Wednesday, April 30, 2025

I promise you

  

I PROMISE YOU.

(NINAKUAHIDI.)






SURA  YA KWANZA.


UBAYA WA POMBE.


“Umenizingua job, umenizingua kwa muda mrefu sana mpenzi wangu…….kwanini lakini? Kwanini unanifanyia hivyo?” Brenda alinilalamikia. Machozi yake yakimtiririka kwa wingi kama mvua inayomwaga maji yake jangwani, mara baada ya ukame wa muda mrefu sana kulitikisa hilo jangwa.

               Ni ukame? Ndio ni ukame na ukame huo kwangu mimi Job naweza kuuita umasikini, umasikini uliokithiri, umasikini mkubwa haswa, umasikini wa kutupwa, umasikini ambao kamwe mpenzi msomaji hauwezi kuuokota, lakini looh! Sina jinsi ninakubaliana na hali halisi ya maisha  yangu mimi na huyu anipendaye Brenda. Machozi yake yanaumiza tena yanaumiza sana. Brenda wangu analia lakini nifanyaje mie job ningali bado ninafikra zile zile kwamba ipo siku mimi na Brenda tutakuja kuuaga umasikini na kuja kuishi maisha ya furaha na starehe.

                “Ipromise you, Ipromise you Brenda, I will fulfill all of your demand, you just have to wait , a beautiful time and a beautiful moment will come.” Ilo lilikua jibu langu, jibu ambalo nimekuwa nikimjibu Brenda kila siku ya leo, nikiziona hasira zake zinamtuma kugadhibika mambo yasije kuharibika.

               “Mpaka lini Job? Mpaka lini mpenzi? Niambie ni lini utatafuta mahari ili niwe wako  milele? Ni lini utaniweka ndani ya nyumba yako ili siku moja nije nipate kuishi kwa furaha pamoja na wewe? Ni lini Job?” Brenda aliongea tukiwa tungali ndani  pori lenye nyasi fupi,  wawili tupendanao .

             “Tambua kwamba na mimi pia ni mwanamke, tena ni mwanamke sawa sawa na wanawake wengine walio olewa, ndani na nje ya kijiji chetu wapo mikononi mwa waume zao wanafurahia mapenzi, nina imani kwamba mapenzi yao ni zaidi ya mapenzi, mapenzi matamu kama pipi, hayo ndiyo nina haja nayo, ya kwamba nina kuhitaji sana Job, ninahitaji niwe moyoni mwako nipate raha na furaha, nipendwe kama wanavyopendwa wanawake wengine” Brenda alilia.

               Nilimsikiliza tena nilimsikiliza vizuri sana Brenda wangu daima sina ile tabia ya kumkwaza mwanamke huyu, daima nimekuwa msikilizaji wa  wa shida na malalamiko yake lakini ubaya wa masikio dume niliyo nayo nimekua mgumu kumtimizia yale yote ambayo Brenda wangu amekuwa king’ang’anizi wa hayo anayo yatamani.

              “Hupaswi kutumia imani pekee mpenzi wangu Job, imani isipokuwa na matendo hiyo sio imani imani hiyo ni imani iliyokufa, imani batiri. Tafuta kazi, kazi nzuri itakayo kulipa mshahara mnono, au  jaribu kutafuta mtaji jiajiri, kazi yako binafsi. Mpenzi nimekuwa nikikushauri kila siku juu ya jambo hilo la thamani ajabu sikio la kufa halisikii dawa, unanipuuza mpenzi, wanisikiliza lakini hautendi kama ninavyokushauri, ushauri bora kama huu.” Brenda alinishutumu.

              Alikuwa na haki ya kunishutumu, kwa sababu mimi binafsi nimekuwa mzembe sana kwake,daima sina mbele wala sina nyuma, nipo nipo tu hapa kijijiini  goigoi ndilo jina langu, kila mwanakijiji ananijua na kunitambua kwa jina hilo, jina la goigoi, yaani mvivu mzembe, kijana dhaifu. Burudani yangu kuu ni kushinda kwenye bunge la walevi huko nitayapiga maji, nitapiga nitapiga hadi nivae miwani nikiisha kuvaa miwani nitajikokota kokota kwa kujilazimisha nifike nyumbani kwa babu na bibi yangu waliionilea kama yai la kuku. Njiani nitajibwaga bwagaza nitaongea kila neno la kilevi nitachekwa na wapitao njia, watoto watanizomea hilooo! Hiloooh! Hilooo! Yuuuuuu! Yuuuuu! Yuuuuu! Lilevi hilo, goigoi hilo!” loo! Mazomeo hayo ni mazomeo ya kila siku, watoto hawachoki kunizomea


            Watoto wataniimbia nyimbo za dhihaka, yote kwa sababu mimi mwenyewe ninafanya dhihaka. Pombe sio chai, tayari sarawili yangu imeloa mkojo, imezingarwa na inzi kibao wanaoimba ‘ziii….. ziii…ziii’ nyuma ya matako yangu, looh! Jamani kweli pombe sio chai, mwenzenu tayari nimejinyea tena nimeharisha. Vibaya mno, watoto hawakomi kunidhihaki kwa nyimbo zao.

