiberiti, hazifai wala hazipendezi machoni. Kazipata wapi hizi picha? Hakika dunia sio ndogo ina mengi ya kuhadithia. Nilijisemea mie na moyo wangu.
Benito kasema ana stress, mawazo. Nalikumbuka kauli ile aliyoitoa Benito mwana wangu wa kufikia.
Stress gani zamsumbua? Kwanini nimeruhusu aondoke na Gari? Mmh! Asijepata ajari, asije gonga Waja wa Maanani huko barabarani. Kwa sababu ya stress asije kamatwa na polisi wa barabarani! Hapana jamani yasimpate mabaya mwanangu Benito…… Ewe Mola umwepushe. Mwanangu na dhiki za ulimwengu. Nilimwombea mwanagu Beni nikapanda ngazi za Horofa ya tatu nikamfate Haika Mtumishi wangu nimpashe kazi ile ndogo anayopaswa kuifanya ndani ya chumba cha Benitho
TUENDELEE KESHO

No comments:
Post a Comment