Jobu akilewa lewa,
Anashindwa kujielewa lewa.
Kikojozi huyo, kikojozi huyo,
Avishwe nepi huyo, kajinyea huyo,
Huyoooo, huyoooo, huyooo,
Mtu mzima ovyo.

Oosh nyimbo zao haziniingi ndani ya ubongo wangu, ninaona ni kama burudani , nami ninaimba kwa kuwaigiliza, ninacheza kama wanavyocheza wenyewe, looh! Ama kweli pombe sio  chai, watoto wamenizoea vibaya sana, hawachoki kunikebehi kwa nyimbo zao haweshi kunizomea, haweshi kunirushia mawe haweshi kunipiga kwa bakora, yaani hadi aibu, aibu jamani aibu mtu mzima ovyo ninapigwa kwa bakora, ninapigwa kama mwanafunzi wa praimari skuli.

                 Hili jicho langu la mashoto halijapotea bure, nimekuwa chongo kwa sababu ya kujitakia mimi mwenyewe, nilijitakia kijana wa kijijini, ndo’ kusema pombe sio chai, walinena wahenga; “kipofu akimwongoza kipofu mwenziwe wote watatumbukia ndani ya shimo.” Mimi ni kipofu wa pombe (ulevi) na pombe yenyewe pia ni kipofu ambaye hachoki kunipotosha pamoja na kunipitisha njia zenye hitilafu.

                Pombe ni kipofu, ndio ni kipofu, kwa sababu haoni mdudu huyu, haoni mbele, haoni nyuma, kazi yake kubwa kupotosha vijana wa kijiji ninacho ishi.
Ninaukumbuka ule usiku usio na mbalamwezi, usiku ambao almanusura niwe kipofu wa macho yangu yote mawili lakini hata hivyo ninamshukuru sana mwenyezi Mungu, niliponea chupu chupu kufa, nusu kufa, mjiti uliniingia ndani ya jicho langu la kuume, duh! Ni kama vile ulikua mtego, mtego uliotegwa kwa makusudi ili unikomeshe mie goi goi nisiye taka kufanya kazi.

               Niliteleza kwenye tope ambalo lilijikusanya pahali mara baada ya mvua kunya usiku kucha. Ilikua ni usiku, usiku usio na mbalamwezi, sikumbuki ilikua yapata saa ngapi, usiku ule mie kijana goi goi mvivu nisiyetaka kufanya kazi nilitoka kwenye bunge letu, bunge la walevi. Nimegida mitungi ya kutosha, sina hofu, nimekwisha kuzoea kwenda bungeni saa za majogoo na kurejea nyumbani saa za kulia kwa mabundi na mapopo. Mimi ni Mbunge mtiifu wa  gongo, changaa na matapu tapu mengine mengi yaliyopitwa na wakati.

Daima nipo, sikosekani kwenye bunge letu la walevi wa kijiji chetu,  huu ni mwaka wangu wa tano ningali bado nipo bungeni na uzuri wake  kwa sababu nina maudhurio mema sina budi kujitapa kwa cheo chema nilichopewa na walevi wa kijiji chetu. Spika wa bunge la walevi, hilo ndilo jina langu, jina tukufu ulevini.

                Nisikufiche mpenzi msomaji, nilijikuta najistafisha kuhudhuria vikao vya bunge la walevi, nilijiuzuru mimi mwenyewe pasina shinikizo la wabunge au mawaziri wa bunge letu, bunge la walevi, sababu kuu ikiwa ni kukumbwa na mkosi huu mzito wa kugeuka chongo na chongo yenyewe niliivuna kutokana na ulevi wangu wa kupindukia.

                Usiku ule nilikua bize nagara gara ndani ya dimbwi lenye tope, ili nipate chance ya kujiokoa na kutoka ndani ya lile dimbwi nililo tumbukia kutokana na ulevi. Nilikuwa bwii kwa pombe ya gongo,  nilifanya kila niwezalo nipate kujiokoa kutoka kwenye lile shimo lenye tope,  nikiwa bado ndani ya lile dimbwi nilijiuliza nitatokaje ili nipate chance ya kwenda nyumbani kwa babu na bibi nikajibwage kitandani, niusake usingizi wa pono ili nipate kujiandaa  asubuhi na mapema niwahi bungeni  kupiga mitungi. Haki nilikuwa mlevi, mlevi mbwa, mlevi aliyeshindikana.

Jitihada za kutoka ndani ya lile dimbwi hazikuzaa matunda, nikajikuta napiga kelele za zilizotokana na maumivu makuu, maumivu yasiyo na kipimo, maumivu yasiyo na kikomo.

                 “uwiii! Uwiii! Uwiiii! Yallah toba we! Jicho langu jamani jicho langu! Nafwa mie, nafwa jamaa” kilio kilinitoka, kilio cha mlevi mwendawazimu, kumbe nilidondoka, kumbe nilidondokea kwenye shimo lililokuwa na miiba mirefu, mikavu iliyochongoka kama pini, ikauchoma choma mwili wangu na ubaya wake jicho langu la kuume(kulia) halikupona lilikua ni miongoni mwa sehemu zilizoonja shubiri ya mwiba, lilikua kwenye ile ajari ajari ya mlevi, ajari ya kujitakia.

                Ndio maana nimekwambia mpenzi msomaji nilijikuta naachana na ulevi, nilijikuta naachana na mazowea ya kwenda kwenywe bunge la walevi, nilijikuta najiuzuru cheo na wadhifa wakuwa spika wa bunge la walevi, ilinibidi niachane kabisa na pombe. Walisema wenye hekima asiye fundwa na mamaye ulimwengu utamfunda. Mama na baba yangu walikwisha tangulia mbele za haki sikupata nafasi ya kufundw a na wazazi wangu, malezi yaliyo jaa madekezo mapendeleo na matunzo ya kiyai yai ndiyo niliyapata kutoka kwa babu na bibi wazazi wa baba.

                Mapendeleo yasiyo  na kipimo, mtoto toka utotoni hadi baleghe sikua na nafasi ya kujishughurisha na shughuri yoyote ile ndani ya nyumba ya babu na bibi yangu, ni madekezo tu madekezo na mapendeleo, nililishwa vizuri, nilinyweshwa vizuri, niliogeshwa, nilibebwa nikapewa kila kitu nilicholilia na baya zaidi nikawa mtoto msumbufu, mwenye masumbufu makuu.

                Kila lenye mwanzo halikosi mwisho, kwenye kuzaliwa kuna kufa, kwenye raha kuna karaha, kwenye amani vita pia ipo, sikutilia imani mawazo hayo hapo juu , ubongo wangu ulikorea pombe, pombe ya matapu tapu, ubongo huu mbovu usojua la muadhini au mnadi swala maisha yangu yalikua ni maisha ya kunywa matapu tapu ya aina mbali mbali, iwe umkombothi, iwe ulanzi, iwe mbege, iwe chibuku, ubwala, gongo, pombe ya minazi, pombe,  pombe, pombe,  pombe…….. Kila aina ya pombe kali mie nilikunywa, pombe kali kuliko sumu ya panya mie nilikunywa, pombe chungu kuliko nyanya chungu mie nilikunywa, nilijisikia fahari kunywa, nikalewa, nikasaza nikaburudika nikausuuza mtima wangu.

                 Leo nimeona wacha nifanye maamuzi magumu, maamuzi ya kuachana na pombe, pombe ni kipofu hawezi kuniongoza, ndiye aliyesababisha nitumbukie kwenye dimbwi lenye tope na katika harakati za mie kujiokoa nikajikuta natumbukia tena kwenye shimo lenye miiba iliyonigeuza chongo  jicho la kulia. Leo nifanye maamuzi ya kuikacha pombe, sio tu kuikacha pamoja na kujiweka mbali na pombe kusisitisha yale mazoea ya kwenda bunge lao bunge la walevi. Kama ni hasara jamani hasara kubwa nimeipata, hasara ya kulipoteza jicho langu la upande wa kuume. Sio hasara hiyo tu pia kuna ile hasara ya kujifedhehesha na kujiaibisha mbele ya watoto waliokuwa wakinizomea na kunichapa bakora.

                Katika kipindi chote hicho Brenda alinivumilia, Brenda hakuniacha japo nilikuwa mlevi nisiye na kikomo, na uzuri wa Brenda yeye kama mwanamke alijiweka tayari kunishauri niachane na hiyo tabia mbaya ya kupiga miknge, nalikuwa sikio lililokufa halisikii dawa, Brenda aliponiongelesha sikio la mashoto mie  nilijigeuza kiziwi, tena kiziwi anayesikia sauti lakini maneno hayaingii sikioni, Brenda akiniongelesha sikio la kulia bado nalijigeuza kiziwi nisielewe wala nisijielewe.

                Wanasema mtoto wa nyoka ni nyoka, tena wanasema ukijenga urafiki na mwendawazimu tegemea na wewe pia kuwa mwendawazimu, waswahili wako sahihi . mwanzo mgumu, lakini mwisho ni mazoea Brenda aliyekuwa kinara wa kunipinga nisinywe  matapu tapu kwa utundu wangu mie mwenyewe nikamuweka mtu kati nikamwonjesha matapu tapu kidogo kidogo, pole pole ndio mwendo, tabia ni mazoea Brenda akawa nguli wa kunywa matau tapu, akaifuata tabia yangu, tabia ya kunywa  kama mwendawazimu na kwa hilo mwenzangu mbona alitia fora. Alikunywa zaidi ya chupa kumi  za matapu tapu, zile chupa zenye ujazo wa bia aina ya Safari zilimtosha  usiku na mchana, Jua likichomoza jua likizama siku nzima.


                #########################################

Itaendelea



No comments:

Post a Comment

I promise you

   I PROMISE YOU. (NINAKUAHIDI.) SURA  YA KWANZA. UBAYA WA POMBE. “Umenizingua job, umenizingua kwa muda mrefu sana mpenzi wangu…….kwanini l...